The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Ujitokeze Kuhesabiwa Msimu Huu wa Sensa?

Sensa ni hatua muhimu kwenye mchakato mzima wa kuwaletea wananchi maendeleo.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine mbalimbali, imeendelea kuendesha kampeni mbalimbali zinazolenga kuwahamisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotegemewa kuanza hapo Agosti 23, 2022.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012. Hivyo, sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Lakini kwa nini Watanzania wajitokeze kushiriki kwenye zoezi hili? The Chanzo imefanya mazungumzo na Mtakwimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Wilaya ya Dodoma Calista Makacha ambaye amebainisha kwamba zoezi hilo ni muhimu sana kwenye upangaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.

Mwananchi atakayeshiriki kwenye zoezi hilo atatakiwa kujibu jumla ya maswali 93 ambayo yanalenga kupata taarifa zinazohusiana na demografia, umri, eneo la makazi, shughuli zao za kiuchumi, hali zao za mazingira, upatikanaji wa maji na vitu vyote vinavyomzunguka yeye kama mwananchi.

Makacha ameieleza The Chanzo kwamba matokeo yatakayopatikana kutoka kwenye zoezi hili yatasaidia kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 na Mpango wa Pili wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA) II.

Pia, yatasaidia kupima utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo 2021/2022 hadi 2025/2026, kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 pamoja na kupata takwimu za msingi za kufanya maandalizi ya Dira ya Taifa ambayo mchakato wake unaendelea ndani ya Serikali.

Kwa pamoja, mikakati yote hii inalenga kuboresha juhudi za Serikali kwenye kuwapatia huduma stahiki wananchi ili kuondokana na ugumu wa maisha.

Tofauti na kupiga kura

“Sensa ni tofauti na kupiga kura kwamba [mtu] anakwenda kwenye kituo cha kupiga kura,” anasema Makacha. “[Kwenye sensa] karani anakukuta nyumbani kwako. Kwa hiyo, mwananchi wa Dodoma awepo siku hiyo nyumbani kwake. Shughuli za kiuchumi zitaendelea lakini wanaweza kuacha mtu mmoja ambaye anazijua zile taarifa zinazohusu watu waliolala kwenye kaya zao kuamkia usiku wa Agosti 23, 2022.”

Akiendelea kueleza kwa nini wananchi washiriki kwenye zoezi hilo, Makacha anasema mbali na Serikali, sensa pia husaidia wadau wengine kama Asasi za Kiraia, taasisi za utafiti, taasisi za elimu ikiwemo vyuo vikuu ambavyo zote, kwa pamoja, hufanya kazi mbalimbali za kuwahudumia wananchi kwenye nyanja mbalimbali.

Wakati anakiri uwepo wa watu wenye mtazamo hasi juu ya zoezi zima la sensa, Makacha anabainisha kwamba tatizo hilo hawajakutana nalo mkoani Dodoma. Anaeleza kwamba Dodoma ni miongoni mwa mikoa 13 iliyofanya sensa ya majaribio ambayo ilifanyika kata ya Dodoma Makulu mnamo Septemba 2021.

“Zoezi lile lilikuwa zuri sana kwani wananchi walijitokeza, tulihesabu kwa asilimia 100,” Makacha anaieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni. “Hakuna aliyeachwa nyuma na mwitikio ulikuwa mkubwa.”

Wenye ulemavu wasifichwe

Makacha anahimiza wananchi kutokuficha watu wenye ulemavu kwenye zoezi zima la sensa kwani na wao ni sehemu muhimu katika zoezi hilo. Anasema ni muhimu wakatolewa na kuhesabiwa ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi ya watu wenye ulemavu nchini.

“Na uzuri ni kwamba kuna swali linauliza, je, fulani ni mlemavu?” anabainisha Makacha. “Na kama ni mlemavu je, ana ulemavu wa nini? Kwa hiyo, Serikali, kiujumla, inahitaji kupata idadi ya watu wote wenye ulemavu na aina za uelamvu walizonazo.”

Makacha anasema kwamba kama mkoa, Dodoma imeweka mikakati thabiti itakayohakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa kwa asilimia zote. Moja kati ya mikakati hiyo ni kuzihamasisha kamati ambazo zimeteuliwa kwa ajili ya kusimamia zoezi la sensa kutoa elimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo.

‘’Kupitia hizo kamati, wajumbe wanaandaa mikutano ya dharura ya hadhara lakini wataongea na wananchi wao kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu sensa,” anasema. “Lakini pia kuna vyombo vya habari, kama hivi nyinyi [The Chanzo], watakaosikiliza au watakaoangalia wataelewa kitu kuhusiana na sensa. Kwa hiyo, ninaamini mpaka kufikia Agosti elimu itakuwa imefika kwa watu wote.”

Sensa kwa maendeleo

Naye Mratibu wa Sensa Mkoa wa Dodoma Idd Muruke amesema sensa ni muhimu kwani itawezesha kupata idadi ya watu ndani ya nchi, makundi mbalimbali ya Watanzania, watoto wangapi wanaotarajia kwenda shule, sehemu yenye mahitaji ya msingi ya huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na vituo vya afya.

“Vitu vyote hivi vinategemea taarifa muhimu ambazo zitakusanywa katika sensa hii,” anaeleza Muruke. “Kwa maana ya kwamba tutaweza kujua idadi ya watu ambao wapo katika kila eneo ambalo linahitaji huduma.”

Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Anne Makinda alisema kwa nchi kufanya sensa kwa mafanikio hutegemea upangaji mzuri wa mipango na utekelezaji na ufuatiliaji wa shughuli za sensa. Jambo la muhimu zaidi kwa Makinda ni kuasisi mfumo mzima wa usimamizi na uongozi kusaidia utekelezaji wa shughuli za sensa.

Makinda aliyasema hayo Mei 21, 2022, wakati akizungumza katika kikao cha kwanza cha Kamati ya Ushauri ya Ufundi ya Sensa ya Watu na Makazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Makinda, mwanamke wa kwanza kuhudumu kama Spika wa Bunge la Tanzania, alisema kwamba Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi kubwa lenye umuhimu wa kipekee kwa nchi kwani kuwa na takwimu za idadi ya watu ndiyo chanzo cha maamuzi ya kisera, upangaji mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma zinazotumia vigezo vya kitakwimu.

“Takwimu za sensa hutumika pia kuweka sampuli za utafiti za kitaifa na ni chanzo cha kufuatilia viashiria vya utekelezaji wa programu za kikanda na dunia kama Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya mwaka 2030,” alisema Makinda.

Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *