The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukiukwaji wa Haki ya Ardhi kwa Wenyeji wa Ngorongoro Umekuwa Kero

subscribe to our newsletter!

Ukiachilia ufugaji ambao ndiyo umekuwa nguzo kubwa na kitega uchumi kwa Wamaasai na wenyeji wa Ngorongoro walio wengi, kabla ya mwaka 2009 Wamaasai walikuwa pia wakijihusisha na kilimo cha kujikimu.

Mwaka 2009, hata hivyo, Serikali Rais Jakaya Mrisho Kikwete iliondoa kilimo cha kujikimu katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), jambo ambalo limepelekea kushamiri kwa janga la njaa katika eneo hilo. Serikali, kwa kutokujali wenyeji wa eneo, ilishindwa kuweka njia mbadala na thabiti ambazo zingewawezesha wenyeji kupata chakula bora.

Badala yake, kaya moja ililazimika kutegemea debe tatu za mahindi ambazo zilikuwa zikitolewa kila baada ya miezi mitatu, mahindi ambayo ni ya msaada, kinyume kabisa na utaratibu uliozoeleka na wenyeji. Kilimo cha kujikimu kilikuwepo karibia kata zote ndani ya tarafa ya Ngorongoro, ikiwemo Ngorongoro, Endulen, Ngoile, Nainokanoka, Olbalbal, Misigiyo na maeneo mengine.

Mnamo mwaka 2017, Serikali ya Rais John Magufuli iliendeleza unyanyasaji huu dhidi ya wenyeji wa Ngorongoro baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupiga marufuku mifugo kushuka katika eneo la Creta ambalo mifugo ilikuwa ikipelekwa kwa ajili ya chumvi na maji kwa baadhi ya vipindi ndani ya mwaka.

Jambo hili pia limesababisha madhara makubwa ambayo ni endelevu kwani mifugo imekuwa ikifa kila mwaka. Ikumbukwe kwamba madini ya chumvi ni umuhimu sana kwa afya ya mifugo.

Mpango wa uhamishaji

Inaonekana hatua hizi ni sehemu ya mpango wa siku nyingi wa Serikali kutaka wenyeji waondoke Ngorongoro. Kati ya mwaka 2019 hadi sasa, kwa mfano, Serikali imeendelea kutekeleza mpango huu wa kuwaondoa wenyeji kwenye eneo ambalo walikusudiwa waishi pamoja na wanyama wengine.

Mnamo mwaka 2019, Serikali ilitoa orodha ya watu zaidi ya 45 ambao walitakiwa nyumba zao kubomolewa kwa madai ya kujenga ndani ya hifadhi. Hata hivyo, mpango huo ulifeli kutoka na shinikizo kubwa kutoka kwa wenyeji na wananchi kwa ujumla walioukosoa kwa nguvu kubwa.

Lakini tangu awamu ya sita iingie inanaonekana kuna nia ya kutaka kuwahamisha wenyeji kutoka Ngorongoro, huku Serikali yake ikichukua hatua kadhaa kufanikisha mpango huo, hatua ambazo wadau wengi wamezielezea kama zinazokiuka haki za msingi za kibinadamu.

Vikao kadhaa vimekuwa vikifanywa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kile kinachoonekana ni kufanikisha mpango huo, huku wenyeji wakilalamika kwamba Serikali imekuwa ikikutana na watu wanaojifanya kama wenyeji wa Ngorongoro wakati ikikataa kukutana na wenyeji wenyewe.

Hii imefanya wenyeji kuwa na wasiwasi na nia ya Serikali, wakihofia kwamba kuna hila inaelekezwa dhidi yao.

Ukinzani dhidi ya uhamisho

Wana Ngorongoro tumekuwa tukipaza sauti juu ya unyanyasaji huu, tukipinga mikakati yote inayohusu uhamisho. Pia, tumekuwa tukiwakemea wote wanaohusishwa katika mkakati wa sisi kuondolewa katika ardhi ya mababu zetu na matendo hasi tunayofanyiwa na Serikali yetu, ikiwemo kunyimwa fedha ambazo zingechochea maendeleo yetu ya huduma za kijamii.

Kwa mfano, mnamo Machi 31, 2022, tumeona fedha za miradi ya UVIKO-19 zaidi ya Sh355,000,000 zikihamishwa kwenda Halmashauri ya Handeni kinyume na taratibu kwani hata viongozi na wajumbe wa Halmashauri ya Ngorongoro hawakushirikishwa katika mchakato huo.

Hata mpango wa Serikali kutaka kuwahamishia wenyeji wa Ngorongoro huko Msomera, wilayani Handeni, mkoani Tanga ni mpango wenye mashaka makubwa. Msomera ni kijiji halali kwa ajili ya wananchi wa Msomera. Hii maana yake ni kwamba hili siyo eneo huru – wala salama – kwa wenyeji wa Ngorongoro kuhamishiwa.

Ni kitu kimoja kwa mwenyeji mmoja au wawili kutoka Ngorongoro na kuanzisha makazi kwenye eneo lolote la nchi kwani hii ni nchi yetu sote na mtu ana haki ya kuishi popote pale anapohisi anataka.

Hata hivyo, ni kitu kingine kabisa kwa wa jamii nzima kuhama wao, mali zao na mifugo yao yote na kuhamia kijiji kingine.

Hii ni lazima itachochea ugumu wa maisha kwenye kijiji hicho, kwa kufanya rasimali kuwa chache kulingana na ongezeko la ghafla la idadi ya watu. Katika mazingira kama hayo, migogoro kati ya wageni na wenyeji itakuwa ni jambo la kawaida.

Hii yote maana yake ni kwamba zaidi ya kutatua tatizo, kupeleka wenyeji wa Ngorongoro Msomera na maeneo mengine yaliyotengwa ni kutengeneza bomu jengine ambalo litalipuka muda ukiwasili.

Wenyeji wa Ngorongoro tumekuwa tukilibainisha hili kadiri tunapopata nafasi ya kufanya hivyo. Ni katika kutahadharisha haya ndipo askari hutukamata, hutuweka kizuizini na hata kutupiga bila ya kuwa na hatia yoyote zaidi ya ile ya kupigania haki yetu ya kubaki Ngorongoro.

Hata hivyo, juhudi hizi hazifanikiwa mpaka sasa kwenye kudhoofisha mapambano yetu.

Maslahi ya kibiashara

Sisi wenyeji tunaamini kwamba chanzo cha mgogoro unaoendelea hivi sasa kati yetu na Serikali unatokana na nia ya Serikali kutaka kutetea na kulinda maslahi ya makampuni ya utalii dhidi ya maslahi ya wenyeji.

Sisi hatuoni sababu nyengine kwani takraban madai yote yanayotolewa kuhalalisha kutolewa kwetu Ngorongoro yameshajibiwa kitaalamu na kuthibitishwa kuwa hayana ukweli wowote lakini bado Serikali imeendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka kutuondoa hifadhini humo.

Wananchi wa Ngorongoro, kwa umoja wetu, tumekua tukikabiliana na tishio dhidi ya ardhi yetu ya asili kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kufunga na kumuomba Mwenyezi Mungu ili awe nasi katika vita hii.

Hii inatokana na imani thabiti tuliyonayo tukiamini kwamba tunachofanyiwa sisi wenyeji wa Ngorongoro siyo haki na dhuluma kamwe – popote pale – haijawahi kushinda haki.

Ardhi Yetu Maisha Yetu.

Maisha Yetu Ardhi yetu.

Hatuondolewi kwa Jina la Uhifadhi!

Tubulu Nebasi ni mwenyeji wa Ngorongoro kutoka kabila la Wamaasai. Kwa maoni, anapatikana kupitia tubulunebasi@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa mawasiliano zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Serikali haiwatoi Wamaasai kwa sababu ya Uhifadhi Inawatoa kwa sababu ya Uwekezaji na Ukitaka kujifunza Maeneo Mengi Yenye Migogoro ya Ardhi serikali Haiwapi hawa Watu Hati Miliki Kwanini??
    Ili iwe Rahisi Wawekezaji Kupewa Kiurahisi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *