The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waethiopia Wanaokimbilia Afrika Kusini Waeleza Maswaibu Wanayokutana Nayo Tanzania

Maswaibu hayo yanajumuisha udanganyifu, unyonywaji, manyanyaso na hata kifo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Raia wa Ethiopia wanaotumia Tanzania kama njia ya kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha bora wameeleza maswaibu wanayokutana nayo wanapokuwa nchini, ikiwemo udanganyifu, unyonywaji, manyanyaso na hata kifo.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Uhamiaji (IOM) iliyotolewa mwishoni mwa Mei 31, 2022. IOM ilifanya utafiti mdogo kuhusiana na wahamiaji wenye asili ya Ethiopia kufuatia ombi kutoka kwa Ubalozi wa Ethiopia nchini Tanzania.

Kwenye ripoti yake, IOM inabainisha kwamba jumla ya raia wa Ethiopia 369 waliohojiwa kwa ajili ya utafiti huo, ambao ni sawa na asilimia 97 ya watu wote waliohojiwa, wameripoti ukosefu mkubwa wa chakula, maji na makazi wanapokuwa safarini kuelekea Afrika Kusini.

Jumla ya raia 270, sawa na asilimia 71, wamekiri kuteswa wanapokuwa safarini. Jumla ya raia 18 wamekiri kushuhudia kifo cha wahamiaji wenzao, muda mwengine vifo viwili mpaka vitatu vya wahamiaji wenzao.

“Kwenye kisa kimoja,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ya IOM, “wahamiaji 15 kutoka kwenye kundi la wahamiaji 60 walifariki,” kwa mujibu wa wahamiaji waliohojiwa. Familia kadhaa zilizohojiwa kwa ajili ya ripoti hiyo zilikiri kupoteza angalau mwanafamilia mmoja kwenye mchakato huo wa kukimbilia Afrika Kusini kupitia Tanzania.

Hii, hata hivyo, haiwahamasishi wazazi kuwakataza watoto wao kufanya safari hiyo licha ya hatari inayoambatana nayo.

“Japokuwa nimempoteza mtoto wangu wa kiume, bado nawahamasisha vijana kujaribu bahati zao kwa kusafiri kwenda Afrika Kusini kwani kila mtu ana hadithi tofauti,” ripoti hiyo inamnukuu mama mmoja akisema. “Maisha yetu [kama familia] yameimarika sana watoto wangu wanne pamoja na mume wangu walikuwa wakiishi Afrika Kusini.”

Matumizi ya Tanzania – na Kenya – na raia wa Ethiopia wanaotaka kwenda Afrika Kusini yamekuwa yakifanyika tangu miaka ya 1990. Lakini kwa mujibu wa ripoti hiyo ya IOM, safari hiyo mara nyingi inakuwa siyo rahisi, kwani wahamaji hukutana na kila aina ya madhila kadhaa kwenye safari zao.

Wakihojiwa na timu iliyoandaa ripoti hiyo, raia wa Ethiopia walieleza kwamba mara nyingi huwachukua kati ya wiki na miezi mitatu kuweza kufika nchini Tanzania. Raia hao hulazimika kulipa $5,000, ambazo ni sawa na takriban Sh11,600,000 kwa safari.

Raia wengi wa Ethiopia wanaokimbilia Afrika Kusini kupitia Tanzania wanatajwa kuwa ni vijana ambao hali zao za kiuchumi nchini Ethiopia huwa siyo mbaya sana. Kwa mfano, ripoti hiyo ya IOM inasema kwamba asilimia 80 ya wahamiaji wana vyanzo vya mapato nchini Ethiopia na hupata mpaka Sh163,030 kwa mwezi.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikiwakamata raia wengi kutoka nchini Ethiopia kwa madai ya kuingia nchini kwa njia zisizo halali. Mara nyingi raia hawa hushitakiwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kufungwa kwenye magereza mbalimbali.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa IOM, kuna jumla ya wafungwa 793 raia wa Ethiopia kwenye magereza mbalimbali ya Tanga, Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam.

Mnamo Januari 2021, hayati Rais John Magufuli aliagiza kuachiwa huru kwa raia wa Ethiopia jumla ya 1,789 waliokuwa wakitumika vifungo kwenye magereza mbalimbali baada ya kuhukumiwa kuingia nchini Tanzania kwa njia zisizo halali.

Uamuzi huo ulifuatia safari ya Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *