The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wengine Wanaitazama Ngorongoro Kama Hifadhi, Sisi Tunaitazama Kama Nyumbani

Tunajivunia kwamba Ngorongoro ni urithi wa dunia lakini hiyo haiondoshi ukweli kwamba kwenye hilo eneo kuna wenyeji wake.

subscribe to our newsletter!

Kwenye mjadala unaoendelea kuhusu hatma ya wenyeji wa Ngorongoro, kuna mambo kadhaa ambayo ningependa na mimi, kama Mmaasai na kama mtu ninayefanyakazi kwa ukaribu sana na jamii za wafugaji, nichangie mtazamo wangu.

Hata hivyo, ningependa kuweka wazi tangu mwanzo kwamba mawazo ambayo nitakuwa nayatoa mimi ni yale yahusuyo mambo ambayo mimi nayajua, yale ambayo siyajui siwezi kuyazungumzia. Hii ni kwa sababu mimi siyo msemaji wa Ngorongoro na wala mimi siyo msemaji wa Serikali. Nitazungumzia kwa uwezo wetu sisi na kwa sehemu yetu sisi kama Asasi ya Kiraia.

Kwanza kabisa niseme tu kwamba Ngorongoro kwa mujibu wa sheria ni hifadhi ambayo ipo kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Ngorongoro ambayo ilikuwa ni sheria ambayo imeanzisha hifadhi hiyo mwaka 1959.

Lakini kabla Ngorongoro haijawa hifadhi kimsingi Ngorongoro ni nyumbani kwa wafugaji. Kwa hiyo, ilikuwa ni nyumbani kwa wafugaji kabla haijawa hifadhi na baada ya kuwa hifadhi bado imeendelea kuwa ni nyumbani kwa wafugaji wa Kimaasai, Wabarbaiki pamoja na Wahadzabe wanaoishi Ngorongoro.

Niseme tu mpaka sasa hilo eneo bado ni hifadhi na ni ardhi yenye matumizi mengi kwa mujibu wa sheria zetu za Tanzania, au kwa mujibu wa sheria yetu ambayo inaongoza hifadhi yenyewe. Kwa hiyo, niseme tu kwamba maana ya ardhi yenye matumizi mengi, ambayo ndivyo ardhi ya Ngorongoro ilivyo, ni kwamba inaruhusiwa shughuli za kibinadamu pamoja na uhifadhi kufanyika kwa pamoja.

Lakini pia niseme tu kwamba wafugaji wa Ngorongoro walikuwa na mkataba ambao wameingia na Serikali ya ukoloni ambayo bado Serikali yetu pia inawajibika. Kwa mkataba huo inatambulika kwamba haki za wenyeji ziendelee kulindwa pamoja na hifadhi na masuala ya mazingiza ya hifadhi yenyewe.

Niseme tu kwa kweli ni lazima tuwe na ulinganifu katika mitazamo kwa sababu sisi kama Mtandao wa Wafugaji Tanzania (TPCF), shirika mahiri ambalo ni la kitaaluma ambapo tunatazama mambo kwa uhalisia lakini pia katika kuchambua, tuseme tu kwamba Serikali imeendelea kufanya hivyo, imeendelea kuangalia pia haki za wenyeji, imeendelea kutunza mazingira lakini mwisho wa siku tumeendelea kushuhudia mara kwa mara uhamaji wa watu.

Idadi ya watu kuongezeka

Kwa hiyo, hii siyo mara ya kwanza kwamba Serikali imejitahidi kupunguza idadi ya watu kulingana na sababu ambazo Serikali, au hifadhi yenyewe, imeweza kuzibainisha, ikiwepo suala la wingi wa watu.

Hilo suala la kuongezeka kwa idadi ya watu ni jambo la kweli na hatuwezi kukataa kwamba siyo jambo la kweli. Wingi wa watu umeweza kuongezeka kutoka watu 8,000 hadi leo 80,000. Kwa hiyo, kimsingi hiyo ni hoja ambayo mtu yeyote ambaye ana akili, au ni mtaalamu, huwezi kusema haipo.

Lakini kimsingi katika upande mwingine kwamba Wamaasai pia hawajafanya makosa kuendelea kuongezeka au kuendelea kuzaa na kuendelea kujaa hapo kwa sababu hapo ni nyumbani kwao.

Na idadi ya watu kwa Tanzania tulipopata uhuru siyo sawa na sasa tulipo, lazima idadi ya watu ilikuwa ndogo baadae tukaongezeka. Kimsingi na hakuna mtu ambaye analaumiwa, au anaonekana kavunja sheria, kwa sababu tu ameongezeka kwa namba.

Kwa hiyo, niseme tu kwamba kimsingi Wamaasai hawana makosa kwenye hilo la kuongezeka kwa namba. Serikali ilipaswa kuweka mkakati mzuri wa kuweza kudhibiti idadi ya watu lakini siyo kwa namna yoyote ile kwa kuwahusisha Wamaasai kwamba ni kwa nini wameongezeka.

Lakini sisemi kwamba Serikali yetu inawahusisha Wamaasai kwa maana hiyo, hapana. Niseme tu kwamba hilo ni suala ambalo tu linatakiwa liendewe taratibu sana. Linatakiwa liendewe kwa njia ambayo kimsingi ni ya kidilpomasia na mwisho wa siku bila kumlaumu mtu mwingine yeyote.

Makazi yaliyotawanyika

Lakini suala lingine ni hilo la makazi yaliyotawanyika, mambo ya ujenzi holela. Hili kimsingi ni lazima tuseme kwamba hifadhi pamoja na wenyeji ndiyo waliokuwa na jukumu la kuweza kujipanga na kuweza kusema hapa ni eneo la matumizi watu wasogee kidogo wajipange kwa namna hiyo.

Lakini mwisho wa siku sasa kama hilo pia linapaswa kuendewa kwa namna ambayo haiwezi kuathiri mtu yeyote au namna nyingine yoyote.

Lakini pia suala la mifugo kuongezeka. Niseme tu kwamba kwenye hili tunaweza tukakiri kwamba huenda mifugo imeongezeka kwa sababu idadi ya watu pia imeongezeka na watu watahitaji mifugo kwa sababu ndiyo chakula.

Lakini niseme tu kwamba Serikali yetu inajukumu la kuweza kuhakikisha kwamba mifugo hiyo kama rasilimali muhimu ya wananchi na nchi pia wangeweza kuwapatia namna nzuri ya masoko na namna ya uboreshaji.

Kwa hiyo, kama wafugaji wameendelea kufuga kwa njia ya kijadi zaidi kila mtu anapaswa kulaumiwa hata Serikali, kwa maana Serikali ya eneo la hifadhi. Serikali inapaswa kulaumiwa kwa sababu, kwa nini hawajaweka mkakati wa kuwasaidia wafugaji waweze kuwa na ngo’mbe wachache wenye tija lakini mwisho wa siku ambao hawawezi kuathiri hifadhi yetu?

Niseme tu kwamba kwa hayo yote niliyokwisha kuyazungumzia kuna jambo moja muhimu ambalo linatakiwa lijulikane na watu wote. Kwamba Ngorongoro kwetu sisi Wamaasai ni nyumbani.

Ngorongoro ni nyumbani

Kwa hiyo, kama Watanzania wengine wanatazama Ngorongoro kama eneo la hifadhi na wanatazama kama eneo la dunia la urithi, sisi Wamaasai tunaitazama Ngorongoro kama ni nyumbani kwetu. Sisi hatuna kwingine, pale ndio nyumbani kwetu.

Kwa hiyo, kimsingi hiyo ndiyo hoja, unakuta kwamba mtu mwingine anatazama kama Wamaasai ni waharibifu na nini lakini mwisho wa siku hiyo Ngorongoro ni nyumbani, pale ni nyumbani kwetu.

Lakini ni ukweli pia kwamba Ngorongoro ni eneo la urithi la dunia. Tunajivunia kama Tanzania kuendelea kulihifadhi. Lakini mwisho wa siku kuna maslahi mengi kwa nyuma, kuna maslahi mengi ambayo yapo nyuma yake, ambayo siyo Serikali tu ya Tanzania na wengine wengi.

Lakini mwisho wa siku sasa maana yake nini? Maana yake ni kwamba watu wengine wanatazama Ngorongoro kama eneo la burudani la kwenda kujifurahisha na nini. Lakini sisi Wamaasai tunatazama kama nyumbani.

Joseph Parsambei ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Wafugaji Tanzania (TPCF).  Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *