The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau wa Elimu Wahoji Ukimya wa Dira ya Taifa Katika Kutambua Nafasi ya Kiswahili Kwenye Elimu.

Tuwekeze katika Kiswahili na elimu bora ili tupate wahitimu wa shule na vyuo ambao ni wadadisi na wanaoweza kuhaurisha maarifa waliyoyapata kwa manufaa yao na jamii.

subscribe to our newsletter!

Wadau mbalimbali wa elimu waliokutana Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) hii leo kujadili kuhusu lugha ya kufundishia kwenye ngazi zote za elimu, wameshauri  Dira ya Taifa ya Maendeleo kutilia mkazo matumizi ya kiswahili kama lugha ya kufundishia. Hii ni ili kuweza kuondokana na kikwazo kimojawapo kinachozuia upatikanaji wa elimu bora na yenye manufaa kwa jamii.

Mjadala huo ambao uliwakutanisha wasomi,  wanafunzi, viongozi na wananchi mbalimbali ni sehemu ya mijadala iliyoanza siku mbili zilizopita kama sehemu ya maazimisho ya kumi na tatu ya Tamasha la  Kigoda cha Mwalimu Nyerere ambalo hulenga kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na mambo yahusuyo bara la Afrika.

Mmoja wa wasilishaji mada Prof. Humphrey Moshi wa Shule kuu ya uchumi ya Chuo kikuu cha Dar es salaam amesema tangu mwaka 1962 Kiswahili kilipotangazwa kuwa lugha ya taifa, haijawahi kupewa uzito wowote katika dira za maendeleo ya taifa zilizokuwepo.

“Tunategemea kuandika Dira mpya ya taifa baada ya hii iliyopo kukamilika 2025.  Ni wakati sasa Dira mpya iseme kitu kuhusu umuhimu wa lugha ya Kiswahili katumika kufundisha katika ngazi zote za elimu” alisema Prof. Moshi akisisitiza kwamba wakati wa kuchukua maamuzi hayo ni sasa kwa kuwa lugha ya Kiswahili tayari ni lugha ya taifa hivyo hakuna sababu ya kutotumika kufundishia.

Prof. Aldin Mutembei Mkurugenzi wa Taasisi za Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es salaam amesema tunahitaji kukipa umuhimu kiswahili kwa sababu za kulinda utambulisho wetu kama Waafrika na kwa kuwa kinasadifu mazingira yetu.

“Tuwekeze katika Kiswahili, tuwekeze katika elimu bora kwa ujumla” alisema Prof. Mutembei kuwa hiyo ndio namna ya “kujenga jamii ya wahitimu wa shule na vyuo ambao ni wadadisi na wanaoweza kuhaurisha maarifa waliyoyapata shuleni kuweza kuyatumia kwenye mzingira yao”.

Naye mwanazuoni nguli wa lugha chuoni hapo, Prof. Martha Qorro katika kuchokoza mada alisema kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia haina maana kwamba Kiingereza au lugha nyingine za kigeni zitupwe.

“Tunaweza kufundisha kwa kutumia Kiswahili na Kiingereza kikabaki kufundishwa kwa ustadi kama lugha ya kigeni” alisema Prof. Qorro ambaye amekuwa mtetezi wa mapinduzi ya matumizi ya lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu kwa muda mrefu.

Akichangia mada hiyo Prof. Kitila Mkumbo ambaye ni Mbunge wa jimbo la Ubungo alikinzana na wanazuoni hao kwa kusisitiza kuwa matatizo yetu ya elimu yasifichwe kwenye kichaka cha lugha ya kufundishia bali zitazamwe changamoto kubwa nyingine. Prof. Mkumbo pia alisisitiza umuhimu wa Kiingereza kwa sasa hauepukiki duniani kama tunataka kuhusiana na dunia hasa kibiashara.

“Leo hii makampuni mbalimbali duniani yamepitisha Kiingereza kutumika kama lugha rasmi ya kampuni hizo katika kuendesha shughuli zao” alisema Mkumbo ambaye pia ni mtaalumu wa masuala ya elimu kitaaluma.

Prof. Mkumbo pia alisisitiza kuwa “tafiti na sayansi inaonesha kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa endapo tukitumia Kiswahili basi tutaongeza ufaulu wa wanafunzi wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu”

Naye Mwalimu Mabala ambaye anafahamika kwa utetezi wake wa Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia alisema wanafunzi lazima wajifunze kwa kutumia lugha ambayo wanaitumia katika mazingira yao ya kila siku ili waweze kupata maarifa.

“Matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia itawasaidia wanafunzi kuwa na tafakuri tunduizi, ubunifu na utambulisho” alisema Mwalimu Mabala huku akisisitiza “lengo la elimu tsuangalie ufaulu tu, bali kuona wanafunzi wanapata maarifa”.

Mijadala kuhusu lugha imepamba moto kwenye majukwaa mbalimbali siku za hivi karibuni kutokana na kufunguliwa kwa dirisha la kutoa maoni kuhusu marekebisho ya mitaala ya elimu pamoja na uchechemuzi unaofanywa na wadau mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia kama vile  HakiElimu.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *