Dar es Salaam. Serikali imesema leo kwamba imedhamiria kuboresha mfumo wa manunuzi pamoja na ukaguzi wa Serikali, ikiwa ni pamoja na kutoka kwenye mfumo wa kununua kulingana na bei za wazabuni waliopatikana katika mchujo wa zabuni kwenda kwenye mfumo wa kununua kulingana na bei halisi katika soko.
Akisoma bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba amesema hatua hiyo inatokana na kushindwa kwa mfumo huo ambao unajulikana kama transactional procurement kwa kitaalamu kuleta tija kwa taifa.
Kwa kawaida, ofisi za manunuzi huwaalika wazabuni mbalimbali ambao hushindanishwa kwa kuangalia bei na pamoja na sifa zingine kama uwezo wa kiutendaji, uwezo wa kifedha pamoja na uzoefu.
Mzabuni anayeshinda katika mchujo mara nyingi hupewa zabuni. Hata hivyo, mfumo huu wa manunuzi umekuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa, hususan katika kuweka bei zisizo na uhalisia, kitu ambacho Serikali imedhamiria kukishughulikia.
“Mara nyingi bei hizi za ununuzi zimekuwa kubwa kuliko zile zilizoko sokoni kwa ujumla na hata rejareja,” Dk Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (Chama cha Mapinduzi – CCM). “Ingekuwa tunanunua kwa ajili ya nyumbani kwetu, au kwa ajili ya makampuni, bei hizo tusingezikubali.”
Dk Nchemba alipendekeza kwa wabunge uwepo ununuzi wa umma wa kimkakati, akimaanisha ule ununuzi unaozingatia ukubwa wa ununuzi wa Serikali na sekta ya umma kwa ujumla.
Hatua hiyo ya Serikali imefuatiwa na uwepo wa tuhuma kadhaa ziliibuliwa na wabunge na kuungwa mkono na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa juu ya uzidishaji wa bei uliofanywa na Bohari ya Dawa, ambapo bei zilizidishwa kwa wastani wa mara nne mpaka tano wa bei halisi ya soko.
Mabadiliko yatakavyofanyika
Dk Nchemba alisema ili kufanikisha mabadiliko haya Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, itaweka utaratibu wa kuweka orodha za bidhaa na huduma katika mfumo wa manunuzi ya umma, TANEPS, ambapo ofisi za umma hazitaruhusiwa kuvuka bei hizo katika ununuzi.
“Tutaendelea kuboresha mfumo wa kielektroniki wa umma, yaani TANEPS, ikiwemo kuweka ukomo wa bei za bidhaa na huduma zinazotumika serikalini ili kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali,” alisema Nchemba. “Wizara ya Fedha na Mipango itahakikisha kuwa bei zote za bidhaa na huduma zinazotumika sokoni kwa ujumla na rejareja zinakuwa na price catalogue zinaingizwa kwenye mfumo wa TANEPS na kuwa na kikomo cha bei kitakachotumika serikalini.”
Dk Nchemba alisema kwamba wafanyabiashara wamekuwa wakila njama katika miradi mikubwa ya Serikali, ambapo taratibu zinaonekana kufuatwa lakini fedha za umma hutumika bila kujali uhalisia wa thamani.
Dk Nchemba alisema pia licha ya taratibu zote kufuatwa katika ununuzi, na sheria za ununuzi kufuatwa, na hatua zote za ukaguzi kufutwa, fedha imekuwa ikiibiwa.
Kwa mujibu wake, hali hii inatokana na baadhi ya watumishi wa umma kutokuwa waaminifu ambao hupanga njama na wafanyabiashara wasio wazalendo kupandisha bei za bidhaa kwenye zabuni na kujipangia, kitu ambacho kinafanya hata huyo aliyeshindania kwa kiwango cha chini anakuwa bado yuko mbali na bei ya soko au gharama halisi.
Sheria za Tanzania zinatakataza ulaji njama kwenye manunuzi ya umma. Hata hivyo, vitendo hivyo hufanyika katika mazingira ya usiri mno ambapo wafanyabiashara hukubaliana, au mfanyabaishara mmoja kuwa na makampuni feki mengi yanayoingia katika zabuni kama makampuni ya kawaida. Katika nyakati nyingine, ni ushirika wa moja kwa moja kati ya watumishi wa umma na wafanyabiashara.
“Kwenye mchezo wa aina hii wanafuata sheria zote za ununuzi,” Dk Nchemba alieleza. “[Watu hawa] wanafuata taratibu zote za kumchagua aliyeshindana kwa bei ya chini. Ila kwa kuwa hiyo iliyoshindaniwa kuwa bei ya chini ni ya chini tu ukilinganisha na wale wengine walioshindana kwenye zabuni, hiyo inakuwa wamefanya njama, basi bei hizo zinakuwa juu ukilinganisha na bei za bidhaa hizo katika soko. Hawa ni watu wanaoiba japo wamezingatia sheria. Ni watu wanaoiba kwa mujibu wa sheria.”
Katika kupambana na wizi huu wa kisheria, Dk Nchemba amesema Serikali inakusudia kujenga uwezo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kwa kumpa uwanda wa kuajiri watumishi wa kutosha. Lakini pia serikali inakusudia kuzipa nguvu vitengo vya ukaguzi wa ndani katika kufanya ukaguzi wa kitaalamu (technical audit), na ukaguzi wa papo kwa papo wakati mradi ukiendelea, yaani real time audit na kaguzi za mifumo.
Hili litafanyika kwa kuongeza bajeti ya CAG pamoja na kumpa mkaguzi wa ndani mkuu wa serikali fungu lake peke yake.
Serikali pia inakusudia kuimarisha ukaguzi wa ndani kwa kuongeza wigo wa wakaguzi wenye fani mbalimbali tofauti na sasa ambapo wengi ni wabobezi katika uhasibu tu.
Pia, Serikali imepanga kuweka wigo wa kuruhusu kamati ya ukaguzi kuwa na wajumbe wa ziada watatu. Serikali pia imekusudia kufanya marekebisho ya sheria ya manunuzi ya umma katika kuziba mianya inayoruhusu upotevu wa fedha za Serikali na kuweka mkazo kwenye thamani ya fedha.
Sehemu kubwa ya mabadiliko ambayo Serikali imeyataja yamekuwa ni sehemu ya mapendekezo yaliyokuwa yakiibuliwa mara kwa mara na wadau wa uwajibikaji, akiwemo CAG, hali inayoashiria uimarikaji wa sekta ya manunuzi ya umma katika nyakati zijazo.