The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ushirikishwaji Unahitajika Kupunguza Mivutano Ngorongoro

Tumeona kwenye wanaodaiwa kuwa ni viongozi wa wananchi wa Ngorongoro wapo watu walitambulishwa kama wanatokea Ngorongoro lakini tunajua fika siyo watu wa Ngorongoro.

subscribe to our newsletter!

Wakazi wa tarafa ya Ngorongoro, ambao leo hii tunasikia kuna mpango wa kuwahamisha baadhi yao, mwaka 1959 walihamishwa kutoka maeneo ya Serengeti na walisainishwa mikataba kwamba hawatasumbuliwa tena baada ya kuhamishiwa kwenye eneo walilopo hivi sasa la Ngorongoro. Kwa hiyo, hawa watu waliungana na wale wenzao ambao walikuwa wanaishi hilo eneo kwa karne na karne.

Kuna kipindi wakaambiwa kwenye eneo la kreta, ambayo ipo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, hawatakiwi kuwepo na walikubali, wakapisha. Changamamoto nyingi zimekuwa zikiwakumba hawa Watanzania wenzetu wanaoishi ndani ya hii hifadhi lakini hawakukata tamaa nao wamekuwa wakipambania haki zao.

Kuna kipindi wenzao wa eneo la Loliondo walipeleka mashitaka mpaka Mahakama ya Afrika Mashariki na wakashinda kesi, kwamba hawapaswi kunyang’anywa hilo eneo. Kwa hiyo, hivi sasa tunaona hatari ya haya maeneo ya jamii za wafugaji wa asili yanakwenda kuchukuliwa. Kwa mfano, huko huko  Loliondo ambayo kuna kilometa za mraba zaidi ya 1,500 ambazo zinategemewa sana na Wananchi wa wilaya ya Ngorongoro kwa ajili ya ufugaji, zimemegwa.

Sasa tujiulize kati ya hawa Watanzania wenzetu ambao wanaishi eneo hilo kwa muda mrefu ambao hata nyumba zao zinafanana na uhifadhi na hayo mahoteli makubwa yaliyojengwa humo ndani ya hifadhi kipi unadhani kinatakiwa kuondolewa? Kwa mtazamo wangu, mahoteli ndio yanapaswa kwanza kuondolewa.

Haki ya jamii

Mpango wa kuwaondoa wakazi wa Ngorongoro wanaokadiriwa kuwa ni takribani zaidi ya 90,000 unakwenda kuvuruga mpangilio wa jamii yenyewe. Ni muhimu kufahamu kwamba sehemu ya Ngorongoro ni sehemu pekee ambayo inachukuliwa utaupata Umaasai wenyewe hata baada ya miaka 100 ijayo. Kwa sababu hivi sasa jamii imetawanyika na muingiliano ulivyo baadhi ya tamaduni zinakwenda kupotea kitu ambacho siyo kibaya kwa sababu wapo wanaotawanyika kwa maamuzi yao.

Lakini hawa wa Ngorongoro kwa sehemu kubwa wameweza kuhifadhi, sasa sina imani kama utawaondoa wale wana Ngorongoro ukawapeleka Tanga utaweza kuwapanga kama ni ukoo mmoja basi wakae sehemu moja, kama ni watu wa kata moja basi wakae kata moja. Sidhani kama kuna huo uwezekano. Bila shaka kabisa haiwezekeni, tutavuruga mpangilio wa hii jamii.

Ukiangalia mwenendo wa suala hili zima, unaweza kujiuliza kwa nini jambo hili limepewa nguvu kubwa hivi? Na jambo limechukuliwa kwa uharaka ni kwa nini? Hii inazua wasiwasi mkubwa.

Msukumo uliopo unatia wasiwasi ndio maana mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 kule bungeni mmoja ya wabunge, ndugu Ole Sendeka alisimama na kusema kwamba  kama hili suala mtaamua nitasimama na wananchi wa Ngorongoro kwa sababu ukiangalia majibu ya Serikali  ni kama walishafikia hitimisho.

Na kama wamefikia hitimisho unajiuliza msukumo uliopelekea kufikia hitimisho hilo unatoka wapi? Ni wananchi wenyewe wa Ngorongoro au ni nani huyo?

Kukosekana kwa ushirikishwaji

Kama kweli lengo ni uhifadhi kwa nini ile jamii isishirikishwe kwa ukaribu? Kwa nini sasa kinachofanyika ni ushawishi badala ya kukaa na hao wananchi kwa pamoja kujadiliana namna ya uhifadhi?

Tumeona hata mikutano iliyoitishwa Arusha mjini na wanaodaiwa kuwa ni viongozi wa wananchi wa Ngorongoro wapo watu walitambulishwa kama wanatokea Ngorongoro lakini tunajua fikra siyo watu wa Ngorongoro, ni viongozi wa mila wa Kimaasai wa maeneo yao lakini siyo wa Ngorongoro.

Wakati huo huo kuna kiongozi mwingine akajitambulisha ni kiongozi wa jumla wa Wamaasai, hakuna kiongozi wa namna hiyo kwenye jamii za Wamaasai. Wamaasai wana viongozi wa rika na maeneo lakini hakujawahi kuwa na kiongozi wa jumla.

Sasa unajiuliza hizi hadaa zote lengo lake ni nini? Sasa unapomchukua mtu anayeishi kilomita mia mbili kutoka Ngorongoro kwenda kuwasemea wananchi wa Ngorongoro huo ni uongo. Sasa hii mikanganyiko inazua maswali mengi badala ya majibu.

Kama kweli jambo lina lengo zuri ukishirikisha jamii, jamii itaona na italipokea. Hakuna anayebisha kwamba idadi ya watu inaongezeka, hilo halipingiki. Tunachosisitiza ni kuweka mikakati inayoshirikisha jamii katika kukabiliana na hizo athari zinazoweza kujitokeza kutokana na ongezeko la watu.

Sasa huwezi kuja na suluhisho la kuwaondoa wananchi halafu wawekezaji unawaacha. Kwa mfano, humo ndani ya hifadhi kuna mahoteli yamejengwa. Mbona hatusikii kama nayo yataondolewa? Kwa hiyo, hili ni suala tunalopaswa kuliangalia kwa upana huu.

Uhai kwa Wanangorongoro

Ni haki ya Wanangorongoro, kama Watanzania wengine, kubaki kwenye ardhi yao, hasa ni asili yao wamekuwa wakiishi hapo kwa miaka na miaka. Kama alivyosema mbunge wa Simanjiro Ole Sendeka kuwa hata kama wataondolewa kwa nguvu bado itabaki pale pale kuwa wamedhulumiwa haki yao.

Ardhi yao wanaitegemea kwa ajili ya maisha yao na ufugaji ambayo ndiyo shughuli kuu ya uchumi.

Ni vyema mamlaka ziheshimu haki za hao wakazi na kuwasikiliza pasipo kutanguliza mitazamo hasi dhidi yao. Ni wakati muhimu sana kwa wananchi na jumuiya za kiraia kushikamana na Wanangorongoro kuhakikisha nao wanasikilizwa ili waweze kupata haki zao.

Wananchi wa Ngorongoro wasiachwe peke yao!

Eliud Letunga ni Eliud Letunga ni Mshauri wa masuala ya wakulima na wafugaji  anapatikana kupitia baruapepe ellyletungaa@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *