Dar es Salaam. Balozi wa Ufaransa nchini Nabil Hajlaoui amesema leo Jumatano, Juni 23, 2022, kwamba Serikali yake iko tayari kuishirikisha Serikali ya Tanzania namna bora zinazotumiwa na taifa hilo la Ulaya katika masuala ya uhifadhi wakati ambao Tanzania inatawala vichwa vya habari kuhusiana na zoezi lake linaloendelea huko Ngorongoro.
Hajlaoui alikuwa akichangia kwenye mjadala ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Watch Tanzania kupitia mtandao wa Zoom uliokutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo Serikali, NGOs na wasomi kujadili zoezi linaloendelea hivi sasa la kuwahamisha wenyeji wa Ngorongoro kwenda Handeni, Tanga.
Serikali inasema inalazimika kuendesha zoezi hilo kulinda uhifadhi wa urithi huo wa dunia, ikidai kwamba shughuli za kibinadamu hifadhini humo, kama vile ufugaji, zinahatarisha urithi huo wa dunia kutoweka. Uamuzi huo, hata hivyo, umekosolewa vikali na wenyeji wa Ngorongoro na wanaharakati wengine, wakisema unakiuka haki za msingi za binadamu.
Wakati wa mjadala huo wa Jumatano ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Maliasili na Utalii Pindi Chana na mwenzake wa TAMISEMI Innocent Bashungwa, Balozi Hajlaoui alitegemewa kutoa uzoefu wa Ufaransa kama taifa linaloongoza kwa kuvutia watalii duniani juu ya namna inavyokabiliana na suala zima la uhifadhi.
Katika mchango wake, Hajlaoui alisema utaratibu wa uhifadhi ambao Ufaransa umekuwa ukiutumia na kuwa na manufaa makubwa kwa taifa hilo ni ule utaratibu jumuishi ambapo wenyeji na mamlaka za Serikali hushirikiana katika kuhakikisha maliasili zinahifadhiwa na manufaa kwenda kwa wenyeji na Serikali kwa pamoja.
“Wazo ni kutengeneza mashirika ya wenyeji, ambayo bila shaka yatakuwa ni ya umma, ambayo yatakuwa na kazi ya kuendesha hizi hifadhi, katika hali ambayo inazingatia maslahi ya pande zote – maslahi ya ekolojia na uhifadhi; maslahi ya watu wanaoishi kwenye maeneo hayo; na kampuni ambazo zinaweza kuwa na maslahi na maeneo haya,” alisema Balozi Hajlaoui.
“Njia jumuishi ya kuendesha maeneo haya inalenga kuyahifadhi haya maeneo lakini pia kuyafanya haya maeneo kuwa endelevu na yenye manufaa na kuleta manufaa zaidi kwenye haya maeneo,” aliongeza Hajlaoui.
Mwanadiplomasia huyo aliongeza kwa kuwashirikisha washiriki wa mjadala huo kwamba baada ya miaka 60 ya kutekeleza utaratibu huu, hifadhi hizo zimekuwa zinavutia zaidi kwa aina za uwekezaji ambazo zinaheshimu mazingira, zinaheshimu wenyeji wanaoishi kwenye maeneo haya na pia kuleta kipato zaidi kwenye maeneo haya.
“Kwenye utaratibu huu tunaoutumia sisi Ufaransa, kila mdau anakuwa anafaidika,” aliongeza Hajlaoui. “Kwanza, tunahifadhi mazingira kwenye haya maeneo. Pia, tunaongeza utajiri zaidi kwa wenyeji wa haya maeneo. Lakini pia kwa Serikali na mashirika binafsi yanayofanya kazi kwenye maeneo haya.”
Hajlaoui aliongeza kwa kubainisha kwamba kwa uzoefu wao nchini Ufransa, kitu cha muhimu ni kujikita kwenye thamani ya ziada ambayo mamlaka za Serikali zinaweza kuongeza kwenye haya maeneo ya uhifadhi. Kwa mfano, aliongeza, Ufaransa hairuhusu aina ya utalii ambayo inaweza kupelekea uharibifu wa maeneo haya.
“Hivi ndivyo tunavyofanya sisi nchini Ufaransa,” alidokeza Hajlaoui. “Na bila ya shaka tuko tayari kugawa uzoefu wetu huu na marafiki zetu nchini Tanzania.”
Ushauri huu unalingana kwa kiasi fulani na mapendekezo yaliyotolewa na chama cha ACT-Wazalendo kwenye mapendekezo yake ya namna Serikali inavyoweza kushughulika na suala la Ngorongoro.
ACT-Wazalendo imependekeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ivunjwe na badala yake iundwe kampuni yenye kumilikiwa kwa ubia kati ya wananchi waishio ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na Serikali.
Chama hicho kinataka wananchi wamiliki asilimia 51 kwenye kampuni hiyo na Serikali imiliki asilimia 49, huku uendeshaji wa kampuni hii ubaki mikononi mwa Serikali.
Mapendekezo haya, hata hivyo, yanaonekana kutokuwavutia wafanya maamuzi. Akiongea wakati wa mjadala huo, kwa mfano, Waziri Pindi Chana alisema wizara yake imeanza mchakato wa kupitia upya sheria inayosimamia hifadhi ya Ngorongoro ili kukomesha matumizi mseto ya ardhi hiyo.
“Tunaanza kupitia hiyo sheria ya NCA na kuifanyia marekebisho kwa sababu haiwezekani leo 2022 tukasema tuache tu watu waishi na wanyama,” alisema Dk Chana. “Tukiacha wananchi wakiishi na wanyama miaka 10 baadae itakuwaje, miaka 20 baadae itakuwaje? Haya ni maswali ya msingi ambayo lazima tujiulize.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.