The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?

Wadau wengi wanaamini jamii itakuwa na ustawi mzuri zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

subscribe to our newsletter!

Arusha. Nini jamii inaweza kutegemea kutokea pale wanawake wengi wanapopata fursa ya kuwa kwenye nafasi za maamuzi, hususan yale ya kisiasa?

Hili ndiyo swali ambalo washiriki wengi walikuwa wakijaribu kujibu kwenye kongamano la hivi karibuni lililowakutanisha wabunge kutoka Afrika Mashariki kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wao kuhusiana na nafasi ya mwanamke kwenye siasa.

Kongamano hilo la siku tatu – Juni 15 mpaka Juni 17 – liliandaliwa na Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia na Usaidizi wa Uchaguzi (IDEA) lilifanyika jijini hapa na kuhudhuriwa na wabunge wa kiume na kike, maspika wa bunge, wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika (AU) pamoja na wageni wengine wengi.

Likifanyika chini ya dhima iliyopewa jina la Kukuza Sauti na Chaguo: Wanawake Wanaongoza Afrika, kongamano hilo lililenga kutathmini nafasi ya mwanamke wa Kiafrika kwenye nafasi za maamuzi, kwa lengo la kushajihisha wanawake wengi zaidi wanafikia ngazi hizo.

Akiongea wakati wa kongamano hilo, Mbunge wa Viti Maalum (Chama cha Mapinduzi – CCM) Anastazia Wambura alisema kwamba ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za maamuzi ni muhimu kwani hilo litaifanya demokrasia kuwa jumuishi.

“Ni lazima tuhakikishe kwamba wanawake, kutoka nyanja mbalimbali za kijamii, wanakuwa na fursa sawa zinazoweza kuwaingiza kwenye nafasi za kisiasa pamoja na nafasi zingine za ushawishi,” alisema Wambura. “Hilo inabidi lifanyike kama kweli tumedhamiria kutengeneza demokrasia ambayo ni jumuishi.”

Spika wa EALA Martin Ngoga, akizungumza kwenye kongamano hilo, alisema kwamba ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za maamuzi ni muhimu kwani huiwezesha jamii kunufaika na vipaji na uwezo ambao wanawake wanao.

“Ushiriki wa wanawake kwenye siasa ni muhimu kwani huchochea haki, usawa, demokrasia na maendeleo endelevu,” alisema Ngoga. “Wanawake wanapokuwa kwenye nafasi za maamuzi hufanya chaguzi ambazo husaidia ustawi wa jamii zao na usawa kwenye kufikia na kuwa na udhibiti wa fursa mbalimbali.”

Ngoga alitoa uzoefu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi baada ya jumuiya hiyo kuanzisha sheria yenye kutia maanani mahitaji ya kijinsia.

Ushiriki wa wanawake kwenye EALA umeongezeka zaidi ya kile kiwango kilichokuwa kimewekwa.

Wakati wa Bunge la kwanza, ambalo lilianza 2001 mpaka 2006, kulikuwa na wanawake tisa kati ya wabunge 27 wa kuchaguliwa, sawa na asilimia 30. Bunge la sasa, ambalo ni la nne, lina wanawake 22 kati ya wabunge 54 wa kuchaguliwa, sawa na asilima 40.7.

Akiongea wakati wa kongamano hilo, Dk Roba Sharamo, ambaye ni Mkurugenzi wa IDEA kwa Kanda ya Afrika na Asia Magharibi alisema kwamba hakuwezi kuwa na demokrasia ya kweli wala chaguzi za huru na haki kama hakutakuwa na ushiriki kamili wa wanawake kwenye michakato hiyo.

“[Wanawake] tuna uwakilishi wa asilimia 25 tu kwenye ngazi zote za mabunge barani Afrika – ya juu na chini – na hiyo siyo takwimu nzuri,” alisema Dk Sharamo, akitaka jitihada zaidi kufanyika kubadili hali hiyo.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts