The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Matarajio ya Serikali Kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Kusimamia Usafirishaji Mifugo

Moja kati ya faida za mfumo huo ni kuondokana na madalali na kuirahisishia Serikali kukusanya mapato.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza rasmi matumizi ya mfumo maalum wa kieletroniki wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi uitwao Mifugo Integrated Management Information System (MIMIS).

Mfumo huo wa kieletroniki utatumika kote nchini na taasisi zote za sekta ya mifugo zilizo chini ya wizara kwenye minada pamoja na vituo vilivyo chini ya mikoa na halmashauri ambapo utawezesha kutoa vibali vya kusafirishia mifugo na mazao yake vikiwemo vyakula vya mifugo.

Akizungumza na The Chanzo kwa njia ya simu, Joseph Nkwabi ambaye ni afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi alisema mfumo huo umeanza kutumika rasmi Julai 1, 2022, na utasaidia kutoa huduma kwa watumiaji wa sekta ya mifugo kwa njia ya mtandao ili kuepusha usumbufu wa kwenda ofisini kwa ajili ya kuomba vibali.

“Mfumo huu si tu kwa ajili ya wizara bali ni pamoja na sekta zake, taasisi zake kwa maana ya Bodi ya Nyama hata wale wenye mabucha watakuwa sasa hivi wanajisajili mtandaoni,” alieleza Nkwabi. “Pia, na wale Bodi ya Maziwa nao pia wapo kwenye huu mfumo. Tunatoka analojia tunakwenda digitali. Kwa hiyo, sasa hivi hatutumii karatasi tena.”

Kabla ya kuanza kutumia mfumo huo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na Taasisi ya Trade Mark Afrika (TMEA) iliendesha zoezi la utoaji wa mafunzo juu ya mfumo huo, kwa mujibu wa maelezo ya Nkwabi.

Anasema Serikali ilitoa mafunzo kwa wadau karibu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na watalaam wa wizarani, mikoani na sehemu mbalimbali.

Nkwabi pia alieleza kwamba tangu kuanza kwa mfumo huo Julai 1 hadi Julai 4, 2022, asubuhi alipoongea na The Chanzo, maombi yalikuwa yamefikia 70 ya wanaotaka vibali na kufanya usajili wa biashara za mifugo na mazao yake.

“Wadau watakuwa wanatumia ‘Control Number’ huko huko moja kwa moja kutoka [Mfumo wa Malipo wa Serikali] GePG, anatuma ‘Control Number’ halafu wanalipa huko huko,” alieleza Nkwabi.

“Mfumo una activate moja kwa moja. Baada ya hapo wakuu wanaohusika na upigaji wa saini wanafanya kupitia mtandaoni. Baada ya hapo vibali vinatoka vikiwa na saini kutoka wizarani. Kwa hiyo, yeye anapakua kule anaanza kutumia kwaajili ya kufanyia biashara,” aliongeza.

Serikali inategemea mfumu huo utapunguza muda wa kufika ofisini kufuatilia vibali na hivyo kuondoa urasimu kwa kuwarahisishia wafanyabiashara kuomba vibali wakiwa nje ya nchi ili waweze kuingiza mifugo yao ndani ya nchi.

Pia, mfumo huo unategemewa kurahisisha zoezi la ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

“Hakutakuwa na mtu wa katikati anayehusika katika ukusanyaji wa fedha,” anaeleza Nkwabi. “Kwa hiyo, mapato yataenda moja kwa moja kwa Serikali. Matarajio yetu ni makubwa kwenye hilo suala.”

Nkwabi anahimiza kuwa ni muhimu wafanyabiashara wakatumia mfumo huo ambao amekiri kuwa ni rafiki.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Anapatikana kupitia jackline@thechanzo.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupitia @JacklineVictor5.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *