Dar es Salaam. Watu mbalimbali wameendelea kukimwagia sifa kedekede Kiswahili katika siku ambayo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya lugha hiyo inayokua kwa kasi ulimwenguni na inayotegemewa kuliunganisha bara la Afrika na watu wake kwa maendeleo na ustawi zaidi.
Mnamo Novemba 5, 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliitengaza Julai 7 ya kila mwaka kama Siku ya Kimataifa ya Kiswahili kwa lengo la kuchagiza juhudi za kukikuza na kukieneza ulimwenguni kote.
Kwenye uamuzi wake huo, UNESCO ilisukumwa na ukweli kadhaa kuhusu lugha ya Kiswahili, kama vile Kiswahili kuwa lugha mama kwenye nchi nyingi za Afrika ya Mashariki, Kati na Kusini. Kiswahili pia kinafundishwa kwenye vyuo vikuu kadhaa ulimwenguni.
Kiswahili ni moja kati ya lugha 10 zinazozungumzwa zaidi ulimwenguni, ikiwa na wazungumzaji wanaokisiwa kufikia milioni 200, kwa mujibu wa UNESCO. Kiswahili pia ni moja kati ya lugha rasmi zinazotumika katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwenye miaka 1950, Umoja wa Mataifa (UN) ulianzisha kitengo cha lugha ya Kiswahili kwenye Radio ya Umoja wa Mataifa na leo hii Kiswahili ni lugha pekee ya Kiafrika inayotumika katika Kurugenzi ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa.
Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, akizungumza kwenye taarifa ya video, alisema kwamba ana uhakika kwamba Kiswahili ni lugha yenye uwezo wa kuvuka mipaka, akitolea mfano namna lugha hiyo inavyozungumzwa kwenye ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
“Lugha hiyo [ya Kiswahili] imeonesha kwamba Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuja pamoja na lengo moja,” alisema Rais Ndayishimiye. “Mahusiano ya kimataifa, utamaduni, utalii, muziki na burudani vimesafirisha Kiswahili kote ulimwenguni. Ni vizuri kuzungumza lugha moja kwa sababu tunapozungumza tunakuwa kitu kimoja.”
Naye Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amekielezea Kiswahili kama kielelezo cha pekee cha desturi na utamaduni wa Waafrika, pamoja na ustaarabu na fikra zao.
“Kiswahili kinarahisisha na kutuwezesha kupata habari, mawazo mapya, elimu na maarifa na pia kumiliki sayansi na teknolojia,” alisema Nyusi kwenye taarifa yake. “Kiswahili kinatumika na kusikika katika mataifa mengi, ikiwemo nchi yangu ya Msumbiji.”
Angalau matukio mawili makubwa yamesindikiza siku hii mwaka huu. Moja ni lile la Serikali nchini Uganda kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya shughuli zake nchini humo, na kufanya ufundishaji wake kuwa wa lazima katika ngazi ya shule za msingi na sekondari.
Kiingereza kimekuwa lugha pekee rasmi nchini Uganda tangu mwaka 1962. Kiswahili kilipendekezwa kuwa lugha rasmi nchini humo mwaka 2005 lakini kikaishia kufundishwa kama somo la hiari katika shule za sekondari kuanzia mwaka 2007.
Tukio jingine kubwa ni lile la Serikali ya Tanzania na ile ya Afrika Kusini kuingia makubaliano yatakayowezesha walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania kwenda kufundisha lugha hiyo nchini Afrika Kusini.
Mkataba huo uliingiwa kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini Angelina Motshekga mapema wiki hii.
Taifa la Afrika Kusini lilianza mchakato wa kukiingiza Kiswahili kwenye mfumo wake wa elimu tangu mwana 2018 lakini utekelezaji wake ulikwamishwa na kile Motshekga amekielezea kama janga la UVIKO-19 lililoikumba dunia miaka mitatu iliyopita.