The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

MOI Yapokea Wastani wa Majeruhi Sita wa Ajali za Bodaboda kwa Siku

Lakini abiria wanasema wataendelea kutumia usafiri huo, wakisema ajali ni jambo la kawaida na inaweza kutokea popote.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wito umetolewa kwa madereva na abiria wa usafiri wa pikipiki, maarufu kama bodoboda, kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokana na usafiri huo unaoendelea kushika kasi barani Afrika.

Wito huo umetolewa huku taarifa kutoka Taasisi ya Tiba za Mifupa ya Muhimbili (MOI) zikionesha kwamba taasisi hiyo hupokea wastani wa majeruhi sita wa ajali za bodoboda kila siku, huku majeruhi wa bodoboda wakitajwa kuwa wengi zaidi ya wale wa ajali zingine kama vile za magari.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Hamad Masauni pia aliliambia Bunge hivi karibuni kwamba katika kipindi cha kati ya Julai 2021 hadi Machi 2022, Tanzania kulikuwa na jumla ya matukio 1,594 ya ajali za barabarani ambapo ajali 300 zilisababishwa na madereva wa bodaboda.

Dk Bryson Mcharo ni daktari bingwa wa mifupa na viungo kutoka MOI ambaye ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba tatizo la ajali za bodaboda limekuwa likiongezeka Tanzania tangu usafiri huo uanze kuingia nchini kwenye miaka ya 2009.

“Kuna siku unapata wagonjwa watano kuna siku kumi, kwa hiyo wastani ya wagonjwa ni watano mpaka sita kwa siku wa bodaboda,” Dk Mcharo alieleza kwenye mahojiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake. “Tukilinganisha majeruhi tunaowapata wa bodaboda na majeruhi tunaowapata wa ajali zingine, inaonekana bado wa pikipiki ni wengi kuliko wale wa magari na vitu kama hivyo.”

Dk Mcharo alitolea mfano wa mwaka 2015 ambapo anasema MOI ilikuwa na wagonjwa 3,692 ambao ni kutoka kwenye ajali za bodoboda huku majeruhi wa ajali za magari wakiwa ni 1,062 tu.

“Na mwaka 2021, ambao ni mwaka jana, kulikuwa na wagonjwa takribani 5,400 wa bodaboda,” aliongeza Dk Mcharo. “Lakini ambao ni wa magari walikuwa ni nusu ya hao, takribani 2,300. Kwa hiyo, ajali za pikipiki ni changamoto.”

Kwa mujibu wa maelezo ya Dk Mcharo, wanaume walio na umri wa kufanya shughuli za uzalishaji, ikiwa ni miaka kati ya 20 na 40, ndiyo wahanga wakubwa wa ajali huku madereva wakiongoza kwa idadi ya majeruhi wakifuatiwa na abiria kisha watembea kwa miguu.

Ukiukwaji wa sheria za barabarani

Wakati wa hotuba yake bungeni, Masauni alihusanisha ajali hizi na kushindwa kwa madereva wa bodoboda kufuata sheria za usalama wa barabarani kwa ukamilifu, akisema hali hiyo ni lazima ibadilike kama Tanzania inakusudia kuwa na idadi chache ya majeruhi wa bodoboda.

The Chanzo ilimuuliza Faustina Ndunguru, ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu kuhusu tathmini ya ajali za bodaboda ambapo alibainisha kwamba ni kweli ajali za bodaboda ni nyingi, akisema hiyo inasababishwa na kushindwa kufuata matakwa ya sheria za usalama wa barabarani.

“Na limekuwa ni tatizo kwa sababu wengi sasa wanaingia kwenye biashara hii ya usafirishaji bila kupata mafunzo, haswa yanayohusiana na matumizi sahihi na salama ya barabara, kitu ambacho kinapelekea sasa wapanda pikipiki wengi kusababisha ajali za barabarani,” alisema Ndunguru aliyehojiwa na The Chanzo katika maadhimisho ya Sabasaba yanayoendelea hivi sasa.

“Sisi kama Jeshi la Polisi tunachukua hatua kuweza kupambana na hizi ajali za barabarani na hasa za wapanda pikipiki,” aliongeza. “Kwanza kabisa, hatua tunayoichukua ni utoaji wa elimu ya usalama barabarani, tunatoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi yote yanayotumia barabara.”

Madereva, abiria watia neno

Madereva wengi wanaojihusisha na biashara ya bodaboda wamekiri pia ajali zinazotokana na usafiri huo zimeongezeka, huku wakiihusanisha hali hiyo na sababu mbalimbali.

Hizi ni pamoja na madereva wengi kuendesha kwa mwendokasi; kutovaa kofia ngumu za kichwani; kupishana maeneo yasiyokuwa sahihi; kufuata matakwa ya abiria wanaodai mwendo wa haraka kwa ajili ya kuwahi; pamoja na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika hivyo kupelekea akili kuchoka.

“Unatakiwa uzingatie sheria za barabarani kwanza uwe umekamilika, uwe na kofia, angalau na viatu, hata kama ukipata ajali angalau kama una viatu, una kofia, inaweza ikakuzuia kidogo,” anasema Omary Sadick ambaye ni dereva wa bodaboda kutoka katika kituo kilichopo Msasani kona ya Zantel. “Wengi hawana hivi vitu.”

Abdi Ali, dereva wa bodaboda ambaye hajawahi kukumbana na ajali katika ufanyaji wake wa kazi, anasema: “Ni kufuata sheria na kwenda mwendo ambao siyo wa kasi zaidi wa kuhatarisha maisha. Kwa sababu ukiwa mwendokasi hata ikitokea kama mwenzako akikuchomekea huwezi kutatua tatizo. Lazima utasababisha tu ajali.”

Licha ya kuwepo kwa changamoto hizi, Zaitun Rajab, mama lishe ambaye usafiri wake mkuu ni bodaboda, anasema bado ataendelea kutumia usafiri huo, akisema anauamini usalama wake.

Hii ni licha ya ukweli kwamba  ameshawahi kukumbana na ajali akiwa amepanda bodaboda, tukio analosema ni changamoto zinazotokana na baadhi tu ya madereva wasiojali sheria za usalama wa barabarani.

Zaitun pia anasema kwamba ataendelea kutumia usafiri huo huku suala la ajali kwake likiwa ni la kawaida kama kwenye usafiri mwingine.

“Mimi nimeshawahi kukutana na ajali ya bodaboda lakini siwezi kuukwepa huo usafiri na kusema sitaweza kupanda bodaboda,” Zaitun aliiambia The Chanzo wakati wa mahojiano naye.

“Hii ni kwa sababu ukipata ajali ni ajali kama ajali nyingine,” anaongeza. “Unaweza ukapanda bajaji, ukapata ajali. Unaweza ukapanda daladala, ukapata ajali. Kwa hiyo, hizo ni changamoto za kawaida.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *