Dar es Salaam. Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar Simai Mohammed Said amejitokeza hadharani kufafanua madai ya ubadhirifu yaliyoibuliwa na chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kuhusiana na zoezi la Serikali kuzitoa baadhi ya nyumba za Mji Mkongwe kwa wawekezaji.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo Ismail Jussa aliwaambia waandishi wa habari visiwani Zanzibar hapo Julai 8, 2022, kwamba Serikali ya Rais Hussein Mwinyi ni lazima ijitokeze kujibu maswali muhimu kuhusiana na zoezi hilo alilodai limegubikwa na “kukosekana [kwa] uwazi, maamuzi ya ubabaishaji na kukosekana uadilifu.”
Jussa, ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya uongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, chama mshirika wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) huko Zanzibar, aliitaka Serikali kwanza kueleza ni watu wangapi waliomba kununua nyumba hizo na bei iliyotolewa na kila mmoja?
Pili, vigezo vilivyotumika katika kuwabariki waliouziwa nyumba hizo? Tatu, kiasi cha fedha kilichopatikana? Nne, maslahi ya umma yamezingatiwa?
Akiongea na waandishi wa habari visiwani Zanzibar hapo Julai 11, 2022, Said alisema kwamba utaratibu uliotumika ni kuwataka wawekezaji ambao wangependa kununua nyumba hizo kujaza fomu ya uwekezaji na kulipa fedha za utangulizi (upfront payment) ndani ya mwezi mmoja baada ya kukubaliwa maombi yake.
Kigezo kingine ni mwekezaji kuwasilisha ramani za asili na za mapendekezo (existing and proposed drawing) kwa ajili ya kupasishwa na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, baada ya hapo hupewa vibali vya ujenzi, ambavyo hutolewa baada ya kuhakikisha kuwa michoro husika inaendana na miongozo ya uhifadhi kwani Mji Mkongwe upo kwenye orodha ya UNESCO ya Urithi wa Dunia.
Kwa mujibu wa maelezo ya Said, majengo kumi na nne (14) tu ndiyo ambayo mpaka sasa yametolewa kwa wawekezaji ambapo majengo matano yanamilikiwa na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango; matatu yanamilikiwa na Shirika la Nyumba; matatu yanamilikiwa na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana; moja linamilikiwa na Wakala wa Majengo; moja linamilikiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali; na moja umiliki binafsi.
Majengo haya yametolewa kwa wawekezaji 13, ambao ndiyo waliokamilisha utaratibu wa kulipa fedha za utangulizi kwa Serikali, alisema Said. Fedha zilizolipwa zinasimamiwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mji Mkongwe, mfuko wenye lengo la kuhifadhi na kuendeleza Mji Mkongwe.
“Jumla ya fedha za utangulizi (upfront payment) Shilingi 5,228,389,910 zimeingizwa kwenye Mfuko huo na zimeanza kutumika katika uhamishaji wa ofisi za Serikali,” Said aliwaambia waandishi wa habari.
Said aliongeza kwamba matumizi ya fedha hizi za Mfuko wa Uhifadhi wa Mji Mkongwe yanalenga kuimarisha majengo yaliyo katika hali hatarishi pamoja na miundombinu ya eneo la Mji Mkongwe ambapo mpaka Julai 10 tayari makisio ya Shilingi 184,402,500 ya kuhamisha nyumba nne yameshakamilika na ukarabati wa baadhi ya nyumba hizo unaendelea.
Hata hivyo, Said alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa katika kufanikisha zoezi hilo, ikiwemo wakaazi ambao wanaishi katika majengo yaliyochaguliwa kwa uwekezaji kukataa kuhama baada ya mwekezaji akipatikana kwa kusema kwamba wako tayari kufanya matengenezo ya majengo wanayoyatumia.
“Wawekezaji wengi wanaokuja kuwasilisha maombi ya uwekezaji wanachagua majengo yaliyo katika hali nzuri,” alieleza Said kwenye mkutano wake na waandishi wa habari. “Mahitaji mengi ya wawekezaji pia yanatofautiana na Mpango Mkuu wa Uhifadhi na Urithi wa Mji Mkongwe.”
Hifadhi ya Mji Mkongwe inajumuisha majengo yasiyopungua 2,711, maeneo ya wazi pamoja na miundombinu mbalimbali, ikiwemo vichochoro, inayopelekea mji kuonekana katika mandhari yake ya kihistoria.
Majengo yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe yanamilikiwa na taasisi za Serikali ikiwemo Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi; Shirika la Nyumba; Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana; Ofisi ya Rais Fedha na Mipango; Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale; Wakala wa Ujenzi; Mamlaka ya Mji Mkongwe; Jumuiya za Kidini; pamoja na wamiliki binafsi.
Zoezi linaloendelea hivi sasa la kutoa baadhi ya nyumba kwa wawekezaji linatokana na ukaguzi maalum uliofanyika mwaka 2020 ambao ulibaini kwamba majengo 127 yapo katika hali mbaya, kati ya hayo majengo 36 yapo katika hali mbaya sana.
Kwenye majengo haya 36, jengo moja linamilikiwa na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda; moja linamilikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango; majengo sita yanamilikiwa na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana; 14 yanamilikiwa na watu binafsi na 14 yanamilikiwa na Shirika la Nyumba la Zanzibar.
Suala la uuzwaji wa nyumba za Serikali lilikuwa ni moja tu kati ya masuala kadhaa ambayo Jussa aliitaka Serikali ya Rais Mwinyi kuyatolea ufafanuzi. Masuala mengine ni pamoja na mradi unaoendelea wa ujenzi wa barabara za ndani; uendeshaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume; ukodishwaji wa visiwa vidogo; na ujenzi wa masoko ya Chuini, Mwanakwerekwe na Jumbi.
Soma pia: Serikali ya Mwinyi ni Muhimu Ikajibu Maswali Haya Muhimu