The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zoezi la Uwekaji Anwani za Makazi Lafikia Asilimia 95

Serikali inaamini mafanikio haya yatarahisisha utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kuanza hapo Agosti 23, 2022.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Innocent-Primus Mungy ameiambia The Chanzo kwamba hadi kufikia Juni 30, 2022, utekelezaji wa zoezi la kuweka anwani za makazi nchini limefikia asilimia 95, akisema mafanikio hayo yatasaidia pia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Sensa ya Watu na Makazi inategemewa kuanza hapo Agosti 23, 2022, ikiwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Zoezi la anwani za makazi lilizinduliwa rasmi hapo Februari 8, 2022, na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alisema kwamba lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na anwani ya makazi katika eneo lake analoishi, kaya, ofisi ama eneo la biashara ili kuweza kuhudumiwa kwa ufanisi.

Wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni, Mungy alisema kwamba Serikali ilikuwa na lengo la kukusanya anwani za makazi 11,582,106 lakini mpaka kufikia Juni 30, 2022, wamepitiliza lengo hilo kwa kukusanya anwani za makazi 12,385,956.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Innocent-Primus Mungy ofisini kwake wakati wa mahojiano

“Katika hizo 12,385,956, anwani ambazo zina majengo, yaani kuna jengo kamili, ziko 12,011,576,” alisema Mungy. “Anwani zenye viwanja vitupu, maana unakuta mtu ana kiwanja ameanza kujenga lakini nyumba haijakamilika, zilikuwa ni 374,380.”

Jumla ya vibao 1,641,000 vimebandikwa kwenye nyumba za watu mbalimbali, alisema Mungy, akiongeza kwamba anwani zilizochorwa, yaani zile ambazo majina yameshaandikwa, ni karibu milioni sita, huku anwani zinazoendelea kufanyiwa kazi ni milioni nne. Kwa nchi nzima, jumla ya nguzo 917,000 zimesimikwa nchi nzima.

Mungy anahusisha mafanikio haya na juhudi ambazo Serikali iliweka kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusiana na zoezi hilo ambayo anakiri imeweza kuwahamasisha wananchi waliowengi kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wake.

“Na mpaka sasa hivi tunaweza kusema hakuna mtu ambaye hajui kuhusu mfumo huu wa anwani za makazi,” alisema Mungy. “Kwa hiyo, kimsingi kile tulichokikusudia kukifanya kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, tofauti na sisi tulivyokuwa tumefikiria. Kwa tathmini tuliyoifanya mikoa yote imefanya vizuri, hakuna mkoa ambao umefanya vibaya.”

Hii, hata hivyo, haimaanishi kwamba hakukua na changamoto zilizojitokeza wakati wa kutekeleza zoezi hili kwani Mungy amebainisha kwamba Serikali ilishindwa kutekeleza zoezi hilo kwenye ardhi zenye migogoro, ikiwemo wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi au yale ya wazi.

Changamoto nyengine zilikuwepo kwenye uandishi, hususan ule wa kuchanganya L na R, hali iliyopelekea kazi hizo kurudiwa na hivyo kuchelewesha ukamilishaji wake. Pia, kulikuwa na changamoto kwenye kuipa mitaa majina, baada ya watu wengine kukataa mitaa kuitwa majina fulani.

“Changamoto nyingine ni uelewa, kwa maana ya kwamba baadhi ya watu hawapendi kushiriki kwenye shughuli za Serikali,” alikiri Mungy. “Sasa kuna watu kabisa hawakuacha taarifa nyumbani kwao. Kuna nyumba ambazo tumeweka namba lakini hatujui nani anakaa, kila ukienda humkuti.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *