The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kashfa ya Loliondo Inatuonyesha Kwamba Uhifadhi Tanzania Upo Kwa Malengo ya Kibiashara, Siyo Kulinda Mazingira

Ndiyo maana uwindaji wa wanyama pori kwa ajili ya burudani unakubaliwa na hata kuhamasishwa.

subscribe to our newsletter!

Nadhani ni muhimu kwenda nyuma kidogo ili kukumbushana kwamba mnamo mwaka 1959, viongozi wa kimila kutoka jamii ya Kimaasai, walilazimishwa kusaini mkataba wa kuwahamisha watu wao kwenda maeneo ya Ngorongoro na Loliondo. Hatua hiyo ilitokana na mpango wa Serikali ya kikoloni ulioitangaza Serengeti kama Hifadhi ya Taifa, au National Park kwa kimombo.  

Ngorongoro na Loliondo ziliwekwa, zote mbili, chini ya mfumo wa uhifadhi pia. Eneo la uhifadhi la Ngorongoro (NCA) lilianzishwa mnamo mwaka 1959 kama “eneo la matumizi mbalimbali ya ardhi,” yaani lilitengenezwa kwa ajili ya kuhimiza uhifadhi wa wanyama pori na maliasili, kulinda maslahi ya wakaazi wenyeji wa asili wa Ngorongoro na kukuza utalii.

Na Loliondo ni ardhi ya vijiji lakini ikawa pia pori tengefu, au game-controlled area (GCA) kwa kimombo, yaani sehemu ambayo binadamu na shughuli zao vyote vinaruhusiwa kufanyika. Tatizo ni kwamba, mfumo wa uhifadhi wa Tanzania umezidi kuweka vikwazo kwa wafugaji wanaoishi humo.

Uhamisho wa wenyeji “kwa hiari”?

Tumeona juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutaka kuhamishia wenyeji wa NCA katika maeneo mengine ya nchi, maeneo ambayo kiasili siyo ya kwao, hizi ni ardhi ambazo watu wengine tayari wapo – kutokana na ukweli huu, siyo ngumu kuelewa kwamba migogoro mingine ya ardhi inaweza kutokea kwenye maeneo hayo.

Uhamisho huu wa wenyeji unatokana, kwa kiasi kikubwa, na majibu ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania yaliyotolewa kwenye ripoti iliyoitwa “The Multiple Land Use Model of Ngorongoro Conservation Area: Achievements and Lessons Learnt, Challenges and Options for the Future (Final Report)”, ya mwaka 2019. 

Ripoti hii iliandikwa kuhusiana na mapendekezo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya mwaka 2019 (na mengine kabla yake), yaliyohimiza uhamisho wa wenyeji “kwa hiari” kutoka NCA. Vinginevyo, eneo la uhifadhi la Ngorongoro lingefikia kupoteza usajili wake kama eneo la Urithi wa Dunia kwenye orodha ya UNESCO. 

Kumbe, hakuna uhamisho wa wenyeji kutoka ardhi za kiasili za mababu wao, ukiwa “kwa hiari.” Kilichopo ni mikakati ya mamlaka ya kufanya wananchi kuamua kuhama kutokana na “idhini iliyotengenezwa,” yaani kwa sababu walinyimwa huduma za kijamii na kukatazwa kuchunga na kulima katika maeneo yao.

Ingawa uhamisho wa wenyeji wa Loliondo unalingana pia, kwa kiasi fulani, na majibu ya Wizara ya Maliasili na Utalii juu ya mapendekezo ya UNESCO, hali ya Loliondo ina vipengele vyake vya kipekee.  Tunachokiona kwa sasa ni jitihada za kuwaondoa Wamaasai katika vijiji vyao, vilivyosajiliwa, ili kutoa fursa kamili kwa ajili ya shughuli za kitalii wa uwindaji katika eneo hilo. 

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kubadilisha aina ya hifadhi: kutoka pori tengefu la Loliondo, au Loliondo game-controlled area kwa kimombo, kwenda pori la akiba, yaani game reserve.

Tofauti kati ya aina hizi za ardhi ni kwamba ndani ya pori tengefu, makazi na shughuli za binadamu kama malisho, kwa mfano, zinaruhusiwa wakati ndani ya pori la akiba shughuli hizi haziruhusiwi. 

Hiyo ina maana kwamba kwa vile pori tengefu la Loliondo linafanywa kuwa pori la akiba ni lazima wakazi wake waondolewe kwenye ardhi. Ni muhimu kubainisha kwamba mchakato huu umefanyika bila idhini ya awali ya wenyeji wa Loliondo.

Na ndiyo maana baadhi yetu tumeona jaribio la wenyeji la kukataa mpango huu. Nasema “baadhi yetu” kwa sababu vyombo vya habari vya Tanzania havisambazi waziwazi habari za mvutano huu mkubwa, wala havisambazi habari za Wamaasai ambao wamepigwa risasi.

Siyo mara ya kwanza

Kwa upande mmoja mabadiliko haya ya ghafla ya aina ya ardhi ni jambo jipya. Kwa upande mwengine, hata hivyo, hii siyo mara ya kwanza kwa watu kufukuzwa na kuteseka kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu za wenyeji wa Loliondo.

Kutoka mwaka 2009 ambapo tukio la kwanza lilitokea mpaka mwaka huu wa 2022, mara zaidi ya sita moto umewahi kurushwa kwenye nyumba za wakazi na vitendo vingine vya unyanyasaji vilifanyika Loliondo. Na kiuhalisia, kufukuzwa na aina nyingine za ukiukwaji wa haki za binadamu kumekuwa kukifanywa zaidi ndani ya mapori tengefu.

Sababu kuu ya hilo ni mwingiliano wa kategoria za ardhi katika sheria za ardhi za Tanzania na matumizi tofauti yanayofanywa kwenye ardhi hizi. Mapori tengefu mengi yanaingiliana kabisa na ardhi za vijiji zilizosajiliwa. Na mara nyingi, matumizi makuu ya wanyamapori katika mapori tengefu ni kwa ajili ya vibali vya uwindaji wa kitalii vinavyotolewa na Serikali ya Tanzania bila ushiriki wa wenyeji au wanavijiji.

Loliondo ni eneo la pori tengefu, linalopakana na vijiji kadhaa vilivyosajiliwa. Sehemu ya eneo la pori tengefu ya Loliondo imetengwa kama kitalu cha uwindaji. 

Vitalu vya uwindaji, au hunting blocks kama vinavyojulikana kwa kimombo, ni maeneo yaliyotengwa kwa makubaliano ambapo makampuni ya kimataifa yanaweza kusaini makubaliano na Serikali ya Tanzania na kutumia ardhi kwa madhumuni ya uwindaji wa burudani kama vile mbuga binafsi za michezo ya uwindaji wa nyara (trophy hunting). 

Mnamo mwaka 1992, familia ya kifalme kutoka Dubai ilipewa eneo la Loliondo kupitia kampuni yake ya kitalii ijulikanayo kama Ortello Business Corporation (OBC). Makubaliano na OBC yalidumu kwa zaidi ya miaka 20 na kuchochea uondolewaji wa watu wengi ulioambatana na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu mara kadhaa.

Kashfa ya Loliondo Gate

“Kesi ya Loliondo” ilijulikana duniani kote, hususani kutokana na kampeni za Avaaz, shirika lisilo la kiserikali la nchini Marekani, ambazo zilipazia sauti vitisho na kufukuzwa kwa lazima kwa wakazi wa vijiji vya Loliondo. 

Hii ilikuwa ni “kashfa ya kimataifa” iliyoibuliwa na msomi Profesa Jwani Timothy Mwaikusa hapo mwaka 1993, alipoandika kuhusu “Kashfa ya Loliondo Gate,” akiibua madhila yaliyotokana na makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na mwana wa mfalme wa kiarabu, yaliyotiwa saini mnamo mwaka 1992. 

Kwenye makala yake, Mwaikusa alisema kwamba “jamii ya wafugaji itaweza kuchukizwa vikali na kuhisi kwamba hawajatendewa haki; kwamba wanafukuzwa kwenye maeneo ya wanyamapori, ambayo yamekuwa maeneo ya watu wao ya kiasili, ili kuwanufaisha watu wengine.”

Ndiyo maana, marehemu Lazaro Moringe ole Parkipuny, aliyekuwa mbunge wa zamani na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Loliondo, aliwahi kusema kwamba: “Wamaasai ni wazuri kwa picha ya mtalii, ni muhimu kwa ajili ya kukubebea mifuko yako hadi kambini, au hata kukuelekeza kwa wanyama, (…) Lakini mwishoni wanyama hao ni wa thamani zaidi kuliko watu.”

Takribani asilimia 40 za ardhi ya Tanzania zimewekwa kwenye mfumo wa uhifadhi kwa sababu sera za uhifadhi nchini humo zinasema ni lazima kulinda wanyama pori na maliasili waliopo nchini humo. Lakini katika mapori tengefu mengi Serikali imeweka vitalu vya uwindaji.

Kumbe! Utalii wa kuwinda wanyama pori kwa ajili ya burudani ni uhifadhi? Je, katika mazingira kama hayo, nia ya kulinda na kutetea mazingira na viumbe hai iko wapi? 

Kwa hiyo, wawindaji wa burudani wanaotoka kwenye Shirikisho la Falme za Kiarabu (UAE), Marekani na kadhalika wanapaswa kuwa na pesa tu ili wapewe vibali vya kutumia vitalu vya uwindaji na kuwaua wanyama pori?

Ndiyo maana tunaweza kuhitimisha safu hii kwa kusema kwamba maslahi ya uhifadhi nchini Tanzania mara nyingi ni mambo ya biashara tu na wala siyo kulinda mazingira.

Na badala ya kuuza maisha ya viumbe hai, vitalu vya uwindaji vya Serikali vinakataa pia kuheshimu maisha ya watu. Mbaya zaidi, maisha ya watu wake, yaani Watanzania. Je, vitalu vya uwindaji ni jinsi ya kuwapa “wageni” haki zote za kutumia ardhi na wanyama pori na kuwazuia Watanzania kutoka nyumbani kwao? Ama Wamaasai si wananchi wa Tanzania?

Aline Rabelo ni mwanaanthropolojia na raia wa Brazil mwenye shahada ya uzamifu (Ph.D.) katika anthropolojia ya jamii. Aline ameishi na kufanya utafiti nchini Tanzania kwa vipindi tofauti tofauti tangu mwaka 2012. Kwa maoni, anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni arabelo.anthropology@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

4 Responses

 1. Good! Very articulated! Chanzo Initiative your doing great! The masai in Ngorongoro and loliondo they have been marginalized for so long, they lack social services for years not because they’re not Tanzanian – but because the Gov plan to evict them from their ancestors land to give Room for trophy hunting!
  It’s misfortune that’s the Tanzania banned social media to report what’s going on in loliondo & Ngorongoro

  Asante chanzo initiative

  1. I havent read on how media freedom in Tanzania has been compromised by legislation, being the reason why the Tanzanian press is all but silent about these injustices. And the massive corruption involved, as one former tourism minister publicly acknowledged! Even the relocation of the maasai is being done at the cost of billions of shillings, the source of which is yet to be known! What a shame for Tanzania!

 2. There is freedom of speech but there is no guarantee of freedom after speech.
  The beginning of someone freedom of speech is the end of someone’s freedom of speech.
  Speaking about freedom of speech is a justification that there is freedom of speech.

 3. There is freedom of speech but there is no guarantee of freedom after speech.
  The beginning of someone freedom of speech is the end of someone’s freedom of speech.
  Speaking about freedom of speech is a justification that there is freedom of speech.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *