Mkanganyiko wa Maagizo Kati ya Wizara, Idara za Serikali: Tatizo ni Nini?

Wadau wabainisha ukosefu wa uratibu serikalini na maamuzi kufanywa bila kushirikisha wahusika.
Lukelo Francis5 August 20225 min

Dar es Salaam. Ile hali ya Serikali kujitokeza na kuzuia utekelezwaji wa utaratibu fulani uliopitishwa na Serikali yenyewe umejirudia tena wiki hii baada ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kulazimika kusitisha utaratibu mpya wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) baada ya kutekelezwa kwa siku tatu tu.

Utaratibu huo ambao ulizua gumzo kubwa mitandaoni ulilenga kumzuia mteja wa NHIF aliyezoea kutibiwa kwenye hospitali fulani kutibiwa kwenye hospitali nyingine mpaka pale atakapopata rufaa au baada ya kupita siku 30.

NHIF wenyewe walisema utaratibu huo ulioanza utekelezaji hapo Agosti 1 ulilenga kupunguza gharama zisizo za lazima. Lakini siku tatu baada ya kutekelezwa, Mwalimu alijitokeza na kusimamisha utaratibu huo.

Mbunge huyo wa Tanga Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM) alisema anakubaliana na nadharia ya NHIF ya kutaka kupunguza matumizi yasiyo ya lazima lakini akashauri kwamba NHIF inahitaji kushirikisha wadau kwanza kwa upana wao kabla ya utaratibu huo kutekelezwa.

Sakata la Mwalimu na NHIF linafanana na lile la Waziri wa Maliasili na Utalii Pindi Chana na Mamlaka ya Usimamizi ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) lililohusisha uondolewaji wa katazo la kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi ambapo katazo hilo lilirejeshwa siku chache tu baada ya kuondoshwa.

Hii pia siyo mara ya kwanza kwa Mwalimu kuingilia kati utekelezaji uliofanywa na Serikali na kutaka usitishwe.

Mnamo Oktoba 9, 2021, akiwa Waziri wa TAMISEMI, Mwalimu alizuia utekelezaji wa utaratibu wa adhabu ya faini kwa wamiliki wa vyombo vya moto wanaoshindwa kufanya malipo yao ya maegesho baada ya kupita siku saba. Utaratibu huo ulitangazwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Maamuzi ya ghafla

Aidan Eyakuze ni Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, asasi ya kiraia inayojihusisha na kuchochea uwajibikaji serikalini, anadhani kwamba hali hii ya maagizo kutolewa na kutenguliwa ndani ya siku chache inaweza kuwa inasababishwa na ukosefu wa uratibu serikalini pamoja na maamuzi kufanywa kwa ghafla.

“Changamoto ni kwamba wanaoathirika hawakupewa taarifa,” anasema Eyakuze wakati wa mahojiano na The Chanzo.

Aliongeza: “Na kama kuna tatizo, basi je, kuna uwezekano wa kuzungumza jinsi ya kulitatua hilo tatizo lisiwe endelevu na siyo kufanya uamuzi ambao ni ghafla, unaumiza, halafu watu hawana sauti yoyote ile ya kujaribu kuchangia suluhisho mbadala.”

Eyakuze anadhani hali hiyo inathibitisha madai ya Rais Samia Suluhu Hassan juu ya ukosefu wa uratibu ndani ya Serikali anayoiongoza.

Mnamo Machi 30, 2022, baada ya kupokea ripoti za uchunguzi kutoka TAKUKURU na CAG, Rais Samia alitaja ukosefu wa uratibu serikalini kama moja kati ya matatizo makubwa ambayo Serikali yake inakumbana nayo.

“Sasa haya yanayotokea ni ushahidi wa kauli hiyo,” alisema Eyakuze. “Ni jambo linalohitaji kufanyiwa kazi. Inabidi watu ndani ya Serikali waweze kuongea na kuweka uratibu kwenye maamuzi yanayofanyika.”

Kukosekana kwa utaasisi

Huu uratibu ndiyo ambao Deus Kibamba, mchambuzi wa masuala ya kiutawala, anauita “utaasisi” ambao ndiyo anaodhani unakosekana ndani ya Serikali na kupelekea aina hii ya mikanganyiko.

“Ninachokiona mimi ni kwamba tuna tatizo la kukosekana kwa utaasisi,” alisema Kibamba wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Serikali inatakiwa ifanye kazi kama taasisi, yaani maamuzi hayawezi kutokana na mtu mmoja.”

Kwa Kibamba, “utaasisi” ni maamuzi makubwa kufanywa na Baraza la Mawaziri na waziri mwenye dhamana kuyachukua na kuyashusha kwa taasisi zilizopo chini yake. Hivi, Kibamba anaamini mikanganyiko hii ambayo imekuwa ikitokea ingepungua.

Lakini kwa Charles Makakala, ambaye hushauri masuala ya kiutawala na kiuongozi, tatizo kubwa analoliona ni nguvu kubwa ya maamuzi kuwekwa kwenye mikono ya wanasiasa.

“Jambo la kwanza ni mfumo ambao unatoa nguvu kubwa sana kwa wanasiasa, nikiwa na maana ya wale watu ambao wanafanya uteuzi,” Makakala anaeleza.

“Inapotokea mwanasiasa anabadilisha uamuzi wa taasisi ya umma, maana yake ni kwamba anavuka mamlaka ya bodi, anavuka mamlaka za utawala, anakwenda kufanya kazi za usimamizi,” aliongeza Makakala ambaye pia ni mwandishi.

Ushirikishwaji

Kitu kimoja kinachojidhihirisha kila wakati Serikali inatengua maamuzi yake iliyoyaweka awali ni ukosefu wa ushirikishwaji wa kutosha wa watu ambao wanaenda kuathiriwa na utaratibu husika kwa namna moja au nyengine.

Hata hili la NHIF, kwa mfano, Mwalimu amuelekeza mfuko huo kukutana na wadau na kujadili suala husika kabla ya kuurudisha utaratibu huo uliolalamikiwa.

The Chanzo ilimuuliza Kibamba inawezekana vipi utaratibu unabuniwa na halafu unaenda mpaka kutekelezwa wakati wadau wake wakuu hawakushirikishwa ambapo alijibu kwamba ushirikishwaji wa wananchi ni utamaduni mgeni kwenye uendeshaji wa nchi Tanzania.

“Mambo ya msingi yanayohitaji wananchi washirikishwe hawashirikishwi, sembuse la hili la maamuzi kwenye taasisi?” Kibamba anashangaa.

“Kwa bahati mbaya sana mfumo wa maamuzi ya kisera kwenye nchi yetu umemsahau sana mwananchi wa kawaida,” aliongeza Kibamba. “Zipo sehemu chache sana ambazo zimeainishwa wazi kwamba ni lazima wananchi washirikishwe.”

Jumuiya za walaji

Lakini ni rahisi kiasi gani kwa NHIF, kwa mfano, kuwashirikisha wateja katika mazingira ambayo hakuna chombo mahususi kinachowaunganisha na kuwapa sauti moja na nguvu ya mapatano?

Kasoro hii ndiyo ambayo Eyakuze wa Twaweza anatamani kuiona inapatiwa ufumbuzi Tanzania.

“Ni muhimu pakawepo na utaratibu wa kamati, au ushirika wa walaji wa huduma husika ambao wanapigiwa simu, wanahojiwa, tunafanya hiki na hiki je, mnaonaje?” anapendekeza Eyakuze. “Hii itawawezesha walaji kuteta haki zao hata kama huduma inatolewa na taasisi za umma na Serikali.”

Wakati kamati, au vyama, vya walaji vimetapakaa ulimwenguni kote na kutoa mchango mkubwa kwenye kulinda na kutetea haki za walaji, hali ni tofauti nchini Tanzania ambako kunaonekana kukikosekana vuguvugu la waziwazi la kutetea haki za walaji.

Hata kwa zile taasisi za umma zenye bodi za usuluhishi wa wateja – Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kwa uchache, – haijulikani ni kwa kiasi gani haswa bodi hizo zinalinda haki za walaji.

Madhara kwa nchi

Lakini mikanganyiko hii inaweza kuwa na athari gani hasi kwa mustakabali wa Tanzania kama nchi?

Kwa kutumia mfano wa sakata la TAWA na Waziri Chana, mwandishi wa habari wa siku nyingi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Damas Kanyabwoya alionya kwamba Serikali kuwa na sera zisizotabirika kunaweza kuigharimu nchi kwenye suala zima la uwekezaji, hususan ule wa kutoka nje.

Akiandika kwa ajili ya The Chanzo hapo Juni 13, 2022, Kanyabwoya alisema kwamba kubadilikabadilika kwa kauli za Serikali, hasa kwa kuzuia mambo ambayo Serikali yenyewe iliyaruhusu, inatoa ujumbe mbaya kwa wawekezaji.

“Serikali ni lazima ijue kuwa Tanzania haitaweza kupaa kiuchumi kama sera na taratibu za kibiashara zitakuwa zinabadilika kila siku.

Mabadiliko haya ya mara kwa mara yanayotia hasara wafanyabiashara ni ya ajabu ukizingatia kuwa nchi hii imekuwa chini ya chama kimoja cha siasa tangu uhuru,” aliandika Kanyabwoya.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Lukelo Francis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved