The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Serikali Inaifahamu Dhana ya Utamaduni Anuai?

Nchi yenye kutambua dhana ya utamaduni anuai haiwezi kuja na mwongozo wa maadili ya kitaifa.

subscribe to our newsletter!

Nimesoma habari ya jarida la mtandaoni liitwalo Pambazuko, toleo namba 005 la Agosti 8–14, 2022, ambalo kwenye ukurasa wake wa tano, uliopewa jina la Mada ya Wiki, habari iliyochapishwa hapo, yenye kichwa cha habari Tanzania yaongoza kwa ‘matiti dhalili,’ imenifikirisha sana.

Habari hiyo ilihusu matokeo ya ‘utafiti’ ambao jarida hilo liliufanya kuanzia Julai 12 mpaka Agosti 6, 2022, kwenye nchi tatu za Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya na Uganda, ili kuchunguza ni nchi gani inaongoza kwa wanawake “wanaopenda kuachia matiti” wazi. Tanzania iliongoza, Pambazuko ilitwambia.

‘Screenshot’ ya ukurasa wa tano wa jarida la Pambazuko kuhusiana na uchunguzi wa jarida hilo wa nchi inayoongoza kati ya Tanzania, Kenya na Uganda kwa wanawake wake kutembea “matiti wazi.”

Kwangu, naona habari hii ni sehemu ya tatizo kubwa linalohusiana na changamoto nzima ambao mwili wa mwanamke umekuwa ukikabiliana nayo.

Nadhani changamoto hii huchagizwa zaidi na ukweli kwamba tafsiri ya mwili wa mwanamke mara nyingi hutokana na mtazamo wa macho ya mwanaume.

Kwenye habari husika, kwa mfano, waandishi wamejipa wadhifa wa kuhukumu bila kuainisha vigezo na masharti kwa vipi muonekano wa matiti ni ‘uchi’ au yasiyo na ‘staha.’

Huenda waandishi wana namna yao ya kufikiri lakini ni wazi kwamba majiji ya Nairobi na Kampala yana hali ya hewa ya baridi kuliko Dar es Salaam na hivyo watu wake hupenda kujifunika kwa sababu ya hali ya hewa.

Waandishi hawa labda kama wangeenda London, Hamburg au Paris wakati wa majira ya baridi wangewasifu sana wazungu kwa tabia yao ya kusitiri matiti.

Hakuna data

Kitu kingine ni kwamba baada ya uchunguzi wa mwezi mzima Waandishi Wetu – kama ambavyo walitambulishwa kwenye habari hiyo – hawakuwa na data au namba zozote zile walizoziweka hadharani.

Pia, Waandishi Wetu wameshindwa kufafanua ‘kuonyesha matiti’ maana yake ni nini? Ni eneo gani la matiti? Ni muhimu Waandishi Wetu wakumbuke kwamba matiti ni sehemu ya mwili inayotofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.

Pengine walipaswa kutafuta rula kama wale maafisa wa Wizara ya Uvuvi waliowapima samaki wakati wa Rais John Magufuli. Naandika huku nacheka.

Waandishi Wetu wamefafanua kwamba walienda sehemu za vyuo vikuu na mapito ya watu wengi. Yote haya ni maeneo yenye vijana wengi zaidi.

Kama Waandishi Wetu wangetambua kwamba ni mila za makabila yote ya Kiafrika kuacha matiti wazi, na hivyo kuita kiujumla jumla ‘matiti dhalili’ au ‘uchi maeneo ya matiti’ nahisi huenda na wao wamejikosesha staha kiasi.

Serikali na maadili

Nilianza makala haya kwa kusema kwamba habari hii imenifikirisha sana. Imenifikirisha kwa sababu kwa namna moja au nyengine inahusiana sana na kile kinachoendelea hivi sasa nchini Tanzania kwenye eneo zima la utamaduni na maadili.

Serikali, kupitia wizara yake ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, imetoa kijitabu kiitwacho Mwongozo wa Maadili na Utamaduni wa Mtanzania ambacho kimepokelewa kwa hisia tofauti tofauti na Watanzania. Kupitia kijitabu hiki, Serikali pia imeonesha haipendi saana kuona matiti.

Kwenye ukurasa wa 26 wa Mwongozo huo, kuhusu mapendekezo ya namna ya kudhibiti mmomonyoko wa maadili, Serikali inasema: “Ili Mtanzania aonekane kuwa ni mtu mwenye maadili mema ni lazima avae mavazi yenye heshima na staha, yaani yenye kusitiri mwili kulingana na umbo la mwili wake.”

‘Screenshot’ ya ukurasa wa 26 wa kijitabu cha Mwongozo wa Maadili na Utamaduni wa Mtanzania kilichotolewa na Serikali hivi karibuni.

Serikali inaendelea kusema: “Mtanzania yeyote hapaswi kuvaa mavazi yenye kuacha wazi baadhi ya maungo muhimu ya mwili, hasa kwa wanawake, na nguo za mlegezo kwa wanaume.”

Ni kwa bahati mbaya sana kwamba Mwongozo huu haujatoa tafsiri ya maneno ‘maungo muhimu.’ Pia, haifahamiki mpaka sasa ‘kusitiri mwili kulingana na umbo’ inamaanisha nini haswa.

Mwongozo huo umeambatana na picha za watu waliopendeza, wenye afya tele na furaha ambao kwa vyovyote vile hawawakilishi Watanzania wa hali ya chini ambao ndiyo wengi kwenye nchi hii.

“Baadhi ya watu wazima pia hukaa vifua wazi hadharani bila kujali wanakutana na nani,” Mwongozo unatamka. “Lazima tupige vita uvaaji usiokubalika katika jamii zetu ili kulinda hadhi ya utamaduni wetu kwa kizazi cha sasa na hapo baadaye.”

Utamaduni anuai

Hii haijalishi ukweli kwamba nchini Tanzania hakuna sheria inayoelekeza watu jinsi ya kuvaa, au sehemu gani ya matiti ni sahihi kuonekana.

Tafsiri ya yote haya, kwa maoni yangu, ni kwamba Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine nyingi tu za Afrika, inakabiliwa na changamoto kwenye eneo la usimamizi wa mabadiliko ya kiutamaduni.

Je, tunatambua kwamba uanuai (diversity) wa kiutamaduni wetu kabla ya kusimika amri au matamko?

Nakumbuka miaka michache iliyopita aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto alimdhalilisha kijana mwenye tattoo mwilini mwake mbele ya vyombo vya habari.

Muroto, ambaye sasa amestaafu, alifanya hivyo bila kujua kwamba mtu kuwa na tattoo mwilini mwake havunji sheria yoyote ya nchi na kwamba kuwa na tattoo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Mwafrika.

“Mavazi yasiyositiri mwili ni ambayo huonesha baadhi ya viungo vya mwili au nguo za ndani, kubana sana, kutobolewa na kuchanwa na mavazi ambayo yanaacha baadhi ya sehemu za mwili wazi kama vile kiuno, kitovu, [na] kifua,” unasema Mwongozo katika ukurasa wa 15 kifungu C. “Aidha, uvaaji wa suruali au kaptura kwa mtindo wa mlegezo ambao husababisha nguo ya ndani (chupi) kuonekana haufai.”

Kama Serikali itaenda kusimamia utekelezaji wa Mwongozo huu, nini hatma ya Mmaasai na lugeba yake? Au raia wa Kitanzania wenye asili ya India ambao mavazi yao mengi yanaonesha vitovu, hawa hatma yao pia itakuwa ni nini?

Utamaduni ni mali ya nani?

Utakuwa umegundua mpaka sasa mkanganyiko mzima unaoletwa na hili vuguvugu na shinikizo la kutaka kusimamia ‘maadili’ na utamaduni wa Mtanzania.

Lakini swali ni je, utamaduni wetu ni mali ya nani? Na mpaka utachorwa wapi linapokuja suala la usimamizi wa hayo maadili ya Kitanzania?

Basi tuunde na kamati ya usimamizi wa matiti bora kama tulivyofanya kwenye mdundo wa taifa na vazi ka taifa.

Hapa, nashauri hadidu rejea ziweke wazi ubora/udhalili wa matiti ili unaendane na menegimenti ya ashiki za mwanaume. Ikiswihi basi kamati ipendekeze SUMMA JKT watengeneze sidiria za maadili, tena za mbao, kwa wale wenye matiti ‘saa sita.’

Tukimaliza hapo hakuna kulala tuunde kamati ya Serikali ya ‘kusitiri mwili kulingana na umbo.’

Hii itatupa umbo la taifa. Mtu mwenye makalio makubwa apangiwe mavazi ya kumsitiri na mwenye umbo la kutepeta akae kando asituharibie ushupavu wetu.

Robert Mwampembwa ni msanii, mwandishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT). Kwa maoni, anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni ‎robert@ubunifu.co.tz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *