Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?

Nani kati yetu asiyekerwa na kitu kimoja au kingine kinachofanywa na watu wengine kwenye nchi hii? Tutavikataza vyote hivyo?

Sherehe kubwa ya klabu ya Simba – Simba Day – iliyofanyika hapo Agosti 8, 2022, jijini Dar es Salaam na ambayo iliambatana na mchezo wa kirafiki kati ya Wekundu hao wa Msimbazi na timu ya Saint George kutoka nchini Ethiopia imeingia dosari baada ya mwanamuziki Tunda Man kuingia jukwaani kwa kutumia sanaa ya mchezo wa kuigiza akiwa amebebwa ndani ya jeneza, akisindikizwa na ‘mchungaji’ na wasaidizi wake.

Lengo, inaonekana, lilikuwa ni kuchagiza utani wa jadi uliopo kati ya Simba na mahasimu wao klabu ya Yanga, ambapo Tunda Man alilenga kuonesha ni kama vile Watoto hao wa Jangwani ni sawa na wafu. Siku moja baada ya igizo hilo, hata hivyo, Serikali ilimpangia “kazi nyengine” Godwin Nsajigwa, ambaye ni Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, “kwa kushindwa kusimamia matumizi endelevu ya uwanja.”

Baadhi ya viongozi wa dini na waumini wao pia wamejitokeza kulaani igizo hilo. Ukurasa wa Facebook wenye jina la Askofu Methodius Kilaini umelaani kitendo cha matumizi ya alama za kidini katika mchezo ule wa kuigiza, akisema: “Kutumia msalaba kudhihaki ni dharau na kufuru kubwa kwa waamini Wakristu na wote wanaoamini kwamba walikombolewa katika msalaba huo.”

Naye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima amelaani vikali kitendo hicho cha Tunda Man. Akiandika kwenye mtandao wa Twitter, Gwajima, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chama cha Mapinduzi – CCM), alikiita kitendo hicho “mzaha uliopita kiwango,” akiitaka Klabu ya Simba “kuomba radhi hadharani.”

Klabu ya Simba imejitokeza hadharani na kuomba radhi kama ilivyoagizwa, ikisema imelazimika kufanya hivyo “kwa kuheshimu imani za watu wote.” Hata hivyo, sakata hili zima limenifanya nitafakari sana juu ya namna watu na makundi mbalimbali wanavyoichukulia sanaa nchini Tanzania na athari zake.

Siyo mara ya kwanza

Hii siyo mara ya kwanza kwa imani za dini kuja kwenye msuguano na ubunifu wa kisanii.

Mtakumbuka kwamba mnamo Aprili 29, 2022, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilivipiga marufuku vyombo vya utangazaji – redio, televisheni na mitandao– kutokupiga video ya wimbo wa Mtasubiri Sana wa msanii Diamond Platnumz aliokuwa amemshirikisha Zuchu.

TCRA ilidai kwamba ililazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kipande kimoja (scene) kwenye video hiyo kuleta “ukakasi” kwa waumini wa madhehebu ya dini ya Kikiristo ambao wamekitafsiri kama “dharau kwa madhehebu yao.”

Kipande kinacholalamikiwa hapa kiliwaonesha Diamond Platnumz na Zuchu wakiwa kanisani wakiimba kwaya kabla ya kuwaonesha wakiwa sehemu nyengine.

Lakini tatizo liko wapi msanii akiamua kutumia Kanisa na mavazi au nyimbo zinazohusishwa na imani za kidini kama lengo siyo kukashifu?

Kuna hatari kubwa sana endapo kama mamlaka za nchi zitapiga marufuku vitu au kufungia kazi za sanaa kwa sababu tu eti zinaleta “ukakasi” kwa watu fulani.

Nani kati yetu asiyekerwa na kitu kimoja ama kingine kinachofanywa na watu wengine kwenye nchi hii? Tutavikataza vyote hivyo?

Sanaa ni kazi kweli?

Serikali yetu kwa muda mrefu sasa imekuwa ikipiga kelele kwamba sanaa ni kazi. Sasa kama kweli viongozi wanamaanisha wanachokisema, kwa nini wasanii wakifanya kazi zao wanashambuliwa kwa vigezo vya “ukakasi?”

Tunataka kukuza filamu halafu unasema hutakiwi kuonyesha Kanisa au kwaya na msalaba. Hii itawezekana kweli? Eti msanii Tanzania hutakiwi kutumia sare za Jeshi la Polisi wala za Jeshi la Wananchi. Sasa hapo sanaa inakuwaje kazi?

Watanzania wametokea kuwa wapenzi wakubwa wa mchekeshaji maarufu duniani Mr Bean ambaye komedi zake nyingi zinafanyika katika mazingira ya kanisani. Sijasikia filamu yoyote ya Mr Bean ikipigwa marufuku Tanzania.

Nyimbo nyingi, (rudia neno nyingi, tafadhali) za wasanii wa kigeni zenye kutumia Makanisa, misalaba na kadhalika zinatumika kila siku bila wasiwasi. Wimbo wa Church Heathen, kwa mfano, wa msanii nguli wa Marekani Shaggy umetengenezwa kanisani na hautofautiani na ule wa Mtasubiri Sana wa Diamond Platinumz na Zuchu. Hatujasikia wimbo huu ukifungiwa.

Kwa nini nyimbo ikiwa ya Mtanzania tu ndiyo inakuwa nongwa na Serikali kuhisi inajukumu la kuingilia kati ili kikundi fulani cha watu kisihisi “ukakasi” au “kisikereke?”

Basi, ikiwezekana, na Serikali ifungie na wimbo wa Tabu Ley wa Muzina maana wimbo ule ni sala ya Baba yetu katika wimbo. Tukimaliza hapo tuwakataze wachonga vinyago wetu wa pale Mwenge, Dar es Salaam kuchonga misalaba, maana wanatukosea adabu Wakistro.

Ikiwezekana pia, wasisahau kufungia filamu zote zenye misalaba, kwaya, chetezo au Makanisa kwa sababu ni makosa makubwa kutumia vitu hivi. Nisisahau wachora katuni na michoro mingine. Kama tutafanikiwa kwenye hao, basi tukimaliza tuhamie kwenye dini nyingine bila kusahau zile za jadi.

Tanzania haina dini?

“Tanzania haina dini lakini watu wake ndiyo wana dini,” alisema muasisi wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere.

Je, haimshangazi huko aliko hivi sasa kuona salamu rasmi za Serikali siku hizi ni Bwana Asifiwe na Tumsifu Yesu Kristo? Sikuitaja makusudi As-salamu Alaykum, kwa sababu hii siyo salamu ya kidini na kiuhalisia ni Kiswahili sanifu chenye asili ya Kiarabu.

Kabla sijatamatika niwarudie  wasanii wenzangu, huku nikicheka. Mazee, nashauri ikiwezekana kuanzia sasa tutumie vyombo, alama, nyimbo, video na mavazi ya shetani katika nyimbo, filamu na picha zetu kwa sababu nina uhakika hakuna atakayetuhukumu wala kutulaani.

Mwisho, ni imani yangu kwamba mbele ya Mungu, Maaskofu na Tunda Man wote ni sawa tu na hatupaswi kusubiri miaka takriban 350 – ambayo Kanisa lilisubiri kabla ya kumuomba msamaha mwanafizikia na mnajimu Galileo baada ya kumhukumu kwa kusema ukweli kuwa dunia haijasimama na inazunguka jua na siyo jua kuzunguka dunia – kuweka makabrasha yetu sawa.

Robert Mwampembwa ni msanii, mwandishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT). Kwa maoni, anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni ‎robert@ubunifu.co.tz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts