The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maswali Muhimu Uchaguzi Mkuu wa Kenya Ukielekea Mahakamani

Wakenya na dunia nzima wanasubiri kwa hamu kujua endapo Ruto atakuwa Rais wa tano wa Kenya au uchaguzi utarudiwa.

subscribe to our newsletter!

Mara baada ya kurejea kutoka Kisumu na Kilifi kama mwangalizi wa uchaguzi wa Agosti 9, 2022, nchini Kenya, nilikuwa sehemu ya mjadala mzito uliofanyika kwa muundo wa kipindi cha runinga uliandaliwa na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) hapo Agosti 20, 2022.

Mjadala huo ulijikita kwenye kujadili mafunzo makuu ya uchaguzi huo kwa nchi jirani, hususan nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Wakati wa majadiliano, hoja zangu zilijikita kwenye kuangalia maandalizi yalivyokuwa.

Hii ni kuanzia uandikishaji hadi uteuzi wa wagombea; kampeni za uchaguzi na hamasa ziliyoibua kati ya mashabiki na wanachama wa Muungano wa Azimio la Umoja chini ya Raila Amolo Odinga na wale wa Kenya Kwanza chini ya William Somoie Ruto; upigaji kura; kuhesabu; na kuhakikiki matokeo.

Nilijadili pia utata uliogubika utangazaji wa matokeo kutokana na kumeguka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) na kuwa vipande viwili, kimoja kikiongozwa na Mwenyekiti wa Tume Wafula Chebukati na makamishna wengine wawili huku kipande kingine kikisalia na makamu mwenyekiti wa Tume pamoja na wajumbe wengine watatu.

Utata wa kikatiba, kisheria

Wakati wa majadiliano hayo, nilisema kuwa somo moja linalotokana na uchaguzi wa Kenya ni utata wa kikatiba na kisheria juu ya maamuzi katika tume na mamlaka aliyonayo mwenyekiti bila ridhaa ya wajumbe wenzake.

Nionavyo mimi, Katiba nyingi za Afrika zina utata kuhusu mamlaka ya mwenyekiti katika kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa ngazi ya urais. Hii imekuwa ikipelekea sintofahamu kubwa kuhusu nani haswa mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais katika nchi kadhaa za Afrika.

Kwa mfano, katika nchi kama Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC) ambako tume za uchaguzi zina uwakilishi wa makundi, inaweza kuwa ni rahisi na hatari kwa tume kugawanyika kwa misingi ya makundi wanakotokea makamishna wa tume.

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Kenya Umekwisha. Tanzania Imejifunza Nini?

Hapo Zanzibar, kwa mfano, uchaguzi wa mwaka 2015 ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya visiwa hivyo (ZEC) Jecha Salim Jecha, akituhumu kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba, sheria na taratibu za uchaguzi.

Katika tangazo la kufuta uchaguzi, Jecha pia alirusha lawama kwa baadhi ya makamishna kuwa wameisaliti tume kwa kugeuka wawakilishi wa vyama badala ya kusimama kama makamishna wa tume.

Wakati Jecha akifuta uchaguzi huo mnamo Oktoba 28, 2015, matokeo ya uchaguzi katika majimbo 23 kati ya 54 ya uchaguzi yalikuwa bado kuhakikiwa na kutangazwa.

Vivyo hivyo, Chebukati wa IEBC ametangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Kenya 2022 hapo Agosti 15 pasipo na makamishna wenzake wanne katika saba kuwa naye ukumbini, Bomas.

Madai ya kuburuzwa

Kwa upande wa Kenya, tuhuma zilianzia kwa makamishna wanne, wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa IEBC  Juliana Cherera ambaye kwa niaba ya wenzake watatu alitangaza kujitenga kwao na matokeo yatakayotangazwa na Chebukati jioni ya siku hiyo. Wengine aliokuwa nao ni Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya.

Wanne hao wanamtuhumu Chebukati kwa kuwaburuza katika hatua za mwisho za kukubaliana mambo ya msingi kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais. Aidha, wanalalamikia sehemu ya kura zilizotangazwa na Chebukati, wakisema hawajui zimetoka wapi hadi kufikisha jumla ya asilimia 100.01 badala ya asilimia 100 pekee.

Makamishna hao pia wanajitenga na matokeo yaliyotangazwa kwa sababu wakati Chebukati anayatangaza, sehemu ya kura za majimbo zilikuwa bado kuhakikiwa na kujumlishwa katika matokeo ya jumla.

Kwa ujumla, makamishna hao wanne wanahoji demokrasia ya utangazaji matokeo ambayo wanadai ilikosekana kutokana na usiri na ubabe alioutumia Chebukati na hivyo wanaomba siyo tu kujitenga na matokeo bali pia wanataka matokeo hayo yawe ni ya kwake Chebukati na siyo ya IEBC.

SOMA ZAIDI: Ado Shaibu: Hivi Ndivyo Tanzania Inaweza Kupata Tume Huru ya Uchaguzi

Ili kuzuia wale watakaotoa hoja kuwa ibara ya 138 ya Katiba ya Kenya inamfanya mwenyekiti kuwa ndiye mamlaka halali ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Kenya, makamishna hao wamenukuu kesi mashuhuri ya Maina Kiai dhidi ya IEBC Na. 106 ya mwaka 2016 ambapo Mahakama Kuu iliamua kuwa:

“Kwa dhana ya tafsiri ya nia waliyokuwa nayo waasisi au waandishi wa Sheria na Katiba, ibara hiyo haikumaanisha kuwa wananchi wa Kenya wanarundika mamlaka yote na bila mipaka juu ya utangazaji wa matokeo ya uchaguzi kwa mwenyekiti wa tume kama mtu binafsi.”

Tafsiri ya hukumu hii ni kuwa mwenyekiti anatarajiwa kuwa atatangaza matokeo ya uchaguzi kutokana na makubaliano yaliyoafikiwa na tume nzima yenye makamishna saba kwa mujibu wa taratibu za ufanyaji maamuzi.

Maswali muhimu

Swali litakalotawala viwanja vya Mahakama hapa ni, je, mwenyekiti alishauriana na kupata ridhaa ya wajumbe wote wa tume? Au, je, utaratibu wa kufanya maamuzi ulitumia maridhiano (consensus) au akidi (quorum)?

Je, upande wa mwenyekiti, ambao ulikuwa na makamishna watatu tu ikilinganishwa na makamishna wanne upande wa makamu mwenyekiti, una nguvu na uhalali wa kutangaza matokeo bila wenzao?

Je, inakuwaje sasa kuhusu majimbo ambayo hayajafanya uchaguzi na yanapaswa yapangiwe tarehe na taratibu nyingine ili Wakenya wa majimbo hayo watimize haki yao ya kikatiba, ni tume ipi itakayoratibu zoezi hilo katika majimbo hayo?

Wakati Wakenya wakisubiri kama kesi ya kupinga Matokeo ya Uchaguzi wa Rais itafikishwa mahakamani, tayari kuna mashauri mawili mahakamani yaliyowasilishwa hata kabla ya Kenya kupiga kura hapo Agosti 9, 2022.

SOMA ZAIDI: Jinsi Uchaguzi Mkuu 2020 Ulivyoacha Simulizi za Majonzi Tarime

Shauri moja ni la wanaharakati 11 wanaopinga Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua wasiapishwe kuwa Rais na Makamu wa Rais kutokana na kesi za jinai zinazomkabili Gachagua ikiwemo ufisadi, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Katika tukio la hivi karibuni, Mahakama iliruhusu Serikali kutaifisha fedha taslimu kutoka kwenye akaunti ya benki ya Gachagua kiasi cha Shilingi za Kenya milioni 202 (takriban Shilingi bilioni nne za Kitanzania).

Kesi nyingine imefunguliwa na Azimio la Umoja dhidi ya Ruto na Gachagua ikidai kuwa wawili hao hawana sifa za kikatiba na kisheria kuweza kushika nafasi ya urais kutokana na vitendo vya kifisadi.

Kesi ya kupinga matokeo

Nje ya kesi hizo, kuna kesi mpya inayosubiriwa mahakamani siku ya Jumatatu, Agosti 22, 2022, ikipinga ushindi aliotangaziwa William Ruto kama Rais mteule na Rigathi Gachagua kama Makamu wa Rais mteule.

Kikosi cha mawakili wa Azimio la Umoja kinachoongozwa na mawakili wabobezi wa kesi za uchaguzi kama James Orengo, ambaye sasa amechaguliwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Siaya, na Otiende Amollo (Mbunge Mteule wa Jimbo la Rarieda) kimeandaa kesi nzito kuiwasilisha Mahakama ya Juu au ya Katiba, au ya Upeo, kama inavyojulikana huko Kenya.

Wanasheria wengine walio katika jopo la wanasheria wa Raila Odinga ni Phillip Murgor, Tom Ojienda na Paul Mwangi. Kwa upande wa Rais mteule William Ruto, kikosi cha wanasheria kitakachotetea ushindi wa Kenya Kwanza ni pamoja na wakili Kithure Kindiki na Nelson Havi. Wengine ni Kioko Kilukumi, Katwa Kigen na Muthoni Thiankolu.

Kesi hiyo ya uchaguzi itatua mikononi mwa jopo la majaji saba wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome, chini ya usaidizi wa Jaji Mkuu msaidizi Philomena Mbete Mwilu.

Majaji wengine ni William Ouko, Mohammed Ibrahim, Dk Smokin Wanjala, Njoki Ndungu na Isaac Lenaola.

Majaji hawa wana siku 14 kuanzia Jumanne, Agosti 23, 2022, kusikiliza na kuamua endapo ushindi wa William Ruto ni halali au la.

Endapo hukumu itaungana na tamko la mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na kumthibitisha Ruto, basi Rais ataapishwa rasmi siku ya Jumanne inayofuata baada ya wiki moja tangu hukumu ya Mahakama.

Endapo Mahakama itabatilisha ushindi wa Ruto, Kenya itarudia uchaguzi katika kipindi cha siku 60 au miezi miwili.

Maswali yasiyo majibu

Wakenya na dunia nzima wanasubiri kwa hamu kujua endapo Ruto atakuwa Rais wa tano wa Kenya au uchaguzi utarudiwa. Na kwa vyovyote itakavyokuwa, kuna maswali ambayo hayana majibu.

Je, kesi zilizofunguliwa mahakamani kabla ya siku ya kupiga kura dhidi ya Ruto na Gachagua zina nafasi gani kwa sasa?

Je, endapo hatimaye uchaguzi utapaswa kurudiwa, IEBC itawezaje kuendesha uchaguzi ikiwa vipande viwili?

Je, kidiplomasia, nini kinaweza kufanyika kuileta tena pamoja IEBC? Nakaribisha mjadala kuhusu hoja zinazoibuliwa na maswali haya!

Mungu ibariki Kenya na watu wake!

Deus Kibamba ni mtafiti na mchambuzi wa masuala kisiasa aliyekuwa mmoja wa waangalizi wa uchaguzi wa Kenya wa Agosti 9, 2022. Anapatikana kupitia +255 788 758581 au dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts