The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchaguzi Kenya Umekwisha. Tanzania Imejifunza Nini?

Wadau wataja uwazi, matumizi ya teknolojia na uadilifu.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Hatimaye kiu waliyokuwa nayo watu wengi ya kutaka kujua nani ataibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini Kenya kati ya William Ruto na Raila Odinga ilikatwa hapo Agosti 15, 2022, baada ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kumtangaza Ruto Rais wa tano wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Ruto, ambaye awali alikuwa ni Makamu wa Rais, alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 7,176,141, sawa na asilimia 50.49, dhidi ya kura 6,942,930, sawa na asilimia 48.85 alizopata mpinzani wake wa karibu Odinga, hii ikiwa ni tofauti ya kura 233,211.

Watanzania, kama walivyo raia zao wengine kutoka Afrika Mashariki, walikuwa wakiufuatilia kwa karibu uchaguzi huo ambao ulikuwa na ushindani wa kukata na shoka kati ya Ruto na Odinga, huku kila mmoja akieleza hisia zake za nani kati ya vigogo hao wawili wa siasa za Kenya angependa aibuke mshindi.

Lakini nini, kama kipo, Tanzania inaweza kujifunza kutoka Kenya linapokuja suala zima la kuendesha chaguzi za kidemokrasia za vyama vingi? Hili ndilo swali ambalo wananchi, wadadisi wa mambo na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wataendelea kulitafakari kwa siku kadhaa zinazokuja.

SOMA ZAIDI: Ado Shaibu: Hivi Ndivyo Tanzania Inaweza Kupata Tume Huru ya Uchaguzi

Uwazi wa hali ya juu

Tayari baadhi ya watu hawa wameshabainisha mafunzo kadhaa ambayo Tanzania inaweza kuvuna kutoka kwenye uchaguzi huo wa Kenya wa Agosti 9, 2022.

Funzo kubwa ambalo watu wengi wanadhani ni muhimu kwa Tanzania kulichukua ni uwepo wa uwazi wa hali ya juu kwenye mchakato mzima wa uchaguzi, ikiwemo kuwepo kwa mfumo ambao mtu yeyote anaweza kuangalia matokeo nchi nzima.

Hili la uwazi lilimfurahisha hata Rais wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa Kiongozi wa Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Matokeo yanapotoka moja kwa moja kwenye kituo yanakwenda hapo kwenye makao makuu ya IEBC na pale yanakwenda kwenye portal ambayo pia na mtu akitaka kwenda kuangalia pale anaangalia na kuchukua rekodi,” alisema Kikwete baada ya kuulezea utaratibu huo kama moja kati ya mambo mengi “ambayo yamekua bora zaidi kuliko uchaguzi uliopita.”

Pia, watu huru pamoja na vyombo vya habari walikuwa na uwezo wa kukusanya, kuhesabu na hata kutangaza matokeo ya awali hata kabla ya tume kufanya hivyo.

SOMA ZAIDI: Wanasiasa, Wanaharakati Wataka Masheha Wapigiwe Kura Zanzibar

Uhuru wa tume

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, ambaye alikuwepo nchini Kenya kama mwangalizi wa uchaguzi huo kupitia taasisi ya Brenthust Foundation, anadhani kwamba uhuru wa tume ya uchaguzi pia ni jambo Tanzania inaweza kujifunza kutoka Kenya.

Akizungumza wakati wa mjadala wa Zoom ulioandaliwa na Nadj Media Centre wenye jina Tanzania Inaweza Kujifunza Nini Kutoka Uchaguzi wa Kenya 2022?, Kabwe alieza jinsi watumishi wa IEBC walivyo huru katika kusimamia majukumu yao, hali aliyoihusisha na namna wanavyopatikana.

“[Makamishna wa uchaguzi] wanaandika barua ya kuomba kazi kama kazi nyingine yoyote,” alisema Kabwe. “Wanafanyiwa usaili wa wazi na Rais anapelekewa majina ya kuteua kutoka kwenye kamati ya uteuzi. Kwa hiyo, unakuwa na watu ambao ni huru.”

Hii ni tofauti kabisa na Tanzania ambapo Wakurugenzi wa Halmashauri, ambao ni wateule wa Rais, ndiyo huwa Wakurugenzi wa Uchaguzi siku za uchaguzi.

Kila wakati wa uchaguzi Tanzania, wakurugenzi hawa hulalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kupendelea chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Lakini pia tume ya taifa ya uchaguzi ya Kenya inawatumishi wake yenyewe katika ngazi za majimbo, katika ngazi za kaunti,” aliendelea kueleza Kabwe.

“[IEBC] hawawatumii watumishi wa umma kama wasimamizi wa uchaguzi,” aliongeza. “Kwenye ngazi za majimbo hawawatumii watendaji wa kata kama wasimamizi wa uchaguzi. Kwenye ngazi za chini pia [ni hivyo hivyo], kitu ambacho ni tufauti na hapa kwetu.”

Matumizi ya teknolojia

Matumizi makubwa ya teknolojia katika shughuli zake za uchaguzi pia ni jambo ambalo Zitto Kabwe anaamini Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa majirani zake wa Kenya.

“Kenya kwa kiwango kikubwa wanatumia teknolojia kwa hiyo kwenye zoezi la uchaguzi linakuwa la uwazi sana kuliko sisi [Tanzania],” anasema Kabwe.

Aligusia namna alivyoshuhudia wasimamizi wa uchaguzi wakiwahimiza mawakala wa vyama wapige picha fomu za matokeo ya uchaguzi.

“Hapa Tanzania hata kuingia na simu kwenye kituo cha kupigia kura hairuhusiwi,” aliongeza mwanasiasa huyo wa siku nyingi.

“Unaweza ukaona tofauti ni kichuguu na mlima Kilimanjaro,” alisema Kabwe. “Kwamba wenzetu unapiga picha na video unachukua. Hapa Tanzania ukiingia na simu kwenye kituo cha kupigia kura unanyan’ganywa hiyo simu.”

Maadili

Susan Lyimo, mwanasiasa wa chama cha upinzani cha CHADEMA, alisema wakati wa mjadala huo ulioandaliwa na Nadj Media Centre kwamba watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wana vitu vya kujifunza kutoka kwa wenzao wa Kenya linapokuja suala la uadilifu.

“Uadilifu wa watendaji wa tume ya Kenya, tunaona kwamba hapa Tanzania pamoja na kuwa na wakala bado unaibiwa kura pale kwenye kituo,” alisema Lyimo.

Hoja yake ilitokana na kauli ya Kabwe kwamba alishuhudia mmoja ya mawakala akirudisha kura aliyopewa kwa bahati mbaya.

“Sasa fikiria wao wakala hayupo lakini kura ya mpinzani wako unasema hapana hii [kura] siyo yangu,” alieleza Lyimo ambaye ameshawahi kuhudumu kama Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA). “Kwa hiyo, unaona kuna uadilifu wa hali ya juu.”

Lyimo alibainisha kwamba wakati wote wa mchakato wa uchaguzi wa Kenya hakuna mgombea aliyeenguliwa kwa kukosea kujaza fomu, au watendaji kufunga ofisi ili wagombea wachelewe kurejesha fomu ili wakose sifa.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo yaliripotiwa sana wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.

SOMA ZAIDI: Jinsi Uchaguzi Mkuu 2020 Ulivyoacha Simulizi za Majonzi Tarime

“Angalia Tanzania jinsi ambavyo wagombea walienguliwa kwa vitu ambavyo havipo kabisa,” Lyimo alisema.

“Haiwezekani useme mtu profesa mzima anaambiwa ameshindwa kuandika,” aliendelea kusema. “Sasa hayo ni mambo ambayo hata kama kuna kasoro basi ni muhimu tukajifunza.”

Mageuzi ya sheria

Mbunge wa Ubungo (CCM) Profesa Kitila Mkumbo alisema kwenye mjadala huo kwamba Tanzania inachangamoto kubwa sana kwenye sheria zinazoongoza uchaguzi, jambo ambalo ni tofauti na Kenya, na kushauri sheria hizo zibadilishwe.

“Tuna changamoto sana kwenye sheria zetu, kwa hiyo tupiganie mabadiliko ya sheria,” alisema Profesa Mkumbo.

“Kwa jinsi ambavyo sheria zetu zipo, mimi nimejaza ile fomu ya uchaguzi, inachosha sana na ilivyokaa ukikosea hata herufi mwenzako akikuwekea pingamizi kisheria anaweza akakuondoa,” alisema Mkumbo. “Ni sheria ambayo haitendi haki kwa wagombea. Ni muhimu ikaangaliwa upya.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *