Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman anadhani takwa la Katiba Mpya halikwepeki ili kuimarisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini, akibainisha mambo sita yanayopaswa kuzingatiwa kwenye mchakato huo.
Othman, ambaye anatoka chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, chama mshirika kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ya Zanzibar, alitoa pendekezo hilo hapo Agosti 18, 2022, mbele ya Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan juu ya kuboresha siasa za vyama vingi nchini.
Mambo ambayo Othman, aliyeanza kutumikia wadhifa huo mnamo Machi 2021, akichukua nafasi ya Seif Sharif Hamad aliyefariki Februari 17, 2021, alitaja suala la Akaunti ya Pamoja ya Fedha na Suala la Benki Kuu kama “masuala muhimu na ya muda mrefu ya kitaifa yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi.”
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Othman Masoud Ni Chaguo Sahihi Kwa Nafasi Ya Makamo Wa Kwanza Wa Raisi
Masuala mengine yanayohitaji ufumbuzi ni: Suala la mipaka ya baharini na suala la Latham Island au kisiwa cha Fungu Mbaraka na suala la nyenzo za uendeshaji wa uchumi wa Zanzibar kama vile kodi ya mapato, biashara ya nje, bandari, rasilimali ya mafuta na gesi na uchumi wa buluu.
Masuala mengine ni pamoja na lile linalohusu hisa za baina ya pande mbili za Muungano katika mashirika ya Muungano huku jengine likiwa ni utendaji kazi vikosi na mahusiano na polisi.
“Uzoefu wa mchakato wa Katiba Mpya (2011 – 2014) umeonesha kwamba tuliingia katika mchakato wa Katiba Mpya bila kupatia ufumbuzi wa masuala haya,” alisema Othman mbele ya kikosi kazi hicho kwa mujibu wa nakala ya wasilisho ambayo The Chanzo imeiona. “Ni muhimu yakapatiwa ufumbuzi kwenye mchakato mpya.”
Akaunti ya Pamoja ya Fedha
Othman amesema kuna haja ya Serikali kulifanyia kazi pendekezo la Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu gharama na mapato ya Muungano na mfumo wa kuchangia na kugawana nakisi na ziada ya mapato ya Muungano baina ya pande mbili.
Serikali pia haijafanyia kazi pendekezo la tume lililohusu haja ya uanzishwaji na uendeshaji wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha zikiwemo kanuni za uendeshaji wa akaunti hiyo iliyoanzishwa kwa lengo la kuweka mfumo bora wa mahusiano ya kifedha baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Mbali ya kutolipatia ufumbuzi suala hilo, Tume yenyewe ya Fedha inaonekana kutoonekana umuhimu wake,” alisema Othman katika wasilisho lake. “Tokea Tume ya Tatu ilipomaliza muda wake Mae 2019, hadi leo bado Tume mpya haijateuliwa.”
SOMA ZAIDI: Othman Masoud: Mapinduzi ya Zanzibar Siyo Milki Ya Wachache
Suala la Benki Kuu
Othman anashauri Serikali ihitimishe mzozo uliopo kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar kuhusiana na madai kwamba Serikali ya Muungano ilizidai fedha za gawio la Zanzibar kutoka Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki baada ya bodi hiyo kuvunjika.
Zanzibar imekuwa ikidai kwamba fedha hizo za gawio za Zanzibar zililipwa moja kwa moja kwa Serikali ya Muungano ambazo walizitumia kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania.
Madai ya Zanzibar yamekuwa kwamba inastahiki kuwa na hisa asilimia 11 katika Benki Kuu.
Serikali ya Muungano imekuwa ikisema kitu hicho hakiwezekani kwani fedha zilizolipwa na Bodi ya Sarafu kwa Serikali ya Muungano kama gawio la Zanzibar hazikutumika kuanzishia Benki Kuu na kwamba sehemu ya fedha hizo za gawio zilirejeshwa SMZ mwaka 1972.
“Vikao zaidi ya 50 vya kutatua suala hili havijafanikiwa kumaliza mzozo huo,” alisema Othman kwenye wasilisho lake. “Ni muhimu tukaingia kwenye machakato mpya wa Katiba Mpya baada ya kulipatia ufumbuzi suala hili.”
Suala la Kisiwa cha Fungu Mbaraka
Othman pia anashauri ufumbuzi wa haraka ufanyike juu ya umiliki wa Kisiwa cha Fungu Mbaraka au Latham Island kama kinavyojulikana kwa kimombo ambacho kimekuwa kikizozaniwa na Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar.
Kisiwa hicho kwa sasa kipo kwenye udhibiti wa Serikali ya Muungano lakini Zanzibar imekuwa ikidai kwamba kisiwa hicho ni miliki yake na hivyo kuomba kiwe chini ya udhibiti wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya jarida la Africa Intelligence ya Julai 27, 2022, watu mashuhuri kutoka Zanzibar hivi sasa wanamshawishi Rais Samia asaidie kurudisha umiliki wa kisiwa hicho kwenye mikono ya Serikali ya Zanzibar.
“Hadi leo suala hilo halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema Othman akitaka ufumbuzi upatikane haraka. “Kila upande umebaki na msimamo wake.”
Uendeshaji wa uchumi wa Zanzibar
Kwa mujibu wa Othman, suala la Zanzibar kukosa mamlaka katika nyenzo kuu za kiuchumi limekuwa moja ya kiini cha mivutano isiyokwisha katika Muungano na kutaka juhudi za makusudi zifanyike kurekebisha hali hiyo.
Othman anasema tatizo limefanywa kuwa kubwa zaidi kwa kukosekana kwa mfumo wa kuziwezesha pande mbili za Muungano kutumia nyenzo hizo kulingana na mazingira yao ya kiuchumi.
Akitolea mfano kodi ya mapato, Othman anasema kuifanya kodi hiyo suala la Muungano kumeikosesha Zanzibar nyenzo muhimu ya uchumi na shindani katika sera na sekta za uchumi.
“Hali hii inaifanya Zanzibar kukosa uhuru wa kusarifu uchumi wake kuvutia mitaji zaidi kupitia mfumo wa kodi ya mapato ambao kwa sasa si rafiki kwa uchumi wa Zanzibar,” alisema Othman.
Hisa kwenye mashirika ya Muungano
Othman anashauri Serikali itekeleze mapendekezo yaliyotolewa na kamati zilizoundwa kutatua kero za muungano kuhusiana na hisa za Zanzibar kwenye mashirika ya Muungano kama shirika la ndege (ATCL), Posta na Simu (TPTC) na baadhi ya taasisi za fedha kama vile Benki ya Biashara (NBC).
“Haya yalikuwa ni mashirika ya Muungano,” alisema Othman kwenye wasilisho lake. “Hata hivyo, baada ya kuja kwa sera ya Parastatal Reform mashirika hayo yalibinafsishwa bila ya kuweka bayana hisa za Zanzibar.”
Kwa mujibu wa Othman, muafaka uliofikiwa ni Serikali mbili zipitie tena upya suala la mgawano wa hisa. Mpaka sasa, hata hivyo, mapitio hayo hayajafanyika, amesema
Utendaji kazi mahusiano na polisi
Othman anataka kuwepo kwa ufumbuzi juu ya mipaka na mahusiano yaliyopo kati ya Jeshi la Polisi na Vikosi vya SMZ.
“Uzoefu wa miaka ya 1995 hadi 2020 umeonesha kwamba mahusiano, mipaka ya kazi na utaratibu wa mashirikiano baina ya Jeshi la Polisi na Vikosi vya SMZ una mapungufu makubwa,” Othman alikiambia kikosi kazi.
“Hili likiwa eneo nyeti la ulinzi, ni vyema kupatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alishauri gwiji huyo wa sheria aliyewahi kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.