The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CCM, Wanaharakati Walaani Vijana Kutoweka Zanzibar. Wataka Hatua Zichukuliwe

Wadau wahusisha matukio ya vijana kutoweka na ukosefu wa fursa visiwani Zanzibar.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Serikali visiwani hapa imeshauriwa kuongeza nguvu kwenye jitihada zake za kuwapata vijana wanaosadikika kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na kudaiwa kujiunga na vikundi vya kigaidi nje ya sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa haki za binadamu mjini hapa pia wameitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi ambazo zitakuza fursa za ajira visiwani hapa ili kuwapunguzia vishawishi vijana vya kutoweka na kutekeleza familia zao.

Wito huo umetolewa huku taarifa zikionesha kwamba vyombo vya ulinzi na usalama visiwani hapa vimeongeza ulinzi kwenye mipaka yake tangu kuibuka kwa taarifa kwamba makumi ya vijana wametoweka kwenye mazingira ya kutatanisha huku familia zao zikidai kwamba vijana hao wanaweza kuwa wamejiunga na vikundi vya kigaidi.

SOMA ZAIDI: Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani

Dk ​​Abdallah Juma Saadalla ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – Zanzibar ambaye ameiambia The Chanzo kwamba chama hicho tawala kimesikitishwa na taarifa za kutoweka kwa vijana hao, akiitaka Serikali iangalie namna ya kukomesha vitendo hivyo.

“Hatuwezi kuishi katika nchi ambayo haitakuwa na utamaduni; hiyo nchi itakuwa ni shaghalabaghala,” alisema Dk Saadalla wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake Kisiwandui, Zanzibar. “Hivi ni vitendo vya kihalifu ambavyo vyombo vya dola vinapaswa kuvishughulikia.”

The Chanzo ilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Yussuf Masauni na kumuuliza endapo kama Serikali inachukua hatua zozote kuhusiana na suala hili ambapo alituunganisha na mtu aliyesema angetupatia majibu. Lakini licha ya kuwasiliana naye kwa takriban wiki nzima, mpaka wakati wa kuchapisha habari hii mtu huyo alikuwa bado hajafanya hivyo.

Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji Zanzibar iliiambia The Chanzo wiki iliyopita kwamba tayari wameanza kutekeleza agizo la Rais Samia la kuimarisha ulinzi visiwani humo, ikiwemo kwa “kuweka ulinzi mkali kwenye mipaka yote inayoizunguka Zanzibar.”

SOMA ZAIDI: Zanzibar Yaimarisha Ulinzi Kufuatia Taarifa za Vijana Kutoweka Katika Mazingira Tatanishi

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zilichapishwa na The Chanzo kwa mara ya kwanza, wazazi waliopoteza vijana wao na wake waliopoteza waume zao wameziangukia mamlaka za nchi ziwasaidie kuwarejesha wapendwa wao ambao wanadhani kwamba wanaweza kuwa wamejiunga na vikundi vya kigaidi.

Taarifa za kutoweka kwa vijana hao ziliambatana na hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama – ikiwemo Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji – kuingozea Zanzibar ulinzi, akisema visiwa hivyo ni “hatarishi” na ni rahisi kwa “usafirishaji haramu wa binadamu,” pamoja na uhalifu mwengine, kutokea.

Ally Saleh ni mwandishi wa habari wa siku nyingi ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa jimbo la Malindi kupitia tiketi ya CUF kutoka mwaka 2015 mpaka 2020. Akiwa mhanga wa janga hili kwa kupotelewa na mpwa wake, Saleh anasema ipo hatari endapo kama jambo hili halitashughulikiwa kwa umakini.

“Kama wanashawishiwa na kwenda kujiunga na makundi hayo ya kigaidi, na hatua madhubuti zitashindwa kuchukuliwa, basi inaweza kutokea hatari ya kiusalama,” anasema Saleh ambaye kwa sasa ni mwanachama wa ACT-Wazaendo. 

“Maana vijana hawa wanaweza kurudi na kuendelea na maisha yao na siku ambayo watahitajika kufanya tukio watafanya hivyo, tukio ambalo linaweza kuwapoteza watu wengi,” anaongeza mwanasiasa huyo na mwanaharakati wa haki za binadamu.

Kupanua fursa za vijana

Lakini baadhi ya wadau wamebainisha kwamba wakati hatua za sasa za kusambaratisha mtandao unaohusika na kuwatorosha vijana hao ni za muhimu, Serikali haiwezi kukwepa wajibu wake wa kupanua wigo wa fursa ambazo vijana wanaweza kuzikumbatia ili wasiwe katika hatari ya kurubuniwa na mtandao huo siku zijazo. 

Dk Mzuri Issa ni Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari  Wanawake (TAMWA) – Zanzibar ambaye anaamini kwamba kukosekana kwa fursa kwa vijana ambazo zingewawezesha kuendesha maisha yao na kutimiza malengo yao kunaweza kuwa kumechangia kutokea kwa taharuki hiyo ya vijana kutoweka kwenye mazingira ya kutatinisha.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO), ukosefu wa ajira ni moja kati ya matatizo sugu yanayoikabili Zanzibar ambayo asilimia 35.3 ya watu wake ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35. 

ILO inaripoti kiwango cha ukosefu wa ajira cha asilimia 21.3 visiwani Zanzibar, huku kiwango hicho kikiwa ni asilimia 65 kwa vijana wa kike na asilimia 43 kwa vijana wa kiume. 

ILO inasema kutokana na janga la UVIKO-19 hali imezidi kuwa mbaya visiwani humo, hususan kutokana na kuanguka kwa sekta ya utalii.

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo UVIKO-19 Inavyoliza Wafanyakazi Sekta ya Utalii Zanzibar

“Mpango wa kuwaangalia vijana kwenye suala la ajira na uwekezaji kwa hapa Zanzibar ni kama haupo,” anasema Dk Issa wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Sasa unakuta vijana wanasubiri sana kupata fursa za kimaisha jambo ambalo linawezekana kabisa kuwa wanashawishika wanaposikia kuna fursa nyengine.”

“Ni lazima Zanzibar, kama nchi, iwe na mkakati wa pamoja katika kuwafuatilia vijana hao na pia kuwepo kwa uimarishaji wa miundombinu ya vijana kuwezeshwa ili waweze kufanya kazi na kupata ajira,” alisisitiza Dk Issa ambaye shirika lake limejikita katika kuboresha ustawi wa vijana, hususan wanawake.

Hoja yake inaungwa mkono na mmoja kati ya wafuatiliaji wakubwa wa maendeleo ya Zanzibar, Awadh Ali Said, ambaye amewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS).

“Vijana wa sasa wana ndoto kubwa, haswa za kimaisha, ikiwa ndoto hizo hazijafikiwa na kuangaliwa kwa ukubwa wake, ndipo inapowezekana watu wengine wakapata nafasi ya ushawishi na kuwarubuni vijana hao,” Said aliieleza The Chanzo

“Mawazo ya kimaisha ni mengi kwenye kutafuta ajira,” aliendelea gwiji huyo wa sheria nchini Tanzania. “[Kijana] hajui lipi ni sahihi na lipi ni baya. Na kwa vile hakuna uangalizi kutoka ngazi ya familia hadi juu ndiyo ndipo hayo ya kutoweka yanapotokea.”

Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts