The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?

Mshindi wa kwanza wa tuzo hiyo anatarajiwa kujishindia fedha taslimu kiasi cha Sh10,000,000 pamoja na kufadhiliwa gharama zote za uchapishaji.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kile kilio cha siku nyingi kutoka kwa jamii ya waandishi bunifu nchini Tanzania cha kuitaka Serikali iwapige jeki ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi hatimaye kinaonekana kupata ufumbuzi baada ya kuzinduliwa kwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu jijini hapa leo, Jumatatu, Septemba 12, 2022.

Waandishi wa riwaya na mkusanyiko wa mashairi, kazi za fasihi ambazo kwa kuanzia ndiyo tuzo hiyo inazilenga, watatakiwa kuwasilisha miswada yao kupitia barua pepe tuzonyerere@tie.go.tz kuanzia Septemba 13, 2022, mpaka Novemba 30, 2022, ambapo baada ya hapo jopo la majaji, manguli wa Kiswahili, litakuwa na miezi mitatu, kuanzia Disemba hadi Machi, ya kuisoma miswada hiyo bila kujua waandishi wake.

Jopo hilo la majaji litakuja na orodha ya washindi 10 ambapo mshindi wa kwanza atazawadiwa fedha taslimu kiasi cha Sh10,000,000; wa pili Sh7,000,000; na wa tatu Sh5,000,000. Mshindi wa nne mpaka wa 10 watapatiwa vyeti maaum vya kuwatambua.

Tuzo hiyo iliyopewa jina la kiongozi huyo wa kwanza wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wake kwenye fasihi itatolewa ifikapo Aprili 13 ya kila mwaka, tarehe ya kuzaliwa ya Mwalimu Nyerere, ambaye pamoja na kuandika vitabu mbalimbali pia ametafsiri kazi kadhaa za fasihi kwenda kwenye Kiswahili.

Mshindi wa kwanza pia atapata bahati ya mswada wake kuchapishwa na kuwa kitabu, huku Serikali ikiwajibika kwa gharama zote za uchapishaji. Baada ya kitabu hicho kuchapishwa, Serikali pia itasambaza nakala zake kwenye maktaba zote za Serikali nchi nzima, kwenye shule zote za sekondari za Serikali na vyuo vikuu vyote vya Serikali.

Siku ya furaha

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa tuzo hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, ambaye wizara yake ndiyo itakayokuwa inaratibu tuzo hiyo, alisema kwamba tayari Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo zima.

“Leo ni siku ya furaha sana, sana,” alisema Profesa Mkenda punde tu baada ya kuchukua kipaza sauti na kuzungumza na washiriki waliohudhuria uzinduzi wa tuzo hiyo. “Na natumaini ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha kwamba tunachochea upya uandishi wa kazi bunifu na usomaji wa vitabu.”

Profesa Mkenda alisema kwamba lengo la Serikali kuja na wazo hilo ni kukidhi matakwa ya wadau ambao wamekuwa wakiiomba Serikali isaidie kuchangamsha soko la uandishi na uchapaji wa kazi bunifu Tanzania.

“Lakini vilevile tunataka tukuze usomaji [wa vitabu],” aliendelea kusema Mkenda ambaye pia ni Mbunge wa Rombo (Chama cha Mapinduzi – CCM). 

“Hata tukisema kuhusu ubora wa elimu, suala jengine ambao sitalizungumzia sana, kwa sababu tuna kazi kubwa sana tunaifanya kwenye mitaala, sera ya elimu nakadhalika,” aliongeza. “Tutazungumza sana, tutabadilisha mitaala na sera tutabadilisha lakini kama watu hawasomi hatutakwenda popote.”

Akitofautisha na nchi nyengine ambazo utaratibu wake wa kutoa tuzo kwa waandishi umesaidia sana kukuza kazi hizo, Profesa Mkenda amelalamika kukosekana kwa tuzo endelevu nchini Tanzania.

Mwanazuoni huyo alibainisha kwamba licha ya kwamba kumekuwa na tuzo zinazoanzishwa nchini kwa nyakati tofauti, tuzo hizo mara nyingi huishia kufa tu, hali ambayo amesema Serikali itajihidi isijirudie kwenye tuzo hiyo iliyozinduliwa leo.

Wakati kwa kuanzia tuzo hiyo itawalenga waandishi wa riwaya na mkusanyiko wa mashairi, Mkenda alisema kwamba huko mbeleni itajumuisha pia hadithi za watoto, tamthilia na hadithi fupi. 

Tunu adhimu

Profesa Penina Mhando, ambaye pia hujulikana kwa jina la Penina Mlama, ni mwenyekiti wa kamati ya tuzo hiyo ambaye wakati wa uzinduzi wa tuzo hiyo alisema kwamba kila taifa ulimwenguni limejiwekea mifumo na nyenzo za kujenga tabia na mitazamo mbalimbali ya watu wake ili watu hao waweze kuishi pamoja, kuthaminiana na kuheshimiana.

Akiitaja mifumo na nyenzo hizo, Profesa Mlama, moja kati ya waandishi nguli wa tamthiliya za Kiswahili Afrika Mashariki, alitaja elimu, mitazamo na amali zinazopambanua tabia nzuri na mbaya; mifumo inayolinda haki za kila mtu; na mifumo ya lugha inayojenga tabia njema. 

“Maandishi bunifu ni moja ya nyenzo hizo na pia ni tunu adhimu kwa taifa lolote lile kwa sababu maandishi hayo hubeba elimu, mitazamo, na amali muhimu zinazojenga misingi ya jamii husika,” alisema Profesa Mlama. 

“Jamii yoyote iliyostaarabika husisitiza usomaji wa maandishi bunifu kwa watu wake tangu wakiwa watoto wadogo kwa kutambua kuwa hii ni nyenzo muhimu ya kujenga jamii yenye kuthaminiwa,” aliongeza Profesa Mlama.

Mwandishi huyo aliielezea hatua ya Serikali kunzisha tuzo hiyo kama “hatua muhimu sana” kwa maendeleo ya Tanzania. 

Ulawiti, ubakaji

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Elimu nchini Dk Lyabwene Mtahabwa alitoa wito kwa waandishi wa kazi bunifu kutumia sanaa yao kukiokoa kizazi cha watoto ambacho amesema kinakabiliwa na changamoto ya visa vingi vya ulawiti na ubakaji. 

“Mmeandika mengi sana kuhusu utunzaji wa rasilimali, kuhusu mahusiano, kuhusu uongozi, kuhusu siasa; mmeandika sana kuhusu harakati za ukombozi, lakini mkumbuke hakuna rasilimali muhimu waliyopewa wanadamu, ikiwemo Tanzania, inayoweza kulinganishwa na thamani ya watoto,” alisema Dk Mtahabwa.

“Naomba muende mtumie kalamu zenu, kikosi hiki cha jeshi la kutumia kalamu, kumpigania mtoto wa Tanzania,” aliongeza afisa huyo mwandamizi wa Serikali. “Kwa kufanya hivyo, nchi yetu itajenga watoto imara, wenye tabia na mitazamo imara [na] nchi yetu itaendelea mbele kwa ushindi.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com. 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Hongera sana ndugu mwandishi kwa habari hiyo njema kwa waandishi.
    Mimi Ni mwandishi wa habari kwa taaluma na mtunzi wa fasihi. Naomba ushirikiano wako kama itakupendeza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *