The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dorothy Semu: Serikali Haipaswi Kucheza na Suala la Chakula

Mwanasisasa huyo anasema maisha kwa sasa yamekuwa magumu kwani CCM “inacheza na chakula.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu amesema kama chama hicho cha upinzani ndiyo kingekuwa madarakani kwa sasa wananchi wasingekuwa wanalalamikia kupanda kwa gharama za maisha kama wanavyolalamikiwa hivi sasa.

Semu, ambaye pia ni Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo, anasema kwamba kupanda kwa gharama za maisha kunakojitokeza hivi sasa kunatokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) “kucheza na chakula,” hali anayosema ACT-Wazalendo ingejaribu kuiepuka kwa nguvu zake zote.

Semu aliyasema hayo hapo Octoba 4, 2022, wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika katika ofisi za chombo hicho cha habari zilizopo Msasani, Dar es Salaam. 

Semu, akiambatana na maafisa wengine waandamini, waliitembelea The Chanzo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea vyombo mbalimbali vya habari. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo:

 

The Chanzo: Dorothy, nyinyi kama chama, kwa mfano, mngekuwa mupo serikalini muda huu, na mnapokea taarifa kama hizi [za kupanda kwa gharama za maisha], kwamba haya ndiyo matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wa Tanzania, ni hatua gani za haraka haraka ambazo Serikali yenu ya ACT-Wazalendo ingezichukua ili kuwaondoshea wananchi mzigo huu?

Dorothy Semu: Asante sana Khalifa, [Said, mwandishi wa The Chanzo]. Kwanza, sisi kama ACT-Wazalendo tunatambua kwamba ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi wake katika hali yoyote ile na kuwawezesha [wananchi] kuishi maisha yenye ahuweni. Mwisho wa siku, Serikali ifanye kila jitihada ili kurahisisha maisha ya wananchi. 

Kwa hiyo, sisi kama ACT-Wazalendo leo hii tungekuwa madarakani, kitu cha kwanza tungehakikisha kwamba tunanunua bidhaa za chakula kupitia Hifadhi ya Taifa ya Chakula. Tunatenga fedha za kutosha kununua chakula kutoka kwa wakulima kwa bei ambayo itamsukuma mkulima kuuzia mfuko wa Hifadhi ya Chakula badala ya kuuza nje [ya nchi]. 

Kinachotokea sasa hivi ni kwamba wakulima wanavutiwa na bei ya juu ya chakula inayopatikana nje ya nchi kuliko bei ya ndani. Lakini pia, wakulima wanaingia gharama kubwa sana za kufanya shughuli zao za kilimo. Hivyo, ni lazima wafidie na watengeneze faida.

Kwa hiyo, kitu kingine cha pili ambacho tungekifanya, tungejaribu kuimarisha bei ya mazao, kuifanya bei iwe himilivu ya mazao kwa kumuwezesha mkulima kwa kumpa ruzuku mbalimbali. 

Kwa mfano, ruzuku ya mbolea [na] ruzuku ya pembejeo ili aweze kuwa na gharama ya chini mazao yatakapopatikana. Lakini ili pia asiingie mfukoni kwa kutoa hela nyingi zaidi kukiwezesha kile kilimo kitokee.

Suala la tatu kupanda kwa gharama za maisha pia kunaenda sambamba na kupanda kwa gharama za mafuta ya nishati, ambayo tumeona yametokea pamoja na sababu nyingi nyenginezo tumeambiwa moja ni vita kati ya Ukraine na Urusi. 

Sisi kama ACT-Wazalendo tungeondoa sehemu ya kodi ambayo inatozwa na Serikali kwenye mafuta ya nishati. Tungeondoa Sh500 ili kuweza kuhakikisha kwamba bei ya mafuta ya nishati ya dizeli, petroni na mafuta ya taa inakuwa himilivu. 

Kwa sababu bei ya mafuta ya nishati inapopanda hapo hapo maana yake ni kwamba mitambo ya kuendeshea viwanda, usafirishaji wa mali ghafi na kila kitu pale tunapokwenda kutoa bidhaa ya mwisho kwenye viwanda au yule yoyote anayechakata anaijumlisha kule. Kwa hiyo, sasa inakuwa inapandisha bei za bidhaa za kila siku.

The Chanzo: Siyo kwamba hizo ni hatua ambazo sasa hivi Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inazichukua?

Dorothy Semu: Hapana. Kwanza tunafahamu kwamba Serikali imekuwa haitengi fedha za kutosha kwa ajili ya ule Mfuko wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua chakula kwa wingi. Ndiyo maana wakulima wanakimbiza chakula nje [ya nchi]. 

Wale [NFRA] wangekuwa na fedha za kutosha wangenunua kutoka kwa wakulima na wakulima wangewapa bei nzuri, maana suala siyo tu kununua ni kuwa bei nzuri.

Bei ya nje [ya nchi] inawavutia kwa sababu ni nzuri, iko juu ukilinganisha na bei ya ndani [ya nchi]. Kwa hiyo, wanashindwa kuhimili kiasi cha chakula kilichopo ndani ina maana chakula kinatoka nje zaidi. Kwa hiyo, kile kilichopo ndani kinakuwa kichache na bei inakuwa tena juu kwa yule mlaji wa mwisho. 

Lakini pia, kwenye upande wa mafuta tulitegemea na tuliishauri Serikali ifanye hivyo. Serikali ya Rais Samia imetuambia kwamba imeweza kupunguza Sh100 tu. Lakini hata hivyo bado tumeona bei imekuwa ikipanda na kushuka haijawa himilivu na wala hatujarudi kule kwenye Sh2,500.

Sisi kama tungekuwa Serikali ya ACT-Wazalendo leo tungelenga bei isizidi Sh2,500. Kwa hiyo, bado unaona bei inaenda Sh3,000, inaenda Sh2,900. Kwa hiyo, bado yule mlaji wa mwisho anayetumia mafuta ya nishati anatoa hela nyingi mfukoni.

The Chanzo: ACT-Wazalendo kusema kweli mmekuwa mstari wa mbele kwenye kutoa mapendekezo kwa Serikali. Tumekuwa tukiona kupitia matamko yenu [na] taarifa zenu. Unadhani ni nini kimeikwamisha Serikali, kwa mfano, kufanyia kazi ushauri, au mapendekezo, ambayo mmekuwa mnayatoa kama chama kwa ajili ya kuwapunguzia mzigo wananchi wa hizi gharama za maisha ambazo wananchi wamekuwa wakilalamikia?

Dorothy Semu: Kwanza, kama ulivyosema, sisi tunatoa ushauri wetu kwa moyo mzuri kabisa tukiamini kuwa ni sehemu yetu sisi kama chama cha siasa makini kutoa sera mbadala, kutoa masuluhisho, na tumekuwa huru kutoa hata saa nyengine kuwa washauri wa Serikali kama wanapenda iwe hivyo.

Upande wa kwanza nafikiri ni hulka labda. Serikali haiwezi kuchukua kila kitu kutoka kwa mpinzani wake. Lakini upande wa pili naamini Serikali yenyewe ina wataalam, na imekuwa ikipima kipi ambacho inaona ni ahueni kwake kutekeleza na katika mapendekezo mengi sisi tunaamini Serikali hii inatakiwa ijifunge mikanda, ihisi, iweze kuona yule mtu wa chini anavyoumia na kuhisi kila siku.

Ninaamini Serikali ingekuwa na sikio lake kwa yule mtu wa chini kama ambavyo sisi chama cha siasa cha ACT-Wazalendo tunavyofanya ingeweza kuona uzito na jinsi ambavyo hali ya maisha imekuwa ngumu wakati gharama za vifaa kila siku zinaendelea kupanda watu wanapata shida na wanashindwa kuhimili.

The Chanzo: Uwezo upo, au utashi, ndani ya Serikali wa kuweza kufanyia kazi? Kwa sababu siyo chama cha ACT-Wazalendo tu ambacho kinatoa mapendekezo. Kuna Asasi za Kiraia, mashirika ya kitafiti, wataalamu wanatoa hayo mapendekezo na ushauri. Unadhani utashi upo ndani ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweza kufanyia kazi ushauri huu au mapendekezo haya kwa lengo la kuwaondoshea wananchi huu mzigo wa gharama kubwa za maisha?

Dorothy Semu: Nauona utashi huo upo, lakini siuoni kama upo kwa asilimia kubwa sana. Inawezekana kuna ushauri tofauti ambao unaonesha mienendo ya kitofauti kwamba ikiwa tutafanya hivi labda uchumi utashuka, labda Serikali itashindwa kusimamia. Lakini zaidi naona ni tishio, au uoga, kwa Serikali kutenda mambo ambayo ni ya kimabadiliko, mambo ambayo hayajawahi kufanyika wakati mwengine hilo ndio ninaloliona zaidi.

The Chanzo: Na hapo mwanzo nilipokuuliza ulitaja hatua ambazo chama chenu, kwa mfano, kama kingekuwepo serikalini hatua za haraka ambazo kingechukua. Lakini unadhani kuna hatua za kimfumo, ambazo pengine kama chama mngezichukua ambazo pia Serikali ya sasa inaweza kuchukua kuhakikisha kwamba hali kama hii pengine haijurudii siku za mbeleni? Kuna hatua ambazo wewe kwa mtazamo wako unaziona kwamba haya ni matatizo ya kimfumo ambayo Tanzania inapaswa iyashughulikie ili kuboresha ustawi wa wananchi wake. 

Dorothy Semu: Asante. Changamoto za kimfumo nafikiria ni nyingi. Nitataja kadhaa. Kwanza, hawa taasisi ya kuhifadhi chakula, hii ni taasisi ambayo inatakiwa itengewe fedha za kutosha kimkakati ili kila wakati iwe na uwezo wa kununa chakula na kukuhifadhi. 

Lakini tunaambiwa kwamba hapo nyuma bajeti yake ilishushwa, ikawekwa zaidi ya nusu. Kwa hiyo, wakawa hawana uwezo wa kufanya hivyo. Kwa hiyo, sisi kama ACT-Wazalendo tukiwa madarakani tutahakikisha kwamba kuna mambo ambayo tungeyawekea wigo na hayataweza kuchezewa. 

Suala la chakula ni suala muhimu kwa taifa, na sisi tunazalisha chakula cha kutosha. Hatuwezi kuhimili tena kuwa na njaa au kuwa na bei ambazo zinaenda zinatetereka na kupanda. Kwa sababu mwisho wa siku anayeumia ni mtu wa kawaida kwenye jamii ambapo wengi wao hawana kipato kikubwa cha namna hiyo.

Suala la pili ni namna ya kumuwezesha mkulima ili aweze kufanya kazi yake ya kilimo kwa ufanisi huku akilindwa na masuala ya mbolea na pembejeo, kuweka ruzuku kwenye pembejeo na kuhakikisha kila mkulima anatambulika na pia kuweka mipango ya kusaidia bei za mkulima ziwe bei ambazo ni himilivu labda hazitashuka kwa kasi au hazitapanda kwa kasi. 

Kumhakikishia huyu mkulima kwamba anapofanya kilimo, anapotoa mazao yake anapata soko na anaweza kujiendesha na akapata faida na wakati huo huo Serikali ikiweza kulisha wananchi wake.

The Chanzo: Nilitaka kukuuuliza kuhusu mchakato unaoendelea nchini hivi sasa ambao unaitwa wa kutafuta maridhiano ya kisiasa kati ya Serikali, Chama cha Mapinduzi na vyama vya upinzani ambao nyinyi ACT-Wazalendo mmeupokea kwa mikono miwili na mmekuwa washirki wake tangu mwanzo mpaka sasa. 

Na moja kati ya vitu ambavyo vinategemewa sana ni kwamba kutafanyika mabadiliko ya msingi ya kisheria na kikanuni ambayo yatahakikisha uchaguzi kuwa huru na haki hapo mwaka 2025. Nilikuwa nataka kukuuliza unadhani hicho ni kitu kinachowezekana? Au unaamini kwamba mpaka tukifika mwaka 2025, Tanzania itakuwa ina mifumo, taasisi, sheria na kanuni ambazo zinafanya chaguzi zake kuwa huru na haki, wewe unaamini hilo?

Dorothy Semu: Ndiyo, tunaamini kwenye hilo, na mimi mwenyewe binafsi naamini kwenye hilo. Kwa sababu tumeiona nia aliyoonesha Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani. Alitupa mkono wa kheri kuona kwamba tumepita kwenye kipindi kigumu chenye changamoto, lakini yupo tayari kufanya kazi na kuboresha hali halisi. 

Na sisi kama chama tumepita kwenye masuala mengi, unafahamu kwa Tanzania, Zanzibar wenzetu wamekuwa wabobezi kwenye masuala ya maridhianiano walipita kwenye changamoto nyingi, changamoto za kususa lakini mwisho wa siku tumeamua kufanya siasa za kukaa chini kuongea na kukubaliana siasa za maridhiano.

Na hili tumelionesha wazi kabisa kwa kushiriki kikamilifu kwenye kikosi kazi kilichoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Tumetoa maoni yetu na tumechangia pia kushawishi kuleta mabadiliko ya aina mbalimbali, tukijua kwamba kama suala, kwa mfano, la kubadilisha sheria ya uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa, sheria ya polisi, zile sheria zote ambazo tunaona ni kandamizi na ambazo zimekuwa kikwazo kwenye kufika uchaguzi huru na hali zinazoweza kuboreshwa ndani ya muda huu tuliokuwa nao. 

Lakini pia tumetoa maoni yetu jinsi ya ambavyo tunaweza kuanzisha na kurudi kwenye barabara ya kutafuta Katiba Mpya, ikiwemo kupitia ile sheria ya Katiba Mpya, kuleta watu wenye weledi ambao wanaweza kuangalia Katiba ile na kusema mawazo mapya ni yapi na mawazo ambayo hayatakiwi ni wapi na kuja kwenye muafaka wa tutoke vipi kwenye suala la kikatiba.

Kwa hiyo, inawezekana Tanzania kupata sheria mpya na inawezekana tukiamua kuwa na uchaguzi mzuri sana wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025 iwapo hii misingi ya sisi na wengine wengi wamependekeza itafanyiwa kazi, itasimikwa kwenye sheria zetu na watu watakuwa tayari kuishi kwenye mabadiliko.

The Chanzo: Na mambo yakienda kinyume na unavyotarajia utajiskiaje?

Dorothy Semu: Ni kwamba ni siasa, nitaona kwamba haukuwepo utashi kamili na yale tuliyoamini hatukupewa mrejesho kamili ambao tuliutegemea. Nitaona labda ni kuhujumiana, au labda ni watu kama walikuwa wanatuchezea akili. Lakini sitaki kujiweka kwenye upande huo. Nataka niamini kwamba yanayosemwa ndiyo yanaenda kufanyika.

The Chanzo: Mheshimiwa Waziri Mkuu Kivuli, kwa mfano, iamuliwe leo uchaguzi mkuu unafanyika mwakani Januari, na wanachama wenu wa ACT-Wazalendo wawambie nyinyi kama chama ni lazima tuingie kwenye uchaguzi mkuu huu tukiwa tumeshirikiana na vyama vingine vya upinzani. Unadhani kuna vyama gani vya upinzani ambavyo ACT-Wazalendo vinaweza kuwa tayari kushirikiana navyo kung’oa CCM kwenye uchaguzi?

Dorothy Semu: Sisi siyo wageni wa kushirikiana kwenye vyama hata 2020 tulionesha nia yetu ya kushirikiana na vyama vyengine. Sisi tunasema tuko tayari kushirikiana na vyama makini vya siasa. 

Tunataka kushirikiana na vyama ambayo kweli vinataka kuleta mabadiliko kwenye nchi hii na kufanya siasa za kweli. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na vile vyama ambayo ni makini. Sitaweza kutaja kwa sababu makini inatokana na ule wakati tuliokuwa nao. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Najjat Omar na kuhaririwa na Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts