Kwa Nini Tanzania Inahitaji Sera Mpya ya Mifugo, Uvuvi?

Serikali inasema sera mpya ni muhimu kwani siyo tu italenga kuongeza idadi ya mifugo nchini bali pia ubora wa mifugo hiyo

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Serikali iko mbioni kuja na Sera Mpya ya Mifugo na Uvuvi kuondokana na ile ya mwaka 2006 ambayo Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Venance Ntiyalundura licha ya kukiri imeisaidia kuboresha sekta hizo, mchango wake kwenye uchumi wa Tanzania “bado uko chini sana.”

Ntiyalundura alitoa tathmini hiyo wakati wa mahojiano maalum aliyoyafanya na The Chanzo hapo Septemba 14, 2022, ofisini kwake, mkoani Dodoma. Kwenye mahojiano hayo, Ntiyalundura alibainisha kwamba sera mpya hailengi tu kuongeza idadi ya mifugo nchini bali pia ubora wa mifugo hiyo.

“Kwa hiyo, tunatamani wafugaji wawe na mifugo bora lakini pia yenye tija,” alisema Ntiyalundura wakati wa mahojiano hayo. “Wafuge kibiashara pia siyo mtu awe na ng’ombe wengi lakini hawatoi mchango wowote katika uchumi. Uchumi wake binafsi na hata uchumi wake kwa taifa pia.”

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo kati ya Ntiyalundura na The Chanzo:

The Chanzo: Mchakato wa kuchukua maoni kuhusu Rasimu ya Sera mpya ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 ulianza lini?

Venance Ntiyalundura: Hasa ulianza Novemba mwaka 2020/2021. Tumekusanya maoni hayo mpaka Julai mwaka huu [wa 2022]. Ndiyo tukawa tumekamilisha sasa kupata maoni ya wadau ambayo yalishawishi kwamba kuna haja sasa ya kufanya marekebisho ya sera hiyo ya mifugo ya 2006.

The Chanzo: Ni changamoto gani ambazo zipo kwenye sera iliyopita ambayo ikapelekea kuwepo kwa rasimu ya sera mpya ya mifugo ya mwaka 2022?

Venance Ntiyalundura: Tumebaini changamoto kadhaa. Moja wapo ni uhaba wa maeneo ya malisho pamoja na maji kwa ajili ya mifugo. Pia, kuna uhaba wa masoko kwa ajili ya mifugo pamoja na mazao yake. Na tulibaini pia kwenye utekelezaji wa sera hiyo [ya mwaka 2006] kulikuwa na ushirikishwaji mdogo wa sekta binafsi na wadau wengine hususan wafugaji.

Halafu, tulikuwa na mifumo ya usimamizi ambayo haijitoshelezi kwa kweli. Na kumekuwa na kasi ndogo ya tafiti ambazo hata hizo chache zilikuwa haziwafikii wadau ipasavyo. Tukaona pia kwamba katika utekelezaji wa sera hiyo kulikuwa na fursa chache za mitaji na huduma ya bima.

Kwa hiyo, wafugaji wetu walikuwa hawapati huduma za bima. Halafu, kulikuwa na uhaba wa mitaji ya kukuza ufugaji wao. Na bado pia, tuna changamoto ya magonjwa ya mifugo. Halafu kubwa lingine kuendelea na mfumo wa ufugaji usio wa kibiashara.

Kwa hiyo, wafugaji weanapendelea kuwa na mifugo mingi haiwapi tija wala kuinua uchumi wao ipasavyo. Tunachangamoto pia ya uhaba na uchakavu wa miundombinu. Lakini pia bado tunaona kwa soko la ndani, na hata nje, bado ulaji mdogo wa mazao ya mifugo umekuwa dhahiri. Kwamba watu bado hawatumii maziwa ipasavyo, hawatumii nyama kwa kiwango kinachoshauriwa.

Kwa hiyo, bado tuna changamoto hiyo na matokeo yake sasa tukaona kwamba sambamba na hilo kwamba tunapowahimiza watu kuwa wale nyama, wanywe maziwa, bado uzalishaji uko chini.

Kuna lishe duni kutokana na uhaba wa nyama na maziwa. Na lingine tumeshuhudia dhahiri mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, changamoto za ukame, uhaba wa maji ndiyo mambo ambayo tumeyaona kwamba bado ni changamoto katika utekelezaji wa sera ya mwaka 2006.

The Chanzo: Ni mambo gani ambayo hayapo kwenye Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 ambayo kwenye Sera hii yapo?

Venance Ntiyalundura: Yapo mambo kadhaa ambayo katika sera ya mwaka 2006 hayakuwemo [na ambayo yamewekwa kwenye sera hii mpya]. Moja wapo kwenye hii Sera ya Mifugo ya mwaka 2022 tumeingiza kipengele kinachoongelea dhana ya afya moja.

Hili linashughulika na kuangalia afya ya wanyama na binadamu kwa kutambua kwamba kuna wanyama wanaishi na binadamu. Lakini pia, mifugo yetu hii, kwa mfano hii tunayoitumia kama kitoweo, inapokuwa katika afya bora watumiaji tunatarajia afya bora pia.

Kwa hiyo, tumeona tujumuishe afya ya wanyama na binadamu. Kwa magonjwa ambayo wanyama wanaweza kuambukiza binadamu nayo tuyazingatie katika sera. Lingine tumejielekeza kujenga na kurasimisha minyororo ya thamani.

Kwa hiyo, tunahitaji mifugo itambulike thamani yake toka ikiwa hai mpaka mazao yake ya mwisho baada ya kutumika. Mathalani kama ni ng’ombe, tutambue thamani ya ng’ombe kuanzia kwato, ngozi, mifupa, damu waliyonayo pembe zake kwamba ni vitu vinaweza vikatumika hata baada ya kupata ile nyama.

Kwa hiyo, ndicho tunacholenga kwamba minyororo yote ya thamani iweze kurasimishwa.

Lakini pia, lingine jipya katika sera hii ni mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, tumezingatia namna ya kushughulika na mabadiliko ya tabianchi kulingana na mazingira tunayo yakabili sasa. Kingine kipya ambacho kimejumuishwa kwenye hii sera mpya ni mikopo kwa ajili ya wafugaji na huduma za bima.

Kwa hiyo, tumeangalia namna ya kukuza wigo wa ufugaji, kupata mitaji pamoja na kupata huduma za bima ili kuweza kushawishi uwekezaji zaidi katika maeneo hayo.

Lingine jipya tumeweka msisitizo wa uhakika wa chakula na lishe. Kwa hiyo, tunalenga uzalishaji uongezeke zaidi ili watu waweze kupata chakula na lishe ili kupambana na utapiamlo, kupambana na hali ya lishe duni kwa nchi yetu.

Na kama unavyofahamu mengi utakuta yaani nyama ni adimu, bei yake iko juu. Lakini hata ukitembelea kwenye sherehe utaona kwenye mlo nyama inaangaliwa sana kwa sababu wengi wana itamani lakini bado haitoshelezi. Kwa hiyo, tunahitaji tuongeze uzalishaji.

Kingine kipya ambacho tumeongezea kwenye hii sera mpya ni kuongeza matumizi ya TEHAMA katika huduma za mifugo na masoko. Kwa hiyo, tunahitaji maafisa ugani waweze kufikia wafugaji kwa urahisi kupitia mifumo ya TEHAMA ili kama anashida yeyote basi kwa kupitia TEHAMA anawasiliana kwa mtandao na mfugaji na hivyo afisa ugani mahali popote alipo anaweza akamsaidia.

Na tunadhani huduma itawafikia wafugaji wengi zaidi kwa kutumia maafisa ugani wachache. Lingine pia, tunaona wafugaji wetu sasa ifike wakati wawe wanapta taarifa katika masoko ya mifugo na mazao yake kwa kutumia TEHAMA ili kabla hajaenda mnadani awe anajua kabisa soko la mifugo liko namna gani.

Kingine cha mwisho ambacho tumekijumuisha katika sera hii ya mifugo ya mwaka 2022 ni hifadhi ya nasaba za mifugo ya asili na bionuani. Kwa hiyo, tunahitaji kuendelea kujifunza ufugaji bora wa mifugo ili tusije kupoteza zile nasaba za asili.

Hayo ndiyo mambo mapya ambayo tumeyajumuisha kwenye hii sera ya mfugo ya mwaka 2022.

The Chanzo: Sera hii mpya italeta manufaa gani kwa wafugaji hapa nchini?

Venance Ntiyalundura: Kwa kweli sera hii itakapokuwa imepitishwa na Serikali kutakuwa na manufaa makubwa sana kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla. Kwa sababu inalenga kuongeza uzalishaji wenye tija wa kibiashara.

Kwa hiyo, itachochea mchango zaidi wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wafugaji pamoja na kuongeza uhakika wa chakula na lishe na kuongeza zaidi mchango wa sekta ya mifugo kwa pato la taifa.

The Chanzo: Matarajio ya Serikali ni yapi kwenye sera hii mpya?

Venance Ntiyalundura: Sawa, Serikali katika hii sera ya mifugo ya mwaka 2022 inatarajia kwamba sasa thamani na ubora wa mifugo itapanda.

Kwa hiyo, kama ng’ombe alikuwa akiangaliwa kwa maana nyama inayotokana na ng’ombe kwamba thamani yake itapanda zaidi maana muuzaji na mnunuzi atamuona ng’ombe kwa mazao yake yote.

Kwa maana ya kwamba, thamani yake itajumuisha hata mbuzi, itajumuisha matumizi ya mifupa, haya ndiyo tunayoyatarajia. Itajumuisha pia matumizi ya kwato na mazao mengine yanayotokana na mifugo hiyo.

Lakini pia, tunatarajia kuwepo ongezeko la mazao ya mifugo katika minyororo ya thamani. Kwa hiyo, hata maziwa yake tunatarajia hatutaishia kuyanywa tu, [pia] tuweze kuwa na mchakato wa kuzalisha matunda zaidi ya kunywa maziwa hayo.

Lakini pia tunatarajia kwamba kupitia sera hii mpya basi tutapunguza hasara ambazo zinajitokeza kutokana na ukame.

Halafu, tunatarajia kukuza uchumi wa wafugaji na uzalishaji wa mazao ya mifugo. Pia, tunatarajia pia kwamba kutakuwa na ongezeko la wafugaji na wazalishaji wa mazao ya mifugo na hivyo kuchangia ajira kwa watanzania.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts