Uraghbishi Ni Nini Na Unaisaidiaje Jamii?

Ni dhana inayohimiza viongozi wa Serikali kuwa na mdomo mdogo, masikio makubwa na macho makubwa.
Na Mwandishi Wetu11 October 202214 min

Dar es Salaam. Jumla ya waraghbishi 150 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walikusanyika jijini hapa kati ya Oktoba 5 na Oktoba 7, 2022, kwa lengo la kuhamisishana, kutatua matatizo kwa pamoja na kufahamiana.

Wakikutana chini ya Twaweza, shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na uwezeshaji wa wananchi kusimamia uwazi na uwajibikaji serikalini, waraghabishi hao walipata fursa ya kuelezea uzoefu wao, changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na mafanikio uraghbishi yamezilitea jamii zao husika.

Ili kufahamu dhana nzima ya uraghbishi na namna jamii inavyoweza kunufaika na shughuli hizo, The Chanzo ilifanya mazungumzo maalum na wataalam wa uraghbishi na waraghbishi mbalimbali pembezoni mwa mkutano huo wa Twaweza uliofanyika katika kituo cha mikutano cha APC, kilichopo Bunju A, Dar es Salaam.

Mwandishi Sammy Awami alisimamia mahojiano hayo. Endelea …  

 

Sammy Awami: Bila ya kupoteza muda naomba nianze na ndugu Aidan Eyakuze, [Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza], yeye ataanza kwa kutuambia uraghbishi ni nini hasa kwa ufupi kabisa lakini kwa nini Twaweza, wakishirikiana na mashirika mengine ya kijamii maeneo mbalimbali nchi, wamekumbatia dhana hii?

Aidan Eyakuze: Asante sana bwana Sammy Awami. Habari za mchana, ndugu wasikilizaji na watazamaji. Niseme tu kwanza kwa kuitambulisha Twaweza, Twaweza ni taasisi ambayo inajaribu kuchochea mambo matatu makubwa.

Jambo la kwanza ni uwazi wa utekelezaji wa mipango ya Serikali. Na uwazi huo unawalenga wananchi ili wananchi wajue ni nini kinafanyika kwa niaba yao na kwa manufaa yao. Pili, ni ushiriki wa wananchi katika maamuzi na ufuatuliaji wa mipango hiyo na utekelezaji huo kwa Serikali. Na tatu, ni uwajibikaji wa Serikali na uongozi na viongozi kwa wananchi.

Sasa hapo sijui kama mmeweza kuzingatia kwamba neno lililojirudia mara tatu ni wananchi. Wananchi wako katikati. Wao ndiyo walengwa wa mambo yote yanayofanywa na Serikali na viongozi kwa niaba yao na manufaa yao.

Kwa hiyo, dhana ya uraghibishi ni kuwaweka wananchi haswa na wao wajitambue kuwa wao wanamaamuzi makubwa, kwamba wao wana uwezo kwa kujipangia vipaumbele. Wao ndiyo wana uwezo wa kudai taarifa na kufuatilia mwenendo wa matumizi ya rasilimali ambazo ni ya kwao. 

Kwa mfano, kodi au ardhi na vitu vingine. Wao [wananchi] ndiyo wanahaki ya kuhoji utekelezaji huo na kuiwajibisha Serikali, iwe Serikali ya kijiji, kata, mtaa, halmashauri hata Serikali Kuu.

Kwa hiyo, uraghibishi ni mbinu, ni juhudi, jitihada ambazo tunashirikiana na taasisi nyingine na wadau wengine hapa Tanzania kuhakikisha wananchi wanalitambua hilo jambo, kwamba wao ndiyo walengwa wakuu na wao ndiyo waamuzi wakuu na wa mwisho. 

Wanalitambua hilo na wanalifanyia kazi na wanatumia hiyo dhana kutatua matatizo yao wao wenyewe na nadhani tutasikia kutoka kwa waraghibishi ambao tumekusanyika nao hapa mafanikio ambayo wanayapata pamoja na changamoto za kuamka kama wananchi kujitafutia maendeleo. Asante sana nashukuru.

Sammy Awami: Sawa nashukuru kwa tafsiri hiyo rahisi kabisa. Sasa kabla sijawapa nafasi waraghibishi nizungumze na Dada Annagrace [Rwehumbiza] ambaye umekuwa ukishughulika na masuala ya uraghibishi kwa muda mrefu. Mtu mwengine anaweza kufikiria kuwa hii mbona kama inafanana na uanaharakati, labda utusaidie utofauti hapo kidogo kwamba uraghibishi utofauti wake ni nini? Kuna utofauti gani na ule wa kupigia kelele labda kutoka suala moja kwenda jengine? uraghibishi unafanya nini tofauti na harakati ambazo tumezizoea?

Annagrace Rwehumbiza: Labda tofauti na harakati ambazo tumezizoea, sisi tunaamini kwamba uraghibishi kwanza hauendi na ajenda kwenye jamii. Tunaamini kwamba jamii ina uwezo wa kukaa chini ikaibua masuala yao ambayo yanawauma wao wenyewe, yanawaumiza wao wenyewe na kuyachanganua na kuyachambua na kuweza kupanga mikakati ni namna gani wanaweza kufuatilia. 

Kwa hiyo, katika kufanya uraghibishi inahusisha watu wengi, makundi mbalimbali, hasa yale makundi ambayo unakuta yamekandamizwa sana na mfumo. Maana haya makundi unakuta yamejenga utamaduni wa ukimya, kukata tamaa, kupuuzia lakini pia usiri unakuwepo mtu asije kuumizwa na nini. 

Kwa hiyo, wao wenyewe wananchi wanasema sasa tunanyanyuka na tunaweza kusema tunafuatilia hiki kitu ikiwemo kushiriki kudai na kuhoji. Tofauti na uwanaharakati ambao kiukweli siwezi kusemea sana hapa kwa jinsi ulivyoiweka lakini bado ni katika kuhoji, kufuatilia [na] kuchanganua masuala yao wao wenyewe na kuamini kwamba wao ndiyo wenye nguvu, wenye maamuzi, lakini pia wenye uwezo wa kushiriki na kusogeza maendeleo yao wao wenyewe mbele.

Sammy Awami: Asante sana. Kwa hiyo, kama nimekupata vizuri, ni kwamba badala ya kuwaambia wananchi pigieni kelele hili, mnawauliza nyie mnasemaje? Mnataka nini? Kitu gani kifanyike, si ndivyo? Asante sana. Nirudi kwa ndugu Hamza hapa. Wewe ni mraghalibishi kutoka Kigoma Ujiji, hebu tuambie uraghibishi huko Kigoma Ujiji unafanyikaje?

Hamza Seleman Mbugamo: Asante sana. Kama alivyonitambulisha kwa jina naitwa Hamza Seleman Mbugamo, ni Katibu wa CBO Waraghibishi Manispaa ya Kigoma Ujiji. Kwa upande wa Kigoma, neno uraghibishi ni neno ambalo limesaidia sana wananchi kwa sababu uraghibishi unahusisha jamii moja kwa moja kwa sababu [Waraghibishi] ndiyo wanaibua, wanafuatilia, wanapanga vipaumbele, nini cha kufanya, kipi kianze na kipi kifuate.

Kwa hiyo, kuna mafanikio mengi yanapatikana kupitia uraghibishi. Mfano, Manispaa ya Kigoma Ujiji tuna kata 19, nitataja tu baadhi ya kata ambazo zina mafanikio kutokana na hii dhana ya uraghibishi. 

Moja wapo ni kata ya Kipampa. Kata ya Kipampa pale kulikuwa na mradi wa maji unatokana na chanzo cha mto Rutale. Hapo awali kile chanzo kilikuwa kinaisaidia kata katika kuendesha maendeleo yao kwa sababu pale kuna tozo, kuna vijana wamejiajiri pale kwa kwenda kuchota maji na kuuza mitaani.

Kwa hiyo, unapokuwa unachota maji pale unalipia Sh500, lakini wananchi wa kawaida ambao hawauzi maji wanachota bure. Kwa hiyo, kupitia hio tozo ambayo wale watu wanauza maji mitaani wanatoa kwa hiyo kata inakusanya na kufanya maendeleo mbalimbali. 

Kwa mfano kupitia chanzo cha mto Rutale tumefanikiwa kujenga vyumba vitano vya madarasa Shule ya Msingi Rutale. Lakini pia kile kile chanzo kinatusaidia kufanya maendeleo mengine. 

Kwa mfano, tulikuwa na ujenzi wa [Shule ya] Sekondari ya Kipampa kwa sababu kata ya Kipampa haina sekondari. Tumefanikiwa. Tulianza na nguvu za wananchi wanaochangia lakini chanzo pia kinatusadia na pia tumepata wafadhili. Kwa hiyo, ni kazi ya uraghibishi.

Tukitoka Kipampa, mfano mwengine ni kata ya Kagera. Kata ya Kagera kule kulikuwa na mradi wa maji ambao hapo awali wananchi walichangia Sh5,000 [kila mmoja] lakini baada ya kuanzishwa mradi wa maji ukaja umejitosheleza, ikaonekana kwamba zile pesa ambazo wananchi wamechangia hazina kazi. 

Ukaitishwa mkutano wa hadhara lakini waraghibishi nao walichangia mawazo kusema kwamba kwa kuwa mradi wa maji umejitosheleza basi tutafute kitu kingine ambacho ni kipaumbele cha wananchi ili tuweze kuzifanyia maamuzi. 

Uliitishwa mkutano kwa sababu tulikuwa na changamoto ya vyoo Shule ya Msingi Kagera, lakini pia tulikuwa na ujenzi wa chumba kimoja cha darasa Shule ya Sekondari Wakulima. Kwa hiyo, wananchi walivyoitishwa wakafanya maamuzi kuwa zile pesa ziende zikafanye kazi wapi.

Lakini baada ya kufanyika kwa ule mkutano wananchi wakapendekeza pesa zikatatue suala la choo kwa sababu ilionekana Shule ya Msingi Kagera haina vyoo. Kulikuwa na matundu mawili yanatumika, choo cha awali kilididimia, lakini pia alijitokeza mfadhili akakubaliana hilo suala. Kwa hiyo, zile pesa zetu zikaendelea kubaki hazina kazi.

Kwa hiyo, mkutano ukafanyika tena, Mheshimiwa Diwani akaita mkutano na wananchi wakazifanyia maamuzi kuwa zile pesa hazikutumika kwenye masuala ya choo kwa hiyo ziende moja kwa moja kwenye masuala ya madawati. Wananchi walikubaliana sasa hivi tumepata madawati.

Sammy Awami: Asante sana. Tunafahamu uraghibishi umefika Maswa pia, hebu tueleze nini kinafanyika Maswa pia, uanze na kujitambulisha kwanza. Asante sana.

Hamisa Sahani: Asante. Kwa jina naitwa Hamisa Sahani nimetokea Maswa, wilaya ya Simiyu kata ya Shanwa mtaa wa Stendi Mpya. Uraghibishi sisi umetufikia. Hivi sasa tumekaribia kumaliza mwaka, kwa sababu umeanza mwaka jana mwezi Oktoba. 

Mpaka hivi sasa tumekaribia kumalizia, tunaushukuru sana uraghibishi kwa sababu tumeona umeturahisishia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanatusibu hapo siku za nyuma, ikiwemo pale kwetu mtaani Stendi Mpya tulikuwa na shida ya mitaro, yaani mitaro ilikuwa ni mibovu, maji hayana pa kwenda mvua zikinyesha. 

Maji yanatiririkia kwenye makazi za watu hayana njia za kupita, ambapo yaende kule yanakotakiwa yaende. Lakini kwa sasa hivi tunaushukuru uraghibishi kwa kuchochea maendeleo na kuamsha wananchi wajue umuhimu wao katika maeneo yao wanayoyaishi, kwamba kuna tatizo gani wao wenyewe waibue, wachanganue ili wanaanze na lipi na wamalize na lipi.

Matatizo waliyoyaibua moja wapo sasa likawa limepewa kipaumbele hilo la mitaro pamoja na kwamba barabara zingine zilikuwa hazijafunguliwa lakini hazipo kwenye ubora. 

Hivyo basi, baada ya tulipofikiwa na uraghibishi tuende tukasome semina ya uraghibishi, baada ya kurudi pale tukawa tumepewa maelekezo tukawa tumejua nini cha kufanya. Kumbe mazingira yanayokuzunguka unapaswa ujue namna yakujikimu nayo endapo kutakuwa na matatizo. 

Baada ya hapa sasa tukagundua sasa kumbe hata matatizo ya mitaro, barabara ambazo bado hazijafunguliwa kumbe tunapaswa tufanyeje kwa ushirikiano wa viongozi ngazi ya mtaa, kata tuliweza kujua nini cha kufanya. 

Hivyo, ilibidi kushirikisha jamii na kuweza kukubaliana kwamba kuanzisha nguvu za pamoja tuweze kuzibua mitaro, tuweze kutengeneza, kuzibua barabara ambazo bado hazijazibuliwa na viongozi nao wakaliitikia na kulipokea kwa namna moja au nyingine na kwa kweli tulifanikisha.

Sammy Awami: Asante sana. Nirudi kwako Dada Teddy, haya masuala ya wananchi kushiriki mikutano, kuibua hoja zao ni masuala ya pembeni tu Dar es Salaam, sisi huku hayatuhusu? Haya masuala [ni] ya kijiji huko sisi tuko bize na maisha, miji mikubwa hatupaswi kufanya hivyo vitu. Uraghibishi upo Dar es Salaam na unafanya nini Dar es Salaam?

Teddy: Kwa kweli hiyo imekuwa ni dhana ya watu wengi kuwa uraghibishi Dar es Salaam haiwezekani, na sana sana ni kuwa watu wa Dar es Salaam wako bize halafu ni miundombinu inayoonekana hata kwenye vyombo vya habari barabara za juu, maji yaani vinaoneshwa vile vitu vizuri vya Dar es Salaam, lakini bado maendeleo yako duni. 

Bado kuna maeneo yaana hizi changamoto ambazo wananchi wenyewe wana uwezo wa kuibua na kusema sasa basi inatosha. Ndiyo tuko Dar es Salaam lakini hatuna maji yanayoonekana huko ni kwamba sisi tunastarehe.

Nikitolea [mfano] upande wa Kinondoni, kwa kweli sisi tumekuwa na tatizo la maji kwa muda mrefu, watu wenye uwezo wanaagiza, lakini wapo wale wenye hali wa chini hana uwezo wa kuagiza maji safi. Kwa hiyo, anakwenda kwenye kidimbwi. 

Kwa hiyo, tulivyofanya ni ule uchokozi wa fikra ndani ya jamii kuwa jamani tusiposimama sisi kama sisi hiki kitu hakitafika. Kwa hiyo, lile vuguvugu la uchokozi wa hiyo fikra tukisimama tunaweza kupata maji kushirikisha sasa wale viongozi wa mitaa. 

Kwanza tuliandika barua mpaka wizarani tukaona hakuna majibu. Kilichofuata mara ya pili ni matumizi ya vyombo vya habari, tuwaite wachukue picha halisi ya huku tunapoishi baada ya kuirusha ile habari ikachukuliwa na vyombo vya habari tukashangaa mradi unakuja ndiyo umefika katikati, pamoja bado kuna maeneo mengine hayajifikiwa lakini maji sasa hivi yako karibu. Lakini nini chachu ya kufika kule ilikuwa ni uraghibishi. 

Yako maeneo mengi Dar es Salaam yanapitia hali kama hiyo, sio maji tu, hospitali, zahanati hakuna, barabara hakuna. Lakini kwa sababu waraghibishi wengi hiyo dhana ya kuwa uraghibishi ni ya watu walioko pembeni, huko Geita, huko vijijini lakini bado Dar es Salaam kuna maeneo watu wanapitia changamoto.

Kwa hiyo, uraghibishi nadhani ni chachu ya maendeleo ya jamii, yanayomilikiwa na jamii husika.

Sammy Awami: Asante sana. Twende kwa kaka mwisho kule. Ukisikia hivi unaona kabisa kwamba nyinyi kama waraghibishi mmekuwa tishio kwa wanasiasa, ni kama mnataka kuchukua kazi zetu [wanasiasa], maanake sisi ndo tunapaswa kwenda kwa wananchi na kuwahamasisha, hii iko vipi katika uzoefu wako? Mnahusiana vipi na viongozi na wanasiasa?

Daniel Peter: Kwa jina naitwa Daniel Peter kutoka wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu, Kijiji cha Gushtana. Kwa kweli ipo changamoto kubwa kati ya waraghibishi na wanasiasa upande mwengine sisi tunapofanya uraghibishi.

Upande mwingine sisi tunapofanya majukumu yetu ya uraghibishi wanasiasa wanatuona kama watu ambao tunawachafulia mambo yao kwa sababu sisi tunachokifanya kinaonekana sana kwenye jamii.

Nikiangalia sisi, au nikitazama kwa upande wa Maswa, sisi wilaya ya Maswa tuna kata 36 na uraghabishi umeweza kufika katika kata 18. Niseme kwamba ni kata kama tatu tu tayari zimefanya kazi vizuri pamoja na viongozi wanasiasa kwa sababu ya kuwa karibuni nao. 

Nichukulie mazingira ambayo mimi ninatoka pale Bushtara, kwa kweli ninaweza kusema kwamba pale mwanzoni wakati tunaipokea hii elimu ya uraghibishi ilitupa shida sana kwa wanasiasa. Kila mahali ambapo tulikuwa tunaenda kuibua [changamoto], kukutana na makundi mbalimbali ya wanajamii kwa ajili ya kiibua [changamoto] ilituingiza katika wakati mgumu kati yetu sisi na wanasiasa.

Baada ya hapo tukaona kumbe ni vizuri mraghibishi akae karibu sana na viongozi ili kupashana zile habari. Tunapojaribu kufanya vile sasa tunawaita wale viongozi ambao tayari wapo kwenye madaraka nikimanisha kwamba Mwenyeviti wa kijiji, Mheshimiwa Diwani na Wenyeviti wa vitongoji tunakaa pamoja kama timu ili kusaidiana pale ambapo ni sehemu ambayo inaweza kuleta utata.

Sammy Awami: Asante sana. Sasa mwengine atakuwa anajiuliza tunasikia ndiyo mraghibishi siyo viongozi, siyo wanaharakati, hawa waraghibishi ni kina nani haswa? Sifa zao ni zipi haswa? Hebu tusaidie Dada Annagrace. Na mtu yoyote anaweza kuwa mraghibishi au mpaka uwe na sifa fulani, unakuwa na sifa gani mraghibishi?

Annagrace Rwehumbiza: Kwanza, nisema mtu yoyote anaweza kuwa mraghibishi kama ameweza kubebe hizi sifa. Kwanza, unamtambuaje mraghibishi? Kama tulivyosema, uraghibishi ni imani na uwezo wa kuona, ni namna unatenda na unatendaje. 

Kwamba, ukiamini kwamba watu wana uzoefu wa pale walipo na siyo ndiyo kusema kila wakati utawaletea maarifa tu. Na hicho ndicho kinachotuangusha mara nyingi, kuamini kuwa tunajua kila kitu na tunaweza kutatua matatizo ya wananchi. 

Watu wanasema masuala ya kijamii ni mapana sana kwa hiyo kila jamii haiwezekani ukatoa suluhisho moja likafanikisha jamii yote hiyo.

Kwa hiyo, kila jamii ina namna yake ambayo ingeweza kushiriki kutatua matatizo. Kwa hiyo, mtu anayebeba imani ya hivyo, kwamba wanajamii wana akili na uzoefu na elimu ya pale walipo na wana uwezo wa kuleta utatuzi wa namna ya kutatua matatizo yao, huyo amebeba fikra za kiraghibishi.

Na kuamini kwamba maendeleo hayaletwi na mtu mmoja tu, huwezi kusubiri kuletewa, kuna hamu, kuna namna ambavyo nyinyi mnaona pale. Kwa hiyo, lazima ushiriki wa wananchi ni kitu cha msingi. Na ushiriki wa wananchi ni wananchi gani, makundi mbalimbali kwenye jamii. 

Kwa sasa hata tunaposema ni nje ya mji ni kijiji, ni kijijini wapi, kwa nani, wakina nani, ni sehemu gani ya kijiji, kwa sababu na umbali wao unatengeneza ukandamizaji au tabaka la namna yake. 

Kwa namna yake na jinsi mtu anavyowekwa mbali ndivyo ushiriki wake unakuwa mdogo unakandamizwa, anatengenezewa utamaduni wa ukimya unatengeneza usiri. 

Anategeneza nini sasa, ili uweze kupata yule anafikiria nini na mawazo yake ni yapi ndo unatumia sasa mbinu za kiraghibishi katika kujaribu kuinua ushiriki wake kuchochea mawazo yake, kuchokoza akili zake, ni namna gani anaweza kushiriki tupate naye mchango wake katika maendeleo. Maana maendeleo ni [mchakato] jumuishi. 

Kwa hiyo, mtu anayebeba hizo sifa ndiyo anakuwa mraghibishi. Kwa hiyo, mimi natamani kuongeza hata viongozi kama wangekuwa wanatumia sifa hizi wangeweza kuwajibishwa na maisha yangekuwa ni mepesi. 

Kwa sababu kuwa kiongozi siyo kwamba ndiyo umekuwa na uwezo, yaani umekuwa na vitu tayari umeshaweza vitu vyote. Hapana. Pata maarifa kutoka kwenye jamii.

Sammy Awami: Kwa hiyo, kwa maneno mengine lile suala, ile hali ya kusikiliza zaidi wananchi wanasema nini? Kuuliza zaidi wananchi wanasema nini na kuwahamasisha nini, huo ndiyo uraghibishi?

Annagrace Rwehumbiza: Maana yake wanasema kusikiliza, kumsikiliza mtu ni kumpa nguvu na mara nyingi sana katika kufanya uraghibishi hicho ndiyo kitu ambacho kinanifurahisha na nasema hicho ni kitu ambacho kinanipa tuzo kubwa sana. 

Unaangalia yale mabadiliko ya mwanamke yule, natolea mfano tu wa mwanamke ambaye hajazoea kuongea mbele za watu mnapofanya uraghibishi. Ndani ya wiki moja unaangalia yale mabadiliko, mtu ambaye alikuwa haongei kabisa sasa leo ana mawazo ambayo wanaweza kujengana ari, ana moyo wa kutaka kushiriki. 

Unaangalia hayo mabadiliko mpaka unabaki unasema kumbe, kwa nini hatushirikishi hawa watu, umeelewa?

Sammy Awami: Naona Aidan Eyakuze amenyoosha mkono, labda kabla hujajibu nikuulize swali halafu utajibu yote. Tunapowafuata wananchi kuwauliza vipaumbele vyao, Serikali inakuwa na vipaumbele vyake pia, kwa hiyo Serikali inapeleka vipaumbele vyake lakini wananchi kumbe nyakati zingine unakuta wana vipaumbele vya tofauti. Hivi vinaoana vipi sasa na uraghibishi? Unataka wanachi wasikilizwe zaidi na Serikali inasema sisi tunajua nini cha kufanya, nini kinahitajika na hicho ndicho tutakachokifanya tunaoanisha vipi haya? Halafu unaweza kuchangia.

Aidan Eyakuze: Nadhani labda nijibu hilo swali kwa kukupa mfano ambao uko nje ya mipaka yetu. Mfano ambao tumeusikia jana kutoka kwa mkurugezi wa mipango na bajeti kwenye Kaunti moja ya Kenya inaitwa Elgeyo-Marakwet. Bwana John alikuwa anatueleza jinsi walivyokuwa wanaoanisha mipango ya Serikali pamoja na vipaumbele vya wananchi. 

Kwanza, jambo la kwanza walikiri wao kama Serikali pale kwamba wanapaswa kuwasikiliza wananchi siyo tu kuwapelekea vipaumbele vya Serikali pasipo kuwa na maoni na mawazo na mchango wa wananchi kuanza kwa hiyo mipango.

Labda Serikali ilidhamiria kujenga barabara lakini wao walikuwa wanataka kitu kingine, labda zahanati, au josho la kupitisha ng’ombe wao ili wapate afya bora zaidi . Kwa hiyo, hilo ni jambo moja Serikali inabidi idhamirie iweke mipango na sera. 

Mpaka wamebadilisha hata sheria ndogo pale kwamba hakuna mpango wa Serikali kupitishwa pasipokuwa na majadiliano na kushirikisha wananchi. Kwa hiyo, hilo ni jambo moja ni la muhimu sana. 

Na pili wamehakikisha kwamba ushiriki wa wananchi unakuwa mpana, kwa sababu wakati mwengine unaweza kukuta kwamba kijiji, mji, mtaa una vigogo pale ambao wao ndiyo wasemaji wa wananchi lakini wamejitwishwa tu hayo madaraka, hao wananchi wa pembezoni, hao wananchi ambao wamekandamizwa wakina mama walemavu hawasikilizwi kabisa. 

Kwa hiyo, na wao wameweka sera, mpango kwamba pale lazima pawepo na ushiriki wa wananchi ambao unajumuisha vijana, walemavu, wazee na kina mama. Bila ya kuwa na hayo makundi manne angalau basi huo mjadala, au maoni, hayajakamilika. 

Kwa hiyo, Serikali inaweza ikafungua masikio. Uraghibishi unasema mdomo mdogo, masikio makubwa, macho makubwa.

Kwa hiyo, ni kuwashauri [na] kuwashawishi washauri wa viongozi wa Serikali kwamba wapunguze saizi ya mdomo wa kusema matamko mengi sana, mipango yetu, tunalifanyia kazi, tumetengea bajeti. 

Jamani tukae chini nyinyi mnasemaje tumeona hili na hili na lingine hivi ni kweli, uhalisia huu ndiyo upo. Sisi tumesikia hili na hili hebu tueleze ni kwa nini? Tuchambue pamoja. Tuibue pamoja masuala halafu pamoja tuchukue hatua. 

Huo mfano tuliosikia huko Kenya unakuja na changamoto zake lakini angalau wamedhamiria kubadilisha mfumo wa uongozi na utekelezaji wa sera za wananchi.

Sisi kama wananchi tunakasimisha mamlaka na madaraka kwa viongozi wetu. Lakini waamuzi wakubwa, wenye mamlaka na madaraka makubwa, ni sisi wananchi. Kwa hiyo, ni lazima tulitambue hilo kama wananchi na tulifanyie kazi kwa maana ya kujihusisha katika maendeleo yetu. 

[Maendeleo] hayatatoka kutoka sehemu nyengine. Sisi [wananchi] je, tunajua shida zetu ni zipi? Vipaumbele vyetu ni vipi? na matumaini yetu ni yapi kwa watoto wetu na wajukuu zetu?

Kwa hiyo, inabidi tusikae pembeni tuletewe mambo kwa sababu watakayotuletea saa nyengine yatatufaa, saa nyengine hayatatufaa tusibaki kunung’unika, tujiingize pale ili tufanye haya mambo. 

Na uraghibishi ni njia moja ya kukumbushana nadhani kwamba tuna majukumu, tuna wajibu kama wananchi, kama waajiri wa Serikali, na waajiri wa viongozi wetu, kujishirikisha na kushiriki katika hayo maamuzi, mipango. 

Kuibua, kuchambua na kuchukua hatua. Hilo ni jambo la msingi sana kwetu sisi kama wananchi. La sivyo, tutabaki pembeni, la sivyo takuwa watazamaji ambao haturidhishwi. Sisi kama wananchi tuna wajibu huo mkubwa na tuna nafasi hiyo kubwa ya kujiletea sisi maendeleo.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Najjat Omar na kuhaririwa na Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved