The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fahamu Baadhi Ya Vumbuzi Zilizofanyika Tanzania 2022

Ni vumbuzi zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Idadi ya Watanzania wanaoendelea kubuni mbinu mpya na za kisasa zinazolenga kutatua matatizo yanayoikabili nchi yao imeendelea kukua kila kukicha wakati ambao taifa hilo la Afrika Mashariki likikabiliwa na changamoto kadhaa za kimaendeleo.

Tukiwa tunaelekea kufunga mwaka wa 2022, The Chanzo inakuletea baadhi ya vumbuzi muhimu zilizofanywa na vijana wa Kitanzania kwa lengo la kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii zetu.

Orodha hii inajumuisha vumbuzi zilizofanyika ndani ya mwaka huu wa 2022 tu, huku zikionesha uwezekano wa umaarufu na uhitaji wake kukua na hivyo kuinufaisha sehemu kubwa ya jamii ya Kitanzania:

Drone isafirishayo madawa ya binadamu

Mwanateknolojia Faidha Hussein, binti wa miaka 24, ndiye aliyevumbua ndege hiyo isiyo na rubani, au drone kama inavyojulikana kwa kimombo, kwa ajili usafirishaji wa madawa ya matumizi ya binadamu, kumwagilia na kutumika katika kusaidia zoezi la uzimaji moto. 

“Kuna maeneo ambayo gari zinazotumika kusafirisha madawa, kwa mfano gari za [Bohari Kuu ya Dawa] MSD zinakuwa haziwezi kufika kutokana na, labda, ubovu wa miundombinu,” Faidha aliiambia The Chanzo

“Ndege yetu inakuwa na uwezo wa kusafirisha madawa hayo kuanzia hapo na kuyafikisha sehemu husika ndani ya muda mchache.”

Faidha ameeleza kwamba muda mwingine watu hulazimika kubeba maboksi ya dawa kichwani kwa muda wa masaa mawili kuyasafirisha, hali ambayo ndege yao inategemea kuitatua kwani ina uwezo wa kurahisisha zoezi hilo kwa kutumia dakika tano tu kwenda na dakika zingine tano kurudi.

Faidha anasema kwamba alipata hamasa ya kufanya uvumbuzi huo alipokuwa amesafiri kuja jijini Mwanza ambapo aliona kuna maeneo kama Ukerewe wanatumia mitumbwi kusafiri. 

“Kuna mama alitakiwa kutoka kijijini alipo kwenda sehemu nyingine kupata huduma, alilazimika kujifungulia hapo kutokana na kukosa huduma ya vifaa, kwa hiyo, alifariki,” anaeleza Faidha.

Wakulima pia kutumia mikono, ama kubeba mgongoni lita 20 za dawa, ni kitu kingine kilichompa Faidha hamasa ya kuvumbua ndege hiyo ambayo itawarahisishia kunyunyizia dawa kwa haraka zaidi. 

“Kwa sasa ndege yetu ina uwezo wa kubeba lita tano lakini kadri inavyoendelea ukomo wa madawa kwa Tanzania ni lita 20, maana yake ni kwamba tutaiongezea uwezo zaidi ndege yetu kufikia kubeba angalau lita 18,” anasema Faidha kwa kujiamini.

Katika upande wa kusaidia zoezi la uzimaji moto, ndege hizo zitakuwa na uwezo wa kubeba mipira ambayo ina hewa yenye uwezo wa kuzima moto. 

“Ufanyaji wake wa kazi ndege yetu ni kwamba ikifika sehemu husika itadondosha mpira,” anaeleza Faidha. 

“Baada ya kudondosha mpira, drone itakaa kwa dakika moja, baada ya hapo huo mpira utalipuka, ambapo kitendo cha kulipuka inatoa hewa inayoweza kuzima moto. 

“Ndege hii ina uwezo wa kutembea kilomita mbili kwa kuendeshwa na rimoti, bila rimoti ina uwezo wa kutembea hadi kilomota 10.”

TWENZAO App

Hii ni app inayomuunganisha mtu mwenye gari binafsi anapokuwa na safari ya kwenda sehemu fulani na abiria mwenye uelekeo huohuo. 

Lengo ni kuweza kumpunguzia gharama za kusafiri mmiliki wa gari, kwa mfano, fidia ya gharama ya mafuta kwa kumpatia mteja ambaye atakuwa ni abiria wake na atamlipa kiasi ambacho watakubaliana. 

Vilevile, kumsaidia abiria kupata usafiri wa uhakika na kwa gharama nafuu.

Amos Mushumbusi, mkazi wa Dar es Salaam mwenye umri wa miaka 30, ndiye aliyevumbua app hii ambaye ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba anaamini itasaidia kuondosha usumbufu unaowakuta madereva na abiria katika safari zao za kila siku.

“Kwa mfano, mtu una safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, huna sababu ya kusafiri peke yako wakati kuna siti zingine hazina watu,” anaeleza Mushumbusi. 

“Vilevile, huna sababu ya kuchukua mtu yoyote barabarani ambaye humfahamu kwa sababu za kiusalama.”

Mushumbusi anasema kwamba TWENZAO inampa mtu uwezo wa kuweka taarifa za safari yake, kwamba unasafiri siku gani na unaelekea sehemu gani. 

TWENZAO imeanza kupatikana Januari 2022, na inapatikana kwa watumiaji wa Android na IOS. 

Vilevile, kwa asiyekuwa na simu janja ana uwezo wa kuipata kwa kutumia kivinjari, au browser kama inavyojulikana kwa kimombo.

Drone inayonyunyizia mazao

Tukulapa Mwalyolo ni mhandisi wa kompyuta, mwenye umri wa miaka 23, anayeishi jijini Dar es Salaam ambaye amevumbua ndege isiyo na rubani yenye uwezo wa kubeba lita tano za dawa na ina uwezo wa kutembea mita 4,900 ndani ya dakika 15 kwa ajili ya kunyunyizia dawa mashambani. 

Kwenye mahojiano na The Chanzo, Mwalyolo alisema kwamba lengo la kuja na aina hiyo ya uvumbuzi ni kuwasaidia wakulima wa Tanzania ambao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali wakati wa kunyunyizia mazao yao kwa kutumia njia za kienyeji, ikiwemo kunyunyizia mazao kwa mkono.

“Mimi ni mtoto wa mkulima, wazazi wangu wanajishungulisha na masuala ya ukulima,” anaeleza mvumbuzi huyo. 

“Hivyo, nikaona jinsi wanavyopata changamoto kwenye suala zima la umwagiaji, nikaona ujuzi nilionao unaweza kufanya kitu,” anaongeza. “Siyo kwao tu, bali hata kwa taifa langu kwa ujumla.”

KISSA App

Hii ni programu ya kuchumbiana iliyovumbuliwa na kijana mwenye umri wa miaka 26 Samwel Lucas, mkazi wa Dar es Salaam, lengo kuu ikiwa ni kutoa elimu ya maambukizi ya VVU/UKIMWI, madhara yake na namna ya kujilinda. 

Teknolokjia hii imeanza rasmi kutumika Januari, 2022.

“Tulianzisha hii programu ili kuweza kuwapata vijana wengi na kuwapa elimu bure ya maambukizi ya UKIMWI,” Lucas anaiambia The Chanzo

“Unapokuwa unatumia programu yetu, kuna taarifa za elimu ya UKIMWI zinakuwa zinatokea hapo juu ya screen ya simu yako,” anasema.

AFYA YA AKILI App

Hii ni programu ya simu yenye uwezo wa kumtathimini mtumiaji kama ana msongo wa mawazo au la iliyoanzishwa hapo Februari mwaka huu wa 2022 na Samwel Lucas ambaye ni muanzilishi wa KISSA App.

Akizungumza na The Chanzo, Lucas amesema: “Application yetu inampa mtu uwezo wa kujitathimini kama ana msongo wa mawazo au hana, kama anao msongo ni kwa kiasi gani, na ikampa ushauri anaweza akafanya kuondokana na msongo wa mawazo.”

Zoezi la kujipima hufanyika kupitia maswali ambayo mtu atakuwa anaulizwa pale atakapotembelea app husika.

Mfumo wa kudhibiti, kulinda vifaa vya umeme

Huu ni mfumo wenye uwezo wa kutumika mahali popote duniani kudhibiti na kulinda vifaa vya umeme majumbani, maofisini, mahospitalini na sehemu nyenginezo. 

Teknolojia hii imezinduliwa rasmi Aprili, 2022. Mussa Charles, kijana mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Dar es Salaam, ndiye mvumbuzi wa teknolojia hii. 

“Hii ni Android Application ambayo mtu anaweza kuunganisha kifaa chake chochote kinachotumia umeme na kuweza kukidhibiti akiwa mbali,” Charles ameiambia The Chanzo

“Mtu anaweza kuunganisha kwa njia ya Bluetooth,” anaongeza mvumbuzi huyo. 

“Kwa mfano, kama kifaa cha umeme kinatumia switch, mtu ana uwezo wa kuzima na kuwasha kifaa chake cha umeme kutokea popote alipo.”

Rahma Salumu ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: salumurahma1@gmail.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *