Zitto Kabwe: Hizi Ndizo Nyimbo Kumi Kali Za Nyumbani Zilizonikosha 2022

Nyimbo hizi 10 ni kati ya nyimbo ambazo zimetolewa kati ya Januari na Novemba 2022 na nimezisikiliza na kuzipenda zaidi.

subscribe to our newsletter!

Hatimaye mnamo nusu ya pili ya mwaka huu wa 2022, nilisaidiwa kujiunga Spotify ili, naamini, ndivyo mke wangu Anna Bwana alitaka, nitumie muda pia kusikiliza muziki badala ya kufanya siasa na kusoma vitabu tu.

Hakika imenisaidia sana, kusema ukweli, nimeweza kugundua tena hobby yangu ya muziki. Nyimbo hizi 10 ni kati ya nyimbo ambazo zimetolewa kati ya Januari na Novemba 2022 na nimezisikiliza na kuzipenda zaidi.

Sikuwa na uchaguzi mkubwa mwaka huu lakini hizi ndizo nyimbo zilizonikosha mwaka huu, 2022:

Huyu Hapa – Mbosso

Huu ni wimbo unaoonesha mapenzi ya dhati ambayo kijana anayo kwa mwenzake lakini amekuwa akiogopa kuyaonesha. Huyu Hapa inakupa hamu ya kuusikiliza kwa namna unavyoanza kwa kicheko.

Mpangilio wa mashairi yake pia umepangwa kwa vina na misemo ya mtaani ambayo inaeleweka kwa watu wa kawaida kabisa. Kwa mfano, Sizi la masufuria halisafishwi kwa jiki.

 

Fire – Zuchu

Huu ni wimbo wenye mdundo mzuri na pia mashairi yenye kuvutia.

Namna mwimbaji anaimba ni kama kuendeleza utamaduni wa mtaani wa kutamba.

Sauti nzuri ya Zuchu na namna anavyopanda na kushuka kutokana na maneno ya mashairi kunaufanya wimbo huu kusikilizika bila kuchoka.

 

Nakupenda – Jay Melody

Unaweza kusema ni wimbo uliopangwa na kupangika. Jay Melody akiwa msanii anayechipukia (nimemsikiliza mara ya kwanza katika wimbo huu) ametoa kibao ambacho itachukua muda mrefu kusahaulika.

Mashairi hayana misemo na methali kama nyimbo nyingi za Kiswahili lakini lugha ya mtaani, lugha ya kitaa, inavutia kuusikiliza.

Huyu ni kijana wa kutazama sana maana kipaji chake ni kikubwa mno.

 

Vimba – Maua Sama

Kuna wasanii ambao wanachukuliwa poa sana, mmojawao ni Maua Sama. Kibao hiki cha Vimba hakichoshi kusikiliza na maudhui yake ni mazuri sana.

Mwimbaji anamhakikishia mpenzi wake kuwa yeye hajali hali yake ya maisha bali amempenda tu na atakuwa naye tofauti kabisa na mwelekeo wa sasa wa dunia ambapo vijana hutazama zaidi uwezo wa mali wa mtu.

Maua ana kipaji kisichoelezeka. Anaimba vizuri na mashairi kupangiliwa vizuri sana. Kinachoshangaza ni kwa nini havumi kwa kiwango anachostahiki katika anga la muziki?

 

Mwambieni – Zuchu

Huu ndiyo wimbo umenifanya nimjue Zuchu, kwa kweli. Sikuwa naujua mpaka nilipofanya safari ya kazi kisiwani Pemba baada uchaguzi mkuu wa ndani ya chama ambapo Mzee Juma Duni Haji alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa.

Nikiwa katika mkutano wa kufungua ofisi za chama mwezi Machi mwaka huu, wimbo huu ukapigwa na ukumbi mzima ukasimama kuimba kwa hamasa, bashasha na kutamba.

Nilipouliza kulikoni, kumbe wanamuimba aliyekuwa mshindani wa Babu Duni. Wasaidizi wakaniambia wimbo wa Zuchu huo. Kabla ya hapo sikuwa nimewahi kumsikia Zuchu.

Nilipoingia Spotify ulikuwa wimbo wa kwanza kuutafuta.

Mwambieni mwambieni, Jimbo lishachukuliwa inagonga kwenye ngoma za masikio na huwa natabasamu kila nikiisikia maana inanijia picha ya wanachama wetu Pemba wakiruka na kuimba na vidole juu!

 

Mtasubiri – Diamond Plutnumz Ft. Zuchu

Huu wimbo unachekesha sana. Kila nikiusikiliza nacheka haswa kwa maneno yake kama:

Wanasema eti umeniroga, hunipendi unanichuna; Wanasema wewe ni kicheche, unanichezea kisha uniache; Ni kweli ila inawahusu nini?

Ni wimbo unaokufanya ujisikie vizuri, unaweza kuusikiliza hata mara 10 bila kuchoka. Ni wimbo wa wapenzi wawili walioshibana kiasi cha kutojali maneno ya watu wengine.

 

Kilometa Ziro – Mwasiti

Huu ni wimbo wa mashairi bora kabisa. Mwasiti anadhihirisha ukongwe wake katika wimbo huu kama ilivyokuwa kwa ule wa Gengeni.

Maudhui yake ya wimbo huu ni mazuri na yenye mafunzo makubwa katika jamii. Natamani Mwasiti aimbe na kuimba zaidi kwani nyimbo zake hazichoshi.

Maji kupwa maji kujaa, haieleweki, anaimba kwenye wimbo huo.

 

Naogopa – Marioo Ft. Harmonize

Naweza kusema kwamba hii ni moja ya nyimbo zilizotulia sana. Marioo ni moja ya vipaji vikubwa katika muziki hapa nchini.

Wimbo huu unawasemea watu wa hali ya chini kabisa ambao wanahangaika na maisha lakini wanaogopa kama wapenzi wao hawatanyakuliwa na wenye mali.

Ni wimbo wa kusikiliza ukiwa umetulia mahala. Lakini hakikisha kuwa riziki yangu ya papatu papatu haikuhusu.

 

Asali – Ali Kiba

Kuna mfalme mmoja tu naye ni Ali Kiba. Kwenye Asali, Kiba ametukumbusha ubora wake kwenye mpangilio wa mashairi.

Kama kulia, nitalia na yeye; Kuimba nitaimba na yeye ni maneno yanayothibitisha mapenzi makubwa kwa umpendaye.

Nikisikia wimbo huu natulia na kupeleka mawazo yangu mbali sana kwa tafakuri.

 

Umeniweza – Ommy Dimpoz

Huu ni wimbo wa kuimbiwa katika shughuli kama siku ya kuzaliwa au kama hiyo.

Kama kawaida, Ommy ana sauti nzuri sana na ameitumia vizuri katika mashairi haya ambayo mpenzi mmoja anamhakikishia mwenzake mapenzi ya dhati.

Kila nikisiliza wimbo huu nashindwa kujizuia kutabasamu kutokana na mpangilio wake wa maneno ya Kiswahili na namna Ommy anavyoyaimba.

 

Zitto Kabwe ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo. Unaweza kumpata Twitter kupitia @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts