The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Siasa za CCM Zilivyoibua Msisimko 2022

Hadhi yake ya kuwa chama tawala nchini Tanzania kunawafanya Watanzania wafuatilie kila nyendo ya CCM.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) siyo chama tawala tu nchini Tanzania bali ni chama ambacho hakijawahi kutoka madarakani tangu taifa hilo la Afrika Mashariki lipate uhuru wake kutoka kwa Mwingereza hapo Disemba 9, 1961.

Hiki ni chama ambacho unaweza kusema kimeishikilia hatma ya Tanzania na ile ya raia wake na ni kutokana na ukweli huo ndiyo maana watu wengi hufuatilia kila kinachotokea ndani ya chama hicho tawala cha pili kwa ukongwe barani Afrika.

Bila shaka utakuwa unafahamu kwamba ni Serikali ya CCM ndiyo inayokusanya kodi na kutunga na kupitisha sera zinazowanufaisha au kuwaumiza Watanzania, ndiyo maana siasa za ndani ya chama hicho huibua msisimko wa kipekee miongoni mwa watu katika jamii.

Mwaka huu wa 2022, CCM imeshuhudia matukio kadhaa ya kisiasa yakitokea ndani yake na kuibua hamasa kubwa miongoni mwa wanachama na wafuasi wake na hata wapinzani wao au watu wasiofuatilia siasa kwa ujumla.

Bashiru na kauli ya ‘Mama anaupiga mwingi’

Tukio la hivi karibuni kabisa ni lile lililomuhusisha Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho Dk Bashiru Ally lililohusiana na onyo la Katibu Mkuu huyo Kiongozi mstaafu kwa wakulima wadogo nchini juu ya kushiriki katika wimbo wa “Mama anaupiga mwingi.”

Bashiru alitoa onyo hilo wakati wa kongamano lililoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kujadili mustakabali wa wakulima wadogo huko Morogoro, Novemba 18, 2022.

“MVIWATA, mkifika hatua za kusema lugha za mnaupiga mwingi, uhai wenu upo mashakani,” Bashiru alisema kwenye kongamano hilo. “Kwa sababu, [MVIWATA] siyo chombo cha kusifu, siyo chombo cha kushukuru.”

Tukitumia lugha iliyozoeleka na wengi, tunaweza kusema kwamba kauli hiyo ya Bashiru ilichafua hali ya hewa ndani ya CCM. Makada mbalimbali walijitokeza hadharani na kumshukia bosi wao huyo wa zamani, wakimtaka afute kauli yake hiyo na aombe radhi.

Kauli hiyo ilizua gumzo kubwa sana kwenye majukwaa mbalimbali ya mijadala kiasi cha kumfanya Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Yussuf Makamba aliibue suala hilo kwenye mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma hapo Disemba 8, 2022.

“Kuupiga mwingi maana yake ni mtu aliyefanya kazi nyingi na kubwa,” Makamba alizungumza kwenye mkutano huo wa CCM, mbele ya Rais Samia. “[Bashiru,] wenzako wakiamua kusema ‘Mama anaupiga mwingi’ tatizo inakuwa ni nini?”

Ni sakata ambalo bila shaka CCM itaingia nalo kwenye 2023, huku likiendelea kubaki kwenye kumbukumbu za wale wanaofuatilia siasa za Tanzania kama tukio muhimu kutokea kwenye siasa za CCM kwa mwaka 2022.

Ndugai na mikopo

Tukio la Bashiru lilikuwa la msisimko, ndiyo, lakini wafuatiliaji wa siasa za nchi hii wataafiki kwamba msisimko huo haukuuzidi ule ulioambatana na kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai iliyohusiana na onyo lake kwamba kuna siku Tanzania itapigwa mnada kutokana na kasi yake ya kukopa.

Unafahamu kilichotokea, sivyo? Kauli hiyo haikumuacha salama Ndugai, ambaye ni Mbunge wa Kongwa (CCM), kwani alilazimika kujiuzulu kwenye nafasi yake ya uspika kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa makada wenzake ndani ya CCM.

Kimsingi, kauli ya Ndugai kwamba Tanzania inakopa kwa kasi ya upepo iliwakera sana makada wa CCM kiasi ya kwamba hata leo wanaendelea kutoa kauli zinazoashiria kukerwa na kauli hiyo.

Mmoja wa watu hao ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwenyekiti wa CCM.

Akizungumza hapo Disemba 20, 2022, baada ya kushuhudia utiliaji saini wa mkataba wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Tabora mpaka Kigoma, Samia alitoa kauli iliyokumbushia sakata la Ndugai.

“Kwa hiyo, wale wanaosema awamu hii imekopa sana [watambue kwamba] ndiyo awamu ambayo imejenga reli yote pia,” Samia alisema kwenye hafla hiyo. “Na tusingeweza kujenga kwa pesa za ndani,ilibidi tukope, tujenge.”

Rushwa chaguzi za ndani CCM

Utakumbuka mwanzoni mwa makala hii tulieleza kwa nini matukio ndani ya CCM huibua hamasa sana miongoni mwa wafuatiliaji.

Ni kwamba wao ndiyo wanaoendesha Serikali kwa sasa, na kwa kufanya hivyo wao ndiyo wanaokusanya kodi na kuwa na wajibu wa kusimamia matumzi sahihi ya hizo fedha.

Sasa ili hilo litimie ni lazima kiwango cha uadilifu kiwe cha juu sana miongoni mwa watendaji wa Serikali, hii ikijumuisha kutokuwepo kwa uvumilivu juu ya vitendo vya ufisadi vya aina yoyote ile, ikiwemo rushwa.

Lakini rushwa ilitawala kwenye michakato ya uchaguzi ya kujaza nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho, hatua iliyopelekea CCM kufuta matokeo ya chaguzi kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikisema inafuatilia kwa karibu madai hayo.

Iwe rushwa ni jambo geni kwenye chaguzi za vyama vya siasa Tanzania au la hiyo haiondoshi ukweli kwamba hili lilikuwa ni tukio kubwa ndani ya CCM lililoibua msisimko mkubwa miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo hapa nchini.

Mkosoaji wa Mwinyi apigwa, atengua kauli

Tukivuka maji na kutupia jicho upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano, tunaona kwamba ndani ya CCM-Zanzibar nako yapo matukio yaliyokihusu chama hicho na kuibuwa msisimko mkubwa miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo visiwani humo.

Moja ya matukio hayo ni lile lililomuhusisha kada wa siku nyingi wa CCM Baraka Mohamed Shamte aliyeshambuliwa mnamo Juni 12, 2022, siku chache baada ya kuikosoa hatua ya Serikali ya Rais Hussein Mwinyi kukodisha visiwa vidogo kwa wawekezaji.

SOMA ZAIDI: Zanzibar Kuendelea Kukodisha Visiwa Licha ya Kuwepo Kwa Ukinzani

Shamte, kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari visiwani humo, aliukosoa vikali uamuzi huo, akienda mbali zaidi na kupendekeza kwamba Rais Mwinyi hastahili kugombea urais kwa muhula wa pili, akisema hana sifa ya kuwa kiongozi wa nchi.

Kufuatia kauli yake hiyo, Shamte alishambuliwa vikali na watu wasiojulikana mpaka kupelekea kulazwa hospitali. Siku chache baada ya kutoka hospitali, kada huyo alinukuliwa kwenye vyombo vya habari akitengua kauli yake hiyo ya awali, na kumuomba radhi Rais Mwinyi.

Mgombea CCM 2025

Kwa ufupi, unaweza kusema kwamba mwaka 2022 haukukiacha salama Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani licha ya matukio haya yapo mengine yanayoashiria kujengeka kwa kambi ndani ya chama hicho, hali iliyopelekea hata Rais Samia kuwafukuza baadhi ya mawaziri kwa kile alichodai wanatumia muda wao mwingi kwa ajili ya 2025.

Hili la nani atagombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025 kupitia tiketi ya CCM lilimalizwa kwenye mkutano wa chama hicho hapo Disemba 8, 2022, ambapo viongozi waandamizi wa CCM, akiwemo Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, walimtoa wasiwasi Rais Samia kwa kumwambia kwamba hakuna atakayejitokeza kumpinga ifikapo 2025.

“Mheshimiwa Rais [Samia], usisikilize porojo za watu, kwamba sijuwi  kijana gani atagombea [2025], sijuwi na mzee gani atagombea, ni upuuzi mtupu,” Kikwete alisema. “Siyo kwamba nasema nawazuia lakini simuoni mwana CCM, 2025, atakayechukua fomu kukupinga.”

Bila shaka ni hakikisho ambalo Rais Samia ataingia nalo mwaka 2023 kwa kujiamini zaidi, akifikiria mitikisiko iliyotokea ndani ya CCM chini ya uenyekiti wake kwa kipindi cha miezi 12 ya 2022.

Hadija Said ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam anayepatikana kupitia hadijasaid826@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *