Zanzibar Kuendelea Kukodisha Visiwa Licha ya Kuwepo Kwa Ukinzani 

Mamlaka visiwani humo zinasema kama kuna mtu mmoja hafurahishwi na jambo linaloweza kunufaisha watu 500, Serikali itaenda na watu 500.
Lukelo Francis27 June 20223 min

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharif Ali Sharif ameeleza kwamba Serikali visiwani humo itaendelea na mipango yake ya kuhakikisha inakodisha kwa wawekezaji baadhi ya visiwa vilivyopo ambavyo vimefanyiwa tathimini licha ya kukiri kuwa kuna watu ambapo wanapinga mpango huo.

Sharif aliyasema hayo hapo Juni 25, 2022, wakati akichangia mjadala ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Watch Tanzania kupitia mtandao wa Zoom ambapo wadau mbalimbali, wakiongozwa na viongozi wa Serikali pamoja na mabalozi, walikutana kujadili maendeleo ya miundombinu na faida za uwekezaji katika visiwa vinavyoizunguka Zanzibar.

“Nakubali kuna watu wanasema kwamba kisiwa fulani hatutaki kiwekezwe,” Sharif alisema wakati wa mjadala huo. “Lakini ukiangalia tija, au sababu anayokupa, siyo ya msingi wala haileti tija ambayo tunaihitaji. Kwa hiyo, tunapotathimini sisi tutakwenda kwenye ile tija kubwa zaidi.”

“Unajua ni imani ya mtu,” aliendelea kueleza Sharif. “Unaweza ukafanya kitu kwa ajili ya watu 500 lakini akatokea mmoja akasema mimi hapana, mimi hili silitaki. Sisi tutakwenda kwa wale watu 500. Sisi zaidi tutaangalia wengi wanataka nini na wengi wanataka maendeleo ya nchi yetu.”

Wakosoaji wa mpango huo visiwani Zanzibar wameubandika jina la “uuzwaji wa Zanzibar kupitia mlango wa nyuma.” Moja kati ya watu waliothubutu kuelezea mawazo haya hadharani, kada wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Baraka Mohamed Shamte, alishambuliwa na watu wasiojulikana siku chache tu baada ya kusema hadhani kwamba Rais Hussein Mwinyi anastahili muhula wa pili.

Kufuatia ukosoaji wake huo, CCM pia ilimfuta uanachama Shamte kwa kile ilichodai ni “kumdhalilisha Rais Mwinyi hadharani.” Wakosoaji wengine wa mpango huo ni pamoja na Balozi Ali Karume, aliyepambana na Mwinyi kwenye kura za maoni za urais ndani ya CCM 2020 na Haji Omar Kheir, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Tumbatu, moja kati ya visiwa vinavyounda Unguja.

Kwa mujibu wa maelezo ya Sharif aliyoyatoa wakati wa mjadala huo wa Zoom, Zanzibar ina julma ya visiwa 52 ambavyo vimefanyiwa utafiti. Kati ya visiwa hivyo vipo ambavyo ndani yake kuna watu wanaishi lakini pia vipo visiwa vidogo ambavyo watu hawaishi lakini vinatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Sharif alisema kwamba jumla ya visiwa 17 vimetangazwa katika awamu mbili tofauti kwa ajili ya uwekezaji endapo kama watafuzu masharti yaliyowekwa. Serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha visiwa vingine vilivyopo vinapata wawekezaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kukuza uchumi, alisema Sharif.

Akizungumza katika mjadala huo Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Ali Jabir Mwadini ameeleza kuwa kuna tabia ya wananchi wa kawaida kuzuiwa kufika katika maeneo ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar, jambo ambalo amesema linashusha hamasa na maendeleo.

“Zanzibar kuna maeneo mengi yameendelezwa, mahoteli makubwa lakini mtu hawezi kufika, kuna kuta kubwa kubwa na ulinzi mkali,” alisema Mwadini wakati wa mjadala huo.

“Uwekezaji kwenye kisiwa usiende kupelekea wananchi kushindwa kufika katika vile visiwa kwa sababu yoyote ile kwa shughuli zao za halali lakini pia kwenda kuona uzuri wa kile kisiwa,” aliongeza. “Wananchi wakifika wanapata hamasa kwamba kumbe kuna mambo mazuri yanayotokea hapa nchini lakini pia wanapata hamasa kumbe mambo makubwa yanawezekana.”

Akizungumzia uwepo wa maeneo mengi ambayo yamezungushiwa mabati visiwani humo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar Dk Khalid Mohammed ameeleza kuwa hiyo ni ishara kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ikiwa ndani yake kuna shughuli za ujenzi zinaendelea.

“Hiyo ni ishara moja kwamba nchi hii kwa sasa ipo katika maendeleo makubwa ya kiuchumi,” alisema Dk Mohammed, akiongeza kwamba ndani ya mabati hayo shughuli za ujenzi wa shule, hospitali, nyumba pamoja na miradi ya sekta binafsi inaendelea.

“Katika Serikali hii ya awamu ya nane kuna ujenzi mkubwa sana unafanyika,” alisema Dk Mohammed. “Hiyo ni ishara moja kubwa sana. Shughuli za ujenzi kila mahali inaonesha wazi kwamba sasa nchi inapiga hatua za kimaendeleo kwa maana ujenzi unafanyika katika maeneo mengi.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Lukelo Francis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved