The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Kifanyike Kuboresha Mfumo wa Kodi 2023?

Baadhi ya mambo waliyopendekeza wadau ni pamoja na kuongeza uwekezaji na kutumia njia rafiki za kukusanya kodi

subscribe to our newsletter!

Wakati tukijongea kuumaliza mwaka 2022, Mamlaka ya Mapato (TRA) inamaliza mwaka huu kwa kishindo .

Kwanza TRA imetoa tangazo juu ya kuanza rasmi utaratibu wa kikodi kwa makampuni ya kidigitali ya nje yanayofanya shughuli zake Tanzania (mfano Facebook, Netflix, Google), pili TRA ilitangaza hatua kubwa ya kuajiri wafanyakazi zaidi ya 2000 kwaajili ya kuongeza nguvu. Tatu TRA imeendelea kukusanya kiwango kikubwa cha kodi kufikia malengo yake.

Katika kufunga mwaka kabisa, jana, Disemba 30, 2022, TRA imebidi kutoa ufafanuzi katika mitandao baada ya malalamiko kutoka kwa mmoja wa mteja wake.

Mteja aliyelalamika ni  Diamond Platnumz, msanii na mfanyabiashara mwenye mamilioni ya wafuasi Tanzania, “TRA wamenifanya kama mkimbizi”, alielezea Diamond akihusisha malalamiko yake na TRA kuweka zuio katika akaunti zake pamoja na kuvamia ofisi zake, “ni kama wanataka kuiua Wasafi”. TRA kwa upande wake walielezea kuona malalamiko hayo na kusema kuwa ni masuala ya ukiukwaji wa sheria za kodi ambayo hawawezi kuyaelezea kwa sababu za kisheria.

Haya mambo manne yanatupa taswira fupi ya kuangalia mfumo wetu wa kodi lakini na nini kifanyike uwe bora zaidi kwa mwaka 2023 na kuendelea.

Lazima kodi zikusanywe

Wakati akihitimisha mkutano mkuu wa 10 wa CCM Rais Samia Suluhu alielezea msimamo wa serikali juu ya kodi ambapo alisisitiza umuhimu wa kukusanya kodi, “Serikali yetu haina mashine ya kurudufua fedha uchapaji wa fedha una kanuni na sheria zake”, alielezea Rais Samia “ili tuweze kutekeleza mipango yetu ya maendeleo lazima tukusanye kodi, lazima tukalipe kodi.”

Huu ni ukweli muhimu kwa kila nchi, kwamba rasilimali kubwa ni watu wake na rasilimali hiyo inakusanywa kupitia kodi. Ukweli huu ni dhahiri zaidi Tanzania, pamoja na kuendelea kukuongeza makusanyo, bado nguvu kubwa inahitajika.

Kwasasa takribani kila shilingi 10 inayokusanywa, shilingi 7 mpaka 9 inatumika kulipa mishahara na mikopo. Shilingi moja mpaka tatu ndio inayobaki kununua dawa, matumizi ya kuendesha ofisi na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.

Makusanyo ya kodi kwa kulinganisha na matumizi muhimu
Makusanyo ya kodi kwa kulinganisha na matumizi muhimu

“Hali hii ya kuendelea kukusanya trilioni 1.3 katika mahitaji ya karne hii kwa kweli haitupeleki mbali” anaeleza mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi Jawadu Mohammed akiongea na The Chanzo, “tunahitaji kuiona mamlaka ya mapato Tanzania walau ikikusanya trilioni 3 kwa mwezi”

Ni kwa jinsi gani tunaweza kubadilisha hali hii, ni muhimu kuelewa uwezo wetu pamoja na vikwazo tulivyonavyo.

Makusanyo sehemu zile zile

Moja ya changamoto kubwa inayoikumba mfumo wetu wa kodi ni kuwa sehemu za makusanyo ni chache sana na mara nyingi ndio hizo hizo zinatolewa macho kuongeza kodi.

“Kwa nchi hii tax base (wigo wa walipa kodi) bado ni mdogo kwa hiyo unawakamua watu wale wale” anaelezea Emmanuel Mvula mtaalamu wa fedha ambaye pia ni Msemaji wa fedha na uchumi wa chama cha ACT Wazalendo.

Kwa sasa sehemu kubwa ambayo serikali imekuwa ikiwa na uhakika wa kukusanya kodi ni pamoja na bidhaa maarufu kama pombe, soda, sigara, mafuta na pia kupitia mitandao ya simu. Ukiondoa mitandao ya simu, bidhaa hizi zimeingiza takribani asilimia 6.85 ya makusanyo yote ya kodi, kati ya 2019/20 na 2021/22, bidhaa hizi zimekuwa zikikumbwa na nyongeza ya mara kwa mara ya kodi.

Bidhaa zinazoingiza mapato makubwa zaidi ya kikodi
Bidhaa zinazoingiza mapato makubwa zaidi ya kikodi (mafuta hayajajumuishwa)

Katika mwaka uliopita 2021/22 na 2022/23, serikali iliweza kuingiza tozo mpya katika mafuta na pia tozo katika miamala ya kielektroniki.

Serikali ilijikuta ikiwa katika wakati mgumu katika sehemu zote, katika tozo za miamala sehemu kubwa ya watu waliacha kutumia miamala ya simu hali iliyopelekea makampuni kama Vodacom kupata hasara. Hata hivyo malengo ya makusanyo ya kodi hayakufikiwa, huku ikikusanywa asilimia 36 tu ya lengo lote.

Katika mafuta serikali ilijikuta katika wakati mgumu hasa baada ya bei ya mafuta kupanda kwa kasi kubwa duniani, huku Watanzania wengi wakihusisha tozo, kodi na ada mbalimbali katika mafuta kama moja ya changizo la bei kupanda.

Upandishaji wa kodi katika maeneo yaleyale huondoa morari ya watu kulipa kodi, lakini pia kwa maeneo yaliyozoeleka kama mitandao ya simu huwa na matokeo hasi ikiwemo katika ujumuishi wa kifedha  kama anavyoelezea Jane Magigita, Mkurugenzi wa taasisi ya Equality for Growth.

“Kutokana na tozo wamama wengi hawaweki pesa kwenye simu wameamua kuzishika mkononi, hii inapelekea wengi kudhulumiwa kwa sababu wanatumia pesa taslimu kufanya malipo”, Magigita aliyasema haya katika wiki ya Azaki iliyofanyika jijini Arusha.

Mwenendo wa makusanyo ya tozo za miamala ya simu/kielektroniki toka Julai 2021 mpaka Septemba 2022
Mwenendo wa makusanyo ya tozo za miamala ya simu/kielektroniki toka Julai 2021 mpaka Septemba 2022

Wadau wanaelezea kuna umuhimu wa kutanua wigo wa kodi na katika hali ya kuzingatia mazingira yaliyopo.

Moja ya jaribio ambalo serikali ililifanya katika kutanua wigo wa kodi ni pamoja na kuanzisha kwa vitambulisho la wafanyabiashara wadogo. Jaribio hili liliweza kuonyesha kodi inapokuwa inaendana na uwezo, na mfumo wa kodi unapoongeza thamani kwa watu, watu hulipa kwa hiari.

Thamani waliyokuwa wanaipata wafanyabiashara wadogo ni kutambulika rasmi, na kutobughudhiwa.  Pamoja na changamoto zilizojitokeza, serikali inaweza kuchukua jaribio lile kama mafunzo na kuboresha hasa kwa kutumia teknologia na kwa kuzingatia ulipaji wa kadri ya uwezo na thamani.

Thamani ni jibu juu ya swali la kwa nini huyu mwananchi mwenye sababu nyingi za kukimbia kulipa kodi aje kulipa kwa hiari, hii ni muhimu hasa kwa wale wafanyabiashara wadogo kabisa.

Eneo lingine ambalo serikali imeangalia katika kutanua wigo wa kodi ni kuleta Kodi ya Kidigitali (Digital Tax), kodi itakayolipwa na makampuni makubwa ya kielektroniki kama Google na Facebook ambao wanakusanya fedha nchini lakini hawana ofisi. Ingawa bado iko katika hatua za usajili, wadau wengi  wanalitambua kama wazo bora linaloendana na nyakati.

Kwa kuangalia nchi na mapana yake, wazo la kutanua wigo wa kodi linatakiwa kukaa katikati ya mijadala ya kitaifa, na lisiachwe kwa wanazuoni wachache au kwa TRA pekee, majibu yapo katikati yetu sisi Watanzania.

Mchango wa mafuta katika kodi
Mchango wa mafuta katika kodi

Uwekezaji na biashara ndio njia pekee ya kupata kodi endelevu

Ukiangalia katika nyakati za hivi karibuni, kipindi ambacho Tanzania ilianza kukimbia katika kasi ya ukuaji wa kiuchumi na kasi ya makusanyo ni kuanzia miaka ya 2011 kuendelea. Hiki ni kipindi ambacho uwekezaji mpya mwingi uliingia nchini.

Ukweli wa kodi ni kuwa huwezi ukautoza kodi umasikini, hata watu wawe na moyo kiasi gani, kama hawana mapato hauwezi kupata kodi. Tuangalie kwa mfano kodi za wafanyakazi, hizi ni kodi ambazo ni za uhakika, na zimekuwa zikichangia takribani asilimia 10 ya kodi zote.

Kwa sasa ni takribani watu milioni 2.6 tu ndio wako katika ajira rasmi, mchango huu mkubwa wa kodi unaweza kuongezeka zaidi kama biashara na uwekezaji vitashamiri nchini.

Mchango wa wafanyakazi katika kodi
Mchango wa wafanyakazi katika kodi

Zaidi sana ukiacha wafanyakazi kodi ya pili kwa kuchangia kodi nyingi zaidi kwa mwaka 2021/22 ni kodi ya makampuni, takribani trilioni 3.2 sawa na asilimia 15 ya kodi yote, nyuma ya kodi ya ongezeko la thamani katika bidhaa zilizoingizwa nchini ambayo ilichangia trilioni 3.3.

Ni muhimu kuvutia uwekezaji mpya nchini kwani ndio njia endelevu ya kuongeza kodi, wadau wanasisitiza kuwa sekta ambazo zina tija kama gesi, madini, viwanda na kilimo miradi yake isiendelee kubaki kwenye makaratasi ianze kufanya kazi.

“Makampuni makubwa ya ndani au ya nje yakiwekeza maana yake serikali itakuwa na maeneo mapana zaidi ya kupata kodi” anafafanua Jawadu Mohamed mchambuzi wa masuala ya kiasiasa na uchumi “hilo litapunguza adha ya serikali kujikita katika maeneo yale yale na pengine kuanzisha kodi nyingi ambazo hutengeneza malalamiko, lakini wakati fulani pia husababisha biashara kudumaa.”

Wadau wengi wamekuwa wakielezea mbinu kama za  kufunga akaunti za wafanyabiashara au kuwatishia katika maofisi yao zinaleta taswira hasi ambayo haivutii uwekezaji na wala kuvutia ulipaji wa kodi.

“Namna ya kuchukua kodi lazima iwe rafiki, mbinu za kufunguka akaunti, kunyang’anya mashine za EFD, kutishiwa kufungiwa biashara sio mbinu zinafanya watu walipe kodi”, anaelezea Emmanuel Mavula, Msemaji wa Fedha na Uchumi ACT Wazalendo.

Hili ni jambo ambalo mwanamuziki Nassibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz alilalamikia jana Disemba 30, 2022, akiongea na Wasafi Media.

“Kama unahisi kuna swali, niite tuzungumze usitumie mabavu kuja ofisini, ni kama kutunyanyasa kwenye nchi yetu wenyewe” alisema Diamond moja ya msanii mkubwa barani Afrika, akielezea mahusiano yake na TRA.

“Halafu mtu atawaza ikiwa mimi mwekezaji wa nchini kwangu nafanyiwa hivyo kwenye serikali hii je mwekezaji mgeni akija atafanyiwa kitu gani?”

Kubadili tabia za walipa kodi

Ulipaji kodi wa hiari bado sio tabia iliyozoeleka kwa Watanzania wengi, kama anavyoelezea Jawadu Mohamed katika mazungumzo na The Chanzo.

“Wengi hudhani kile anachokiuza katika biashara zake chote kinapaswa kuwa cha kwake, kwa hiyo pindi ambapo serikali inataka chochote katika kodi huhisi kama ni sehemu ya kuonewa” anaelezea Jawadu huku akilinganisha desturi ya kutolipa kodi na maradhi.

“Kwa hiyo pia yako maradhi fulani ya kukwepa kodi miongoni mwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamejikusanyia ukwasi mkubwa kwa misingi ya kukwepa kodi na kughushi.”

Bado ni muhimu jitihada za kuendelea kubadili tabia za Watanzania katika kodi. Lakini kuna mambo ambayo yanafanya ulipaji kodi kwa hiari uwe mgumu, inapotokea gharama za kulipa kodi ni kubwa kuliko kodi yenyewe, ni lazima watu watakimbia kulipa kodi.

Mifumo bado ni migumu haswa kwa watu wengi wasio na elimu ya kihasibu na kodi. Ni muhimu ulipaji kodi ukawa rahisi kama menu ya M-pesa au Tigo-pesa, kwamba kwa kubonyeza vitufe kadhaa mtu yeyote anaweza kulipa kodi na akaendelea na biashara zake.

Lakini muhimu zaidi ni uwepo wa uwazi na uwajibikaji juu ya kodi, kama anavyoelezea Emmanuel Mvula, “Wananchi wakiona matumizi ya kodi zao na mahitaji yao yanapatikana watakuwa tayari kulipa kodi ili waweze kupata huduma. Makusanyo na matumizi ya fedha lazima yawekwe wazi.”

Fedha inaenda wapi, inatumikaje na kwanini imetumika hivyo, haya ni maswali lazima yawe wazi kila wakati. Hii itafanya watu kuona uhusiano uliopo wa moja kwa moja na kodi zao.

Matumizi ya teknologia

Moja ya eneo ambalo ni la muhimu ni matumizi ya teknologia, eneo ambalo mpaka sasa lina hatua kubwa zilizopigwa.

Baada ya serikali kuja na ubunifu wa kukusanya kodi za majengo kwa kupitia luku, makusanyo yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 250, huu ulikua ni moja ya mfano mzuri wa matumizi ya teknologia.

Mfumo mwingine ni mfumo wa malipo ya kodi mbalimbali kama VAT, kodi za zuio na kodi ya mapato. Mfumo huu umepunguza foleni zilizokuwa haziishi TRA, hata hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha mfumo kuwa imara. Wadau wengi  wamekuwa wakiulalamikia kuwa mfumo unasua sua na hivyo kuwafanya kuchukua mda mrefu hasa katika tarehe muhimu za malipo.

Wakati mambo yako mengi katika kushughulikia mfumo wetu wa kodi ambayo ni injini muhimu, 2023, tuanze na haya, kwani safari ya hatua 1000 huanza na hatua moja na safari ya siku 365 huanza Januari 01.

Heri ya Mwaka Mpya!

Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *