Mwanza. Mwaka 2023 ni mwaka ambao wadau wa sekta ya kampuni zinazoibukia Tanzania, ambazo kwa kimombo hujulikana kama startups, wanaamini kwamba kampuni nyingi zinazoibukia nchini zitapata manufaa zaidi kuliko ilivyokuwa kwa mwaka jana, 2022.
Siyo kwamba 2022 ulikuwa mbaya kwa tasnia ya kampuni zinazoibukia nchini, isipokuwa wadau katika tasnia hiyo wanaamini kwamba yale maendeleo chanya yaliyojitokeza kwenye tasnia hiyo kwa mwaka huo yataendelea kwa kasi kubwa zaidi kwa mwaka huu wa 2023.
Ili kufahamu mwaka huu wa 2023 utakuwaje kwa sekta ya kampuni zinazoibukia Tanzania, mwandishi wetu Rahma Juma Salumu amezungumza na wadau muhimu katika sekta hiyo na haya hapa ndiyo matarajio yao:
Zahoro Muhaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Kampuni Zinazoibukia Tanzania:
“Natabiri kuongezeka kwa uwekezaji wa mitaji kutoka nje ya Tanzania kwa startups zetu. Pia, mazingira ya kufanyia biashara kuboreshwa kwa startups.
“Kwanza kwenye uwekezaji, startups ambazo zinafanya kazi Tanzania zimeonyesha matukio mazuri ya kukusanya fedha kutoka kwa wawekezaji kutoka nje toka mwaka 2020 mpaka 2022, ambapo kila mwaka tumepata startups ambazo zimepata fedha nyingi, mfano Kopagas, Ramani na zinginezo.
“Pia, mazingira ya biashara yataboreshwa [kutokana na] ahadi ya Serikali ya kuweka sera maalum ya startup, yaani [Tanzania] Startup Policy.
“Tofauti kubwa na mwaka 2022, itakua kwenye startups kujitanua nje ya Tanzania, sababu kuisha kwa UVIKO-19 kunaongeza fursa ya mipaka kufunguka na biashara kuanza kurejea kama kawaida.”
Jumanne Mtambalike, mjasiriamali, Muanzilishi Mwenza wa Sahara Ventures, na mwandishi wa kitabu kipya kiitwacho Diary of an African Hub Manager:
“Nafikiri kuna mwenendo unaondelea ambao ni mwenendo mzuri. Nafikiri mwenendo wa kwanza ambao tunaona ni mzuri ni startups kuweza kufanya ushirikiano na makampuni makubwa.
“Nimeona startup kama Wese ikifanya ushirikiano na Benki ya Equity, tumeona startup kama TUNZAA wameweza kufanya ushirikiano na Tigo. Najua watu wa Gasfasta wako kwenye mchakato wa ushirikiano na Vodacom.
“Kwa hiyo, nadhani mwenendo huu mzuri utaongezeka mwaka 2023. Makampuni mengi makubwa ya simu pamoja na bima na mabenki yatashirikiana na makampuni madogo.
“Mwenendo wa pili [ni kwamba] tumeona hivi karibuni kumekuwa na hamu kubwa ya kufanya uwekezaji kwenye startups na kumekuwa kuna juhudi za sekta binafsi na za umma.
“Kwa upande wa sekta za umma kumekuwa kuna MAKISATU chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) ambayo inatoa fedha kwa wabunifu.
“Vilevile tumeona kwenye upande huo wa sekta za umma kuna mfuko wa watu wa UNDP. Funguo tumeona wanafadhili wabunifu.
“Vilevile tumeona kuna mitandao ya wawekezaji malaika, au angel investors kama wanavyojulikana kwa kimombo, zikianzishwa kama Serengeti Business Angel Network.
“Kwa hiyo, labda ninatabiri kwamba kutakuwa na upatikanaji wa fedha zaidi hasa kwa startups zilizo katika hatua ya awali kwa sababu wanaonekana wadau wengi wana nia njema ya kuweza kushughulikia changamoto za upatkanaji wa mitaji hasa katika hatua za awali.
“Mwaka huu [wa 2022] tumeona makampuni mengi kama Ramani wameweza kukusanya mitaji mikubwa, tumeona kina NALA wameweza kukusanya mitaji mikubwa kutoka nje. Lakini hivi karibuni tumeona na hawa vijana wa Swahilies wamepata pesa kutoka Baobab Network.
‘’Kwa hiyo, hiyo ni mienendo mizuri. Tunategemea mwakani tutasikia zaidi makampuni ya vijana wa Kitanzania wakiweza kukusanya mitaji kutoka kwa wawekezaji wakubwa wa nje, kitu ambacho ni kizuri.
“Nimeona kuna muamko kutoka kwa jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushirikiana na startups na mfumo wa ikolojia wa uvumbuzi Tanzania. Kuna kujitolea sana kwa kuunga mkono startups, kitu ambacho ni kizuri.
“Ukiangalia wenzetu Kenya na Nigeria wanaoishi nje wanacheza nafasi nzuri sana kwenye mfumo wa ikolojia zao. Kwa hiyo, naamini na sisi wa kwetu 2023 wataamka zaidi, tutaona vitu vizuri vikitokea pamoja na ushirikiano.”
“Lakini vilevile kumekuwa na juhudi kutoka upande wa Serikali. Serikali kwa upande wa Zanzibar kuna ile Silicon Zanzibar ambao wanasimamiwa na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi na Serikali.
“Kwa hiyo, naamini tutaona na tutasikia mipango mingi kwa upande wa Zanzibar pia.”
Leyla Mohammed, mdau wa teknolojia na muanzilishi wa Sanuka Kidijitali:
“Tutegemee ongezeko la startups za teknolojia ya hali ya hewa [zaidi 2023]. Startups hizi zitahusika na mambo ya hali ya hewa ambapo watahusisha na teknolojia, yaani ishu za mtandao – web 3 – na teknolojia kama vile apps na mifumo mingine.
“Mfano mzuri tayari kuna startup kama Safisha ambao wanahusika na kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa na kuboresha mazingira.
“Kama Serikali itakuwa tayari imeidhinisha, na kama kutakuwa na sera, ninaona dalili zote za kuongezeka kwa biashara ya crypto [mwaka 2023] kwa sababu wanazidi kujiingiza huko na wanazidi kuielewa zaidi.
“Kutakuwa na startups zinazojihusisha na matumizi ya akili bandia, au Artificial Inteligence, kwa kimombo.
“Tumeona tayari kuna startups kama Neural Tech ambao wanahusika na mambo tofauti tofauti, ikiwemo kutumia bots kutoa huduma kwenye kampuni mbalimbali, ikiwemo mabenki.
Kusiluka Aginiwe, mwanzilishi wa Jukwaa la Startups Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Smartdarasa:
“Naona kuna uwezekano mkubwa wa idadi ya wawekezaji kuongezeka pamoja na uwekezaji kwenye startups za Tanzania kuongezeka.
“Mwenendo wa mwaka 2022 kwa startups ulikuwa mzuri kutokana na mafanikio ya startups zilizopata hela za wawekezaji kama Nala, Swahilies, Tunzaa na wengine wengi.
“Uwezekano wa ongezeko la startups Tanzania ni mkubwa sana, maana taarifa kutoka Tanzania Startups Association zilisema kwamba kutoka mwaka 2020 kwenda 2021, idadi ya startups Tanzania walizozisajili ziliongezeka kwa zaidi ya asilimia 90!
“Mwaka 2023 pia utashuhudia kuongezeka kwa taasisi zinazosaidia startups kama incubators na vichapuzi, ama kwa kimombo accelerators, hasa vyuoni na kuongezeka kwa uelewa wa vijana juu ya kuanzisha startups mbalimbali za kutatua matatizo katika jamii
“Naweza kutabiri kwamba uwekezaji kwenye startups mwaka 2023 Tanzania utakuwa ni zaidi ya asilimia 30 ukilinganishwa na 2022.”
Kelvin Paul, muanzilishi mwenza wa MITz Kits:
“[Mwaka] 2023 utakuwa mwaka mzuri kwa startups Tanzania kwa suala la uwekezaji na ufadhili. Waanzilishi watakuwa tayari kutangaza hadharani mafanikio na changamoto katika mfumo wa ikolojia ili kujenga taswira chanya kwa umma.
“Mwaka 2023 kila chombo cha habari kitatafuta namna ya kuweza kushiriki na kujihusisha na startups, na matukio mengi katika vyuo mbalimbali yatatambulisha na kutangaza chama cha Tanzania startups.
“Tumeona mipango mingi mwaka 2022, tukianza na juhudi za Rais [Samia Suluhu Hassan] kulipeleka taifa katika kiwango kipya [na] kikubwa cha kidiplomasia.
“Kutangaza nchi yetu kama eneo linalowezekana la uwekezaji kutasababisha mikataba zaidi mnamo 2023.”
Judith Mwanri, muanzilishi mwenza wa Hamia Hapa:
“Mimi nadhani mwaka 2023 ni mwaka mzuri maana naona mwaka huu unaoisha mambo mengi sana, mfano startups ambazo zilikuwa changa miaka ya nyuma lakini sasa hivi tumeenda kuomba ufadhili, watu sasa hivi wanaomba ufadhili moja kwa moja kutoka nchi za nje.
“Kwa kweli mwaka unaoukuja utakuwa wa tofauti kwani namna gani watu wanaiona Tanzania ecosystem, kwa sababbu kuna watu ambao wamepata ufadhili mfululizo mara tatu au ya nne sasa hivi.
“Tofauti na ile mtu alikuwa akiangalia Afrika anaona kuna wale wanajiita KENGS ambao ni Kenya, Nigeria, Ghana na Afrika Kusini. Kwa hiyo, mtu alikuwa akiangalia Afrika anawaona hao KENGS.
“Lakini sasa hivi Tanzania ni nchi ambayo kwa sasa hivi watu wameanza kuiangalia kwa sababu imeweza kujionesha kimataifa.”
Ashura Babi, muanzilishi mwenza wa GigSpace:
“[Mwaka 2023] kutakuwa na startups bora na endelevu zaidi.
“Kutokana na uzoefu wangu, kama mwazilishi wa Gigspace, [iliyozinduliwa] miaka miwili iliyopita, nimeona utafouti mkubwa ambao unatia moyo kwenye maswala ya teknolojia na watu kutumia teknolojia kujipatia kipato, inatia matumaini zaidi tukielekea mwaka 2023.
“Vijana wamekua wakichacharika sana 2022, wakijfunza na kujiunga na mijadala yenye tija kuhusiana na maendeleo ya kiteknolojia na namna wanavyoweza kujiendeleza kupitia teknolojia. Nadhani hiyo itaendelea 2023.”
Rahma Juma Salumu ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mwanza, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia barua pepe salumurahma1@gmail.com.