Apigania Haki Yake ya Ardhi Kwa Miaka 36 Bila Mafanikio

Ni raia wa Trinidad na Tobago aliyekuja Tanzania miaka ya 1980 anayemuomba Rais Samia aingilie kati.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Raia mmoja wa Trinidad na Tobago anayejulikana kwa jina la Keith Linton Smith amemuangukia Rais Samia Suluhu Hassan akimtaka aingilie kati kwenye juhudi zake za kudai ardhi yake anayodai kudhulumiwa ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miaka 36 sasa bila mafanikio.

Smith alitoa wito huo mara ya kwanza alipotembelea ofisi za The Chanzo zilizopo Msasani, Dar es Salaam hapo Disemba 16, 2022, akiambatana na binti yake Malaika Bergonzoli ambapo, kwa pamoja, walimsihi Rais Samia aingilie kati wakisema ni yeye tu aliyebaki anayeweza kuwasaidia.

Ardhi ambayo Smith anadai kudhulumiwa ipo kwenye eneo lililokuwa likijulikana kama Ndamakai Coffee Estate, lenye ukubwa wa hekari 1750, linalopatikana katika eneo la Oldean, mkoani Arusha. Shamba hilo ambalo kwa sasa haijulikani lipo kwenye milki ya nani linajulikana kama Acacia Hills.

“Nimetembea katika ofisi nyingi za Serikali kutafuta msaada juu ya jambo hili bila mafanikio yoyote, hadi nimechoka,” Smith, 72, ameieleza The Chanzo. “Nipo hapa kuomba kuonana na Rais Samia kwa sababu yeye ni mtu pekee anayeweza kunisaidia nipate haki yangu.”

Alipoulizwa kuhusu kesi hiyo ya Smith, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula aliieleza The Chanzo kwamba hafahamu lolote kuhusiana na kesi hiyo, akiongeza: “Kesi hiyo haijanifikia.”

Kwenye maelezo yake kwa The Chanzo, Smith alisema kwamba tayari ameahidiwa kuonana na Rais Samia, kitu kilichothibitishwa na afisa wa Ikulu anayehusika na kuratibu mkutano huo kwa mwandishi wa habari hii, akisema mlalamikaji huyo yupo kwenye foleni ya watu wanaoomba kuonana na Mkuu wa Nchi.

Mgeni wa Mwalimu Nyerere

Kwa mujibu wa maelezo yake, Smith alikuja nchini Tanzania kwenye miaka ya 1980, akiwa ni sehemu ya watu wengi wenye asili ya Kiafrika walioamua kuhama kwenye nchi mbalimbali walizokuwepo na kuja kuanzisha makazi nchini Tanzania.

Watu hao, wengi wao wakitokea nchi za Amerika Kaskazini, Amerika Kusini na Caribbean, wakiwa ni vizazi vya watu waliosafirishwa kwa nguvu kutoka Afrika na kupelekwa utumwani kwenye maeneo hayo, walikuja kuishi Tanzania kwa mualiko wa Rais wa kwanza wa taifa hilo Julius Kambarage Nyerere.

Smith anadai kwamba alipofika nchini Tanzania alianzisha makazi yake huko Arusha na kufanya kazi na kupata kipato kilichomuwezesha kununua ardhi hiyo kutoka kwa familia moja ya Kihindi kwa makubaliano ya kulipa kidogo kidogo mpaka pale alipofanikiwa kumalizia malipo na shamba hilo kuwa la kwake.

SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama

Wakati akiendelea kufanya shughuli mbalimbali katika shamba hilo, Smith alijikuta matatani baada ya kumuua mtu aliyekuwa amevamia shamba hilo akiwa na wenzake wenye silaha za jadi kwa lengo la wizi, kesi iliyomfanya atumikie kifungo cha miaka saba katika magereza mbalimbali ya nchi.

Baada ya kumaliza kutumikia kifungo hicho, Smith aliamuriwa aondoke nchini Tanzania ambapo alikwenda kuishi nchini Marekani. Smith aliweza kurudi nchini Tanzania kwa kibali maalum hapo mwaka 2017 na kufuatilia umiliki wa shamba lake tangu hapo bila mafanikio yoyote.

“Mimi nataka haki zangu, nataka nyumba yangu irudi kwangu. Kama hawataki kunipa, na wanaamini Mzungu ni muhimu sana kuliko mimi, basi wamwambie Mzungu anilipe, wamwambie anilipe fidia,” Smith aliiambia The Chanzo.

“Nipe sehemu, shambani huko, ambayo naweza kuiita nyumbani,” aliongeza Smith. “Kwa sababu kilichonileta kwenye nchi hii ni kuishi, kuwa na sehemu ambayo naweza kuiita nyumbani. Kwangu, Tanzania ni nyumbani.”

Juhudi za kidiplomasia

Kwa mujibu wa uchambuzi wa nyaraka mbalimbali uliofanywa na The Chanzo, kesi hiyo imekuwa ikienda kwa miaka mingi sana, ikihusisha viongozi waandamizi wa Serikali za Tanzania na Trinidad na Tobago bila kupatiwa ufumbuzi wowote.

Kwa mfano, kwenye barua yake ya Machi 28, 2008, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Trinidad na Tobago Paula Gopee-Scoon alimuomba aliyekuwa Rais wa Tanzania wa wakati huo Jakaya Mrisho Kikwete kumsaidia Smith kupata haki yake hiyo.

“Juhudi zetu za pamoja za kutafuta ufumbuzi wa jambo hili mpaka hivi sasa [2008] hazijazaa matunda, hali inayonifanya nitafute msaada wako kwenye suala hili,” Gopee-Scoon alimueleza Kikwete kwenye barua yake hiyo.

SOMA ZAIDI: Mjane wa Katibu wa Zamani wa Bunge Anayepigania Haki Yake kwa Miaka 23

Aliyekuwa Mbunge wa Karatu (CHADEMA) Dk Willibrod Slaa aliwahi kuiibua kesi ya Smith bungeni, akilalamika kwamba kuchelewa kupatiwa ufumbuzi kesi hiyo “kunalichafua jina la Tanzania kimataifa,” akiitaka Serikali kulitolea ufafanuzi suala hilo.

Wakati akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Helen Kijo-Bisimba alijaribu kulishughulikia suala hilo, ikiwemo kumuandikia Rais Kikwete kuingilia kati, akisema kwamba kwa hatua ambayo kesi hiyo imefikia ni Ikulu tu ndiyo inayoweza kuipatia ufumbuzi.

“Ni muhimu kukuandikia, Mheshimiwa Rais, kwani naamini kwamba haki inahitajika kutendeka na wewe upo kwenye nafasi ya kuhakikisha hilo linatokea,” Bi-Simba aliandika kwenye barua yake hiyo ya Septemba 23, 2008, ambayo The Chanzo imeiona.

Licha ya juhudi zote hizi, Smith bado hajafanikiwa kupata haki yake hiyo.

Kasoro mfumo wa utoaji haki

The Chanzo ilimuuliza Bi-Simba, mwanaharakati wa siku nyingi wa haki za binadamu, kwa nini anadhani imechukua muda wote huu bila Smith kupata haki yake, ambapo alisema ni kutokana na kasoro zilizopo kwenye mfumo wa nchi wa utoaji haki.

“Kuna shida sana kwenye mifumo yetu ya kisheria sana, sana,” alisema Bi-Simba. “Siyo kesi hiyo tu. Zipo kesi nyingi tu ambazo haziendi kwa wakati kwa sababu pia saa nyingine naona hawa waliopo kwenye ofisi hawazitilii maanani hizi kesi.”

SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania

Alipoulizwa ni nini angependa kumuambia Rais Samia, mtoto wa Smith, Malaika Bergonzoli, alisema: 

“Ningependa kumwambia Rais kwamba Tanzania inahitaji haki na baba yangu amekuwa akipigania haki yake kwa kipindi kirefu sana na ni wakati muafaka sasa kwamba Tanzania inahitaji kujua kuhusu wale wanaosababisha uhalifu na wale ambao ni waathirika kwa sababu baba yangu ni muathirika,” alisema Malaika.

“Kwa nguvu zake alizonazo kama Rais, [Samia] anaweza kuona ni kwa namna gani baba yangu amedhalilishwa na anaweza kuwa shujaa wa hadithi hii [kwa] kumsaidia baba yangu kupata kile anachokihitaji, kile anachokimiliki na kile anachostahiki,” alisema binti huyo wa Smith.

 

Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts