The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dk Elisha Osati: Bima Itakuwa na Manufaa Pale Wote Tutakapochangia

Anasema huduma zitakuwa bora kwani watu wengi watakuwa wanachangia kwenye huduma hiyo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Elisha Osati amewatoa hofu wananchi kuhusiana na mpango wa bima ya afya kwa wote, akisema kwamba bima hiyo itakuwa tofauti na ya sasa kwani watu wengi wakichangia itaongeza wigo wa huduma watu hao watapata kutoka vituo vya kutolea huduma.

Dk Osati, ambaye amewahi kuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), alieleza hayo kwenye mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika hapo Januari 26, 2023, jijini Dar es Salaam.

“Watu wamekuwa na uoga kwamba wameona, kwa mfano, bima yetu ambayo tunayo hivi sasa, [Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya] NHIF wakati mwengine mtu anaenda hospitali lakini anakosa dawa, au matibabu, fulani.

“Lakini nataka ieleweke kwamba hali hii inatokana na wanaochangia hivi sasa NHIF ni watu wachache, ni asilimia nane tu ya Watanzania. Lakini hiyo ndiyo inahudumia jamii nzima kwa kiasi kikubwa.

“Hospitali zetu zinategemea mapato ya NHIF kwa asilimia 70. Mimi nafikiri, tukiweza wote kuingia kwenye bima ya afya kwa wote, tukiweza kuingia kwenye mpango huu, maana yake fedha zitakuwa ni nyingi. Sasa hivi tunapata tabu kwa sababu fedha ni kidogo wakati wanaotaka huduma ni wengi,” alisema Dk Osati.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii?

Serikali inategemea kuwasilisha kwenye Bunge litakaloanza Januari 30, 2023, Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote baada ya kuahirishwa hapo Novemba 12, 2022, ili kutoa nafasi kwa wadau kutoa maoni yao kuhusiana na jambo hilo nyeti.

Akiongea hapo Januari 25, 2023, katika TwitterSpace ya gazeti la Mwananchi iliyolenga kuangazia mambo muhimu ya kuzingatiwa kwenye muswada huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema muswada huo unaweka misingi ya kumwezesha Mtanzania apate huduma bora za afya.

“Kwenye suala la ubora wa huduma, tusipokuwa makini wote wenye bima za afya wataenda hospitali binafsi,” alisema Mwalimu. 

“Hilo tuliliona ndiyo maana tumeboresha huduma kwenye vituo na hospitali za Serikali,tumeongeza vifaa tiba, miundombinu na watumishi kilichobaki ni suala la utendaji na uwajibikaji,” aliongeza Mbunge huyo wa Tanga Mjini (CCM).

Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Dk Osati amesema ni muhimu kwa muswada huo ukapitishwa na Bunge na kusainiwa kuwa sheria, akisema hatua hiyo itatoa fursa kwa nchi kubuni mikakati mbalimbali ya kuweza kupata fedha kwa ajili ya kuhudumia Watanzania.

SOMA ZAIDI: Afya Moja Ni Nini Na Kwa Nini Ujali Kuhusu Ufanisi Wake?

“Kwa sasa hivi hali ilivyo ni kwamba kwenye hospitali zetu mbalimbali, wagonjwa wetu wanapata matatizo mengi ya malipo kwa sababu hawawezi kupata huduma bora, kwa sababu wanakosa malipo, wakati mwingine wanakosa fedha kwa ajili ya kulipia vipimo lakini pamoja na matibabu,” alisema daktari huyo bingwa.

“Familia inapata gharama kubwa lakini pia Serikali inaingia gharama kubwa, lakini pia madaktari na watumishi pia wanaingia kwenye mzigo mzito sana wa kuweza kumhudumia mtu ambaye hana fedha.

“Mapendekezo yetu kama madaktari siku zote yamekuwa ni kwamba kuwe na uwezekano wa kutengeneza mfuko wa afya, ambao sasa michango mbalimbali inaweza kuingizwa kwenye huo mfuko na kuweza kutengeneza mfuko utakaowasaidia wale ambao hawana uwezo kiuchumi.

“Kwa hiyo, tunapendekeza kuweza kutengenezwa mfuko na kuweza kuwa na michango midogo midogo kutoka kwenye hizi risk factors zote ziweze kuingia katika huu mfuko na kuweza kusaidia kuchangia huu mfuko wa afya ili uweze kusaidia wale ambao hawana uwezo wa kiuchumi,” alisema Dk Osati kwenye mahojiano hayo maalum The Chanzo.

Hadija Said ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dare es Salaam anayepatikana kupitia hadijasaid826@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *