Kwa Nini Ni Muhimu Kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii?

ACT-Wazalendo wanaamini hatua hiyo ni muhimu ili kumjumuisha kila Mtanzania kwenye utaratibu wa bima ya afya.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kimebainisha kwamba suluhisho pekee ya kudumu ya Watanzania kukosa matibabu pindi wanapougua ni kuifungamanisha bima ya afya na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akiongea na The Chanzo hapo Oktoba 4, 2022, Waziri Kivuli wa ACT-Wazalendo anayesimamia suala la Uwezeshaji na Hifadhi ya Jamii Mwanaisha Mndeme alisema kwamba hatua hiyo ni muhimu kuwasaidia Watanzania walio kwenye sekta isiyo rasmi ambao amesema mara nyingi huachwa nyuma kwenye suala la bima ya afya.

Ifuatayo ni sehemu ya mazungumzo kati ya The Chanzo na Mndeme yaliyofanyika katika ofisi za chombo hicho cha habari Msasani, Dar es Salaam, hivi karibuni: 

 

The Chanzo: Mwanaisha, hali ya maisha, au kwa kupanda kwa gharama ya maisha, kuna uhusiano wa moja kwa moja na uwezo wa wananchi kujipatia huduma za kiafya kwa mfano. Na tumeona ripoti za siku za hivi karibuni kuhusiana na janga ambalo linaukabili Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) mpaka kukawa na ripoti kwamba unaweza ukafilisika au ukashindwa kufanya kazi. 

Na tumeona Waziri [wa Afya Ummy Mwalimu] akitengua maelekezo ambayo yalikuwa yametolewa na NHIF ambayo yalilenga kuwazuia wananchama wa NHIF ambao walikuwa wamezoea kutibiwa kwenye hospitali fulani wasitibwe kwenye hospitali nyingine mpaka baada ya kupita siku 30 au kupata kibali kutoka kwenye mfuko. Unadhani kuna uhusiano gani kati ya mfumo ambao siyo mzuri wa hifadhi ya jamii ambao Tanzania tuko nao na ugumu wa maisha au wananchi kuishi kwenye maisha ambayo ni magumu yanayoathiri ustawi wao?

Mwanaisha Mndeme: Asante. Kwanza, tunafahamu kwamba afya ni rasilimali muhimu sana kwenye nchi. Na ukiangalia kwa nchi ya Tanzania, ukiangalia kwa ripoti ya uchumi ya mwaka 2021, karibia Watanzania milioni 41 walikuwa wapo hospitalini, sawa na asilimia 70 ya Watanzania wote. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni jinsi gani ambavyo kwamba katika nchi ambayo watu wake wengi ni wagonjwa ni jinsi gani ambavyo suala la afya ni la muhimu na la kutiliwa mkazo. 

Na ugumu huo wa maisha pia umepelekea matatizo mengi kwenye upande wa afya ya Watanzania wetu. Ukiangalia kwanza kuna suala la baadhi ya Watanzania kuweza kukataliwa maiti za ndugu zao na hilo tumeweza kulishudia katika hospitali nyingi. Na hii ni kwa sababu tu ya ugumu wa maisha. 

Maana yake inafikia hatua mtu anashindwa kujihudumia na mwisho wa siku anapoteza maisha. Na mwisho wa siku anashindwa kuchukuliwa ndugu zake kwa sababu tu alishindwa kuweza kujihudumia. Lakini pia, tumeweza kushuhudia kwamba kwa Tanzania asilimia 52 ya watanzania ni watu ambao wapo katika sekta isiyokuwa rasmi. Kwa hiyo, kwamba yaani maisha yao mengi, hata katika suala la bima ya afya linakuwa ni tatizo. 

Kwa hiyo, sisi kama chama cha ACT-Wazalendo, tunafungamanisha hifadhi ya jamii na bima ya afya kwa mantiki kwamba tunaitaka Serikali iweze kuunganisha bima ya afya na mfuko wa hifadhi ya jamii.

Na hili, linaweza likafanikiwa kwa njia ipi? Kwa maana kwamba kwa wale watu ambao hawapo katika mfumo usiyokuwa rasmi, hapo tunaongelea mabodaboda,  machinga, wakulima na wafugaji, waweze kutoa asilimia fulani ya pesa iwekwe katika mfumo wa hifadhi ya jamii na Serikali iweze kuchangia. 

Na moja wapo ya vitu ambavyo watavipata kupitia mfuko huo wa hifadhi ya jamii ni pamoja na bima ya afya. Licha wanaweza wakapata mikopo, mafao ya uzeeni lakini bima ya afya iwe ni kitu moja wapo ambacho wanaweza kukipata kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii.

Kwa hiyo, sisi kwa kuona changamoto ambazo wanazo Watanzania, na umeongea vizuri hapo, umeongelea kwamba jinsi ambavyo NHIF imeyumba, ni kweli. Ukiangalia hata kwenye katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/2021 kulikuwa kuna deni la karibia bilioni 109. 

Lakini pia, tumeweza kushuhudia kwamba Serikali imekuwa ni kinara wa kuikopa hii mifuko na mwisho wa siku kuipelekea mifuko kutokuwa imara. Lakini pia, tumeweza kuona kwamba kumekuwa hakuna sheria ambayo inaweza kuwabana wale wanaofanya ubadhirifu ndani ya hii mifuko. 

Kwa hiyo, sisi kama chama cha ACT-Wazalendo tunaona kwamba kuna haja ya Watanzania kuweza kupata bima ya afya wote. Na jinsi ambavyo tunaweza kuifanya kuhakikisha kwamba mfuko wa hifadhi ya jamii ambayo itakuwa ni kwa Watanzania wote iweze kuunganishwa na bima ya afya. 

Na mwisho wa siku Watanzania wote waweze kupata bima ya afya ili kuweza pia kukidhi matakwa na mahitaji ya Watanzania kama unavyosema hali ya maisha imekuwa ni ngumu mtu huyu ambaye anakosa hata Sh2,000 ya siku kwa ajili ya chakula hawezi kupata huduma ambayo ni bora.

Lakini pia, tumeona NHIF ambavyo imekuwa imeweka matabaka, matabaka kwa maana kwamba NHIF ina vifurushi, vifurushi ambavyo Mtanzania wa kawadia hawezi kuvikidhi. Kwa hiyo, suala la kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii na bima ya afya itakuwa ni jawabu zuri na ambalo litaweza kuwasaidia Watanzania kwa ujumla.

The Chanzo: Asante. Na hilo halijazungumziwa kwenye huu muswada ambao unasemwa utapelekwa bungeni kesho kutwa?

Mwanaisha Mndeme: Ni kweli halijazungumziwa. Na mimi kama Waziri [Kivuli] wa wizara husika nauona huu muswada ambao Serikali imeuleta siyo tu hilo yaani kuna vitu vingi sana ambavyo haviko sawa kwenye huu muswada. Kwa hiyo, sisi kama chama cha ACT-Wazalendo, kwanza ukiangalia ule muswada jinsi unavyoelezea kwanza hautoi jibu la moja kwa moja. 

Kwamba utaendaje kuweza kuwasaidia hao wananchi wetu wanasema tu bima ya afya kwa umma. Yaani, haielezi jinsi gani ambavyo itaweza kuwasaidia Watanzania kwa ujumla. Lakini pia, ukiangalia katika huu muswada ambao umekuja hauoneshi, wala hautoi, maelekezo jinsi ambavyo ubadhirifu ambao umekuwa ukifanyika katika katika hii mifuko unaweza ukakomeshwa. 

Lakini pia inaenda kuchukua matatizo ambayo yaliyokuwepo NHIF wanayaingiza katika muswada ambao sasa hivi wameuleta. Kwa hiyo, sisi tunaona kabisa kwamba huu muswada bado haujaenda kukidhi matakwa ya kumsaidia Mtanzania wetu wa kawaida. Kwa hiyo, ndiyo maana pia tunasema kwamba ni muswada ambao inabidi utupiliwe mbali. 

Kitu ambacho kinapaswa kufanyika, na tunaitaka Serikali ifanye hivyo, kupitia Waziri [wa Afya] Ummy Mwalimu ni kwamba njia ambayo ni sahihi ni njia ya kuhakikisha kwamba mfuko wa hifadhi ya jamii ifungamanishwe na bima ya afya ili kuweza kumsaidia Mtanzania huyu ambaye asilimia kubwa ni watu ambao hawapo katika sekta isiyokuwa rasmi. 

Lakini pia ukiangalia hata matabaka imekuwa na matabaka, na pia ukiangalia katika NHIF kuna baadhi ya magonjwa hayatibiwi kupitia hizo bima za afya. Kwa mfano, kama saratani, wakina mama wajawazito kliniki inakuwa haiingii. Lakini kama tutafungamanisha mifuko ya hifadhi ya jamii na bima ya afya ina maana itakwenda kuokoa Watanzania wengi.

Na Watanzania wengi wataweza kupata huduma ya afya ambayo ni stahiki kwa wote. Kwa hiyo, ndiyo maana sisi ACT-Wazalendo tunapendekeza, na tunaitaka Serikali, kwamba moja wapo ya kitu ambacho kinapaswa kifanyike kwenye huu muswada ni kuifungamanisha mifuko ya hifadhi ya jamii na bima ya afya ili Watanzania wote waweze kufaidika na huduma bora kwa kila mmoja.

The Chanzo: Nina suala la nyongeza hapo. Inawezekana vipi, kwa mfano, Serikali inapeleka muswada, kwa mfano, kwenye suala nyeti kama hilo na kukawa kuna watu kama nyinyi, chama cha siasa, au chama cha upinzani makini kabisa, ambao mmekuwa mkitoa mapendekezo na sera mbadala mbalimbali bila kupata mtazamo wenu. Na nilikuwa nataka kufahamu labda kulikuwepo na ushirikishwaji wa wadau kiasi gani kwenye mchakato wa kutengeneza huu muswada ambao Serikali inategemea kuupeleka bungeni?

Mwanaisha Mndeme: Ukiangalia utaratibu wa muswada licha ya kuweza kufika bungeni lazima washikadau waweze kushirikishwa. Na kwenye hili binafsi sijaona kama hilo suala limeweza kufanyika kwa washikadau kushirikishwa. Lakini pia, nadhani tunafahamu wote kwamba Bunge la sasa hivi ni Bunge ambalo asilimia tisini ni CCM. 

Kwa hiyo, kunakosekana ile nguvu ya upinzani kuweza kuyapa changamoto mambo ambayo yanapelekwa bungeni. Nadhani nyinyi wenyewe ni mashahidi mmeweza kuona Bunge zilizowahi kupita. Bunge ambalo alikuwepo kiongozi wetu wa chama Zitto Kabwe alikuwa ni mtu mmoja lakini ambaye angeweza kuongea na akaweza kulitingisha Bunge, yaani wapinzani walikuwa na uwezo wa kwenda kuitengeneza miswada ambayo ilikuwa inaingizwa na mwisho wa siku mabadiliko yakawa yanafanyika na kitu kikawa kinaeleweka. 

Kwa hiyo, kukosekana kwa Bunge ndani ya Bunge ambapo tunavyoona asilimia 90 ni CCM kunakuwa na matatizo mengi moja wapo likiwa ni hili miswada inapokuja inakuwa inapitishwa pasipo kupata mawazo ya upinzani. 

Lakini sisi kama chama cha ACT-Wazalendo ndiyo maana tukaona kuna haja ya kuanzisha hili Baraza Kivuli [la Mawaziri] kwa maana kwamba chombo chochote kile ambacho kinasemwa japo tumekosa nafasi ya kuingia bungeni lakini tunatoa mawazo yetu, tunatoa maoni yetu, mapendekezo yetu na Serikali inayapokea. 

Kuna saa ndiyo wanakuwa hawayapokei lakini tunaona kuna haja ya kuweza kufanya na kuhakikisha kwamba yale ambayo hayapo sawa tunayasemea. Na hata tukiongea kuhusu hili suala la bima ya afya tunaloliongelea, sisi tumeanza kuongea kuhusu suala la bima ya afya kuelezea matatizo na kwamba mfuko wa NHIF unakufa. 

Ummy Mwalimu akaja alikubali ni kweli NHIF inakufa na matatizo mingine sisi [ACT Wazalendo] tuliongea na siku ambayo mimi natoka kuongea na waandishi wa habari yeye pia alikuja akaongea ina maana wanasikiliza ambayo tunayafanya na wanakuja wanayajibia. 

Kwa hiyo, sisi licha ya kwamba tumekosa ushiriki wa nafasi bungeni kwa sababu Bunge ndiyo linalopitisha miswada na mwisho wa siku kuwa sheria bado tunahakikisha kwamba yale ambayo tunayaona hayako sawa katika Serikali kwenye ndani ya Bunge kwenye miswada tunayasemea kwa sababu sisi kazi yetu kama chama cha siasa ni kuweza kuwasemea wananchi ama tupo ndani ya Bunge au tupo nje.

The Chanzo: Tungependa sana kuendeleza mjadala huu hapa lakini kama nilivyotangulia kusema muda siyo rafiki sana na tunakwenda kuhitimisha mazungumzo haya kwa kukupa mgeni wetu nafasi ya mwisho ya kutoa neno lolote lililopo moyoni mwako ambalo mimi hapa nimesahau au nimeghafilika kukuuliza.

Mwanaisha Mndeme: Asante kwanza na mimi pia kwa kipekee kabisa niweze kuwashukuru The Chanzo. Lakini pia niwape hongera nasikia mmepokea tuzo nyingi. Mimi kitu ambacho naweza kukisema kama Waziri bado napambana tu na suala langu la hifadhi ya jamii. 

Kwa hiyo, napenda kusisitiza kwamba Serikali ione haja ya kuhakikisha kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii inaweza kuunganishwa na bima ya afya na mwisho wa siku Watanzania wetu waweze kupata bima ya afya kwa wote kwa ajili ya kuwa na maendeleo katika nchi yetu. 

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Jackline Kuwanda na kuhaririwa na Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts