The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kinachoweza Kukwamisha Mipango ya Serikali Kukabiliana na Njaa

Hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu wanaohujumu juhudi za Serikali, wakiwemo wale wanaochakachua ubora wa mbolea.

subscribe to our newsletter!

Dunia inatarajiwa kukumbwa na janga la njaa kwa mwaka huu wa 2023, janga ambalo limetajwa kuwa ni baya zaidi kuwahi kutokea duniani kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (WFP). Mapigano, mdororo wa uchumi, hali ya hewa na kupanda kwa bei za mbolea zimetajwa kuwa ni baadhi tu ya sababu zitakazolifanya janga hilo kuwa la hatari zaidi.

Nchi nyingi za Afrika zimeathiriwa na mdororo wa uchumi uliotokana na janga la UVIKO-19 pamoja na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, hali inayotokana na utegemezi mkubwa wa nchi za Kiafrika kwenye uagizaji na usafirishaji bidhaa za gesi na mafuta nje ya nchi, utegemezi kwenye sekta ya utalii sambamba na uagizaji wa mbolea.

Nchini Tanzania, Serikali inaonekana kuifahamu hatari hii ya kidunia, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiweka wazi hatua mbalimbali ambazo Serikali yake itachukua, ikiwemo ile ya kuongeza mara tatu bajeti ya Wizara ya Kilimo, huku msisitizo ukiwekwa kwenye umwagiliaji, mafunzo ya ugani, vifaa vya kilimo na ruzuku ya mbolea kwa wakulima.

Sambamba na hilo, Rais Samia amekuwa akifungua maghala kwenye mikoa mbalimbali ya nchi ili mazao yatakayovunwa yabaki kwenye mikoa husika ili janga la njaa litakapotokea liweze kudhibitiwa kirahisi kwenye maeneo husika. 

Hata hivyo, nadhani kuna mambo yanaweza kukwamisha juhudi hizi na kuzifanya zisizae matunda yanayotarajiwa.

Hujuma

Moja kati ya mambo haya ni uchakachuaji wa mbolea za ruzuku ambazo baadaye huuzwa kwa wakulima, huku ubora wake ukiwa umepotea. Hii ni changamoto kubwa ambayo inaweza kukwamisha juhudi za Serikali kufikisha mbolea zilizohakikiwa na zenye matokeo chanya kwa wakulima. 

Mnamo Januari 20, 2023, kwa mfano, ziliibuka ripoti zilizohusisha polisi mkoani Njombe kuwakamata watu 10 kwa tuhuma za kufungasha mbolea feki kisha kuwauzia wakulima mkoani humo.

Mbolea feki, kama ambavyo wengi wetu tunafahamu, bila shaka zinakwenda kupunguza uzalishaji na kuua ubora wa mazao ya wakulima na kuyafanya yasifae kwa matumizi ya binadamu na hata kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya biashara, hususan kwenye mataifa ya Afrika yaliyoingia kwenye mkataba wa eneo huru la biashara.

SOMA ZAIDI: Serikali, Wataalam Wachambua Hali ya Ukame na Upungufu wa Chakula Tanzania

Jambo jingine linaloziweka juhudi hizi za Serikali mashakani ni elimu ndogo ya ardhi kwa baadhi ya wananchi ambayo inaweza kukwamisha uzalishaji wa mazao kwa wingi. 

Hii ni kusema kuwa katika baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakiweka makazi na kufanya shuguli za kilimo kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria kufanya hivyo. 

Hii inapelekea kuhamishwa na Serikali au wawekezaji wenye ardhi husika, jambo linaloleta mdororo wa uzalishaji katika kilimo kwani wananchi wanalazimika kuachana na mashamba yao na kuhamia kwenye maeneo sahihi kwa ajili ya makazi na kilimo. 

Hii inapelekea uzalishaji kuwa mdogo na hivyo mazao yanayopatikana hayatoshelezi kwa ajili ya chakula na usafirishaji wa chakula nje ya nchi kwa ajili ya biashara. 

Mfano wa hivi karibuni kabisa ni uamuzi wa Serikali kuhusu mgogoro wa eneo linalodaiwa kuwemo katika Bonde la Ihefu wilayani Mbarali ambapo vijiji vitano vilifutwa.

Jambo jingine linahusiana na kutokuwepo kwa umilikishaji wa mali kihalali kwa utoaji wa hati kwa haraka, ili kuepuka migogoro na kusaidia uendelezaji wa ardhi. 

SOMA ZAIDI: Nini Kinaweza Kupandisha, Kushusha Bei za Bidhaa 2023?

Ardhi isiyo na mmiliki haiwezi kutunzwa na kuzalisha ipasavyo na kuwafanya wakulima wengi kufanya kilimo cha mazao kwa ajili ya kula tu na siyo biashara, jambo ambalo linashusha uzalishaji kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya biashara nje ya nchi.

Na la kutokusahaulika kwenye orodha hii ni suala la mabadiliko ya tabianchi na athari zake ambazo zinaambatana na upungufu wa mvua kwenye baadhi ya mikoa na mvua kubwa zisizo za kawaida zinasosababisha mafuriko. Bila shaka changamoto hii itakwamisha uzalishaji wa wingi wa mazao ya chakula. 

Udhibiti

Hivyo, Serikali haina budi kufanya uhakiki na udhibiti wa wafanyabishara wa mbolea wanaochakachua mbolea na kuwauzia wakulima mbolea zisizofaa na zisizo na tija. Watu hawa ni kama wauaji na wahujumu wa taifa na dunia. 

Sheria lazima ziwe kali juu ya wafanyabiashara na watu wote wanaohujumu juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau wengine katika kupambana na janga la njaa.

Serikali pia, kupitia Wizara ya Kilimo, haina budi kueneza elimu juu ya mbolea sahihi zinazofaa kutumika kwenye uzalishaji wa mazao husika. 

Hapa ni lazima wakulima wajue nembo na alama zitakazowawezesha kutofautisha mbolea bandia na mbolea sahihi. 

SOMA ZAIDI: Wakulima: Bei za Mbolea Zahatarisha Uzalishaji wa Chakula Nchini

Hii itawawezesha wakulima kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya upatikanaji na uuzwaji wa mbolea zilizoisha muda na zisizofaa kwenye kilimo. 

Hivi, kama nchi, tunawezaje kumvumilia mtu anayezorotesha uzalishaji wa mazao ya chakula ili tukabiliane na janga la njaa? Haiwezekani.

Pia, ipo haja ya kuweka mikakati ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji, hususan maeneo ya vijijini, kwa kuchimba mabwawa na visima vikubwa vitakavyokuwa na maji ya kutosha ili yaweze kutumika wakati wa ukame na mvua zisizotabirika.

Wizara ya Ardhi iwe mstari wa mbele kueneza elimu juu ya umiliki wa ardhi na kuainisha maeneo yasiyoruhusiwa kwa ajili ya makazi na shughuli za uchumi kama kilimo. 

Hii itapunguza kuhamahama kwa wakulima kwa kupisha maeneo ya wawekezaji na maeneo yanayomilikiwa na Serikali, na hivyo kuleta matokeo chanya kwa wakulima kuwa na muda mwingi wa uzalishaji wa mazao ya chakula.

Pia, katika juhudi hizi za mapambano juu ya janga la njaa litakaloikumba dunia, ni lazima viongozi wa Serikali za Mitaa na vijiji washirikishwe kikamilifu. 

Hii ni kusema viongozi hawa ndiyo wapo karibu na maeneo ya wakulima, hivyo basi kama wakieleweshwa juu ya hatari ya njaa itakayoikumba dunia basi watashiriki kikamilifu kuhakikisha mazingira wezeshi kwa wakulima.

Kwa mfano, watahakikisha ulinzi kwa wakulima muda wote ili wafanye uzalishaji wao kwa amani na uhuru kwa kuzuia migogoro na kuzuia matumizi yasiyofaa ya mazao.

Ni imani yangu, kama mwananchi, kwamba kama jitihada hizi zitafanyiwa kazi kikamilifu basi nchini kwetu kutakuwa na chakula cha kutosha na ziada ya mazao ya kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya biashara na hivyo Tanzania kunufaika kwa kiwango kikubwa.

Bakari Mahundu ni mwandishi wa habari na mdau wa maendeleo ya vijana Tanzania. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia bakarimahundu8@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *