The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Kinaweza Kupandisha, Kushusha Bei za Bidhaa 2023?

Serikali imetakiwa kuweka mikakati ya makusudi kukuza uzalishaji wa chakula kukabiliana na athari za mfumuko wa bei.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wamebainisha mambo kadhaa ambayo yanaweza kuchangia bei za bidhaa na huduma muhimu kupanda au kushuka ndani ya mwaka 2023, yakiwemo yale yaliyochini ya udhibiti wa Serikali na yale Serikali isiyokuwa na udhibiti nayo.

Mwaka 2022 umeshuhudia bei za bidhaa na huduma muhimu zikiongezeka hali iliyolalamikiwa na Watanzania walio wengi ambao wamekuwa wakinung’unika kuhusiana na kuongezeka kwa gharama za maisha.

Uchambuzi uliofanywa na The Chanzo Novemba 10, 2022, ulionesha kwamba Mtazania wa kawaida anahitaji kuwa na Sh20,000 kuweza kupata kilo moja moja ya bidhaa muhimu kama vile unga wa mahindi (Sh1,625), mchele (Sh2,750), maharage (Sh2,625), mafuta ya kula lita moja (Sh7,000), viazi (Sh1,000), sukari (Sh2,750), na unga wa ngano (Sh2,250).

Haya ni mahitaji ya kila siku kwa kila kaya kwenye nchi ambayo takwimu zinaonesha kwamba takriban watu milioni 26 waliishi kwenye umasikini wa kupindukia mwaka 2022, wengi wao wakiishi chini ya Dola 1.90 za Kimarekani, ambayo ni sawa na Sh4,436.

Wachumi walikuwa na mitazamo yenye kutofautiana walipoulizwa na The Chanzo kama mwaka 2023 unaweza kushuhudia hali ikiwa tofauti kwenye eneo zima la bei za vyakula na bidhaa muhimu.

Mvua ndiyo kila kitu

Watengere Kitejo, profesa wa uchumi kutoka Chuo cha Diplomasia, kwa mfano, anadhani hali itategemeana na upatikanaji wa mvua, akisema kwamba kama hali itaendelea kama hivi sasa mwaka 2023 unaweza kuwa wa tofauti.

“Kama mvua itakata, tutegemee tena mfumuko wa bei, kwa sababu mfumuko mkubwa wa bei unategema na uzalishaji [wa chakula],” alisema mchumi huyo. 

“Kwa mvua zinazoendelea kunyesha, ukienda shambani chakula kipo, [kama vile] mahindi [na] maharage. Watu wanavyopanda na hali ikiwa hivi mfumuko wa bei hautakuwepo,” aliongeza Profesa Kitejo.

Hoja hii inaungwa mkono na Dk Timothy Lyanga, mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) anaamini kwamba kuendelea ama kukata kwa mvua kutakuwa na athari ya moja kwa moja kwenye bei za bidhaa na huduma muhimu kwa mwaka huu. 

SOMA ZAIDI: Maumivu ya Kutegemea Kwenye Uchumi, Kupanda Bei Vitu Sababu ya Vita ya Ukraine

Lakini Dk Lyanga anatoa kiashiria kingine kitakachoamua bei kushuka au kupanda, nacho ni thamani ya Shilingi ya Kitanzania: kupanda kwake au kushuka kutaleta mtingishiko kwenye bei za bidhaa na huduma. Usalama wa wananchi ni Shilingi kutulia kwenye thamani yake ya sasa.

“Thamani ya fedha inapokuwa iko juu, au iko chini, nayo huwa inachochea bei za bidhaa kuweza kupanda. Kwa sababu, thamani ya fedha inakuwa ni ndogo lakini pia mzunguko wa fedha unapokuwa mdogo maana yake fedha ile mfukoni mwa watu inakuwa ni kidogo nayo,” Dk Lyanga alisema. 

“Sasa ukitazama hali ya hewa ikoje kwa hivi sasa, thamani ya fedha ikoje kwa hivi sasa, hatuwezi kusema kutakuwa na mfumuko wa bei kwani vitu vyote hivyo vinaenda vizuri,” aliongeza mtaalamu huyo.

Licha ya matumaini haya, baadhi ya wachambuzi hawaoni hali ya mwaka 2023 ikiwa tofauti sana na ile ya 2022 kwani mambo yaliyopelekea mfumuko wa bei 2022 bado yapo na athari zake zinaendelea kuathiri chumi mbalimbali duniani.

Mambo kama haya ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo, pamoja na mambo mengine, yanaathiri upatikanaji wa mvua; vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine ambayo imehusishwa na kupanda kwa bei ya mafuta na nafaka muhimu; pamoja na janga la UVIKO-19.

Hali inaweza kuwa mbaya

Walter Nguma ni mchambuzi huru wa masuala ya kiuchumi ambaye anaamini kwamba kimsingi hali inaweza kuwa mbaya zaidi 2023 kuliko hata ilivyokuwa 2022, akitaja vita ya Urusi/Ukraine kama suala kubwa la kutupiwa jicho.

“Mfumuko wa bei unaweza ukakua zaidi kutokana na kwamba mgogoro ambao tulidhani kwamba ungeweza ukawa umemalizika kwa muda mfupi, tunazungumzia mgogoro wa Urusi pamoja na Ukraine,” alisema Nguma. 

“Tunaona [mgogoro huo] umeingia katika taswira nyingine mpya ambapo sasa Urusi amesema kwamba hatauza mafuta wala gesi katika nchi za Magharibi, tunazungumzia nchi za Ulaya. 

“Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba bei ya mafuta ikapanda tena na kama bei ya mafuta itapanda tena maana yake ni kwamba mfumuko wa bei hauwezi kuzuilika,” aliongeza mchambuzi huyo.

SOMA ZAIDI: Infographic: Mwenendo wa Kupanda kwa Bei za Bidhaa na Huduma Tanzania

Hatua hiyo ya Urusi, ambayo ni taifa la pili kwa uzalishaji wa mafuta duniani, ilikuja kufuatia hatua ya mataifa ya Magharibi kuweka ukomo wa Dola 60 za Kimarekani kwa pipa  moja la mafuta, ikiwa ni sehemu ya kuiadhibu Urusi kwa uvamizi wake wa Ukraine.

Nguma anatabiri kwamba hali hiyo bila shaka italeta taharuki kwenye nchi za Magharibi, hali anayosema kwamba haoni ni kwa namna gani nchi kama Tanzania inaweza kukwepa athari za taharuki hiyo.

“Uzalishaji utapungua kwa wenzetu, namaanisha hayo mataifa makubwa, sisi lazima itatupa shida tu,” anaeleza mchambuzi huyo. “Sioni ni kwa namna gani tunaweza kukwepa athari za taharuki hiyo.”

Jitihada zinazohitajika

Wakati ni kweli Tanzania haiwezi kukwepa athari zitokanazo na mtingishiko wa uchumi wa kidunia, baadhi ya wachambuzi wanadhani kwamba zipo jitihada Serikali inaweza kuzichukua kupunguza ukali wa maisha ya Watanzania.

SOMA ZAIDI: Mbivu Mbichi ya Hoja za Wabunge Kuhusu Mafuta na Kwa nini Bei Inaweza Kupaa Zaidi

Moja kati ya jitihada hizi ni kuwaweka wakulima karibu na kuwapatia nyenzo muhimu zitakazowawezesha kuzalisha chakula cha kutosha, ikiwemo mbolea, madawa na teknolojia ya kisasa ya kilimo.

Jitihada nyingine ni ile iliyoibuliwa na Ally Selemani Mkimo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Madini Plus, jukwaa linalozungumza na vijana kuhusiana na masuala ya fedha na uchumi, ambaye ameitaka Serikali kuweka mikakati ya makusudi kuwasaidia wazalishaji nchini.

“Huwezi kudhibiti bei za bidhaa na huduma kupanda kama huwapi kipaumbele wazalishaji,” Mkimo aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum. “Wazalishaji ndiyo wanaolisha taifa, ni lazima watazamwe kwa jicho la tatu.”

Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mbeya anayepatikana kupitia barua pepe mbembelaasifiwe@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts