The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali: Hatutofumbia Macho Adhabu Kali Zinazotolewa kwa Wanafunzi

Yataka utoaji wa adhabu shuleni uzingatie waraka namba 24 wa mwaka 2002 wa Wizara ya Elimu na Utamaduni

subscribe to our newsletter!

Dodoma.  Serikali imetoa wito kwa Maafisa Elimu wa mikoa na Maafisa  Elimu wilaya kuwakumbusha walimu kote nchini kuzingatia muongozo wa utoaji wa adhabu shuleni chini ya kifungu namba 61 cha sheria ya elimu sura ya 353 ya sheria pamoja na kanuni zake.

Wito huu umetolewa Februari 2,2023, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni mjini Dodoma.

Serikali imesisitiza kuwa adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu wa nidhamu au kosa kubwa litakalo fanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.Adhabu hiyo itatolewa kwa kuzingatia umri,jinsia na afya ya mwanafunzi.

Serikali imetoa wito huu kufuatia kusambaa kwa video fupi katika mitandao ya kijamii iliyomuonesha mwalimu wa shule ya msingi Kakanja iliyopo Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera akimpiga vikali mwanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumzia juu ya tukio hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuwa vitendo kama hivyo, vimesababisha madhara mengi ikiwemo kuleta taharuki kwa jamii ,athari ya kimwili ,kiakili na msongo wa mawazo kwa wahanga wa matukio hayo wakiwemo wazazi na walezi.

“Serikali haitofumbia macho na wala kukubaliana na aina hiyo ya adhabu kali. Tayari serikali imechukua hatua za kinidhamu kwa wahusika.’’ anaeleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Anasema serikali imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto awapo kwenye mazingira yote.Licha ya kuwepo kwa mifumo hiyo kuna ukiukwaji wa sheria na taribu kwa makusudi , hivyo kusababisha madhara makubwa kwa jamii .

Pia, Waziri Majaliwa amezitaka Mamlaka za elimu nchini kuhakikisha kuwa utoaji wa adhabu shuleni unazingatia waraka namba 24 wa mwaka 2002 wa Wizara ya Elimu na Utamaduni ambao umeainisha utaratibu wa utoaji wa adhabu.

“Mwanafunzi wa kike atapewa adhabu ya viboko mkononi na mwalimu wa kike isipokuwa kama shule hiyo haina mwalimu wa kike”

“Adhabu ya viboko itakapotolewa iorodheshwe katika kitabu kilicho tengwa kwa kusudi hili ikiwa ni pamoja jina la mwanafunzi aliyepewa adhabu ,kosa alilotenda,idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu hiyo.’’ anafanua Majaliwa wakati akielezea taratibu zinazo paswa kuzingatiwa wakati wa utoaji adhabu.

Hatua zingine zilizotajwa katika muongozo ni pamoja na Mwalimu mkuu kusaini katika kitabu kila  mara adhabu hiyo inapotolewa  na endapo mwanafunzi akikataa adhabu ya viboko atasimamishwa shule.

Sambamba na hilo Waziri Majaliwa ameeleza kuwa walimu wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuliko mapungufu machache yanayoonekana kupitia mitandao ya kijamii. Hivyo kuitaka jamii kutoyarusha matukio yanayo fanywa na baadhi ya walimu  kwenye mitandao, kwani yanajenga chuki kwa walimu na taswira hasi kwa walimu wote badala ya wahusika wachache.

“Bahati mbaya kwa jamii zetu jambo baya linasambaa zaidi kuliko jema.’’ anasema Majaliwa, “hata hivyo , licha ya mapungufu kutoka kwa baadhi ya walimu, walimu wanafanya mambo mengi makubwa malezi kwa watoto wetu ambayo pengine hayakusambaa na kuonekana. Jamii haipaswi kubeza juhudi zinazo fanywa na walimu badala yake muwatie moyo.’’

Majaliwa amesisitiza lengo siyo kuficha taarifa bali kuzuia taharuki,chuki na  uhasama ndani ya jamii, katika nyanja zote kama afya ,vyombo vya ulinzi na usalama na maeneo mengine yanayofanana na hayo.

Waziri Mkuu amewataka walimu na wakuu wa shule kutumia walimu wa malezi ushauri ,unasishi pamoja na viongozi wa dini kuwarekebisha watoto kwa kuwajenga kimaadili ili kuepukana na matumizi ya viboko pale ambako si lazima kutumia viboko.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *