Elon Musk: Tunasubiri Ruhusa Ya Serikali Ya Tanzania Kuleta Internet Ya Kasi Ya Starlink

Waziri wa Habari Nape Nnauye alisema Starlink wanatakiwa kukamilisha nyaraka ili mchakato uendelee.
Na Mwandishi Wetu7 February 20232 min

Bilionea namba mbili duniani Elon Musk ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space X, Twitter na Tesla ameeleza kuwa wanasubiri ruhusa kutoka Serikali ya Tanzania kuweza kuleta intaneti ya kasi ya Starlink.

Elon Musk, mwenye utajiri wa Shilingi trilioni 437,  alieleza hilo alivyokuwa akijibu swali kutoka kwa moja ya mtumiaji wa mtandao wa Twitter aliyemwandikia Elon na kumwambia afanye huduma za Starlink zipatikane Afrika Mashariki, hususan Tanzania. Elon alimjibu na kusema, “Tungependa iwe hivyo, tunasubiri tu ruhusa ya Serikali.”

Starlink ni huduma ya intaneti iliyo chini ya kampuni ya utafiti wa mambo ya anga za juu ya Space X. Huduma hii inatumia teknolojia ya satellite ambazo zinaiwezesha huduma kupatikana sehemu yeyote duniani bila kuhitaji mnara wala uunganishwaji wa kawaida.

Katika tovuti yao, Starlink wameonyesha kuwa wanategemea kuingia Tanzania mwaka 2023. Tayari Starlink wameshaaingia nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Nigeria.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mpaka Disemba 2022, Tanzania ilikua na watumiaji wa intaneti 31,172,544, huku asilimia 99.9 wakitegemea mitandao ya simu za mkononi. Hata hivyo, ufikiwaji wa huduma ya intaneti ni asilimia 72, ikimaanisha zaidi ya robo hawajafikiwa na huduma, huku gharama ikitajwa kama kikwazo.

Wakati wastani wa kasi ya juu ya intaneti ya mitandao ya simu Tanzania ni mpaka Mbps 10.51, spidi ya Starlink ni kati ya Mbps 100 mpaka Mbps 500 kwa intaneti isiyo na kikomo, huku bei yake ya huduma kwa mwezi ikiwa ni Sh230,000.

Kauli ya Elon Musk aliyoitoa jana, Februari 06, 2023, inakuja katika wakati ambao Naibu Waziri wa Biashara wa Marekani Marisa Lango amezuru nchini ambapo amekutana na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknologia ya Habari, Nape Nnauye pamoja na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Biashara Dk Ashatu Kijaji.


Alivyoulizwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter juu ya suala hilo, Waziri wa Habari Nape Nnauye alisema Stalink walishajibiwa  siku nyingi wana nyaraka wanatakiwa kukamilisha ili mchakato uendelee.

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2023 © All Rights Reserved