The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Pembejeo za Ruzuku Zahusishwa na Kushuka kwa Uzalishaji wa Korosho Mtwara

Mwaka 2022/2023, Serikali ilitoa pembejeo za viuatilifu vya unga tani 15,000 na viuatilifu vya maji lita 2,600,000 kwa wakulima wa korosho nchi nzima.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Baadhi ya wadau na wazalishaji wa zao la korosho mkoani hapa wameonesha kuwa na mashaka na pembejeo za ruzuku zinazotolewa bure na Serikali, huku wakizihusisha na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo la biashara kwa msimu wa mwaka 2022/2023.

Wakiwa kwenye kikao cha tathimini ya kilimo mkoa wa Mtwara kilichofanyika Februari 9, 2023, wadau hao walibainisha kwamba kumekuwa na mabadiliko hasi tangu wakulima waanze kutumia viuatifu vilivyotelewa na Serikali miaka ya hivi karibuni, hali iliyopelekea uzalishaji wa zao hilo kushuka.

Baisa Baisa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba ambaye pia ni mkulima wa zao la korosho. Akizungumza kwenye kikao hicho, Baisa alisema kwamba tangu aanze kutumia viuatilifu vilivyotolewa na Serikali uzalishaji umekuwa mdogo.

Baisa alidai kuwa kwa msimu wa mwaka 2022/2023, shamba lake lilikuwa la mfano likihudumiwa na Bodi ya Korosho kwa kutumia viuatilifu vya ruzuku na watalaam kutoka TARI Naliendele kwenye mchakato mzima wa kupuliza mikorosho.

Hata hivyo, mwisho wa siku uzalishaji wake ulishuka akilinganisha na msimu uliopita ambao alidai kuzalisha tani sita mpaka saba za korosho.

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara

“Hata wapuliziaji walikuwa wakwao na mashine zao, wamehudumia yale mashamba kwa mizunguko ya kupuliza zaidi ya minne lakini sijavuna hata gunia nane,” alilalama Baisa kwenye kikao hicho.

“Na hizo dawa zilikuwa ni za ruzuku. Lakini miaka ya nyuma ambayo tulikuwa tunatumia dawa tofauti na hizi za ruzuku tulikuwa tunapata tani sita mpaka saba,” alisema.

Baisa aliongeza kwamba baadhi ya wakulima mkoani Mtwara ambao hawakutumia viuatilifu vya ruzuku uzalishaji wao umekuwa mkubwa.

“Madawa mengi hayakuwa na ubora, tuwe wakweli, pamoja na sababu za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi, lakini madawa mengi hayakuwa na ubora,” aliongeza Baisa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Francis Alfred katika kikao hicho, kwa msimu wa mwaka 2022/2023, Serikali ilitoa pembejeo za viuatilifu vya unga, yaani sulfur, tani 15,000 na viuatilifu vya maji lita 2,600,000 kwa wakulima wote wa zao la korosho hapa nchini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara iliyosomwa kwenye kikao hicho hadi kufikia tarehe Januari 13, 2023, jumla ya minada 24 imefanyika na tani 94,222 zimekusanywa na kuuzwa ambapo msimu uliopita wa mwaka 2021/2022 zilikusanywa tani 125,000.

SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara Saidi Nyengedi, akizungumza kwenye kikao hicho, alisema kwamba suala la viuatilifu kukosa ubora na kupelekea uzalishaji kushuka amelizungumzia mara kadhaa, huku akielekeza lawama zake kwa mamlaka zinazohusika na ukaguzi wa ubora wa viuatilifu hivyo.

“Viuatilifu vinavyotolewa havina ubora, wapo Watanzania wasiokuwa wazalendo kwenye nchii hii,” alisema Nyengedi. “Tuwaambie, tusione aibu, kwa sababu tunachokifanya ni kwa ajili ya ujenzi wa taifa.”

Juma Napinda ni Katibu wa Chemba ya Biashara mkoani Mtwara ambaye alisema kwamba wakulima walikuwa wakifuatilia namna mikorosho ilivyokuwa inatoa maua kabla na baada ya kutumia viuatilifu vilivyotolewa na Serikali.

Alisema wakulima waligundua kuna mabadaliko ambayo yalionesha kuathiri mikorosho na kupelekea uzalishaji kuwa mdogo miongoni mwa wakulima kwenye maeneo mengi ya mkoa wa Mtwara.

“Pembejeo ambazo zimetumika kwenye msimu uliopita hazikuwa na ubora unaotakiwa kwa sababu sisi wote ni wakulima na kilimo kinapoanza kunakuwa na muelekeo kwa mkulima anaona kabisa shamba linapendeza kiasi gani,” alisema Napinda.

“Lakini mara tu baada ya kuanza kutumia zile pembejeo ndipo mikorosho ikaanza kubadilika. Kwa hiyo, tukaona kabisa kwamba kwenye suala zima la pembejeo kulikuwa na changamoto,” aliongeza.

SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama

Napinda alishauri kwamba taasisi husika ziwe zinachukua hatua kuchunguza na upande wa pili kuona kama pembejeo wanazopewa wakulima zinakidhi ubora unaohitajika.

Akijibu hoja hizo, Alfred kutoka Bodi ya Korosho alisema kuwa pembejeo hizo huingizwa nchini kwa kushirikiana na mamlaka zote zinazohusika na udhibiti ubora, akiongeza kwamba kutokana na hoja zilizotolewa ipo haja ya wao kama mamlaka kufanya uchunguzi zaidi.

“Hii ni muhimu kwa sababu hata hao wanaopima tunajua ni binadamu kama sisi,” alisema Alfred. “Kwa hiyo, tutaenda mbali zaidi kuangalia ubora wa viuatilifu kwa kina zaidi.”

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Tunaelekea kubaya kwa hili jambo.Jitihada za serikali kumkwamua mkulima zinakwamishwa na wazembe wachache wasiopenda maendeleo wawajibishwe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts