The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hali ya Uchafu Mbeya Yazisukuma Mamlaka Kuibuka na Mikakati Mipya

Jiji linasema mbali na kuongeza faini pia litaongeza utolewaje wa elimu kwa umma.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Hali ya kutapakaa kwa uchafu jijini hapa kumezisukuma mamlaka za jiji kuunda kikosi kazi maalum ambacho kazi yake maalum itakuwa ni kudhibiti ukusanyaji taka katika jiji hilo ili kukabiliana na hali ya uchafu iliyokithiri na kuwakwaza wananchi.

Mtaalamu wa Mazingira kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya Nimrodi Kipoloza ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba hatua hiyo inakuja kufuatia kushindwa kwa mikakati ya awali ambayo jiji ilijiwekea kukabiliana na hali ya uchafu.

Mkakati wa awali wa kuondoa taka ulikuwa unawataka wananchi wanaozalisha taka kuzibeba taka zao na kupeleka kwenye vizimba na kwa wafanyabishara sokoni kukiwa na watu maalum ya kukusanya taka na kuzipeleka kwenye vizimba vya taka.

Hata hivyo, hilo limekuwa likifanyika kwa kiwango kidogo sana, hali iliyofanya takataka kutapakaa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji na kuhatarisha usalama wa wakazi wake kwani uchafu unatajwa kuwa chanzo cha magonjwa mbalimbali.

Kikosi kazi hicho kinachoundwa na Mstahiki Meya, Mkurugenzi wa Jiji, Afisa Mazingira, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Huduma za Jamii na Kamati ya Mazingira na Mipango Miji kitakuwa kinatembelea na kukagua kata zote za jiji ambazo zimeshindwa kusimamia zoezi la kuondoa taka katika maeneo yao husika.

Akiongea na The Chanzo, Kipoloza alisema wamekusudia kupita kwenye kata zote ambazo ni kinara kwa uchafu na watakapobaini kuwa kuna uchafu viongozi wa maeneo hayo wataulizwa wameshindwa vipi kusimamia usafi.

SOMA ZAIDI: NEMC Kufanyia Kazi Madai ya Uharibifu wa Mazingira Unaofanywa na Kiwanda cha Wachina

“Tutashughulika na kata zote zenye changamoto, tutamuita diwani, wanaitwa watendaji wa mitaa na kata wote, kwa nini kata yenu ni chafu wakati dhamana ya kusafisha hii kata mlipewa nyinyi,” Kipoloza aliiambia The Chanzo.

Kipoloza amesema kwamba katika hali ya kawaida, Jiji la Mbeya limekuwa likikusanya angalau kati ya tripu 10 na 20 za taka ambazo zinazalishwa kwenye kata takribani sita za Iyela, Ruanda, Uyole, Sinde, Maendeleo, pamoja na kata ya Ilemi ambazo pia ndiyo kinara kwa kuzalisha taka nyingi.

Kukabiliana na hali ya uchafu, jiji limepanga kutumia gari maalumu la taka kukusanya taka ambapo wananchi watapewa ratiba ya siku ambazo gari litakuwa linapita kwa ajili ya kukusanya taka kwenye nyumba zao.

Zoezi hilo litakuwa linaratibiwa na kata husika kupitia michango ya wananchi.

Kupitia mpango huo mpya wa kikosi kazi cha ufuatiliaji wa taka, kila kata itapaswa kuweka ratiba ya wazi ya ni lini gari litapita kwa ajili ya kila mwenye taka kusogeza barabarani ambapo gari maalumu litakuwa linapita na kuzoa hizo taka.

Hatua hiyo inategemewa kuleta nafuu kubwa kwa wananchi ambao kwa siku nyingi wamekuwa wakizilalamikia mamlaka za jiji kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki zinazolenga kukabiliana na hali ya uchafu.

Yasini Mlotwa ni mkazi wa Soweto ambaye aliiambia The Chanzo inakuwaje jiji likusanye mapato kupitia taka lakini linashindwa kudhibiti ukusanyaji wa taka hizo.

SOMA ZAIDI: Kutibu Wanyama Wetu Ni Kulinda Afya, Ustawi Wetu Kama Binadamu

“Takataka zinazagaa mitaani, tunajiuliza hii halmashauri ni halmashauri ya namna gani, wanakusanya tu mapato,” Mlotwa alilalamika.

John Juma ni mfanyabiashara mdogo katika Soko la Sido jijini hapa aliyebainisha kwamba taka kutotolewa kwa wakati kunapunguza mzunguko wa wanunuzi waenda kwa miguu na magari.

“Uchafu pale [sokoni] umezidi halafu pale kwenye lile dampo, ile ni barabara kwamba uchafu umezidi mpaka umezidi barabara hata sehemu ya kupita inakuwa haipo,” Juma, mfanyabiashara wa viatu, alisema.

Pamoja na mkakati ambao umeanishwa wa kuundwa kwa kikosi kazi, Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekusudia kuongeza gharama za faini kwa mwananchi ambaye atakuwa amezitupa, ama kuzitelekeza taka, hovyo hovyo.

Pia, jiji litawekeza zaidi kwenye utoaji wa elimu kwa umma.

“Tunaamini kwenye elimu,” alisema Kipoloza. “Sisi tutakagua na kutoa elimu. Kuna wananchi wanahitaji kuelimishwa mara kwa mara juu ya umuhimu wa kuweka mazingira katika hali ya usafi.”

Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mbeya anayepatikana kupitia barua pepe mbembelaasifiwe@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *