The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kutibu Wanyama Wetu Ni Kulinda Afya, Ustawi Wetu Kama Binadamu

Je, unatambua kwamba wanyama tunaofuga ni chanzo cha magonjwa ya kuambukiza kwa binadamu?

subscribe to our newsletter!

Naomba nianze makala haya, labda, kwa kukuuliza maswali haya ndugu msomaji. 

Je, hapo nyumbani kwako kuna mnyama yeyote wa kufugwa? Je, katika mazingira unayoishi kuna wanyama wanaozagaa mitaani kama hawana wamiliki? 

Je, unamjua afisa au daktari wa mifugo anayehudumia eneo lako? Je, mara ya mwisho kuchanja mifugo yako ilikua lini?

Je, mifugo yako ikiugua, huwa unaenda kununua dawa na kuwatibu mwenyewe au unaandikiwa na mtoa huduma aliyeidhinishwa baada ya kumuona mnyama magonjwa? 

Je, ni wapi huwa unanunua madawa na chanjo za mifugo?

Nimeuliza maswali hayo siyo ili nipate majibu hapa bali yatusaidie katika tafakuri ya namna tunavyoishi na mifugo yetu kwani zaidi ya nusu ya idadi ya kaya zilizopo nchini zinamiliki mfugo angalau mmoja. 

Mifugo imekua sehemu ya maisha yetu ikitupatia furaha, ulinzi, nguvu kazi, chakula na kipato. 

Lakini je, tunatambua kwamba wanyama hawa hawa pia ni chanzo cha baadhi ya magonjwa ya kuambukiza kwa binadamu kama vile kichaa cha mbwa, brusela, kimeta na mengineyo?

Ulinzi wa wanyama

Sheria ya magonjwa ya wanyama ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake na sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009 kwa pamoja zinamtaka kila mwananchi kutoa taarifa za wanyama wanaougua au kufa kwa mamlaka husika iwe ni afisa, daktari au uongozi wa Serikali. 

Lakini pia sheria ya ustawi wa wanayama ya mwaka 2008 inaongelea haki za wanyama ambazo ni pamoja na kutibiwa, kukingwa dhidi ya magonjwa pamoja na kuishi sehemu safi na salama. Kufanya kinyume ya hayo yote ni kosa kisheria.

SOMA ZAIDI: Afya Moja Ni Nini Na Kwa Nini Ujali Kuhusu Ufanisi Wake?

Katika tafiti zangu nimegundua watu wengi kuwa na mazoea ya kutibu mifugo yao wenyewe. 

Yaani, mtu anaenda dukani ananunua dawa na kuja kumchoma au kumpatia mnyama mgonjwa. Hii ni hatari sana! 

Ni hatari kwa sababu kwanza unaweza usijue kwa uhakika kwamba dalili ulizoziona ni za ugonjwa uliouzoea.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba miaka ya hivi karibuni kumeibuka magonjwa mapya ambayo dalili zake zinashabihiana sana na magonjwa yaliyopo. Hivyo, siyo rahisi sana kutofautisha kwa macho.

Ndiyo maana upande wa afya ya binadamu wamekuwa wakisisitiza kwamba siyo kila homa ni malaria

Pia, kama ilivyo kwa binadamu, daktari wa wanyama hutoa matibabu na dawa kwa kuzingatia umri wa mnyama, uzito pamoja na vigezo vingine. 

Kufanya kinyume na hapo unaweza kumsababishia madhara au kusababisha usugu wa vimelea vya magonjwa ambayo athari zake huvuka hadi kwa upande wa binadamu.  

Hivyo basi, ni muhimu kutoa taarifa kwa wataalamu ili kupata huduma stahiki. Hakikisha unakua na namba ya mtaalam wa mifugo katika simu yako!

Kinga ni bora kuliko tiba

Suala jingine ambalo ni takwa la kisheria ili kulinda ustawi wa mnyama pamoja na afya ya binadamu ni kuchanja wanyama kulingana na maelekezo ya kitaifa na kimataifa. 

Hii ni katika kufuatisha ule usemi usemao kinga ni bora kuliko tiba kwani gharama za kutibu ugonjwa mara nyingi, kama siyo zote, huwa kubwa sana ukilinganisha na kukinga. 

Kwa mfano, chanjo ya kichaa cha mbwa kwa wastani ni kati ya Sh3,000 hadi Sh10,000. Lakini pindi mbwa asiyechanjwa anapomng’ata mtu gharama za kuchoma sindano ya ‘Post Exposure Prophylaxis’ si chini ya Sh150,000 (sindano tano).

SOMA ZAIDI: Wananchi Waishio Bonde la Mto Msimbazi Hatarini Kupata Tatizo la Usugu wa Dawa

Hapo bado gharama za kwenda hospitali na kurudi, kipato kinachopotea wakati wa kuugua, na huenda hata mgonjwa akapoteza maisha ambayo ni hasara kubwa zaidi kwa familia na taifa kwa ujumla! 

Huo ni mfano mmoja tu! 

Kwa kutambua umuhimu wa chanjo, Serikali imewekeza katika uzalishaji wa chanjo za wanyama na kutoa mwongozo wa utoaji chanjo kwa nchi nzima kulingana na majira na uwezekano wa milipuko ili kukupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa kutochanja.

Hivyo, nimalizie makala haya kwa kutoa wito kwa wananchi wenzangu kwamba tujitahidi sana kutoa taarifa za wanyama wanaougua.

Pia, tutibu wanyama wetu wagonjwa kupitia wataalamu waliodhinishwa pamoja na kuchanja kulingana na miongozo iliyopo ili tuweze kujikinga sisi wenyewe dhidi ya magonjwa yatokayo kwa wanyama lakini pia kulinda haki za viumbe hao ambao ni sehemu ya maisha yetu. 

Mlinde mnyama ili naye akulinde!

Dk Janeth George ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na mtafiti wa masuala ya Afya Moja. Pia, huchambua mifumo ya afya. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia jnthgrg10@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *