Wananchi Waishio Bonde la Mto Msimbazi Hatarini Kupata Tatizo la Usugu wa Dawa

Ni kutokana na uwepo wa matumizi holela ya dawa za kutibu kuku na nguruwe yanayofanywa na wafugaji wa eneo hilo.
Dk Zuhura Kimera8 April 20224 min

Wananchi wanaoishi katika Bonde la Mto Msimbazi wapo katika hatari kubwa ya kupata tatizo la usugu wa dawa endapo kama juhudi za haraka na mapema hazitachukuliwa na wadau na mamlaka husika kudhibiti matumizi holela ya dawa kwa kuku na nguruwe yanayofanywa na wafugaji wa eneo hilo.

Usugu wa dawa ni ile hali inayojitokeza baada ya dawa mbalimbali ambazo awali zilikuwa zikitibu magonjwa kwa binadamu na kwa wanyama kushindwa kutibu tena magonjwa hayo.

Bonde la Mto Msimbazi, ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 271, lina idadi kubwa ya wakazi wanaokadiriwa kufikia milioni nne, hali ambayo inalifanya eneo hili kuwa miongoni mwa maeneo nyeti yenye wakazi wengi sana nchini Tanzania.

Shughuli mbalimbali zinazofanyika ndani na kwenye mwambao wa bonde, zikiwemo kilimo na ufugaji, viwanda vya madawa na vya bidhaa mbalimbali, uvuvi na uchimbaji wa mchanga, zinahusishwa na kuwepo na kuenea kwa vimelea sugu vya magonjwa ambavyo husababisha magonjwa kwa wanyama na binadamu.

Bonde hili linaloanzia katika safu ya milima ya Pugu, eneo la Msitu wa Kazimzumbwi, na kuishia katika Bahari ya Hindi eneo la Salander Bridge, limegubikwa na uchafuzi mkubwa sana wa maji taka yanayovuja kutoka katika mabwawa ya maji taka, machinjio, na majitaka ya majumbali na kwenye vyoo kutoka katika jamii zilizo katika mwambao wa bonde hili.

Aidha, ukosefu wa elimu ya ugani, matumizi holela ya dawa, shughuli za kilimo zinazotumia mbolea kutoka kwa wanyama na ukosefu wa utekelezaji wa sheria na kanuni za ufugaji bora, pamoja na uchafuzi wa mazingira, ni tishio la kukua na kusambaa kwa vimelea sugu vya magonjwa kwa wanyama na binadamu.

Uwepo wa mwingiliano mkubwa wa watu na wanyama, uchafuzi wa mazingira na shughuli mbalimbali za kibinadamu zilifanya uwepo wa umuhimu mkubwa sana wa kufanya utafiti katika eneo hili uliolenga kutambua uwepo wa vimelea vya magonjwa aina ya Eschrichia coli na Klebsiella pneumoniae kutoka kwa kuku, nguruwe na mazingira vyenye usugu kwa makundi mbalimbali ya dawa na kubaini vinasaba vya vimelea hivyo vinavyohusika na usugu.

Urahisi wa upatikanaji wa dawa

Taarifa zilizokusanywa kwa njia ya madodoso na mwandishi wa makala haya zilibainisha kuwa asilimia 87.6 ya matumizi ya dawa za mifugo hutumika kwa ajili ya kukinga magonjwa na asilimia 80.5 ndio matumizi ya dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa kwa wafugaji.

Aidha, matumizi haya makubwa ya dawa yamekuwepo kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa dawa hizo na unafuu wa bei. Asilimia 89.4 ya dawa zinazotumika zinapatikana kwa urahisi sana sehemu mbalimbali pasipo  kuzingatia sheria zilizopo.

Pia, asilimia 62.8 ya wafugaji wananunua dawa na kuzihifadhi nyumbani katika mazingira ambayo huchangia uharibifu wa dawa hizo. Idadi kubwa ya wafugaji (asilimia 95.6) hawajatembelewa na maafisa ugani na kupewa elimu ya ufugaji ambapo hutegemea kuelimishwa na wafugaji wenzao au kutumia uzoefu  katika kutibu mifugo yao.

Vilevile, asilimia 78.8 ya wafugaji waliripoti utupaji wa taka kutoka majumbani usiothibitiwa, asilimia 85 waliripoti kutupwa kwa dawa za binadamu na mifugo katika mazingira na asilimia 92.9 waliripoti uwepo wa shughuli za kilimo unaotumia mbolea za kuku na nguruwe ambao huchangia uchafuzi wa mazingira.

Vipimo vya maabara vimeonyesha uwepo wa vimelea sugu vya aina ya Escherichia coli na Klebsiella pneumoniae ambavyo vimeonesha usugu kwa madawa mbalimbali ambayo yanatumika mara kwa mara kutibu mifugo kama vile tetracycline, nalidixic acid, doxycycline, sulfamethoxazole-trimethoprim na ampicillin. Aidha, vimelea hivi vimeonesha usugu kwa makundi zaidi ya matatu  ya dawa zinazotumika sana kwa matibabu ya wanyama.

Tatizo linaloisumbua dunia

Usugu wa dawa ni tatizo ambalo kwa sasa limeikumba dunia na linaathiri zaidi nchi zinazoendelea. Kwa nchi hizi, ikiwemo Tanzania, ufugaji wa kuku na nguruwe unahusisha  matumizi makubwa na yasiyodhibitiwa ya dawa za binadamu na wanyama, hali ambayo inatishia kutokea na kusambaa kwa vimelea vya magonjwa ambavyo ni sugu kwa madawa ya kawaida yanayotumika kutibu wanyama na binadamu.

Vimelea hivi vya magonjwa vinasababisha magonjwa ya kuambukiza kwenye mazingira ya hospitalini na kwenye jamii tunayoishi.

Kuongezeka kwa mahitaji ya vyakula vya nyama na mazao yake nchini Tanzania kumesababisha kuongezeka kwa ufugaji wa kuku na nguruwe katika maeneo ya mijini na kwenye miji midogo.

Takwimu kutoka serikalini zinaonyesha kuwa uzalishaji wa nyama ya kuku umeongezeka kutoka tani 130,000 hadi tani 465,000 mwaka (2017 – 2020) na ule wa nguruwe umeongezeka kutoka tani 22,000 hadi tani 37,200 kutoka mwaka 2017 hadi 2020.

Mara nyingi wanyama hawa wanafugwa katika mazingira magumu yanayoambatana na msongamano mkubwa na mazingira duni ya usafi unaopelekea uwepo wa magonjwa mbalimbali.

Matokeo yake, wafugaji wanalazimika kutumia madawa mbalimbali kwa ajili ya kutibu magonjwa ya mifugo yao. Baadhi ya madawa ambayo hutumika sana ni pamoja na tetrasiklini, kwinini, salfa, penisilin, na dawa za minyoo.

Matumizi haya ya dawa yasiyo ya lazima na ya muda mrefu yamekuwa yakihusishwa na kutokea na kusambaa kwa vimelea sugu vya magonjwa ambavyo husambaa kwa wanyama wafugwao, mazingira, na hata kwa binadamu.

Uwepo wa juhudi za pamoja

Tafiti mbalimbali zilizofanyika zimebainisha kuwa vimelea vyenye vinasaba sugu vinaweza kusambaa kati ya binadamu na wanyama kupitia mazingira. Shughuli za kibinadamu na tabia zao ambazo huchangia kusambaa kwa vimelea sugu vya madawa ni nyingi sana kwa Tanzania na nchi zingine zinazoendelea.

Madawa mbalimbali, hasa ya kutibu wanyama, yanatumika pasipo kufuata taratibu, sheria na miongozo iliyopo na wakati mwingine madawa haya huuzwa hadharani bila ushauri wa wataalamu wa mifugo.

Kwa hali hii kuna uwezekano wa dawa kutolewa kwa ugonjwa ambao siyo sahihi, kukosewa kwa kiasi (dozi) anayopaswa kupewa mnyama na kushindwa kufuatilia na kutekeleza kipindi cha muda wa kuisha kwa dawa  (kinachoshauriwa kitaalamu) kabla ya kuuza mifugo na/au mazao yake.

Kwa bahati mbaya, sheria na kanuni za ufugaji bora pamoja na sheria zinazohusu ulinzi wa mazingira hazifuatwi kwa kiasi kikubwa. Hali hii hutoa mwanya wa kuwepo na kuenea kwa vimelea sugu vya magonjwa kwa wanyama ambavyo husambaa kwenye mazingira na hata kwa binadamu.

Tunashauri uwepo wa juhudi za pamoja, hasa uanzishwaji na utekelezaji wa miradi ya “afya moja”  ambayo itahusisha wadau kutoka sekta mbalimbali kutafiti, kuweka mikakati na kutekeleza mipango iyakayozuia kuwepo na kusambaa kwa vimelea sugu vya dawa kwa binadamu na wanyama.

Dk Zuhura Kimera ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na mtaalamu wa maswala ya usalama wa chakula na Afya moja. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia zuhurakimera@gmail.com. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Dk Zuhura Kimera

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved