The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kuna Ugumu Gani Kwa Serikali Kuwasikiliza Wamachinga?

Purukushani kati ya Machinga na mamlaka za miji zinaweza kumalizwa kwa mazungumzo yenye nia ya dhati baina ya pande hizo mbili.

subscribe to our newsletter!

Kwa mara nyingine tena Watanzania wameshuhudia mivutano kati ya wafanyabiashara wadogo, maarufu kama Machinga, na mamlaka za miji, mara hii ikiwa ni zamu ya Machinga wa jijini Mwanza walioamua kuingia barabarani kupinga kile kinachoitwa na Serikali “zoezi la kuwapanga.”

Mnamo Februari 8, 2023, majira ya asubuhi, Machinga katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini waliandamana kupinga uamuzi wa jiji la Mwanza kuwaondosha katikati ya jiji na vitendo vya askari wa jiji, maarufu kama mgambo, kuwachukulia bidhaa zao.

Ingawaje maandamano hayo yalisitishwa dakika chache tu baada ya kuanzishwa kwake, hatua ya wafanyabiashara hao wadogo kuamua kuchukua hatua hiyo inaashiria kushindwa kuzaa matunda kwa jitihada wanazochukua kufikisha kilio chao kwa mamlaka husika.

Ni katika mazingira haya ndiyo nauliza, kuna ugumu gani kwa Serikali na watendaji wake kukaa chini na Machinga na kuzungumza nao na kuona namna bora mifarakano hii isiyokuwa na faida yeyote kwa Machinga wenyewe na Serikali inaweza kuhitimishwa?

Swali hili nadhani ni la msingi ukizingatia ukweli kwamba hii siyo mara ya kwanza kwa Machinga katika maeneo mbalimbali ya nchi kukwaruzana na mamlaka za jiji, hali ambayo kwa kasi sana imeanza kuzoeleka kwenye macho na masikio ya Watanzania.

Kundi muhimu

Machinga ni kundi muhimu sana kwenye nchi yetu, likiwa ni kundi linalojumuisha Watanzania wa kila aina – wasomi na wasio wasomi – na mchango wanautoa kwa taifa hauwezi kudogoshwa.

Ni muhimu sana pia kufahamu kwamba kundi hili si kundi tunaloweza kulikwepa kwa kuzingatia namna ambavyo watawala wameamua kujenga uchumi wetu wa nchi na kuwahudumia wananchi wao. 

Kama tunavyofahamu, uchumi wetu uliojengwa katika misingi ya kibepari umekuwa ukiweka watu wa tabaka la chini pembezoni, hali inayowalazimisha watu hao kujiingiza kwenye biashara zisizo rasmi, kama hizo za umachinga. 

SOMA ZAIDI: MAKALA: Ni Nini Hatma ya Wamachinga Tanzania?

Ndiyo maana leo hii kundi hili la Machinga linazidi kukua kwa sababu, ukweli lazima usemwe, namna tunavyopangilia uchumi wetu unatufanya tushindwe kukabiliana na changamoto zinazotukabili kama taifa, kama vile janga kubwa la ukosefu wa ajira. 

Ni katika muktadha huo ndipo nashauri kwamba mtazamo wetu kama taifa juu ya Wamachinga lazima ubadilike. 

Badala ya kuwaona Machinga kama watu wanaochafua mazingira, tuwaone kama waathirika wa sera zetu mbovu za kiuchumi na kijamii zinazoshindwa kukabiliana na matatizo yanayotukabili.

Tukibadilisha mtazamo kutatusaidia kufanya mazungumzo ya kimkakati na Machinga kwani hatutawaona tena kama mizigo inayohitaji “kupangwa” ili kuweka mandhari ya jiji safi; hatutawaona Machinga kama wajinga wasiojua suluhu bora za namna ya kufanya biashara zao.

Machinga, kote nchini, wana majibu yote ya maswali ambayo maafisa wa mamlaka za miji hudai kuyatafutia majibu. 

Machinga, kwa mfano, wanajua ni maeneo gani wanaweza kukaa bila kuathiri maslahi ya jiji na kwenda mbali zaidi hata kupendekeza utaratibu mzuri wa kufanya shughuli zao.

Kule Mwanza, kwa mfano, Machinga waliogoma waliwaambia waandishi wa habari kwamba yapo maeneo ambayo wao wakiruhusiwa kufanya shughuli zao huko hawawezi kulalamika. 

Waliyataja maeneo hayo ni kama vile Makoroboi, Saharana na Dampo. 

Kitu hicho hicho kimeshawahi kupendekezwa na Machinga kutoka maeneo mengine ya nchi, ikiwemo Dar es Salaam, jiji kuu la biashara Tanzania.

Haki jiji

Kitu kingine ambacho Machinga hao walinukuliwa wakisisitiza ni haki yao ya kutumia jiji. Hii, kwa kweli, ni hoja ya msingi sana ambayo mamlaka za jiji zinapaswa ziichukulie kwa uzito mkubwa sana. 

Tusijenge miji yetu ikawa ni miji ya kibaguzi kwa kuwepo kwa miji ya watu wa chini (walalahoi) na miji ya watu wa juu (walalaheri na walalahai). 

Mmoja wa Machinga kule Mwanza alisema kwamba anaona kama kuna matabaka yamewekwa, kwamba baadhi ya watu sehemu yao ni mijini na wengine ni vijiji. 

Ni muhimu sana kwa mamlaka za nchi kuhakikisha kwamba hofu hii ya Machinga kama huyu, na naweza kusema hayuko peke yake katika kuwaza hivyo, inashughulikiwa kwani madhara ya kupuuzia yanaweza kuwa ni makubwa kuliko tunavyoweza kufikiria.

Waswahili wanasema usipoziba nyufa, utajenga ukuta! 

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hili la Wamachinga Linanisononesha Sana

Kila mtu anapaswa kuwa na haki ya kutumia jiji kwa namna ambayo haileti madhara kwa mtumiaji mwengine. ‘Haki jiji’ ni haki kama zilivyo haki zingine na ni lazima mamlaka za nchi ziiheshimu.

Ni muhimu kuondokana na mtazamo kwamba mji kuwa msafi ni kuwaondoa Machinga na makundi mengine kama vile ombaomba, wasio na makazi na mama ntilie. 

Wamachinga na matabaka mengine ya chini si sehemu ya kuchafuka kwa miji. Tunaweza kuja na kampeni za kuweka majiji yetu safi na Machinga kuendelea kufanya shughuli zao bila kuathiri kampeni hizo.

Machinga ni watu ambao wanatafuta maisha yao kwa kupitia biashara zao halali. Kwa hiyo, mtazamo kwamba Machinga ni sawasawa na uchafu ni lazima upigwe vita na uondolewe. 

Lazima iwekwe namna ya Machinga kuwa katika maeneo ya mjini na kufanya biashara zao kwa uhuru. 

Na kwangu mimi, tafsiri ya Machinga inaenda mbali zaidi ya hii ya watu wanaofanya biashara zisizo rasmi. 

Kwangu, Machinga pia hujumuisha madereva wa bajaji na bodaboda, mamalishe/mamantilie, baba ntilie, wavuvi wadogowadogo, wauza miwa na karanga barabarani.

Ni muhimu tuipe miji yetu tafsiri ya kwetu sisi, siyo ile ya Ulaya. Sisi tuna muktadha wetu tofauti na nchi za Ulaya, lazima tujue hili. Sisi huku walio wengi ambao masikini ndiyo wanatumia bidhaa, na usafiri wa tabaka hili la Machinga. 

Kwa hiyo, maamuzi yetu kwenye sera na sheria zetu lazima zitambue kuwa uchumi wetu unazalisha matabaka ya hali ya chini haya na jukumu letu ni kuwasikiliza na kujadiliana nao katika namna ya kuendesha biashara zao.

Tuzungumze 

Lakini hatuwezi kufikia hatua hiyo kama hatutakaa chini na Machinga na kuwa na mazungumzo ya kijitukizima na wao. Mazungumzo haya yatatufanya tuelewe Machinga wanatafsiri vipi biashara zao? Wanapata vipi faida zao? 

Tusiishie tu “kuwapanga” na kukaa na kikundi kidogo cha viongozi wao. Lazima tuchukue jitihada za makusudi zinazolenga kutufanya tuelewe maisha yao ya kila siku: wanaishije, mitaji yao ni ipi, hali zao nakadhalika. 

SOMA ZAIDI: Machinga Aliyevua Nguo Kuzuia Meza za Wenzake Kuhamishwa Afunguka

Kwa hiyo, rai yangu ni kwamba tutumie muda mwingi kujielimisha juu ya hali za Machinga kabla ya kutekeleza hilo zoezi la “kuwapanga.” 

Hofu kubwa ya Machinga ni uhuru wao wa kufanya biashara zao na kuishi maana bila kazi huwezi kuishi. 

Na nadhani ni jukumu la waliopewa dhamana ya uongozi wa nchi kuwahakikishia Machinga kwamba wataendelea kuwa huru kufanya biashara zao na hivyo kuendelea kuishi kwenye nchi hii.

Ni ipi basi njia nzuri ya kufanya hivyo mbali na kuchukua uamuzi wa kuwasikiliza Machinga, uamuzi ambao msingi wake unatokana na nia ya dhati ya kutaka kufahamu masaibu yao na kutafuta suluhu za pamoja?

Nassoro Kitunda ni Mhadhiri Msaidizi wa Sosholojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *