The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zitto Kabwe: Hili la Wamachinga Linanisononesha Sana

Kwenye sehemu ya pili ya mahojiano na mwanasiasa huyo, Zitto anafafanua kinachoendelea nchini Ethiopia pamoja na kutoa tathmini yake ya Serikali ya Rais Samia.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Hii ni sehemu ya pili ya mahojiano maalum kati ya The Chanzo na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mnamo Novemba 27, 2021, ambapo pamoja na mambo mengine mbunge huyo wa zamaoni Kigoma Mjini anafafanua mgogoro unaoendelea hivi sasa nchini Ethiopia baina ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa TPLF ambao mpaka sasa umegharimu maelfu ya maisha ya raia wa Ethiopia na kuwafanya wengine wengi kukimbilia uhamishoni.

Zitto anatueleza kiini cha mgogoro huo na kipi anadhani kinapaswa kufanywa kurejesha hali ya utulivu nchini humo, akisisitiza umuhimu wa majadiliano katika juhudi za utafutaji wa suluhu. Pia, anaeleza tathmini yake ya juhudi zinazofanywa na Umoja wa Afrika katika kuleta amani nchini humo pamoja na nini Tanzania kama nchi inaweza ikafanya kuchochea juhudi hizo.

Kwenye sehemu hii pia ya mahojiano yetu na Zitto, mwanasiasa huyo anaeleza tathmini yake ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na takribani miezi 10 tangu achukue hatamu za kuliongoza taifa la Tanzania hapo Machi 19, 2021. Zitto anaeleza unafuu wa kisiasa uliokuja na uongozi wa Rais Samia, akisema angalau sasa hatembei akiangalia nyuma kama kuna mtu anamfuata.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo anaeleza kusikitishwa na baadhi ya hatua ambao Serikali ya Rais Samia imezichukua ambazo anadhani zinawarejesha nyuma Watanzania kisiasa na kiuchumi. Hatua hizi ni pamoja na uamuzi wa Serikali kumfungulia mashtaka ya ugaidi Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe; Samia kusita kukutana na viongozi wa vyama vya siasa licha ya kuahidi kufanya hivyo; pamoja na uhamishaji wa wamachinga kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya miji kwa kile mamlaka inakiita ni ‘kuwapanga.’

The Chanzo: Tuje kwenye kinachoendelea hivi sasa nchini Ethiopia. Watu wamekupa jina Balozi wa Tigray [nchini Tanzania]. Sasa sijui hiko cheo una kikataa au una kikubali, lakini kusema ukweli kumekuwa na habari nyingi za kutoka Ethiopia zinazo ripotiwa kwenye vyombo vya habari. Wasiwasi wangu ni kuwa mwananchi wa kawaida anaweza kuwa hafahamu kiundani nini hasa kitakuwa kinaendelea kule. Nilikuwa nataka tutumie fursa hii kutueleza kwenye lugha ambayo hata bibi yangu kule kijijini anaweza akaelewa, nini haswa kinaendelea hivi sasa nchini Ethiopia?

Zitto Kabwe: Ethiopia kuna mgogoro wa kisiasa, ni mgogoro wa kisiasa haswa. Chama ambacho kina ufuasi mkubwa katika mkoa wa Tigray, chama cha TPLF, ambacho hapo kabla kilikuwa chama ambacho kina ushawishi mkubwa kwenye uongozi wa Ethiopia nzima. Hata huyu Waziri Mkuu wa sasa alikuwa ni sehemu ya muungano wa vyama ambavyo TPLF ilikuwemo. Chama kile kimegombana kimtazamo na Waziri Mkuu aliyopo madarakani Abiy Ahmed.  Wamegombana kwa sababu Abiy Ahmed muono wake ni Ethiopia ya miaka ya sabini. Himaya. Ethiopia moja, Ethiopia ambayo haitambui utofauti wa jamii mbalimbali ndani ya Ethiopia.

Kwa sababu unajua watu wanasema Ethiopia haikutawaliwa na wakoloni, ndio sifa kubwa ya Ethiopia.  Ila kitu kimoja ambacho hakisemwi sana ni kuwa Ethiopia ilikuwa ni mkoloni ndani ya Ethiopia. Kwa sababu kinachoitwa Ethiopia leo ni mchanganyiko wa mataifa tofauti tofauti, na kuna mataifa ambayo yalikuwa watawala kama wa Amhara na kuna mataifa yaliyokuwa wanakandamizwa kama wa Oromo ambao ndio wengi, zaidi ya asilimia 36 ya Waethiopia wote, na ndio wamekandamizwa kwa muda mrefu sana toka wakati wa Wafalme, toka wakati wa Meneliki, toka wakati wa Haile Silas, toka wakati wa Mengistu Haile mariam.

Hata baada ya TPLF kuingia serikalini na kuwa kwa miaka 30 hawakutenda mazuri kwa hao wa Oromo. Kwa hiyo, ni taifa ambalo limekuwa likikandamizwa kwa muda mrefu. Sasa Abiy Ahmed anataka kurudi kwenye Ethiopia hiyo ya kihimaya. Ethipia moja. Lakini hawa TPLF ni watu wanaoamini katika kitu kinaitwa ethnic federalism, kutambua haki ya jamii zingine ndani ya Shirikisho la Ethiopia. Kwa hiyo, wakati Abiy Ahmed amekuwa Waziri Mkuu amekuwa akifanya juhudi kutaka vyama vyote vilivyokuwa vinaunda chama tawala wakati ule ambacho ulikuwa muungano wakati ule vijivunje kuwa chama kimoja kinachoitwa Prosperity Party.

TPLF wakakataa na hapo ndipo taharuki zilipoanza na mwaka jana, Novemba 4, 2020, Jeshi la Ethiopia likavamia huo mkoa wa Tigray. Yaani tuseme kama Jeshi la Tanzania likavamie Mtwara.

The Chanzo: Kwa nini lilivamia?

Zitto Kabwe: Lilivamia kwa sababu ya huo mgogoro uliotokana na TPLF kukataa [matakwa ya Aby Ahmed]. Maana walipokataa kujiunga  kwenye hiko chama kimoja cha Prosperity Party wao wakaamua kurejea Tigray, wakaita uchaguzi ndani ya Tigray, Waziri Mkuu akaukataa ule uchaguzi ndani ya Tigray kwa sababu aliamuru uchaguzi Ethiopia nzima usubiri kupisha UVIKO-19, wao [TPLF] wakaendelea na ule uchaguzi na wakachaguliwa. Kwa hiyo, ikaonekana wanaenda kinyume na maagizo ya Serikali ya shirikisho.

The Chanzo: Si kweli kwamba wanamgambo wa TPLF walishambulia kambi ya kijeshi [ya Jeshi la Ethiopia], si ndio?

Zitto Kabwe: Hiyo ndio propaganda ya Abiy Ahmed.

The Chanzo: Wewe unasema propaganda lakini si ni taarifa?

Zitto Kabwe: Hiyo ndio propaganda  ya Abiy Ahmed. Hakuna ushahidi wowote [kwamba hilo shambulio lilitokea]. Hata jumuiya ya kimataifa walipofanya kutafuta chanzo cha vita ni dhahiri kabisa TPLF haikuishambulia kambi ya jeshi.

The Chanzo: Yawezekana kuna huo mvutano tayari, kwamba wao hawaungi mkono  hiyo Prosperity Party, lakini nini haswa kilipelekea vikosi vya Ethiopia kuvamia Tigray?

Zitto Kabwe: Abiy Ahmed aliamini sasa TPLF hawana uwezo wa kupigana,  aliamini ni dhaifu. Kwa hiyo, ulikuwa ni muda wa kushambulia, hilo moja. Lakini pia kumbuka Abiy Ahmed ameivamia Tigray na majeshi yake siku ya uchaguzi wa Marekani. Abiy Ahmed na utawala wa Donald Trump walikuwa na ukaribu mkubwa sana na Abiy Ahmed aliamini yanaweza yakatokea mabadiliko ya kisera ya Marekani. Kwa hiyo, akaona awahi kuivamia na kuishika Tigray kabla Rais mpya wa Marekani hajaingia madarakani.

Ndio maana ilikuwa ni vita vya kikatili, ndio maana walivamia kutoka pande tatu tofauti. Amhara walikuwa upande wao. Jeshi la Eritria lilikuwa upande wao na ENDF [Jeshi la Ethiopia] liliingia upande wao. Watu wengi waliuwawa, wanawake walibakwa, watu wengi walikimbia kwenda ukimbizini kwenda Sudan. Hiko unachokiita kilipelekea huo uvamizi kwa uchambuzi wangu mimi ilikuwa ni kuwahi mabadiliko Marekani kama yangetokea yakute tayari ameshashinda ile vita. Lakini bahati mbaya kafanya [Abiy] alipiga mahesabu yake vibaya kwa sababu  ni vita ambayo iliendana na propaganda kubwa dhidi ya watu wa Tigray.

The Chanzo: Kwa hiyo kiini cha mgogoro ni kipi, kwani kweli watu wa Tigray wanaona wametengwa kwenye chama kipya cha Prosperity Party?

Zitto Kabwe: Hapana, kwa sababu waliambiwa waungane kwenye Prosperity Party walikataa, na walikataa kwa sababu wana historia, wanajua.

The Chanzo: Kwa hiyo kiini ni nini? Kwa mfano, mtu akitaka kujua madai ya watu wa Tigray, ni yepi?

Zitto Kabwe: Katiba ya sasa ya Ethiopia iheshimiwe. Katiba ambayo inatambua uhuru wa mikoa mbalimbali ndani ya Shirikisho. Kitu ambacho  Abiy Ahmed anakiogopa. Hilo tu.

The Chanzo: Hicho tu?

Zitto Kabwe: Umezidiwa maneno? [kicheko]

The Chanzo: Kitu kingine ninachotaka kufahamu, wewe binafsi kwa nini unawahurumia TPLF?

Zitto Kabwe: Naungana na watu wanaokandamizwa, huo ndio msimamo wangu. Kwa sababu wanateswa na mimi kanuni ya maisha yangu ni kusimama na ambaye anateswa popote. Ukitazama nyuma kabla ya Novemba 4 mimi nilikuwa mshabiki mkubwa wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed.  Angalia mpaka nyakati ambazo Ethiopia Airlines inabeba misaada ya UVIKO-19 kusambazwa kwenye nchi mbali mbali za Afrika au wakati Abiy Ahmed anashughulikia mgogoro wa Sudan, 2019. Utaona nilikuwa mshabiki mkubwa wa Abiy Ahmed.

Lakini kwa kuwa aligeuka kuwa katili, akaanza kuua raia wake, kuanza kubaka wanawake wa taifa lake, kunyima misaada ya  chakula kwa watu kwa sababu ya kabila lao, kuwaondoa kwenye kazi zao watu wote wanaotokea kwenye kabila hilo la Tigray.  Na Khalifa [Said, mwandishi] katika kukua kwangu nimeshuhudia madhara ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, sisi peke yetu, familia yetu iliwapokea zaidi ya wakimbizi 20 wa familia moja waliokuwa wamekimbia Rwanda wakafika mpaka Kigoma, tukaenda kuwachukua barabarani na kuweza kuwatunza mpaka pale Umoja wa Mataifa ilipoanzisha mahali pa kuwahifadhi.

Kwa hiyo, nimeona madhara ya mauaji ya kimbari.   Kwa hiyo, nikiona mauaji yoyote ambayo yana lenga rangi au kabila yanapelekea mauaji ya kimbari nahuzunishwa sana.

The Chanzo: Kwa nini Abiy anakuwa na wasiwasi na mataifa ya Magharibi?

Zitto Kabwe: Huo ni wasiwasi wa ujanja wa kivita tu, Abiy amekuwa akisaidiwa na watu wa Magahribi muda wote.

The Chanzo: Namaanisha katika huu mgogoro unaoendelea?

Zitto Kabwe: Kwa sababu mataifa ya Magharibi yametaka ukweli. Kwa sababu mataifa ya magharibi yametaka watu wakae mezani wajadiliane. Yeye [Abiy] anataka kutumia mbinu ya kivita kwamba ni Afrika dhidi ya mabeberu. Mbinu ambazo watu wengi wamekuwa wakizitumia kukandamiza watu wao. [Robert] Mugabe alitumia dhidi ya Wazimbabwe. [John] Magufuli alitumia hiyo kwa kiasi kikubwa mpaka tulikuwa tunaitwa hapa makuwadi wa mabeberu. Ni sawa sawa tu [na anachokifanya Abiy]. Ni maneno matupu. Abiy hajawahi kujitambulisha na Umajumui wa Afrika hata mara moja. Hakuna ushahidi wa Abiy kujitammbulisha na Uafrika wake, hakuna ushahidi. Anatumia hili ili kuweza kutafuta kuungwa mkono na Afrika lakini amechelewa.

The Chanzo: Unajua yeye ni Waziri Mkuu wa nchi, pengine anazo taarifa za kiusalama kwamba kuna mataifa yanaipa Tigray kiburi?

Zitto Kabwe: Kama kweli kuna mataifa yanaipa kiburi TPLF au watu wa Tigray yatakuwa mataifa ambayo yanaumizwa na mauaji ya kimbari. Kumbuka baada ya mauaji ya Rwanda kumekuwa na kovu duniani, hasa kwa mataifa ya magharibi, kwa sababu yalipuuzia mauaji ya Rwanda na hatimaye watu wengi walikufa na ndio hali hiyo hiyo hasa inayoendelea Tigray.

The Chanzo: Wana mgambo wa Tigray wanaweza wakawa wanapata wapi silaha zao?

Zitto Kabwe: Kumbuka kwamba Jeshi la Ethiopia asilimia 70 lilikuwa na watu wa Tigray. Kumbuka kwamba watu wa Tigray ndio waliikomboa Ethiopia mwaka 1991. Anayeongoza vita sasa Army General wa TPLF alikuwa Mkuu wa Majeshi ya Ethiopia. Kwa hiyo, watu wanaohoji TPLF wanapata wapi silaha, wanapata wapi nguvu ni watu ambao hawajui historia ya TPLF.

The chanzo: Kwa hiyo wanaweza wakawa wanapata wapi, wanapata toka kwa Jeshi la Ethiopia?

Zitto Kabwe: Wanazo.

The Chanzo: Na si kwamba wanaweza kupata silaha kutoka sehemu nyingine?

Zitto Kabwe: Kama ambavyo Abiy anapata silaha toka Umoja wa Falme za Kiarabu. Juzi umeona habari ya kiuchuguzi ambayo imetolewa na Al Jazeera kuonyesha U.A.E na Uturuki pia wakimsaidia Abiy.

The Chanzo: Lakini Ethiopia si ni nchi? Unadhani Tigray ina mamlaka ya kupokea misaada ya silaha?

Zitto Kabwe: Wapiganaji wa Tigray wanavamia kambi za majeshi ya Ethiopia, wanashinda wanachukua silaha. Hivyo ndivyo vuguvugu la waasi linavyokuwa.

The Chanzo: Hivyo ndivyo wanavyopata silaha zao?

Zitto Kabwe: Ninavyo elewa mimi na sijaona ushahidi wowote dhidi ya hilo.

The Chanzo: Juhudi zinazoendelea sahizi ni za kutafuta amani hali irudi kama ilivyokuwa zamani watu waendelee na shughuli zao kama za kiuchumi. Tanzania, kwa mfano, ina nafasi gani katika kuhakikisha amani inarejea Ethiopia?

Zitto Kabwe: Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kusimama na wanaoonewa. Haijafutwa sera hiyo ya mambo ya nje ya Tanzania. Kwa hiyo, Tanzania inapaswa kumwambia wazi wazi Abiy Ahmed kaeni mzungumze mumalize mgogoro huu wa kisiasa ambao mpaka sasa umesababisha mauaji ya watu wengi sana na unaweza kusababisha mauaji ya watu wengi zaidi. Kwa hiyo, Tanzania ichukue uongozi kama ambavyo imekuwa siku za nyuma kuhakikisha pande zote mbili zinazopigana zinakaa chini kuzungumza.

The Chanzo: Wewe ni mwanasiasa na ni kiongozi pia, ungekuwa kwenye nafasi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ungechukua hatua gani kwa hali hii inayoendelea?

Zitto Kabwe: Nisingefika hapo ambapo hali ilipo.

The Chanzo: Ndio umeshafika.

Zitto Kabwe: Nisingeruhusu nifike. Kwa sababu Abiy Ahmed alikosea sana kwenye mahesabu yake ndiyo maana leo tuko hapa. Kama angekuwa anasikiliza wenzake [tusingefika hapa].   Mimi mwaka 2019 nilikutana na mmoja wa viongozi wa Ethiopia, mmoja wa Mawaziri Wakuu wastaafu wa Ethiopia na akanambia Ethiopia itawaka moto. Kwa sababu moja, Abiy Ahmed anaamini Uwaziri Mkuu amepewa na Mungu. Kwa hiyo, chochote anachokifanya ametumwa na Mungu. Kwa hiyo, hawezi kumsikiliza mtu yoyote. Anaweza kumsikiliza Mungu tu. Hakuna mtu yoyote anayeweza akaingia kati kati.

The Chanzo: Lakini alianza vizuri, alifungua wafungwa wa kisiasa na wewe mwenyewe unasema ulikuwa mshabiki wake.

Zitto Kabwe: Ni kweli lakini baada ya mwaka mmoja akaanza kuwafunga. Leo tunapozungumza kiongozi wa wa watu wa Oromo alikuwa yupo nje [ya nchi] karudi [Ethiopia] kwamba kuna uhuru, sahizi yupo ndani hivi tunavyoongea.

The Chanzo: Ungefanya nini sasa kama ungekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia?

Zitto Kabwe: Nisingeifikisha Ethiopia hapa.

The Chanzo: Ndio tumeshafika, tupo kwenye mgogoro ndugu Zitto.

Zitto Kabwe: Nisingefika hapa na kama ingekuwa imefika hapa, labda sasa ndio nimekuwa Waziri mkuu wa Ethiopia ningekwenda mezani kuzungumza kupatajawabu.

The Chanzo: Na unazungumza nini?

Zitto Kabwe: Kuzungumza namna gani ya kutatua tatizo hili. Mazungumzo tu ndio yanayoweza kumaliza hili jambo. Hakuna atakayeshinda vita msituni.

The Chanzo: Tigray wao wanataka wajitenge?

Zitto Kabwe: Watu wa Tigray wanataka Katiba ya Ethiopia iheshimiwe. Katiba ya Ethiopia inaruhusu watu kujitawala. Ni Katiba pekee katika bara la Afrika ambayo imewapa uhuru wananchi  kwa kupiga kura ya maoni kuamua kama wanataka kuwa sehemu ya himaya fulani au hapana. Na watu wa Tigray wanachokitaka ni Katiba ya Ethiopia iheshimiwe. Hakuna cha ziada.

The Chanzo: Una tathmini vipi mchango wa Olusegun Obasanjo na Umoja wa Afrika katika juhudi za kutafuta suluhisho la mgogoro unaoendelea Ethiopia?

Zitto Kabwe: Wakati Abiy alipovamia Tigray mara ya kwanza AU walitoa tamko la kumpongeza Abiy kwa uamuzi ule. Kwa hiyo, jambo kama hilo tayari limevunja imani kabisa ya watu wa Tigray kwamba [AU] wana upande [kwenye huu mgogoro]. Mzee Obasanjo mpaka sasa amefanikiwa kuonana na pande zote na amesema wazi wazi kwamba jawabu la mgogoro wa Tigray ni la kisiasa sio la kivita.

Lakini kama unavyofahamu leo tunavyozungumza Waziri Mkuu wa Ethiopia yuko mstari wa mbele kuongoza wanajeshi wake. Kwa hiyo, vita bado inaendelea licha ya hizo juhudi Obasanjo amezifanya. Nimezungumza na timu ya mzee Obasanjo. Matumaini yao yalikuwa juu sana na natumaini watajitahidi kuweza kufanya.

Lakini nadhani kuna wakati Umoja wa Mataifa waliteua mjumbe maalum kufanya kazi na mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika wakati ule wa mgogoro waJamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati ule wa mgogoro wa M23 ambao Tanzania ilipeleka kikosi kuwaondoa wale M23. Ili kuondoa hiyo kutokuaminiana ambayo watu wa Tigray na uongozi wa TPLF wanayo dhidi ya Umoja wa Afrika.

Nadhani Umoja wa Mataifa ungeteua wajumbe maalum wawili, yaani mmoja wa Umoja wa Mataifa na mwingine wa Umoja wa Afrika waweza kufanya kazi kwa pamoja ili huyu wa Umoja wa Mataifa aweze kuweka sawa hiyo kutokuaminiana.

Lakini naona Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wameamua huyu Obasanjo awe mjumbe maalum wa wote kwa pamoja nadhani ni kwa sababu ya mafanikio ambayo alikuwa ameyafikia katika majadiliano.

Lakini hatuyaoni hayo mafanikio. Watu wapo vitani wanapigana.  Umoja wa Afrika una hiyo nakisi ya kutokuaminika. Kuna ambao hawaiamini wanaona ni kama klabu ya viongozi ambao wanabebana tu hawawezi kukosana, hawawezi kuelezana kwamba hapa umekosea, hawawezi kuwajibishana na hilo ndio nadhani tatizo kubwa zaidi la Umoja wa Afrika.

The Chanzo: Tuishie hapa kwenye hili suala, turudi nchini Tanzania. Machi 19, mwakani [2022] Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa anatimiza miaka miwili kamili tangu awe Rais wa awamu ya sita wa Tanzania. Kama ungepata fursa kwa kipindi hiki ambacho ameongoza tangu Machi 19 mwaka huu, kama ungekuwa na fursa ya kumpa maksi kati ya moja mpaka kumi. Yaani moja ni nzuri sana na kumi ni mbaya sana, wewe ungempa maksi ngapi?

Zitto Kabwe: Tatu.

The Chanzo: Tatu, kwa nini?

Zitto Kabwe: Kwa sababu, kwanza hakuna mtu anayeweza kupata moja, hakuna kiongozi yoyote wa kisiasa anayeweza kupata moja akafanya vizuri sana kwa asilimia mia moja.  Yoyote yule hata [Mwalimu Julius] Nyerere [Rais wa kwanza wa Tanzania]. Hakuna.

The Chanzo: Unampa tatu chini ya kumi?

Zitto Kabwe: Umesema moja ni nzuri sana na kumi ni mbaya sana.

The Chanzo: Ndio ndio.

Zitto Kabwe: Kwa hiyo hapati mbili kwa sababu hapa tunapozungumza nchi haijaletwa pamoja kama alivyohaidi yeye mwenye. Tunapozungumza hapa kiongozi wa chama cha upinzani, [Freeman Mbowe, Mwenyikiti wa CHADEMA], chama kikubwa kabisa nchini yuko jela. Hiyo inamuondoa kupata mbili kwa sababu hilo tu ni jambo linalozidi kuweka watu mbali.  Kwa hiyo, mbili naiondoa. Tatu, kwa sababu sasa angalau tuna uhuru wa kuzungumza [na] wa kutembea. Kama nilivyosema [hapo awali kwamba hivi sasa] huangalii nyuma nani anakuona nani hakuoni. [Vyombo vya habari] mnafanya mahojiano yenu bila matatizo yoyote. Kwa hiyo, moja na mbili kwangu hapana, angepata tatu.

The Chanzo: Kwa mtazamo wako unadhani ni changamoto gani za kimsingi ambazo Rais Samia na uongozi wake wanakabiliana nazo kwa sasa?

Zitto Kabwe: Hofu ya mabadiliko ndio changamoto kubwa. Namna ambayo Rais Samia ameingia madarkani sio namna ya kawaida, kwa sababu baada ya mtu kufariki. Amerithi mfumo ambao umewekwa sio tu kwamba na mtangulizi wake ni mfumo wa muda mrefu wa Chama cha Mapinduzi [CCM, chama tawala]. Chama ambacho kimeshika dola kwa muda mrefu. Kutegemea kwamba anaweza kubadilisha mara moja, mtu yoyote ambaye ni mwanasiasa na anafikiria vizuri, sio kufikiria kwa mrengo wa kisiasa, atakuwa anakosea sana, haiwezekani.

Kwa sababu ni mfumo uliojikita vilivyo, unajua yeye [Samia] ni Rais mwanamke wa kwanza na unajua ni kwa kiwango mfumo dume umejikita nchi hii. Lakini ni Mzanzibari wa pili kuwa Rais, unajua mahusiano ya kimtazamo ambayo hayaandikwi, hayasemwi lakini tunajua namna ambavyo Watanganyika wanavyowatazama Wazanzibari na Wazanzibari wanavyowatazama Watanganyika. Kwa hiyo, kwa mtu yoyote anayejua vizuri muktadha wa utawala na historia ya  nchi yetu anaelewa ni kwa nini anaenda taratibu.

Lakini ingeweza kufanyika bora zaidi. Kwa mfano, hoja yangu mimi siku zote nini kilipelekea Serikali ya Rais Samia kumuweka ndani Mbowe? Kwa sababu ni jambo ambalo halina faida yoyote kwa Serikali. Haliiongezei Serikali chochote. Inaongeza chuki tu.

The Chanzo: Nini kimefanya Samia ashindwe kukutana na nyie viongozi wa kisiasa mpaka sasa?

Zitto Kabwe: Sasa hili nadhani anapaswa yeye mwenyewe kulijibu. Sisi mara kwa mara tumekuwa tukikumbusha. Kwanza, alisema mwenyewe na pili tumekuwa tukiandika barua mara kwa mara. Juzi tu hapa kama Mwenyekiti wa [Kituo cha Demokrasia Tanzania] TCD nimetoka kuandika barua nyingine kukumbushia na hakuna iliyozaa matunda mpaka sasa. Nini kinapelekea hivyo, ni vigumu sana sisi kama viongozi wa upinzani kufahamu. Ila siku ukipata nafasi ya kumfanyia mahojiano utamuuliza ni nini kinafanya usikutane na viongozi [wa vyama vya upinzani].

The Chanzo: Sijui kama nimekuelewa vizuri, umesema unadhani ni ngumu sana kwa Rais Samia kubadilisha mfumo ambao ameukuta?

Zitto Kabwe: Kubadilisha kwa haraka, sio kwamba haiwezekani, inawezekana.

The Chanzo: Wewe ni mzoefu umekuwepo bungeni, umekuwa Mwenyekiti wa Kamati [za Bunge]. Unadhani inaweza ikachukua siku ngapi kuweza kuandaa muswaada unaobadilisha sheria mbali mbali ambazo ni kandamizi?

Zitto Kabwe: Sio rahisi kama hivyo unavyofikiria. Inaweza ikachukua siku moja na inaweza ikachukua muda mwingi usioelezeka. Inategemeana na mazingira ya kisiasa ya wakati huo. Kwa sababu unapoingia madarakani kwa namna ambayo Rais wetu wa sasa ameingia madarakani, ni lazima uwe na muda wa kufanya kitu kinachoitwa power consolidation. Ukishakuwa ume consolidate power sasa unaweza kutengua  vitu vilivyofanya na mwingine. Kutokana na asili na msingi wa mfumo wetu jinsi ulivyo, lazima tufahamu mfumo huu ni mfumo ule ule wa Chama cha Mapinduzi. Ni mfumo hodhi, ni mfumo ambao dola halitaki kuachia kabisa. Kwa hiyo, unahitaji kiongozi ambaye ameishika sawa sawa dola, ameyashika madaraka yake sawa sawa kuweza kufanya mabadiliko anayoyatakiwa kufanywa.

The Chanzo: Sasa hivi maana yake hana hiyo sifa?

Zitto Kabwe: Hiyo sio sifa.

The Chanzo: Uwezo?

Zitto Kabwe: Huo sio uwezo, huo ni mchakato. Samia, baraza lake la mawaziri wangapi ni wapya? Mfumo wa polisi ni wale wale, usalama ni wale wale, jeshi ni wale wale na kadhalika. Mfumo bado ni ule ule na haina maana lazima uwatoe hao unaowakuta ila ni lazima ujihakikishie sasa naweza nika waamuru. Lakini nani ametuambia yeye anaamini katika hayo mabadiliko [ambayo sisi tunayataka ya kisheria?].

The Chanzo:  Unadhani yeye haamini?

Zitto Kabwe: Mimi sijui, sijui kwa sababu hatuwezi kumuwekea maneno mdomoni. Mimi ninachokifahamu kwamba CCM ni ile ile. Mfumo ni ule ule wa Chama cha Mapinduzi tofauti ni kwamba yeye si sawa na Magufuli. Na hiki kitu napingana na watu wengi. [Samia na Magufuli] ni watu tufauti kabisa, wana utofauti mkubwa walivyojitabanaisha kwenye siasa na maisha yao, labda inawezekana sisi tunadhani tukitumia mbinu ile ile  ya wakati wa Magufuli ndio tutafanikiwa kupata mabadiliko sasa au tunahitaji kuyatazama mazingira na kuifikira upya mbinu inayoweza kuleta mabadiliko yanayotakiwa. Na hapa isiwe tu  unatazama upande mmoja tu kuna haja pia ya sisi wenyewe kujitazama.

The Chanzo: Nyie kama wapizani?

Zitto Kabwe: Wana mabadiliko. Kwa sababu sio wapinzani tu wanaotaka mabadiliko na watu wengine pia. Asasi za kiraia zinataka mabadiliko.

The Chanzo: Na waandishi pia tunataka mabadiliko.

Zitto Kabwe: Sheria kandamizi zimeumiza waandishi wa habari, wafanyabiasha na kadhalika. Inahitajika kujenga mshikamano mkubwa wa makundi mbalimbali kuweza kuharakisha hayo mabadiliko unayoyataka.

The Chanzo: Mimi na wewe tumekuwa tukifuatilia kwa karibu Hayati Magufuli alivyokuwa anaendesha hii nchi na ameweza kusukuma nyuma mambo mengi. Kwa kuangalia, kusema kweli, unaweza kusema yalitokana na utashi wake binafsi yeye mwenyewe, sasa inawezekana siko sawa. Alikuwa na uwezo, kama tulivyosema hapa, kupiga marufuku watoto waliopata ujauzito masomoni na wewe umezungumza ilikuwa kinyume na sheria na sera lakini likaenda kutekelezwa.  Watu wake wa Chama cha Mapinduzi wakawa wanamtetea, wabunge walimtetea na unaweza kusema alitumia utashi wake …

Zitto Kabwe: Kuteka watu, kuua vyama. Kwa hiyo, na Samia atumie utashi wake?

The Chanzo: Subiri nimalize, hapana simaanishi hivyo. Kwamba atumie utashi wake kusukuma mambo mbele, kukutana na wana mabadiliko umezungumza, atumie utashi wake kukutana na wanamabadilko, awatoe watu walio ndani kwa kesi za kubambikiwa kitu ambacho kilifanyika na tunashukuru. Unadhani huo utashi unashindikana vipi kwa sababu tunajua kuna masheria mengi yalipitishwa kwenye awamu iliyopita, huo utashi unakosekana vipi wakati Magufuli aliutumia utashi huo huo kurudisha mambo nyuma miaka ishirini iliyopita, nini kinakosekana kwa Rais Samia kutumia utashi huo huo kupeleka mambo mbele?

The Chanzo: Hilo ni swali ambalo unapaswa yeye mwenyewe kumuuliza.

Zitto Kabwe: Nakuuliza wewe kama mchambuzi.

The Chanzo: Kama mchambuzi nitakuambia kitu kimoja. Hawa ni watu wawili tofauti. Hawa ni watu wenye mtindo tofauti wa uongozi. Huwezi kumfanya mmoja kufuata mtindo wa mwingine. Ni njia hiyo hiyo watu walikuwa wakijaribu kumtazama Magufuli na [Jakaya] Kikwete au Kikwete na [Benjamin] Mkapa au Mkapa na [Ali Hassan] Mwinyi au Mwinyi na Mwalimu [Nyerere]. Kila kiongozi ana namna yake.

Ila kitu kimoja ninakijua hawa viongozi kwa muda mrefu wanatokana na CCM, wamekuwa angalau wana ile hali ya mambo kufanyika kwenye majadiliano ndani huko kwao, kitu ambacho kwenye miaka mitano ya Magufuli hatukushuhudia, aliua huo utamaduni. Unakumbuka wakati wa awamu ya nne ilitokea hali ya sintofahamu ya kisiasa ilikuwa jambo la kawaida kabisa Rais kukutana na kuzungumza na viongozi wa vyama vya upinzani. Wakati wa mjadala wa Katiba ilivyokuwa kitu ambacho kilivunjwa vunjwa wakati wa Rais Magufuli.

Sasa nini ambacho kinafanya Rais Samia asirudi kwenye hali hiyo na kwa haraka ambayo sisi tunaitaka kinaweza kikaelezwa na Rais Samia mwenyewe. Lakini kwetu sisi ni kuendelea kusukuma. Kuna haja ya kukutana. Kuna haja ya kufanya mazungumzo. Kuna haja ya kuangalia ni namna gani tunaweka mazingira ili watu wafanye siasa kwa uhuru, vyombo vya habari viandike kwa uhuru, Asasi za Kiraia zifanye shughuli zake kwa uhuru, wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru. Ni  lazima tuendelee kusukuma hali hii mpaka tuweze kufanya mazungumzo yanayoweza kutuletea hayo mabadiliko ambayo tunayataka kuyafanya.

The Chanzo: Pale mwanzo uligusia vitu vinavyo vinmtofautisha Rais Samia na Rais Magufuli. Kwamba angalau kwa sasa waandishi wa habari wanao uhuru fulani wa kufanya kazi zao, tunaweza kutembea bila  wasi wasi kwamba tunafuatwa au tunaweza tukawa tunaongea na simu bila wasiwasi kwamba simu zetu zinarekodiwa kitu ambacho mimi nakubaliana na wewe.

Lakini huku mtaani kuna mambo ambayo yanatokezea na ambayo licha ya huu unafuu uliopo, unafanya baadhi yetu wananchi kumkumbuka Magufuli. Mambo kama mgao wa umeme ambao ni mkubwa kusema ukweli unaweza ukakatika umeme siku nzima na ukarudi usiku ukakatika tena. Mambo kama mgao wa maji kitu ambacho watu wanadai hakikuwahi kutokea wakati wa Magufuli. Mambo kama bomoa bomoa ya vibanda vya wamachinga. Ukiyachukua haya yote sasa watu wanakaa wanafikiria ni kweli kuna mambo Magufuli alikuwa hayapatii lakini haya mambo ya sasa yalikuwa hayatokei. Hii wewe inafanya ujisikiaje kuona kuna baadhi ya mambo yanatokea yanafanya watu wamkumbuke Magufuli?

Zitto Kabwe: Sijisikii chochote. Hiyo ndio hali ya kawaida ya mwanadamu. Kila Rais ambaye ameingia madarakani hapa nchini baada ya muda watu wakasema bora fulani. Ilikuwa hivyo wakati wa Mwinyi. Ilikuwa hivyo wakati Mkapa anaingia. Mkapa alikuwa anaitwa ‘Mzee wa Ukapa,’ watu wakasema bora Mzee Rukhsa. Kuna wakati Mzee Rukhsa alikuwa akienda uwanjani kwenye shughuli za kitaifa kama Uhuru au Muungano, uwanja unalipuka wanamwambia mzee tunakukumbuka kwa sababu ya ukapa wa wakati wa Mkapa.  Kikwete wakati anaingia madarakani mwanzoni kulikuwa na hali mbaya kidogo kwa Mzee Mkapa kuhusiana na masuala ya rushwa na kadhalika, ziliibuka habari nyingi ambazo zinamchafua Mkapa na utawala wake yale mambo ya mgodi wa Kiwira, mambo ya mkopo wake aliochukua na Benki ya biashara NBC.

Llakini baadae watu wakaona bora Mkapa. Wakati wa Magufuli ndio sisemi kabisa. Eidha lilikuwa ni jambo la wananchi au lilotengenezwa ki-propaganda mimi sisemi lakini wewe unafahamu hali iliyokuwa inamkuta Rais Kikwete wakati wa Magufuli. Nyakati nyingine Magufuli mwenyewe alikuwa anasema wastaafu waache kuwashwa washwa.  Kwa hiyo, sio jambo geni kwamba mabadiliko yanapokuwa yametokea watu kuanza kusema bora fulani.

[Zama za Magufuli] hapakuwa na mgao wa umeme lakini kwa sisi ambao tunafahamu haya yangetokea hata kama Magufuli angekuwepo.

The Chanzo:  Kwa sababu gani?

Zitto Kabwe: [Magufuli] asingeweza kuzuia ukame na sio tu Tanzania ni eneo lote la Afrika Mashariki kuna ukame [kwani] mvua zimechelewa kunyesha. Asingeweza [kuzuia hilo]. Asingeweza kutupa umeme kwa sababu bwawa alilojenga na kuweka rasilimali fedha zake nyingi huko, yaani fedha za nchi, halijakamilika na lisingekamilika ndani ya miaka miwili kuanzia sasa.  Wakati aliacha kutekeleza mkakati kabambe wa umeme Power System Master Plan  kwa ajili ya gesi, lingetokea tu [hili la mgao wa umeme].

Hili la maji  lingetokea vile vile kwa sababu namna ya kutatua tatizo la maji jiji la Dar es Salaam ilikuwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Taifa. Ilikuwa ni ujenzi wa bwawa la Kidunda, Morogoro ambalo lingeweza kuleta maji Dar es Salaam nyakati kama hizi ambazo mvua zimechelewa.  Lakini yeye mwenyewe ndio aliuondoa huo mradi katika utekelezaji. Tuna mradi wa visima Kigamboni, visima karibu 20 sijui ambavyo visima 13 sasa vimeshakamilika vina maji ya kutosha na vinaweza vikaingiza asilimia 50 ya maji yanayohitajika Dar es Saalm.

Lakini mradi ule ulichelewa kipindi chake kuunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Maji Safi Dar es Salaam [DAWASA] ili maji yaweze kusambaa kwa wananchi. Kwa hiyo, kwa sisi tunaojua, tuliokuwa katika Bunge na kuona mambo haya yakipangwa na kupanguliwa, hatuwezi kusema kwamba tunamkumbuka kwa sababu wengine tunatamani angekuwa bado yupo ili haya yamtokee ayaone yeye mwenyewe. Kwa sababu, tulikuwa tunamkumbusha maamuzi anayoyafanya sio maamuzi sahihi.

Hili la machinga linanisononesha kidogo kwa sababu ni jambo ambalo linaonekana ni kama dola inaona biashara ndogo ndogo ni uchafu. Oparesheni inayoendeshwa na Mkuu wa Mkoa [wa Dar es Salaam Amos Makalla] ni kama inaonesha uchafu ni hawa wamachinga na usafi ni pale ambapo wamachinga hawapo. Hiki ni kitu kibaya.  Inanisononesha sana mimi sababu hautatui tatizo la msingi.

Tatizo la msingi ni uchumi wetu. Uchumi ambao hauzalishi ajira. Uchumi ambao unalazimisha hata watu ambao wamemaliza vyuo vikuu kuanza kufanya machinga ili waweze kuishi.  Umachinga umekuwa ni njia ya kuishi na ukitazama hata takwimu za Serikali yenyewe asilimia kubwa ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo inayofuata ni biashara. Sehemu kubwa ya hizi biashara ni biashara ndogo ndogo ambazo sio rasmi.

Kwa hiyo, unapochukua hatua ambazo Serikali imechukua bila kufanyia uchambuzi wa kina ili kupata majawabu ya kudumu [inasikitisha]. Kwa sababu  leo utawabomolea mwaka huu si kuna watu wamemaliza mitihani ya kidato cha nne na uwezo wetu sisi ni kuchukua asilimia 25 tu kuingia elimu ya sekondari ya juu. Sasa, asilimia 75 ya watakaomaliza mitihani ya kidato cha nne sasa wataingia barabarani, wengine watabaki vijijini huko na wengine watakuja mjini. Jawabu ni lazima liwe la kudumu.

Kwa hiyo mimi hili linanisononesha na kama machinga wanamkumbuka Magufuli inanisononesha zaidi kwa sababu aliwadanganya. Aliwapa matumaini ya uongo kwa sababu aliwaaminisha ukiwa na kitambulisho umeukata wakati hiki kitambulisho kilikuwa hakitatui tatizo la kudumu la ongezeko la wafanyabiashara wadogo kwenye nchi yetu.

Magufuli katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, bajeti ya kilimo imeshuka kwa asilimia 60, unategemea nini? Kwa maana kama huwaweki watu vijijini walime watakuja tu mijini kutafuta shughuli kwa ajili ya maisha yao. Sasa huwekezi kwenye kilimo ambacho kinabeba watu wengi zaidi halafu unawapa vitambulisho [kwa bei] ya Sh20,000.

Kwanza, unawanyonya  kwa kuchukua hizo Sh20,000 zao lakini huwapi haki yoyote ile kwa sababu hiko kitambulisho hakipandishi hadhi yoyote ile. Kwa vyovyote vile haya yanayowakuta sasa yangewakuta tu. Sasa kama wao [wamachinga] wanamkumbuka [Magufuli] kwa hiyo pia inanisononesha. Huwezi kuwalaumu kwa sababu watu wanaangalia leo.

Mimi na jirani zangu hapo kuna sehemu kuna mtu anauza magazeti, walikuwa wanauza kahawa, ni kituo cha daladala, jana nimepita nilikuwa naenda kunyoa nywele nimekuta wameondolewa. Nikasema nini kimetokea hapa? Wakajibu Serikali imevunja. Nikasema hapa kuna shida gani? Hapa ni kituo cha daladala, mtu anaposubiri daladala atahitaji kununua pipi, maji  au atahitaji kununua matunda labda ayapeleke nyumbani, kwa nini wanavunja? Mimi nilichoona jirani pale kuna kokoto zimewekwa na uzio umezungushwa, nikauliza hii ni nini?  Nikaambiwa  huyu mwenye mgahawa hapa anajitanua mpaka huku [walikotolewa Machinga].

Kwa hiyo pia, watendaji wa Serikali wa ngazi za chini, wanatumia hiyo nafasi kuungana na wenye uwezo wa kifedha kuwaondoa machinga hata kwenye maeneo ambayo hawatakiwi kuondolewa. Kuna watu kama mmepita hapa wanauza chakula jirani zangu, huku [Masaki, Dar es Salaam] shughuli za ujenzi zote zinazofanyika zinafanywa na watu kutoka nje ya Masaki. Hawa watu lazima wale. Anatoka nyumbani, tuchukulie labda mtu anatoka Buza saa 10 alfajiri hajanywa chai, akifika hapa lazima aende kwa mama ntilie apate chai na kitumbua au na andazi ili aweze kufanyahiyo kazi. Unapowaondoa hawa wanakula wapi?  Hawawezi kula Seacliff, hawawezi kula Sleepyway, hawawezi kula Double Tree [zote hoteli za kifahari zinazopatikana Masaki, jijini Dar es Salaam].

Kwa hiyo, vitu ambavyo vinafanyika, vinafanywa bila tafakari ya kutosha. Kitu ninachoweza kuishauri Serikali, mambo haya yanaweza kufanywa bila kuathiri maisha ya watu. Kwa mfano, kwa nini usigatue madaraka kwenye suala la usimamizi wa wafanyabiashara wadogo? Jambo la hapa Masaki kwa nini lisisimamiwe na wakazi wa hapa Masaki na Serikali yao ya mtaa, wakakaa wakajadiliana eneo hili wamachinga watafanya shughuli zao kama kawaida, hapa na hapa, hapa na huku hapana. Kwa hiyo, huyu machinga akienda kwenye eneo ambalo haliruhusiwi yeye ndio atakuwa mkorofi, lakini unapomwondoa kote anakula wapi huyu mtu?

Mtu ambaye anafanya kazi anategemea atashuka ataenda kununua sigara kwa mmachinga, unamlazimisha aende kununua sigara supermarket? Mtu ambaye ametoka zake Buza huko, Yombo huko, wanaofanya kazi ya kubeba nondo kwenye maeneo ya ujenzi? Kwa hiyo, hivi ni vitu ambavyo vinafanywa bila kufikiria.

Sisi wito wetu, sisi kama chama sasa, tumeagiza idara yetu ya sera na tafiti kufanya tafiti na kuja na rasimu ya kushughulika na suala la wafanyabiashara wadogo ili tuitangaze na kuiambia Serikali na wananchi kwamba sisi tungefanya hivi tofauti na nyinyi mnavyofanya, hilo la kwanza.   Kama unavyojua sisi chama chetu hatulalamiki tu, tunakuja na mbadala kwamba mmekosea hapa, sisi tungefanya hivi ili kama Serikali inaweza  kufanya kama vile sisi tungefanya waweze kufanya.

Kwa hiyo, hivi tunavyoongea timu yetu ya watafiti ipo barabarani inafanya kazi hiyo.  Lakini la pili ni wito kwa Serikali: iache hizi bomoa bomoa na vunja vunja. Serikali za mitaa zikae na wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye maeneo yao wakubaliane katika mashirikiano juu ya maeneo ambayo hawa wanaweza wakaendelea na shughuli zao bila bughudha ili maisha yaweze kuendelea. Huu ndio wito wangu kwa Serikali.

Fuatilia pia:

Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu

Zitto Kabwe: Taasisi za Kimataifa Zina Nguvu Sana Tanzania Kuliko Watanzania

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *