The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zitto Kabwe: Taasisi za Kimataifa Zina Nguvu Sana Tanzania Kuliko Watanzania

Kiongozi huyo wa kisiasa anasema hilo limejidhihirisha kwenye hatua ya Serikali kubatilisha marufuku yake ya awali iliyokuwa inawazuia wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua, akidai hatua hiyo imetokana na shinikizo kutoka Benki ya Dunia.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema kwamba taasisi za kimataifa zinaushawishi mkubwa sana katika nama Serikali inaendesha mambo yake nchini kuliko hata wananchi wenyewe wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Zitto alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano maalum aliyofanya na The Chanzo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mnamo Novemba 27, 2021. Alikuwa anaongelea mafunzo aliyoyapata kwenye harakati zake na wadau wengine zilizolenga kuifanya Serikali itengue agizo lililokuwa likiwazuia wasichana waliokatishwa masomo kwa sababu ya ujauzito kuendelea na masomo kupitia mfumo rasmi wa elimu wa taifa.

Agizo hilo lilitenguliwa mnamo Novemba 24, 2021, na Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako, akisema kwamba Serikali imechukua hatua hiyo ili kuhakikisha kwamba watoto wengi nchini Tanzania wanapata fursa ya kupata elimu. Wakati wa mahojiano yake na The Chanzo, Zitto alisema ameupokea uamuzi huo wa Serikali “kwa hisia kali.”

Yafuatayo ni sehemu ya kwanza ya mahojiano hayo kati ya The Chanzo na mbunge huyo wa zamani. Endelea …

The Chanzo: Karibu sana ndugu Zitto Zuberi Kabwe.

Zitto Kabwe: Asante sana comrade Khalifa Said, [mwandishi].

The Chanzo: Sawa sawa. Sasa unajua tunaenda kufunga mwaka wa 2021,  unajua sisi ni viumbe unaweza usimalize au ukamaliza mwaka. Ninapenda tuanze haya mazungumzo kwa kupata tathmini yako kwa ufupi juu ya mwaka 2021 ulikuwa vipi kwako kama mtu binafsi lakini vile vile [kama] kiongozi wa kisiasa?

Zitto Kabwe: Asante Khalifa. Kama ulivyosema, mwaka haujaisha lakini kuisha nako ni majaliwa hata kama mwaka ungekuwa unaisha ndani ya masaa machache yajayo lakini kuwepo ni majaliwa. Lakini hii miezi kumi na moja inatosha kabisa kufanya tathmini. Kwangu mimi mwaka ulianza vigumu sana kwa sababu ni mwaka ambao ulikuwa umetokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Kwa hiyo, ulikuwa very depressing, ulikuwa na hali ya kutokuwa na matumaini na mwanzoni mwaka ulianza kwa mimi na wenzangu kujitafuta, kujitathimini ili kuweza kujua …

The Chanzo: Wenzako ndani ya ACT-Wazalendo?

Zitto Kabwe: Kuweza kujua ni nini ambacho tutafanya ndani ya miaka mitano ili kukabiliana na mazingira tuliyokuwa nayo kipindi hicho. Lakini kabla kidogo ya robo ya kwanza ya mwaka kuisha yakatokea mabadiliko makubwa na ya kudra za Mwenyezi Mungu. Lakini kabla ya hapo sisi tulipata msiba mkubwa sana, tulifiwa na Mwenyekiti wetu wa chama taifa [Maalim Seif Sharif Hamad].

Hii iliongeza hiyo hali ya kujitafakari, kujitafuta kwa sababu tuliingia kwenye mchakato wa kumtafuta mtu wa kuziba nafasi yake kwenye Serikali [ya Umoja wa Kitaifa] kule Zanzibar. Tukaanza kufikiria mchakato wa kuziba nafasi yake kama mwenyekiti ambao bado hatujaukamilisha. Lakini mwezi mmoja tu baada, exactly mwezi mmoja baada [ya msiba huo] tukapata msiba wa taifa zima sasa wa kuondokewa na Rais aliyekuwa madarakani [John Magufuli] na kupata Rais mwingine [Samia Suluhu Hassan].

Tukaanza kuona matumaini, tukaanza kuona relaxation, hali ya uhuru, tulikuwa na matumaini makubwa sana, badae matumaini yakaanza kushuka baada ya kuona kwamba baadhi ya mambo ni yale yale. Kwa mfano, shughuli za kisiasa na baadae kiongozi wa kisiasa akawa amekamatwa ndugu [Freema] Mbowe [Mwenyekiti wa CHADEMA] na anaendelea na kesi mpaka sasa.

Hivyo ni vitu ambavyo vilishusha kidogo ile hali ya matumaini  makubwa ambayo tulikuwa nayo katika zile siku mia moja za kwanza [za uongozi wa Rais Samia]. Lakini angalau tuna uhuru wa kufanya shughuli zetu. Hautembei tena ukijiangalia nyuma nani anakufuata na kadhalika. Hatuna wasi wasi tena wa kuongea na simu zetu, wasi wasi kwamba tunakuwa taped [kunasa mawasiliano].

Kwa hiyo, imetuondoa kwenye hali ya ukosefu wa matumaini na kutupa matumaini ingawa sio makubwa kama ambayo tulianza nayo mwezi Machi, Aprili, Mei na Juni [2021]. Kwa hiyo, kiujumla, kuna hali fulani ya kuona mwaka unaofuata Mungu akituweka hai utakuwa bora zaidi. Hata ndani [ya chama] tunajipanga. Hivi unavyoniona hapa nimetoka kwenye mkutano mkuu wa chama wa jimbo la Mbagala uliohudhuriwa na watu zaidi ya 150. Mkutano wa ndani bila shaka kwa sababu mikutano ya nje hairuhusiwi lakini tumefanya mkutano wa ndani kitu ambacho huko nyuma ilikuwa hairuhusiwi, mapolisi wangekuwa wamezunguka na kadhalika.

Tunajipanga na tuna matumaini sababu unakaa kwenye mkutano wa viongozi wa ngazi za chini na wanachama wanasema tuiangalie 2024 tunafikaje, 2025 tunafikaje. Kwa hiyo, kuna hali fulani ya matumaini kwenda mbele.  Kwa hiyo, nadhani tutaumaliza mwaka katika hali hiyo sijui kama siku thelathini zilizobakia zinaweza kuwa na jambo lolote ambalo linaweza likarudisha nyuma hali hiyo. Natarajia tunaweza kumaliza mwaka na matumaini.

The Chanzo: Nafahamu watu wengi hawapendi kuzungumzia maisha yao binafsi, naelewa. Nakushukuru sana kwa mtazamo uliotupatia lakini sana sana swali langu lilikulenga wewe kama mtu binafsi. Ujue ukiwa unavaa kofia nyingi kama kiongozi wa chama au kisiasa tunapenda kuzungumza masuala ya kitaifa na tunasahau pia sisi ni binadamu tuna maisha yetu binafsi, tuna matumaini, tuna hofu, unanielewa?

Zitto Kabwe: Ndio.

The Chanzo: Ndicho nilichokuwa nalenga kwako binafsi kama kama Zitto Zuberi Kabwe mwaka 2021 umeuonaje?

Zitto Kabwe: Kama nilivyo kueleza, kama mtu nimeuanza mwaka very depressive tumetoka kwenye uchaguzi na mimi kama kiongozi nilikuwa na mzigo mkubwa wa kutazama watu wetu ambao walikuwa wamepoteza maisha, wameumia. Tulikuwa na uamuzi ambao kwa watu wengi ulikuwa wenye utata sana, [ni uamuzi] wa kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Kwa hiyo ilikuwa kazi kubwa sana, nilikuwa na mzigo sana. Badaye Maalim [Seif] aliondoka kama nilivyosema, mzigo ukawa mkubwa zaidi. Lakini mwaka unavyodhidi kwenda naona kuna ahueni na matumaini. Mimi binafsi naona kuna matumaini na naiona 2022 kama Mungu akitujalia kuingia tutakuwa na matumaini zaidi.

Mimi binafsi nimetoka kwenye hali ya mtanziko wa wala kutokujua tunakwendaje, tunafikaje, nimefikia hali ambayo naweza hata nikafikiri tunafanya hiki, nikashirikiana na wenzangu tukafanya hiki, nikakaa na familia tukapanga nini tutafanya mwezi ujao, miezi miwili ijayo kwa sababu huko nyuma ilikuwa haiwezekani wakati wowote ule unaweza usiwepo.

Nilikuwa naishi kama sitakuwepo kabisa kesho, inawezekana hiyo. Kibinadamu tunaambiwa tuishi kama hutokuwepo kesho, vile vile uishi kama utakuwepo milele.  Lakini kwa hakika mimi binafsi ile burden niliyokuwa nayo mwanzoni [mwa mwaka 2021] imeshuka sana.  Naona matumaini.

The Chanzo: Nashukuru sana. Kwa utangulizi huo, nataka nipate mtazamo wako kuhusiana na uamuzi wa Serikali wa hivi karibuni. Tunafahamu wewe ulikuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele kupinga marufuku iliyokuwa imewekwa, mahususi kabisa na hayati Rais Magufuli ambao wasichana au mabinti wapatapo ujauzito wakiwa masomoni hawapaswi kuendelea na masono katika mfumo rasmi, na akatamka hadharani kadiri yeye atakvyokuwa Rais wa nchi hii hakuna binti atakayepata ujauzito ateendelea na masomo.

Kumekuwa na kampeni kubwa, shinikizo kubwa kutoka kwa watu na makundi mbalimbali, ikiwemo wewe binafsi, na tunashukuru kwamba juzi hapa Serikali kupitia Waziri wa Elimu, mama Joyce Ndalichako, alisema, na waraka ukatolewa, kwamba watu wote wanaoachishwa masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito, watarudi shuleni. Kama mtu ambaye ulikuwa mstari wa mbele kupinga ile marufuku, huu uamuzi uliupokea kwa hisia gani?

Zitto Kabwe: Niliguswa sana. Kwa sababu unakumbuka kwamba uamuzi wangu ulishambuliwa sana. Ndani ya Bunge, wabunge waliongea wazi wazi hisia zao dhidi yangu  na wengine hata kutamka kuwa niuwawe ndani ya Bunge na bila hata Spika, au mtu yoyote, kusimama na kukemea lile.  Kwa hiyo, baada ya kumsikia Waziri wa Elimu ameyatamka yale tuliyokuwa tukipigania, niliguswa sana.

Nilikuwa Nzega, [Tabora] kwenye mazishi ya baba wa Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe. Nilitazama ile video ya Waziri wa Elimu zaidi ya mara tatu. Sio kwamba nilikuwa siamini, bali nilikuwa navuta hisia kwa sababu ya aina ya vitisho na maneno makali yaliyokuwa yanatolewa dhidi yangu na wenzangu tuliokuwa tunashirikiana nao katika hili. Lakini badayee nikafurahi. Mimi nina watoto wadogo wa kike umewaona hapa. Najivunia sana kwamba niliwapigania. Lolote likiwatokea haki yao ya kupata elimu haitaondolewa, hicho ndicho nilichokuwa nakipigania.

Lakini pia nilifurahi kwa maana ilikuwa ni vita ya watu wengi, kuna wengine waliifanikisha vita hii wanaita kufanya linakuwa ambao wengi hatuwajui na wala hawatatambuliwa lakini wamefanya kazi kubwa na ya ziada mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha kwamba amri ile inaondolewa kwa ajili ya hawa watoto. Sasa kuna watu ambao walipiga kelele kubwa kwenye mitandao [ya kijamii] na nje ya mitandao.

Kuna watu waliozishirikisha jumuia za kimataifa. Ndio kama watu wengine tuliandika barua. Sikuandika barua peke yangu. Lakini asasi zingine  zisizo za kiserikali ziliandika barua lakini kwa mazingira ya wakati ule watu hawakuwa tayari kutaja majina yao kwa sababu ya mazingira magumu ya wakati ule na wanaeleweka kabisa. Kuna wakati niliulizwa kwa nini mimi niliweka jina langu, niliwaeleza mi mbunge kwa nini niogope? Ni kazi yangu, siamini kama mtu anaweza kunihukumu kwa sababu ya kuweka maoni yangu kwenye jambo hili.

Ndio maana mimi nikaonekana zaidi na nikashambuliwa zaidi  kwa sababu jina langu lilikuwa wazi. Lakini kwa hakika ni kazi ambayo kuna watu waliifanya kwa zaidi ya hata mimi nilivyofanya. Kuna wengine najua wameshiriki mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha kwamba Serikali inatengua amri hiyo ambayo kimsingi  haikuwa amri halali. Haikuwa inatekeleza sheria yoyote kwa sababu sheria zetu, Sheria ya Elimu na Sheria ya Mtoto hazizuii kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Ilikuwa [ni amri] inayopingana na Sera ya Elimu ile ya mwaka 2014 ambayo imeweka wazi kabisa kwamba Serikali itaweka utaratibu wa watoto kurejea shuleni kwenye mfumo rasmi. Vile vile, inapingana na ilani ya chama kilichowaingiza madarakani [Chama cha Mapinduzi – CCM]. Haikuwa amri halali kabisa. Kwamba makundi yoote haya na kila mtu kwa mchango wake, tunaojulikana na wasiojulikana, wameweza kufanikisha hili ilikuwa ni hali iliyonipa furaha kubwa.

Nimefurahi kwa sababu sasa tumerudi kwenye ustarabu. Hili jambo si kubwa. Kwa nchi nyingine ni jambo la kawaida kabisa. Lakini kwetu sisi linaonekana ni jambo kubwa kwa sababu ya namna ambavyo tulikuwa tumerudi nyuma kwenye ustaarabu.

The Chanzo: Nataka nikuulize, unajua kwanza kuna nchi ambazo mabinti ambao walikuwa wanapata ujauzito na wanaruhusiwa kurudi …

Zitto Kabwe: Sio nchi tu, Zanzibar.

The Chanzo: Ndio Zanzibar, kuna  na nchi nyingine. Lakini pia uajabu wenyewe wa jambo hili ni kwamba hakuna ushahidi  wowote ule kwamba ukiruhusu huyu binti arudi shule hiyo itahamasisha watu wengine. Lakini licha ya hiyo, hili jambo lilikuwa lina aminiwa na watu wengi. Mimi naweza nikawa siamini ni sahihi  kumkatisha huyu mtu na masomo kupitia mfumo rasmi, lakini kulikuwepo na watu wana amini huu ni uamuzi sahihi. Hii unaitafsiri vipi?

Zitto Kabwe: Naitafsiri kwamba sisi ni taifa la ajabu sana. Ndio maana nimetumia neno ustarabu, kwa sababu taifa lolote, au mtu yoyote, ambaye amestaharabika wala asingehangaika. Kwanza, [asingehangaika] kwa huyo aliyetoa amri na kwa waliokuwa wanashabikia. Na mpaka sasa kuna watu wana wana huzuni kwamba kwa nini, kwa nini tunaruhusu jambo hili. Lakini ni watu hao hao unakuta kama ni binti zao  limewakuta jambo la namna hiyo wanawatafutia nafasi ya kusoma.

Nitakupa stori. Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Buhigwe, [mkoani Kigoma] mwaka huu [wa 2021] mwezi wa nne, watano. Nilienda kwenye kampeni kijiji kimoja kipo mbali sana mpakani na Burundi, katika Wilaya ya Buhigwe jimbo la Manyovu. Mzee mmoja akaniuliza swali kwenye mkutano wa hadhara, kwamba wewe ulienda kuzuia hela za Benki ya Dunia, wewe sio mzalendo unataka watoto wetu  wasome na wazazi.

Sasa kwa sababu tulikuwa tunakusanya maswali mengi, mtu mmoja jirani pale akanipenyezea ki-note, [kilichosema kwamba] huyu mzee kuhusu watoto ukimjibu muulize binti yake anaitwa fulani alipata ujauzito kidato cha pili lakini sasa hivi amemaliza chuo kikuu, wewe muulize tu aliwezaje kuendelea na masomo? Kwa hiyo, niliposimama nikaanza kuuliza watu wengine halafu nikafika kwenye lile [swali]. Kwanza, nikaanza kuelezea mantiki kwamba ni  jambo la kishamba kuzuia watoto kwenda shuleni. Na huyo mzee alikuwa anawaka anashangiliwa kwamba ameuliza swali sahihi.

The Chanzo: Na ndio point yangu [kwamba] kuna hao watu.

Zitto Kabwe: Baadaye nikasema lakini mzee, mbona dada yetu fulani, sitamtaja jina kwa heshima yake, mbona dada yetu fulani amepata ujauzito akiwa kidato cha pili, mjukuu ukalea na ukamtafutia shule nyingine,  na sasa hivi amemaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam? Kwa hiyo, wewe unataka mtoto wako asome kwa sababu unao huo uwezo wa kumsomesha lakini hutaki watoto wa wengine wasome na huo ukawa mwisho sababu ilikuwa pigo kwake.

Kwa hiyo, unaweza kuona ni namna gani kijijini ndani ndani  watu wakiamini kabisa wasisome. Sasa kuna kazi, wanaanthropolojia wanapaswa kufanya kazi, sisi ni jamii ya namna gani ambayo  unaweza kushabikia jambo kama hilo ambalo katika hali ya kawaida inatakiwa tulikatae kabisa likitokea katika nchi yetu.

The Chanzo: Sawa sawa. Labda tukirudi hapo nyuma kidogo, kufuatia hili agizo, unadhani hiki walichokifanya Serikali kinatosha au unadhani hili agizo na huu waraka ambao umtolewa  unapaswa uambatane na hatua zingine ili kuboresha zaidi hilo jambo?

Zitto Kabwe: Jambo la kwanza ambalo Khalifa linatakiwa lieleweke vizuri kwanza sheria ilikuwa haikatazi mtoto kurudi shuleni, ila tu sheria ilikuwa haikazii tu mtu atakayefukuzwa shule kwa sababu ya ujauzito baada ya kujifungua anaweza kurudi shule. Sheria ilikuwa kimya. Kwa hiyo, na sheria ya elimu imempa mamlaka  Kamishina wa elimu kutoa miongozo na nyaraka mara kwa mara katika uendeshaji bora wa utoaji wa elimu wa nchi. Ndio maana unaona ule waraka umesainiwa na Kamishina wa elimu.

Sasa kwa sababu huko nyuma, kwa sababu jambo hili lilizuiwa kwa amri, ni sahihi kulitengua kwa amri. Lakini tumeona limeshatokea sheria ipo kimya. Kwa hiyo, mtu yoyote anaweza akaamua kusema hakuna watoto kurudi shuleni. Kwa hiyo, sasa ni muhimu tuende kwenye mchakato wa kutunga sheria, inawezekana ikawa kati ya hizi sheria mbili, Sheria ya Mtoto au Sheria ya Elimu. Yoyote kati ya hizi au zote ili mradi hicho kipengele ioneshe ikitokea sheria nyingine yoyote inapingana na kifungu hiko basi kifungu hiki cha kumfanya mtoto aendelee kupata haki yake ya elimu kitumike zaidi.

Sasa lazima twende kwenye hatua ya kufanya mabadiliko ya sheria sababu hatuna tatizo. Sera imeshatamka, pia Sheria ya Elimu au [Sheria] ya Mtoto. Tatizo langu mimi ni moja, Bunge la sasa lina asilimia 97  ya wabunge ambao wengi wao walishabikia uamuzi ule wa Rais aliyetangulia na kuna baadhi ya watu unaona wanaona si sawa.

The Chanzo: Si sawa kwamba hili [agizo] limebatilishwa?

Zitto Kabwe: Ndio. Kwa hiyo, kwa uzoefu wangu ndani ya Bunge kuna nyakati unaona Serikali inapoteza mamlaka ya utungaji wa sheria. Mimi mara kadhaa nimewahi kupitisha vifungu vya sheria ndani ya Bunge ambavyo Serikali haivitaki. Unaweza tu ku-mobilize wabunge, Bunge linapokaa kama Kamati ya Bunge zima na likapitisha marekebisho.

Wasi wasi wangu ni kwamba, wabunge hawa wanaweza wakatumia nafasi hiyo kuweka masherti magumu sana kisheria kupitia schedules of amendments  na hivyo kulifanya jambo likawa redundant. Kama nilivyosema, mara kadhaa, nakumbuka  wakati tunatunga Sheria ya Fedha ya mwaka 2012, kuna jambo tulikuwa tunalipigania sana bungeni kwa miaka miwili linakwama halafu kama muujiza tu likafanikiwa kwenye Kamati ya Bunge zima.

Sijui nini kilitokea,   wabunge wote wakasema hili la Zitto ni sahihi na walikuwa walishalikataa mwaka uliopita na Spika akamwambia Waziri wa Fedha una shida gani na hili na tukaishinda [katika mazingira ambayo] Serikali mzima ilikuwa haikubaliani nalo. Tulikuwa tunatunga sheria ya kuweka mazingira mtu akiuza mali ambayo ipo Tanzania hata kama awepo popote pale duniani lazima alipe kodi Tanzania, ile ya capital gain tax ambayo ilikuwa imefutwa kama miaka kumi iliyopita, ilifutwa mwaka 2001 na ilichukua jitihada kuirudisha lakini Serikali ilikuwa inagoma na tukaishinda Serikali ikapitishwa ikawa sheria mwaka 2012.

Kutokana na huo uzoefu ndio napata mashaka sasa hivi. Tusiende sana kasi. Madhali huu waraka unawarudisha watoto shuleni, itoshe. Tufikirie tuwe na sheria ngumu zaidi baada ya 2025 ambapo naamini tunaweza kuwa na Bunge ambalo ni la haki zaidi kuliko hili la sasa hivi.

The Chanzo: Pengine kwa kuzingatia kwamba agizo la kuzuia watoto waliopata ujauzito kutoendelea na masomo kwenye mfumo rasmi liliwekwa na Rais, unadhani ni muhimu kwa Rais aliyepo kujitokeza hadharani na kulizungumzia wazi wazi kwamba hata kama sio kusema agizo lilokuwepo ni batili, akasema kitu fulani kwa sababu unajua kauli ya Rais …

Zitto Kabwe: Ninaamini sasa atasema. Nadhani hakutaka kusema kabla kwa sababu kumbuka yeye ndiye ambaye alipokuwa Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Watoto Zanzibar ndiye aliyepeleka kwenye Baraza la Wawakilishi Sheria ya Mtoto Zanzibar ambayo ndio ilitoa haki kwa mtoto kurejea shuleni baada ya kujifungua. Pia, kumbuka wakati Magufuli ametoa ile kauli tulikuwa tunacheza video za viongozi tofauti tofauti kuonesha kwamba Magufuli ameenda kinyume.

Kwa mfano, tulikuwa tunacheza sauti ya Ummy Mwalimu ambaye alijenga hoja lazima watoto warudi, tulicheza sauti ya yeye Samia wakati huo ni Makamu wa Rais. Kwa hiyo, naamini baada ya waraka huu kutoka, kwa sababu sahizi limekuwa ni jambo la kikanuni  ndani ya Serikali kwamba sasa wanarudi shule. Kwa vyovyote vile ni lazima Rais alitafutie nafasi, hata kama atakuwa anazungumza mambo mengine, aseme kwa sababu hizo ambazo umezizungumza. Mimi naamini hana budi lazima atafanya hivyo.

The Chanzo: Tukiweka nukta ya mwisho kwenye mada hii kabla hatujaenda kwenda mada nyingine. Huu mchakato wote — kuanzia agizo ambalo alilitoa Rais Magufuli pamoja na harakati na mavuguvugu ya kuhakikisha hili agizo au hii amri ina batilishwa, na vitu ambavyo viliambatana kwenye hilo vuguvugu, ikiwemo wewe kutishiwa kuuwawa, mpaka leo hii tunaona Serikali inabatilisha hili agizo — mchakato mzima umekufundisha nini?

Zitto Kabwe: Kwanza funzo kubwa sana, kubwa sana ni kwamba taasisi za kimataifa  zina nguvu sana kwa nchi zetu kuliko wananchi wenyewe.  Angalia ilichukua dakika ngapi kwa Benki ya Dunia kutoa tamko kuhusu uamuzi wa Waziri wa Elimu, dakika ngapi? Ni kwamba Benki ya Dunia ilihusika kwa kiwango kikubwa kuhakikisha huu uamuzi unabatilishwa.

The Chanzo: Huu wa sahizi? Mimi nilikuwa sifahamu.

Zitto Kabwe: Huu wa sahizi. Kwa sababu ya carrot. Kwa hiyo, ushawishi wa jumuia za kimataifa kwenye nchi zetu hizi  zinazoendelea ni mkubwa sana. Hii ni lesson ambayo nimeiona kwa sababu mimi nimewa engage hawa. Nimekwenda Benki ya Dunia nimeonana na wakurugenzi wote wa Benki ya Dunia. Waliokuwa wanaunga mkono, waliokuwa wanapinga na waliokuwa vuguvugu na unaona kwa kiwango gani hizi Bretton Woods Institutions zina ushawishi mkubwa sana kuliko wananchi wenyewe.

The Chanzo: Hilo pia linakuja kwenye Sheria ya Takwimu ambapo [Mfuko wa Fedha wa Kimataifa] IMF waliingilia. Hiyo inakusikitisha kwa namna fulani?

Zitto Kabwe:   Ndio, hata unapokwenda kuwa engage unaenda kwa sababu unajua hawa wana nguvu zaidi. Sheria ya Takwimu nadhani unajua asili yake. Ile Sheria ya Takwimu kwenda kubadilishwa ni  baada ya mimi kutoa takwimu kwamba Benki Kuu inatoa takwimu ambazo sio za kweli. Haraka haraka, Rais Magufuli aliagiza nikamatwe, nikakamatwa. Sasa unapelekwa mahakamani kwa kuvunja sheria gani?

Maana ndani ya Sheria ya Takwimu hapakuwa na hiko kifungu cha kumpelekea mtu mahakani kama amefanya uchambuzi kama ule nilifanya. Sheria ikakimbizwa ndani ya Bunge, sasa wakati wanaikimbiza ndani ya Bunge hawakufikiri kuhusu wahisani kama hao IMF na wengine. Kwa hiyo, wakajikuta wanasakamwa. Walinyimwa dola milioni hamsini tu kwamba hatuzitoi hizi mpaka mbadilishe na sheria ikaja ikabadilishwa.

Kwa hiyo, hii ni mifano miwili na ni muhimu sana watu waijue kwa sababu ni lazima ujue ni wapi unabonyeza ili ufanikiwe mabadiliko unayotaka kuyaleta. Kwa jambo kama hili kwa Benki ya Dunia ilikuwa kama kashfa kwa sababu tuliichora Benki ya Dunia kwamba mnawapa watu fedha ambao wanatekeleza sheria ambayo ni yakibaguzi na hilo likawakaa. Kwa hiyo, ilibidi wafanye kazi kwa bidii ili hii alama.

Lakini kuna vitu ambavyo hawajali. Ukizungumza nao kuhusu demokrasia, hawajali. Niliwahi kuzungumza nao kuhusu Erick Kabendera [mwandishi wa habari wa kujitegemea aliyepewa kesi ya uhujumu uchumi na Serikali ya Rais Magufuli]. Erick amewahi kufanya na Benki ya Dunia, nikajenga hoja kwamva huyu mtu amewahi kufanya kazi na nyie kutayarisha kile kitabu cha miaka 50 ya Benki ya Dunia Tanzania. Hawakujali.

Lakini hili [la watoto wa shule] kwa sababu liliwekwa kwa namna ambayo ni kama vita ya kimaneno dhidi yao kulikuwa hakuna namna.  Hili ni somo moja kubwa sana. Lakini pili, jambo lingine nililojifunza [kwenye huu mchakato ni kwamba] Watanzania ni watu wa ajabu sana. Watanzania ni watu ambao wanageuzwa kama chapati inavyogeuzwa.

Wanaweza wakashangilia hili na likigeuka kinyume tena wakashangilia pia. Kwa hiyo, kwa mimi kama mwanasiasa ni somo kubwa sana kwamba watu wetu hawa usiwachukulie tu ukawa makini sana na wao. Ni watu ambao ni rahisi sana kugeuzwa, kitu ambacho si kitu kizuri. Ni kitu kibaya kwa jamii lakini ndio hali halisi tuliyonayo.

Fuatilia pia:

Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu

Zitto Kabwe: Hili la Wamachinga Linanisononesha Sana

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *