The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mambo Muhimu ya Kufahamu Kuhusu Muswada Mpya wa Sheria ya Huduma za Habari Tanzania

Hoja kubwa ni, kwa nini tupunguze makali ya adhabu kidogo tu na siyo kuifumua sheria hiyo yote na kuisuka upya?

subscribe to our newsletter!

Nilialikwa na kukubali mwaliko wa kushiriki kipindi cha runinga kujadili maudhui ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2023 ambao umesomwa bungeni kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Kumi wa Bunge la 12.

Kipindi hicho cha runinga kiliandaliwa kwa lengo la kuujulisha umma wa Tanzania kuwa kuna muswada huo hadharani kwa ajili ya mjadala wa Watanzania na kuyaainisha yaliyomo, japo kwa ufupi. Pamoja nami, jopo la wazungumzaji lilikuwa na wanahabari na wahariri nguli kutoka vyumba viwili vya habari nchini.

Uwepo wangu ulilenga kutumia uzoefu wangu kama mdau mkubwa wa huduma za habari asiye mwanahabari, ikizingatiwa mchango wangu wa miaka mingi katika sekta ya habari kama mwandishi wa makala na mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa katika vyombo vya habari vya aina mbalimbali ikiwemo redio, magazeti, runinga na mitandao ya kijamii. 

Aidha, ushiriki wangu katika Umoja wa Haki ya Kupata Habari (CORI) kama mwanachama kwa miaka zaidi ya 10 tangu mwaka 2010 uliniweka katika nafasi nzuri ya kuweza kurejea historia ya Sheria za Huduma za Habari na Haki ya Kupata Taarifa ambazo mchakato wa utungwaji wake nilishiriki kikamilifu kama mchambuzi, mshawishi na mzengezi.

Jambo moja nililolibaini na kulisema katika mazungumzo hayo ni kwamba Muswada huo muhimu umeandaliwa kwa lugha ya Kiingereza, jambo linalowanyima fursa mamilioni ya Watanzania ambao hawakufikia kiwango cha elimu kuweza kuelewa Muswada ulioandikwa kwa Kiingereza cha kisheria. 

Nilieleza pia kuwa Muswada wa aina hii ungefaa uletwe na kusomwa bungeni kwa lugha ya Kiswahili ili wadau wa habari wa mijini na vijijini waweze kuyajua maudhui yake na kuchangia mawazo yao. 

Tatizo la uwasilishaji

Jingine la kimchakato ambalo nililisema ni kwamba mtindo wa kuleta Muswada kama huu wenye maslahi mapana kwa Watanzania mmoja mmoja kama sehemu ya muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ulikuwa unawapoteza zaidi wasomaji, hata wale wanaokijua Kiingereza cha kisheria.

Kwa uzoefu wangu, wananchi wengi sana, wakiwemo baadhi ya mawakili wasomi, waliwahi kushindwa kufungua mashauri yao mahakamani kwa sababu vifungu vya sheria walivyorejea vilikuwa siyo sahihi kutokana na kwamba vilikwishafanyiwa marekebisho kwa mtindo kama huu wa Miswada ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Written Laws Miscellaneous Amendments). 

Kwa jadi, mtindo huu wa kubadili sheria hufaa pale ambapo marekebisho yanayopendekezwa ni madogo madogo sana, kama vile neno au herufi iliyosahaulika, nukta au mkato uliowekwa pasipo sahihi, na sentensi inayonyooshwa au kukamilishwa.

Kwa jinsi Muswada huu ulivyo, kuna mambo mengi na mazito yanayopendekezwa kurekebishwa. Kurasa tano za vifungu takribani kumi vyenye hoja na masuala kibao yanayohitaji marekebisho haviwezi kuletwa katika Muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali. 

SOMA ZAIDI: Zanzibar Mbioni Kuzifanyia Marekebisho Sheria Zinazolalamikiwa na Wadau wa Habari

Kufanya hivyo ni kuchezea mantiki ya Miswada ya Marekebishoya Sheria mbalimbali na kuuhadaa umma wa Watanzania. 

Aidha, nilieleza pia, na hili inafaa nilirudie kwa msisitizo, kwamba Muswada muhimu kama huu ulipaswa usiishie kuchapishwa katika toleo maalum la Gazette na kupandishwa katika tovuti ya Bunge pekee bali ilipaswa kuuchapisha kwa Kiingereza na Kiswahili katika magazeti ya kila siku yanayosomwa zaidi angalau mfululizo kwa muda wa wiki nzima ili Watanzania waweze kuupata, kuusoma na kuchangia maoni yao kupitia namba zilizotajwa.

Kwa sasa, huko Muswada ‘ulikofichwa’ wanaoingia ni Watanzania wachache sana walio na uwezo, upeo na bahati ya kuingia. Nilikumbusha kuwa wakati wa Bunge la 10 la Tanzania chini ya Spika wa kwanza mwanamke, Anne Semamba Makinda, Miswada iliyoletwa bungeni ililazimika kuwa katika lugha ya Kiswahili na tafsiri ya Kiingereza. 

Wakati mmoja, Muswaada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliondolewa bungeni na kurudishwa serikalini kwa kosa la kuletwa ukiwa umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza. 

Akitoa maelekezo, Spika aliiagiza Serikali kwenda kuuandika upya kwa Kiswahili ndipo uletwe tena bungeni kusomwa na akaongeza kuwa kuanzia wakati huo, hiyo ndiyo itakuwa jadi mpya ya Serikali kuzingatia wakati ikiandaa Miswada. Sasa ninashangaa, utaratibu ule umekufa kwa kuwa Spika Makinda amestaafu uspika?

Ahueni

Ukiacha mambo ya Kimchakato, nilijadili pia maudhui ya Muswada huo. Katika hilo, niliishukuru Serikali kwamba imeleta Muswada ambao unalenga kuondoa mapungufu, japo machache, ya Sheria ya Huduma za Habari iliyopitishwa kwa mbwembwe mwaka 2016 huku ikilalamikiwa sana na wadau wa habari kwa kusheheni vifungu kandamizi kwa wadau wa huduma za habari, hususan wanahabari. 

Hili la kukaa, kujitafakari na kuona umuhimu wa kuondoa mapungufu hayo kutoka kwenye sheria ni jambo zuri na la kupongezwa. 

Hata ukiangalia kifungu kimoja baada ya kingine, nilisema kuwa katika vifungu vyote tisa au kumi vinavyopendekezwa kurekebishwa, hakuna kifungu hata kimoja kinacholeta kikwazo cha ziada katika utoaji wa huduma za habari.

SOMA ZAIDI: ‘Sheria Kandamizi Zinavifanya Vyombo vya Habari Visitekeleze Wajibu Wao Ipasavyo’

Badala yake, vifungu takribani vyote vinalenga kuboresha maeneo yaliyolalamikiwa mwaka 2016 katika sheria yenyewe ya Huduma za Habari. 

Kwa hiyo, nilitumia msemo wa Kiswahili kuwa mnyonge mnyongeni ilahaki yake mpeni, nikimaanisha tuungane kuipongeza Serikali iliyoona umuhimu wa kuwasikiliza wadau wa huduma za habari katika malalamiko yao ya miaka yote kuhusu sheria hiyo tangu ipitishwe bungeni na kutiwa saini na Rais hayati John Pombe Magufuli mwaka 2016.

Nikichambua kifungu kimoja kimoja, nilianza kwa kufurahishwa na pendekezo la kufutwa kwa kifungu cha 5 (l) cha Sheria ambacho kilikuwa kinaleta ukiritimba wa ajabu katika eneo la matangazo ya biashara katika vyombo vya habari.

Kwa wasioifahamu sheria hiyo, kifungu hicho kilimpa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo jukumu la kupokea matangazo, ambayo mengi hutokea serikalini, na kuamua ayapeleke katika chombo kipi na kipi. Hii peke yake ililalamikiwa kwa sababu mbili. 

Kwanza, matangazo ni biashara na ni vema biashara ikaachwa ifanyike kwa misingi ya nguvu ya soko. Pili, kumpa mtu mmoja, au hata ofisi moja, iwe na maamuzi juu ya matangazo ya kibiashara yataenda kwenye chombo gani ni kutengeneza mwanya mkubwa wa rushwa. 

Chukulia kuwa ninamiliki gazeti, nikaona nimekosa matangazo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), au bandarini, kwa muda mrefu sasa huku jamaa yangu fulani akiniambia jinsi anavyoletewa matangazo na Idara ya Habari Maelezo kila siku mpaka amezidiwa. 

Bila shaka nitapenda kujifunza mwenzangu anatumia mbinu gani kupata matangazo hayo yenye pesa nyingi, sivyo? 

Mwisho wa siku, nilieleza kuwa nitaishia kuomba niunganishwe na idara husika ili ‘niwaombe’ waanze kuleta matangazo kwangu pia. 

Badala ya chombo kuletewa matangazo kwa sifa na kigezo cha mtawanyiko wake na idadi ya wanaofikiwa na chombo hicho, ‘itapenyezwa rupia kuondoa udhia.’ Pendekezo la kufutwa kwa kifungu cha 5 (l) limenifariji sana.

Vifungu vingine ambavyo vinapendekezwa kurekebishwa ni pamoja na kifungu cha 50 (1) (a) (ii) na 50(1) (c) (ii). Hapa kulikuwa na tatizo kubwa sana la kisheria ambalo limelalamikiwa miaka yote tangu kutungwa kwa sheria hii. 

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Wabainisha Changamoto Zinazoikabili Tasnia ya Habari Tanzania

Vifungu hivi viko katika Sehemu ya VII ya Sheria ambayo inahusu makosa katika utoaji wa huduma za habari na adhabu zake. Kwa nchi za Jumuiya ya Madola, sheria hii imekithiri kwa idadi ya makossa katika kazi ya huduma za habari. 

Aidha kuna adhabu kali kwa makossa ya kawaida ya kitaaluma kana kwamba kuna mtu ameua mtu. Kwa mfano, kuchapisha taarifa ya uongo kwa makusudi, au kwa uzembe, ni kosa kwa mujibu wa sheria hii na kuna adhabu kali ikithibitika kosa limetendeka.

Katika kifungu cha 50 ((1) (a+c) (ii), habari isiyo ya kweli ikitamkwa, kutangazwa au kuchapishwa na ikalalamikiwa kuathiri hadhi au heshima, haki na uhuru wa mtu yeyote ni kosa na inaweza kupelekea mhusika kupatiwa adhabu ya kulipa faini hadi Shilingi milioni 20 au kifungo jela hadi miaka mitano au vyote kwa pamoja. 

Hivi adhabu hizi zinamfaa mtu ambaye anafanya kazi ya huduma za habari kama vile mwandishi, mtangazaji, mchambuzi wa makala au mhariri? Hizi si ni adhabu za mwizi wa mifugo na magari?

Katika Muswada unaopendekeza marekebisho, jambo hilo limebaki kuwa kosa linalostahili adhabu. Hata hivyo, imependekezwa kuwa adhabu zipungue kidogo na kuwa kati ya Shilingi milioni tatu na milioni 10, faini, au kifungo jela kati ya miaka miwili (badala ya mitatu) na mitano au vyote. 

Kwa maoni yangu, kiwango cha ahueni kilicholegezwa ni kidogo mno na adhabu hizi bado ni kali kiasi cha kutishia watoa huduma za habari wasifanye kazi zao kwa uhuru. 

Katika nchi zinazoheshimu uhuru wa habari, kuchapisha, au kutangaza habari ya uongo, hufuatiwa na ufafanuzi kutolewa na mhusika na chombo kilichochapisha, au kutangaza, habari hiyo hupaswa kuomba radhi na kuchapisha, au kutangaza, ukweli ulioletwa na mhusika.

Adhabu pia zimelegezwa kidogo kwa makossa mengine katika kifungu cha 51 (1) (a +b); Kifungu 53 (a) (1); Kifungu 54 (1); kifungu 55 (2); kifungu 63 (a) (1) na kifungu 64 (2). 

SOMA ZAIDI: Wabunge Wataka Sheria, Kanuni Kandamizi za Uandishi wa Habari Kurekebishwa

Vifungu hivi vyote vina masharti ya kikoloni kwa wadau wa huduma za habari, ikiwemo kuweka masharti kuwa endapo chombo kitakuwa kimechapisha habari ya umbea, au uzushi, basi mwandishi husika ataadhibiwa vikali lakini pia mkurugenzi au mkuu wa taasisi au chombo cha habari kilichotangaza, au kuchapisha, habari hiyo naye ataadhibiwa kwa kosa lile lile ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) sheria inaweka adhabu kwa mkuu wa chombo cha habari ya hadi faini ya Shilingi milioni 25. 

Katika marekebisho yanayoletwa kwenye Muswada, adhabu hii inapendekezwa ishuke na kubaki kati ya Shilingi milioni 15 na milioni 20.

Kwingineko, Sheria ina mambo ya ajabu kwamba mashine, au mtambo, uliotumika kuchapisha, au kudurusu, habari ya uchochezi, kuchafua au uongo unaweza kutaifishwa au kushikiliwa na Serikali kwa muda wa kati ya mwaka mmoja na mitatu. 

Kipo kifungu cha 53 (5) ambacho kinaenda mbali na kusema mitambo hiyo inaweza kuuzwa au kupigwa mnada na mapato kuingizwa serikalini. 

Katika Muswada wa marekebisho ya sheria hii, inapendekezwa kuwa kifungu kinachoruhusu mitambo kuuzwa, au kupigwa mnada, na Serikali kifutwe na kisiwepo tena kwenye sheria ya huduma za habari.

Kwa ujumla, nilieleza, na ninaona nirudie hapa kwa msisitizo, kwamba Muswada wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari unalenga kupunguza makali ya Sheria kwa kiasi kiduchu tu. 

Kwa mtu kama mimi ninayeijua vema sheria yenyewe, hoja kubwa ni kwa nini tupunguze makali ya adhabu kidogo tu na siyo kuifumua sheria hiyo yote na kuisuka upya? 

Kwa nini watoa huduma za habari wanatungiwa sheria ambayo inatofautiana kiviwango na tasnia nyingine katika nchi moja? Hivi daktari, au muuguzi, akikosea na kumpasua mgonjwa kichwa badala ya mguu anafungwa jela au anapambana na adhabu za kitaaluma kwa mujibu wa taaluma yake?

Mungu ibariki Tanzania na watoa huduma za habari wote! 

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts