The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zanzibar Mbioni Kuzifanyia Marekebisho Sheria Zinazolalamikiwa na Wadau wa Habari

Waziri wa Habari asema muswada tayari upo katika ngazi ya Makatibu Wakuu.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Serikali visiwani hapa imebainisha kwamba inayasikia malalamiko ya wadau wa habari kuhusu uwepo wa sheria kandamizi za habari na zilizopitwa na wakati, ikisema kwamba iko mbioni kuzifanyia maboresho sheria hizo.

Waziri ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar Tabia Mwita aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba tayari vikao na wadau vimeshafanyika kuhusu sheria hizo na kwamba kwa sasa Serikali iko kwenye hatua ya mwisho ya mchakato wa maboresho ya sheria husika.

“Serikali imepokea maoni ya wadau na muswada [wa marekebisho ya sheria] upo katika ngazi ya Makatibu Wakuu,” Tabia alisema kwenye mahojiano hayo. “Hivyo, kama Serikali tunajitahidi kuweka mazingira rafiki kwa waandishi ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.”

Wadau wa habari wamekuwa wakizilalamikia sheria za habari za Zanzibar kwa siku nyingi, wakisema ni za muda mrefu na zenye vipengele kadhaa vinavyorejesha nyuma uhuru wa habari na sekta habari visiwani humo.

Sheria kandamizi

Zanzibar ina sheria mbili kubwa zinazoongoza uandishi wa habari nazo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 na Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya mwaka 1997.

Chini ya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu, Ofisi ya Msajili inahusika na kuyapa leseni magazeti. Hata hivyo, sheria hiyo inampa nguvu waziri mwenye dhamana kufungia au kuzuia uchapishwaji wa gazeti chini ya kisingizio cha “maslahi ya amani na utulivu.”

Wadau wamekuwa wakilalamika kwamba sheria hiyo haifafanui ni yepi haswa “maslahi ya amani na utulivu,” wakionya kwamba inatoa mwanya kwa wenye mamlaka kukitumia vibaya kifungu hicho cha sheria.

SOMA ZAIDI: Wadau Walaani Kushikiliwa Mwandishi wa Habari Zanzibar, Wataka Aachiwe Huru

Sheria hiyo pia inampa nguvu Rais wa nchi kuzuia uingizwaji wa chapisho lolote visiwani humo linaloonekana kuhatarisha “maslahi ya amani na utulivu.” Rais pia, kwa kupitia sheria hiyo, anaweza kuwafungulia mashtaka watu watakaokutwa na chapisho lililozuiwa kuingia nchini.

Kwa upande wake, Sheria ya Tume ya Utangazaji imekuwa ikilalamikiwa na wadau wa habari kwa kutoa mwanya kwa viongozi wa Serikali kuingilia shughuli za utangazaji visiwani Zanzibar.

Sheria hiyo pia inaipa nguvu Tume ya Utangazaji Zanzibar, chombo cha Serikali ambacho siyo huru, kufungia na kufutia leseni vyombo vya utangazaji, kitu kinachoenda kinyume na viwango vya kimataifa vinavyoitaka tume kuwa huru na inayojitegemea.

Kwenye ripoti yake ya hali ya vyombo vya habari Tanzania kwa mwaka 2021-2022, Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilisema kwamba Zanzibar inahitaji sheria mpya kabisa za vyombo vya habari, ikiitaka Serikali iharakishe mchakato wa kuzifanyia mageuzi sheria hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCT Kajubi Mukajanga aliurudia wito huu wakati wa kikao kati ya ujumbe wa baraza hilo na Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi kilichofanyika Ikulu ya Zanzibar hapo Desemba 22, 2022.

Akijibu ombi hilo, Dk Mwinyi alinukuliwa akikiri kuwa sheria za habari za Zanzibar ni za muda mrefu na hivyo Serikali yake, kwa ushirikiano na wadau wa habari, itaendelea kufanyia kazi pendekezo hilo ili Zanzibar iweze kuwa na sheria nzuri zaidi.

Deus Valentine Rweyemamu, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Centre for Strategic Litigation (CSL), aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba Serikali ya Zanzibar haiwezi kukwepa jukumu la kuboresha mazingira ya uhuru wa habari visiwani humo.

“Vyombo huru vya habari ni vya msaada mkubwa sana kama nia ya Zanzibar ya kutaka kukuza sekta yake ya utalii inatarajiwa kufanikiwa,” Rweyemamu, ambaye ni mfuatiliaji mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar, alisema.

“Nia ya Rais Mwinyi ya kupambana na ufisadi [pia] itakuwa ngumu kufanikiwa endapo kama Serikali haitakuwa na misingi ya uwazi serikalini itakayoruhusu usambaaji huria wa habari na taarifa,” aliongeza mdau huyo.

Wadau wakutana

Ikiwa ni sehemu ya kufanya uchechemuzi kuchochea mabadiliko hayo ya kisheria, wadau wa habari wa Zanzibar walikutana mnamo Februari 4, 2023, mjini hapa kwa lengo la kutathmini sheria hizo na kutafakari kwa pamoja mikakati inayoweza kuchukuliwa kufanikisha mageuzi hayo ya kisheria.

Afisa Uhusiano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) – Zanzibar Mohammed Khamis, ambaye taasisi yake ndiyo iliandaa kikao hicho, aliiambia The Chanzo kwamba ni muhimu kwa mabadiliko ya kisheria kufanyika ili Zanzibar iwe na uhuru wa kweli wa habari.

SOMA ZAIDI: ‘Sheria Kandamizi Zinavifanya Vyombo vya Habari Visitekeleze Wajibu Wao Ipasavyo’

“Jinsi ilivyo hivi sasa ni kwamba uhuru unapewa lakini hapo hapo unapokonywa,” alisema Khamis, akimaanisha ukinzani uliopo kati ya haki zinazotolewa na Katiba na vizingiti vilivyowekwa na sheria. “Sasa hii siyo sahihi hata kidogo. Inahitaji mabadiliko.”

Jabir Idrissa, mwandishi wa habari wa siku nyingi wa Zanzibar na ambaye alishiriki kikao hicho, alisema kwamba ni muhimu kwa mabadiliko ya kisheria kufanyika kwani hiyo itaifanya Zanzibar kuendana na mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uandishi wa habari.

“Tuheshimu mikataba hii kwenye kutunga na kusimamia sheria za waandishi,” Idrissa aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano. “Sasa ikiwa kuna sheria ambazo zitakwenda kinyuma na katiba basi hapo ni kukiuka mikataba ya kimataifa.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *