Suala moja lililoibuliwa katika mikutano ya hadhara ya chama cha ACT Wazalendo inayoendelea katika visiwa vya Unguja na Pemba ni uendeshaji (ground handling) wa ‘Terminal 3’ katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar.
Katika mkutano uliofanyika Nungwi Februari 26, 2023, Kaskazini Unguja, niliwaeleza wananchi kwamba kutokana na maamuzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Zanzibar (ZAA) ya kutoa ukiritimba kwa kampuni moja ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, zaidi ya Wazanzibari 200 wako hatarini kupoteza ajira zao.
Nilieleza kuwa ZAA imevunja sheria za Zanzibar na za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazokataza ukiritimba wa kampuni moja kuendesha shughuli za viwanja vya ndege.
Siku mbili baada ya mkutano huo wa Nungwi, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi alijitokeza kujibu suala hili.
Akizungumza na waandishi wa habari mnamo Februari 28, 2023, katika Ikulu ya Mnazi Mmoja, Rais Mwinyi alisema “madai” yetu ACT-Wazalendo hayana ushahidi wowote na kwamba yana lengo la kuwapotosha wananchi.
Kiongozi huyo alisema kwamba uamuzi wa Serikali yake kuipa ukiritimba kampuni ya Dubai ya Dnata kuendesha ‘Terminal 3’ kumeisaidia Serikali kukusanya mapato mengi zaidi, kitu ambacho ameshangaa kwamba ACT-Wazalendo hatukisemei.
Bahati mbaya sana, Mheshimiwa Rais Mwinyi hajaeleza hoja za msingi zilizoibuliwa katika mkutano ule na kuhusu suala lenyewe la uendeshaji wa ‘Terminal 3’ katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.
“Uungwana unataka uweke maslahi yako wazi [wakati unatetea jambo fulani],” alisema Dk Mwinyi. “Kama una maslahi [kwenye jambo hilo,] uyaseme. Hao wanaowataka wao [ACT Wazalendo,] wana maslahi gani? Upo uhusiano kati ya hizo kampuni na viongozi [wa ACT Wazalendo]. Mbona hawasemi? Kwa hiyo, hapa hawaitetei Serikali na nchi, wanatetea maslahi binafsi.”
Makala haya mafupi yana shabaha ya kueleza msingi wa hoja hii na kwa nini tulitaka Taasisi ya Uchunguzi wa Rushwa Zanzibar (ZAECCA) ifanye uchunguzi wa mkataba wa uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.
Nitaonesha kuwa Rais wa Zanzibar, ambaye ameapa kulinda sheria za Zanzibar na vilevile kulinda sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatetea kuvunjwa kwa sheria na kwa hakika anafanya makosa makubwa.
Mwisho nitarejea wito wetu tulioutoa Nungwi wa kutaka uchunguzi wa kina wa mkataba wa uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.
Uvunjifu wa sheria
Shughuli za uendeshaji wa viwanja vya ndege zinasimamiwa na Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA). Kanuni za uendeshaji hutolewa mara kwa mara na mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa kanuni hizo – Uamuzi Namba 1 wa 2022 – mkataba wowote wa kuendesha viwanja vya ndege haupaswi kuwa na upendeleo na ukiritimba (exclusivity).
Hii maana yake ni kwamba kanuni zinakataza kampuni moja kupewa peke yake eneo la kuendesha huduma.
SOMA ZAIDI: Serikali ya Mwinyi ni Muhimu Ikajibu Maswali Haya Muhimu
Hiki ndicho kilichofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar ambapo Mamala ya Viwanja vya Ndege (ZAA) imewapa mkataba kampuni ya Dnata kutoka Dubai kuendesha ‘Terminal 3’ peke yao.
Kisha ZAA imeelekeza ndege zote za kimataifa kuegesha ‘Terminal 3.’ Hivyo, siyo tu kwamba ZAA wamevunja sheria na kanuni za usafiri wa anga, bali pia wamekuwa madalali wa kampuni moja dhidi ya kampuni zingine ambazo zimekuwa zikitoa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Kampuni zingine – ZAT na Transworld – wamezuiwa kabisa kutoa huduma katika ‘Terminal 3’ na mashirika ya ndege yaliyokuwa yanahudumiwa na kampuni hizo yameelekezwa kuegesha ‘Terminal 3’ na hivyo kuvunja mikataba na kampuni hizo.
Uvunjifu mkubwa huu wa sheria unawezaje kutetewa na Rais wa Zanzibar?
Zanzibar pia ina sheria ya ushindani wa biashara (Fair Competition Act) ambayo ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kama Sheria Namba 5 ya mwaka 2018.
Sheria hii inapiga marufuku mkataba wowote ambao unaondoa ushindani katika biashara yeyote.
Sheria hii inatamka wazi kuwa mamlaka yeyote ya Zanzibar ikiingia mkataba wowote ambao unatoa upendeleo na ukiritimba kwa mtoa huduma, au mfanyabiashara yeyote, mkataba huo ni batili.
Hivyo, kitendo cha ZAA kuingia mkataba (concession) na kampuni ya Dnata ambao unaipa kampuni hiyo peke yake ukiritimba wa kuendesha ‘Terminal 3’ ni kukiuka sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Rais wa Zanzibar aliyeapa kulinda sheria anawezaje kutetea jambo hili?
Hata hilo la la kuongeza kwa mapato, zipo hoja nyingi. Moja, huwezi kulingalinisha ‘Terminal 2’ na ‘Terminal 3.’ Dnata pia ana uhodhi, au ukiritimba, wa kutoa huduma ‘Terminal 3,’ maana yake ni kwamba mapato makubwa kwa gharama ndogo.
Lakini tuchukulie kuwa madai ya kuongezeka kwa mapato ni ya kweli kwani Rais Mwinyi hana sababu yeyote ya kudanganya katika hili.
Kwa nini basi Rais asipeleke sheria katika Baraza la Wawakilishi kufuta sheria ya ushindani wa biashara badala ya kutetea uvunjwaji wa sheria hiyo?
Kwa nini Rais Mwinyi asitumie wabunge wa Zanzibar kupeleka muswada katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuondoa usafiri wa anga katika Mambo ya Muungano, aunde Zanzibar Civil Aviation Authority (ZCAA) itakayotunga kanuni zinazoruhusu ukiritimba wa kampuni moja kutoa huduma katika viwanja vya ndege vya Zanzibar?
Ushindani huleta ufanisi
Kuna sababu gani ya kuwa na sheria za nchi ambazo haziheshimiwi na mamlaka ya juu kabisa ambayo wajibu wake mkubwa ni kuhakikisha sheria zinafuatwa? Samahani Mheshimiwa Rais, umekosea!
Hoja yetu sisi ACT Wazalendo ni kwamba ushindani unaleta ufanisi na huduma bora kwa wananchi. Hatupingi Dnata kutoa huduma Zanzibar kwani tunajua umuhimu wa uwekezaji.
Tunapinga Dnata kupewa ukiritimba, jambo ambalo ni kinyume na sheria za Jamhuri ya Muungano na sheria za Zanzibar.
SOMA ZAIDI: Je, Rais Mwinyi Ni Abiy Wa Zanzibar?
Tuchukulie kuwa Dnata wana uwezo mkubwa kiutendaji na hivyo ni bora kuliko watoa huduma waliokuwepo, kwa nini wapendelewe badala ya kuwashindanisha na waliokuwapo?
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, ilipofunguliwa ‘Terminal 3’ watoa huduma waliokuwepo hawakuondolewa bali mtoa huduma wa tatu aliongezwa kushindana na waliokuwepo.
Kwa nini Zanzibar mtoa huduma wa tatu aongezwe na kuondoa wengine? Tunaamini kuwa kama watoa huduma waliokuwepo uwezo wao ni mdogo ushindani utawaondoa kwenye soko na Zanzibar kupata kilichobora zaidi.
Kwa nini nguvu inayotumika kuwabeba mbeleko Dnata ni kubwa kiasi cha kuvunja sheria za nchi?
Je, ni kwa sababu ya hisa asilimia 35 za wazawa? Mamlaka za Zanzibar zitueleze basi hawa wenye asilimia 35 kwenye kampuni iliyoanzishwa na Dnata ni akina nani.
Hata hivyo, ACT-Wazalendo tutakuwa Tibirinzi, Pemba mnamo Machi 4, 2023, na tutaeleza zaidi kuhusiana na suala hili huko.
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.
2 responses
Nawasubiri Tibirinzi