Je, Rais Mwinyi Ni Abiy Wa Zanzibar?

Tofauti na Ethiopia ya Abiy, Zanzibar ni sehemu ya Tanzania. Ni kiasi gani Mwinyi ‘ataruhusiwa’ kuwashughulikia wahafidhina wa tabaka la watawala wa Zanzibar bila kuingiliwa na mamlaka za Jamhuri ya Muungano?

Waziri Mkuu wa Ethiopia Ahmed Abiy ameishangaza, kisha akaitikisa Ethiopia. Abiy aliingia madarakani Aprili 2, 2018. Kabla ya hapo hakupewa nafasi kubwa kuwa kiongozi mkubwa wa nchi hiyo, licha ya kwamba alishika nafasi ya Waziri wa Sayansi na Teknolojia mwaka 2015, nafasi aliyohudumu kwa miezi 12 tu. Abiy ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ya kikazi kama mwanajeshi na kiongozi mwandamizi katika idara za kijasusi za Ethiopia.

Abiy ana wasifu wa kipekee: ni Mkristo wa Kiprotestant licha ya kwamba baba yake ni Muislam na mama yake ni Mkristo wa dhehebu la Kiethiopia la Kiothodoksi. Licha ya kwamba anatokea eneo la Oromia, wasifu huu unampa taswira ya utaifa wa Ethiopia katika nchi ambayo utambulisho wa kikabila unapewa nafasi kubwa. “Abiy hana utambulisho. Siyo Mmoromo, siyo Muamhara, siyo Mtigray wala si Msidama,” anasema mmoja wa waasisi na washauri wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) – chama cha kisiasa kutoka jimbo la Tigray ambalo sasa lipo vitani dhidi ya serikali ya Addis Ababa.

Abiy aliingia madarakani huku nchi yake ikiwa kwenye mtanzuko mkubwa wa kisiasa. Watu wa eneo lake la Oromia na kwingineko walikuwa wakiandamana kupinga rushwa, utawala wa kiimla,   upendeleo, ukosefu wa ajira, pamoja na mambo mengine. Muda mfupi baada ya kuingia madarakani Abiy alianzisha mageuzi ya kiuchumi na kisiasa. Kiuchumi, alitangaza mpango kabambe wa kubinafsisha mashirika ya umma na kuifungua milango ya Ethiopia kwenye soko huria.

Hatua za mageuzi zazaa maadui wa ndani

Kisiasa, ndani ya miezi michache tangu kuapishwa alifanya mambo makubwa yafuatayo: mosi, aliwaachia huru maelfu ya wafungwa wa kisiasa, wakiwemo walioshitakiwa kwa makosa ya ugaidi. Abiy alikubaliana na hoja kwamba sheria ya ugaidi nchini Ethiopia ilikuwa ikitimuka vibaya kuwaonea na kuwakandamiza wapinzani wa serikali ya Addis Ababa. Sanjari na hili, Abiy aliyahalalisha makundi ambayo watawala waliopita waliyaharamisha, na kulegeza msimamo kandamizi wa serikali dhidi ya vyombo vya Habari.

Pili, Abiy alitatua mgogoro wa mpaka kati ya nchi yake na Eritrea, mgogoro ambao umedumu kwa miongo miwili. Abiy alikubali kuipa nchi hasimu ya Eritrea maeno ya mpakani waliyokuwa wanagombea, kama ambavyo ilipendekezwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kwa miongo miwili, serikali ya Addis Ababa ilikaidi mapendekezo hayo ya Umoja wa Mataifa na kusababisha mapigano yasiyokwisha kati ya majeshi ya Eritrea na Ethiopia. Hatua hii ya Abiy imesaidia sana kuleta mahusiano ya kawaida baina ya nchi hizi mbili.

Tatu, Abiy aliwafuta kazi ‘vigogo’ wa jeshi na watumishi wa umma waliokuwa wakituhumiwa kwa rushwa, pamoja na kuatangaza nia ya kuanzisha mchakato wa kuboresha Katiba. Wengi waliofutwa kazi kwa tuhuma za rushwa ni kutoka kabila la Tigray ambao licha ya uchache wao walihodhi madaraka mkubwa katika Serikali Kuu ya Ethiopia.

Hatua hizi zimemjengea Abiy umaarufu mkubwa. Mwishoni mwa 2019, Kamati ya Nobel ya Norway ilimtangaza Abiy kuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel. Nje na ndani ya Ehtiopia Abiy amejijengea taswira ya kiongozi mwenye uthubutu ambaye yuko tayari kufanya maamuzi magumu.

Lakini Abiy pia amejijengea maadui hasa ndani ya Ethiopia. Miezi miwili tu tangu aingie ofisini kama Waziri Mkuu, Abiy alinusurika kifo baada ya jaribio la kutaka kumuua kwa bomu. Jimbo Tigray ambalo wanasiasa wake wamekuwa wakifaidi mema ya nchi kwa takribani miongo mitatu wanamuona Abiy kama msaliti. Wanaona jitihada za Abiy kuisuka upya Ethiopia kama mbinu za kutafuta mchawi. Mageuzi ya Abiy yamewageuzia kibao na sasa wamekuwa wahanga, na wametangaza nia ya kumuasi. Hiki ndicho kinachoendelea sasa, vita kati ya wapiganaji wa wa jimbo la Tigray (Tigray People’s Libearion Front, au TPLF) na wanajeshi wa jeshi la Ethiopia. Hii ni mada nyingine.

Mwinyi arithi Zanzibar yenye mpasuko wa kisiasa  

Mwinyi aliapishwa Novemba 2, 2020 kuwa Rais wa Zanzibar baada ya kupata ushindi wa kipekee katika muktadha wa siasa za ushindani visiwani humo. Alipata asilimia 76.27 ya kura, huku mpinzani wake Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo akiambulia asilimia 19.87 ya kura zote. Katika chaguzi zilizopita, matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar huakisi mpasuko wa kisiasa visiwani humo kiasi kwamba ushindani huwa mkali. Ushindi wa Mwinyi uligubikwa na shutuma za wizi wa kura, vitisho na mateso dhidi ya wapinzani na taarifa za vifo vya raia. Mwinyi amerithi nchi yenye mpasuko wa kisiasa.

Awali baada ya kutangazwa kuwa mgombea wa CCM Zanzibar, Mwinyi alipigwa vijembe na wapinzani wake kwa kuitwa mtalii – akishutumiwa kwamba sehemu kubwa ya maisha yake amekuwa akiishi Bara. Baadhi walimuona kama si Mzanzibari “kindakindaki.” Ikumbukwe kwamba baba yake, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, aliwahi pia kuwa Rais wa Zanzibar kabla ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Hali hii iliwafanya baadhi ya watu kutabiri anguko la Mwinyi na CCM visiwani Zanzibar hasa kwa kuzingatia kwamba mpinzani wake mkuu, Maalim Seif, ni jabali la siasa za visiwani na mwenye uzoefu wa kugombea tangu 1995.

Tangu aingie madarakani, Mwinyi amejitanabahisha kama kiongozi wa tofauti na waliomtangulia. Mara kadhaa amerejea kauli za kuhimiza usawa kwa kupinga ubaguzi, kuleta mageuzi ya kiuchumi pamoja kujenga umoja wa Wazanzibar. Baada ya kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif amesikika akimsifu Mwinyi kwa kuachana na wahafidhina na kuweka ‘damu mpya’ katika safu yake viongozi. Kwa muongo mmoja, Mwinyi alihudumu kama Waziri wa Ulinzi wa Tanzania. Kama Abiy, ana uzoefu wa masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.

Ingawa ni mwezi mmoja tu tangu aingie madarakani, Rais Mwinyi hajachukua hatua madhubuti kuoenesha uelekeo mpya wa Zanzibar. Ni tofauti kabisa na Abiy. Baadhi ya watu wanamsifu kwa kitendo chake cha kukialika chama kikuu cha upinzani kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), lakini hili ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, na si mara ya kwanza kwa Upinzani kuwa sehemu ya Serikali visiwani humo. Kauli za mara kwa mara za kuhimiza umoja na kujenga misingi ya usawa pekee hazitoshi kuipa Zanzibar, nchi yenye makovu makubwa ya kisiasa, muelekeo mpya. Hivyo hivyo kwa ‘sura mpya’ kwenye safu yake ya uongozi. Sura mpya lazima zifanye kazi kwenye misingi na falsafa mpya vinginevyo zitabaki tu hivyo zilivyo – mpya!

Mwinyi na cosmetic changes

Kama tutakubaliana kwamba Rais Mwinyi amefanya mabadiliko tangu aingie madarakani, bila shaka tutakubaliana pia kwamba mabadiliko hayo ni cosmetic changes tu. Mtu akipaka manukato akanukia, kisha akajiremba kwa wanja na angel face, nywele akazitia kalikiti au super black, mtu huyo hubadilika kwa sura na mwonekano lakini daima hubaki kuwa yule yule. Kinachohitajika Zanzibar si cosmetic changes bali mabadiliko ya kimfumo ambayo yatawafanya Wazanzibar wote kujivunia utaifa wao kwa kuweka misingi ya haki na usawa.  Zanzibar ambayo itatawaliwa kwa mujibu wa sheria bila uonevu, bila kusahau haki na fursa sawa za kiuchumi.

Hata hivyo, Rais Mwinyi ana nafasi ya kuweka historia Zanzibar. Kama Abiy, Mwinyi ana fursa ya kuishangaza Zanzibar na kuifanya iondokane na unyonge, umasikini, rushwa, ubaguzi wa kisiasa, na uonevu. Changamoto ni kwamba, tofauti na Ethiopia ya Abiy, Zanzibar ni sehemu ya Tanzania. Ni kiasi gani Mwinyi ‘anaruhusiwa’ kuwashughulikia wahafidhina wa tabaka la watawala wa Zanzibar bila kuingiliwa na mamlaka za Jamhuri ya Muungano? Vile vile, ni kwa kiasi gani mamlaka hizo zipo tayari kumsaidia Mwinyi kuifanya kazi hiyo? Kwa muundo wa kiserikali, maendeleo ya Zanzibar hayawezi kuongelewa nje ya Muungano, na hiyo ni changamoto.

Lakini pia ni ubashiri halali kwamba wapo miongoni wa makundi ya utawala wa zamani na ya kihafidhina ambayo hayatafurahishwa hata na cosmetic changes za Rais Mwinyi. Kama hawafurahishwi na hayo, watafanya nini pale kiongozi huyo atakapoanza kutekeleza mabadiliko halisi ya kimfumo? Viongozi wa Tigray wao walitangaza vita ya mapigano ya silaha dhidi ya Abiy, hili haliwezekani kwa Zanzibar hususani katika muktadha wa Muungano. Lakini kama Mwinyi atafika huko, atarajie vita ya kisiasa kutoka kwa watu wa kambi yake ya kisiasa ambao sasa watakuwa wahanga wa mabadiliko hayo. Ni hapa ambapo naamini Maalim Seif na chama chake watataka kutumia fursa hii kujiimarisha. Hii nayo ni mada ya siku nyingine.

Kuponya majeraha ya uchaguzi

Bahati nzuri Rais Mwinyi ana pa kuanzia. Ameingia madarakani katika muktadha wa mtanzuko wa kisiasa. Aanze na hili kwa kuponya majeraha ya uchaguzi. Aongozwe na uungwana, akiri alipokosea yeye binafsi na chama chake. Awafute machozi waathirika wa mchakato wa uchaguzi. Awashike mkono waliopoteza ndugu na jamaa zao pamoja na majeruhi. Kisha aahidi makosa ya zamani hayatarudiwa tena kwa kuanzisha mchakato wa kisiasa ambao utajengwa katika misingi ya haki na usawa.

Baadhi ya watu wana shauku ya kuona kama, kwa mfano, Rais Mwinyi atawaachia huru watu ambao sehemu ya jamii inaamini wamefungwa kwa makosa ya kisiasa ya kupachikwa kama ambavyo Abiy alifanya. Je, Rais Mwinyi atatumia ushawishi wake kuongeza kasi ya upelelezi katika kesi dhidi ya Mashehe wa Uamsho au kuachiwa huru kabisa? Je, Rais Mwinyi atawakaribisha nyumbani Wazanzibari ambao wamekimbia nchi yao kwa kuhofia usalama wao? Je, Rais Mwinyi atathubutu kuunda mfumo wa kisiasa unaowapa washindani wa kisiasa nafasi sawa? Je, ni kwa kiasi gani Rais Mwinyi atajikita kwenye kujenga mfumo-shirikishi wenye taasisi imara zinazoheshimu misingi ya sheria bila kujali tofauti za kitabaka, rangi na kisiasa? Je, Rais Mwinyi atathubutu kuondoa dhana ya kwamba Zanzibar inaburuzwa ikiwemo kuchaguliwa viongozi wake na Jamhuri ya Muungano (soma Tanganyika)?

Hivi na vingine kama hivyo ndiyo vigezo vya kupima uelekeo mpya wa Zanzibar. Rais Mwinyi ana fursa ya kuweka historia ya kuanzisha mchakato wa kisiasa ambao utakumbukwa na kuenziwa na vizazi vijavyo. Kinyume na hapo atakumbukwa tu kama miongoni wa watu waliowahi kuiongoza Zanzibar. Kama tunavyoona kwa Abiy, vipo vikwazo ambavyo atakutana navyo kama ana nia thabiti ya kuleta mabadiliko. Ni lazima avishinde vikwazo hivyo, au ajaribu sana kuvishinda.

Muhidin Shangwe ni mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kupitia barua pepe yake ambayo ni shangwez@yahoo.com au kupitia Twitter @ShangweliBeria.

Dr. Muhidin Shangwe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved